Mwandishi:
Mhhariri
ULY CLINIC
Dkt. Benjamin L, MD
Jumatatu, 8 Novemba 2021

Wasiwasi uliopitiliza
Kila mtu hupata wasiwasi kwenye maisha yake, kuna mambo mengi yanayoweza kufanya mtu apate wasiwasi, mfano unapoenda kufanya mtihani, unapofanya interview ya kazi au unapowaza kuhusu kufanyiwa upasuaji. Wasiwasi ni kawaida kwenye maisha.
​
Hata hivyo hofu kwa watu wengi huja na kuondoka, endapo hofu inadumu hupelekea maisha yamtu kupungua thamani kwa kuishi bila kujiamini na kushindwa kushiriki vema kwenye kazi
​
Yapo matibabu yanayoweza kukusaidia kuondokana natatizo hili, matibabu huhusisha ushauri wa namna ya kukabiliana na hofu/wasiwasi pamoja na au kupewa dawa. Matibabu yanayoshauriwa sana ni Tiba ushauri ambapo utapewa dalasa maalumu baada ya daktari kufahamu ni nini kinachokupa wasiwasi na hofu iliyopitiliza.
​
Dalili
Dalili za mara kwa mara za wasiwasi ni hizi zifuatazo;
Kuhofu, kutotulia sehemu moja ama kuwa na fadhaa
Kuwa na hisia za kutokea kwa hatari, kuingiwa na hofu ghafla
Kuongezeka kwa mapigo ya moyo
Kupumua haraka haraka
Kutokwa jasho
Kutetemeka
Kuhisi uchovu na kuwa dhaifu
Kushindwa kufikili kuhusu kitu kingine zaidi ya kuwa na hofu iliyopo
Kupata shida ya kulala
Kushindwa kuzuia hofu
Kuwa na tabia ya kukwepa/kujizuia na vitu vinavyokupa wasiwasi
Aina
Aina tofauti za wasiwasi zinajulikana amabazo ni;
Agoraphobia
​
Ni aina ya tatizo la wasiwasi, huonekana pale mtu anapojizuia kwenda sehemu ama kujiweka kwenye hali ambapo inaweza kukusababisha ashikwe na wasiwasi au kumfanya awe kama amekamatwa, hana msaada au ametahayarika.
Wasiwasi kutokana na ugonjwa
​
Aina hii hutokana na ugonjwa ama tatizo Fulani la kiafya. Mtu anapokuwa na tatizo lolote la kiafya huwa na wasiwasi sana. Mfano ni kipindi cha hofu ya ugonjwa wa COVID-19 ya mwaka 2019/2020 watu wengi walikuwa na hofu na hivyo kuwafanya washindwe kufanya kazi na wengine kupoteza maisha.
Wasiwasi kwa ujumla
​
Mtu huwa na wasiwasi unaodumu na wa mara kwa mara kuhusu kazi, matukio hata mambo ya kawaida sana. Hofu huwa kubwa kuliko kawaida, huwa vigumu kujizuia kutohofu. Hofu hii hudhuru mwonekano wa nje wa mtu na hivyo huweza kutambulika na watu wengine kuwa wana tatizo. Kwa kawaida Hutokea pamoja na aina zingine za wasiwasi.
Wasiwasi wa udhaifu wa kupaniki
​
Hutokea pale ambapo mtu anakuwa na hofu inayoingia ghafla, mtu huwa na huzuni ya ghafla kali na huhofu au hupata hofu kuu inayofikia kileleni ndani ya dakika chache. Unaweza kupata hisia za kuwa ndo mwisho wa maisha, kuishiwa pumzi, moyo kwenda kasi . Hali hizi zinaweza kusababisha hisia za hofu kwamba mambo kama haya yanaweza kujitokeza na hujizuia ama kuzuia hali inayoweza kusababisha kutokea na wasiwasi huo.
Kunyamaza kwenye baadhi ya mambo
​
Hofu hii hujidhihirisha kwa mtoto kwa kushindwa kuzungumza akiwa kwenye hali/jambo/mahari Fulani mfano shuleni. Watoto hawa huweza kuzungumza jambo hilo wakiwa sehemu zingine kama nyumbani ama na ndugu wa karibu. Hali hii huweza kuathiri ufanisi shuleni, kazini na mambo ya kijamii.
Wasiwasi wa kutengana
​
Mtoto huwa na wasiwasi wa kuachana na wazazi wake waliomzaa ama mlezi ambaye anamuhudumia kama mzazi wake au mpenzi wake.
Wasiwasi wa kijamii
​
Katika aina hii ya wasiwasi , mtu anakuwa na hofu kubwa, na hujizuia kwenye mambo/ matukio ya kijamii kwa sababu hujihisi ata aibika/dharaurika, hujitambua na hujihisi kwamba watu watamhukumu na kuonekana hafai.
Wasiwasi wa kitu Fulani tu
​
Wasiwasi kutokana na matumizi ya dawa za kulevya
Mtu anapata wasiwasi endapo hatatumia dawa alizokuwa anatumia- dawa za kulevya.
​Visababishi
Visababishi vya wasiwasi uliopitiliza
​
Visababishi vya wasiwasi uliopitiliza havifahamika vema. Kupatwa na jambo baya la hapo awali katika maisha kama vile kuuguza mpendwa kisha akafia mikononi mwako, kufanyiwa/kushuhudia ajali mbaya au tukio baya huonekana kuamsha tatizo la wasiwasi uliopitiliza kwa watu ambao tayari wana hatari kubwa ya kupata wasiwasi. Kurithi baadhi ya vinasaba pia huonekana kuchangia kupata wasiwasi.
​
Magonjwa na hali za kiafya
​
Magonjwa ya moyo
Kisukari
Kiwango cha juu cha homoni za tezi ya thyroid
Matatizo ya kifua kama COPD na asthma
Kuacha kutumia dawa za kulevya ama kutumia dawa za kulevya
Kuacha kutumia pombe, dawa za wasiwasi au madawa mengine
Maumivu sugu na ugonjwa wa matumbo sumbufu(IBD)
Saratani kadhaa zinazosababisha uzalishaji wa homoni ya kupambana ama kukimbia(adrenaline)
Vihatarishi
Vihatarisho vya kupata tatizo la wasiwasi uliopitiliza ni;
Jeraha
Mtoto aliyebakwa ama alishuhudia kitendo kiovu kama cha kubakwa ama mauaji huwa na hatari ya kupata wasiwasi wakati Fulani katika maisha yake. Watu wazima waliopata majeraha pia huweza kupata wasiwasi maishani mwao. Tatizo hilo huitwa PSD. Soma zaidi kuhusu PSD sehemu nyingine katika makala za ULY CLINIC
Msongo wa mawazo kutokana na tatizo la kiafya
Kuwa na tatizo la kiafya au ugonjwa mbaya husababisha kwa kiasi kikubwa kuwa na hofu iliyopitiliza kuhusu matibabu na mwisho wako.
Kujengeka kwa msongo wa mawazo
Mtu anayepata msongo wa mawazo mkubwa ama kujengeka taratibu kwa misongo midogomidogo huweza kuamsha wasiwasi uliopitiliza. Mfano kifo kwenye familia, msongo wa mawazo katika kazi ama tatizo la kifedha linaloendelea.
Utu wa mtu
Watu wenye utu aina Fulani huweza kupata wasiwasi uliopitiliza kuliko watu wenye utu tofauti na mtu huyu
Matatizo mengine ya akili
Watu wenye matatizo mengine ya kiafya kama huzuniko kwa kawaida huwa na wasiwasi.
Ndugu mwenye wasiwasi
Kuwa na ndugu mwenye tatizo la wasiwasi uliopitiliza humweka mtu huyo kuwa na wasiwasi katika kipindi Fulani cha maisha Fulani.
Matumizi ya dawa ya kulevya ama pombe
Dawa za kulevya na pombe ama kuacha kutumia vitu hivi kwa mtu ambaye alikuwa anatumia kwa mda mrefu husabisha tatizo la wasiwasi uliopitiliza.
Madahara
​
Madhara ya wasiwasi huweza kumfanya mtu akafanya jambo Fulani baya ama kupata tatizo lingine la kiafya kama;
​
Sononeko kuu
Kutumia dawa za kulevya
Kukosa usingizi- insomia
Matatizo ya umengenyaji wa chakula ama matatizo ya tumbo
Kichwa kuuma na maumivu sugu
Kujitenga na jamii
Kufanya vibaya shulenii na kazini
Maisha mabaya
Kujiua
Vipimo na matibabu.
Yapo makundi na aina kadhaa za dawa zinazoweza kutibu tatizo la wasiwasi uliopitiliza, madhumuni ya matibabu ni kutafuta nini kinachosababisha wasiwasi huo na kwa namna gani mtu aweze kuendana na mazingira aliyonayo
​
Namna ya kujizuia kupata wasiwasi
​
Hakikisha unafanya mazoezi
Acha kunywa pombe na kutumia dawa za kulevya
Hakikisha unafanya vitu au mambo unayoyapenda ili yakufanye uwe bize na usiwe na mawazo mengi
Changanya mambo yako. Endapo unaanza kupata mawazo, achana mara moja kukaa sehemu hiyo, unaweza kuanza kufanya kazi ingine au kutembea mwendo kiasi
Jichanganye na watu. Usipende kukaa mwenyewe muda mrefu, jiweke bize na vitu unavyovipenda sana na vinavyokuchukua akili yako, nenda kwa kwa rafiki au kuongea na mpenzi wako
Jifahamu mwenyewe kwanza. Unapaswa kufahamu ni vitu gani vinavyosababisha upate wasiwasi, viandike chini, vitu hivi vitamsaidia daktari wako kufahamu ni namna gani kukusaidia katika tiba ushauri
Fahamu vema kuhusu tatizo lako. Kusoma na kufahamu vema kuhusu tatizo lako itakufanya ufahamu aina tofauti za matibabu yaliyopo na kukupa nafasi ya kufuata matibabu kama yanavyotolewa na daktari wako.