top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Sospeterr B, MD

Imeboreshwa:

16 Julai 2025, 05:21:14

Asherman Sindrome: Kisababishi, Dalili na Uhalisia wa matibabu kwa miti shamba

Asherman Sindrome: Kisababishi, Dalili na Uhalisia wa matibabu kwa miti shamba

Swali la msingi

"Habari daktari, mimi ni mwanamke niliyepewa majibu ya kuwa na Asherman Syndrome baada ya kuharibu mimba. Sasa siwezi kupata hedhi kama kawaida na nina wasiwasi juu ya uzazi. Naomba kufahamu, je, Asherman inaweza kutibiwa kwa miti shamba au njia za asili?"


Majibu

Asherman Syndrome ikifahamika pia kama Asherman sindromu ni hali inayotokana na makovu ndani ya mji wa mimba (kizazi), ambayo huweza kusababisha matatizo ya hedhi, maumivu, au ugumu wa kupata ujauzito. Wagonjwa wengi huuliza kama hali hii inaweza kutibiwa kwa kutumia miti shamba. Makala hii inaeleza chanzo, dalili, matibabu yanayotambulika, na ukweli kuhusu matumizi ya dawa za asili.


Asherman Sindromu ni nini?

Asherman Sindromu ni hali inayotokea pale ambapo tishu ndani ya mji wa mimba (utando laini ndani wa kizazi) hujiponya kwa njia ya kutengeneza makovu au kushikamana kwa kuta za kizazi. Hii huathiri uwezo wa uterasi kujipangilia kwa ajili ya hedhi au ujauzito.


Visababishi

Sababu kuu zinazochangia kusababisha Asherman Sindromu ni kama zilizoorodheshwa katika jedwali linalofuata;

Visababishi

Maelezo

Upasuaji wa kurekebisha mimba (Utoaji mimba kwa kukuna kizazi)

Ndiyo kisababishi kikuu, hasa baada ya kuharibika kwa mimba

Uchunguzi au matibabu ya kuondoa uvimbe wa kizazi (fibroid)

Huweza kuharibu ukuta wa kizazi

Maambukizi ya kizazi

Kama vile kifua kikuu cha uzazi (TB ya kizazi), magonjwa ya zinaa yanayopelekea PID

Uunguzazaji wa kizazi

Kwa sababu za kimatibabu au ajali ya kimatibabu


Dalili za Asherman Sindromu

  • Kukosa hedhi kabisa (amenorea) baada ya kuharibu mimba au upasuaji

  • Hedhi nyepesi isiyo ya kawaida

  • Maumivu ya tumbo kila mwezi bila kutoka damu (kutoingia hedhi)

  • Ugumu wa kushika mimba

  • Mimba kuharibika mara kwa mara


Uchunguzi wa Asherman Sindromu

  • Hysteroscopi – kamera maalum huangalia hali ya ndani ya kizazi kuangalia hali yake.

  • Ultrasound ya 3D – kugundua makovu au kushikamana kwa kizazi

  • Histerosalpingogram (HSG) – X-ray maalum kuonyesha mabaniko ya mji wa mimba na kizazi



Matibabu yanayotambulika kisayansi

Njia

Maelezo

Upasuaji wa kihisteroscopi

Kuondoa makovu na kufungua kizazi kwa njia salama ya kutumia kamera.

Tiba homoni Estrojen

Husaidia ukuta wa mji wa mimba kupona vizuri baada ya upasuaji

Tiba puto au kitanzi ndani ya kizazi

Huwekwa kwa muda kuzuia kuta za kizazikushikana tena baada ya upasuaji

Ufuatiliaji wa hedhi na ujauzito

Hupendekezwa baada ya matibabu hadi mfumo urejee kawaida


Je, miti shamba inaweza kutibu Asherman Sindromu?

Mpaka sasa, hakuna ushahidi wa kisayansi unaoonyesha kuwa miti shamba inaweza kuondoa makovu ndani ya uterasi au kubanduka kwa kuta za uterasi. Hii ni kwa sababu:

  • Miti shamba haiwezi kuingia ndani ya kizazi kuondoa makovu

  • Haifanyi kazi ya kubadili hali ya kushikamana kwa tishu za kizazi

  • Inaweza kuchelewesha matibabu sahihi na kusababisha uharibifu zaidi


Tahadhari
  • Baadhi ya dawa za kienyeji huweza kusababisha uambukizo, kuunguza kizazi au kuathiri uzazi zaidi

  • Wagonjwa wengi huchelewa kupata matibabu sahihi kwa matumaini ya mitishamba

  • Kumbuka: Asherman ni tatizo la kimaumbile, si la homoni peke yake


Ushauri salama
  • Fanya vipimo sahihi kwa daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake

  • Kama upasuaji ulishafanyika, zingatia ushauri wa kufuatilia kwa karibu

  • Usitumie dawa au miti bila uchunguzi wa kisayansi

  • Tafuta ushauri wa kitaalamu mapema kabla ya hali kuwa mbaya


Hitimisho

Asherman Sindromu ni hali ya makovu ndani ya mji wa mimba inayohitaji uchunguzi wa kitaalamu na matibabu ya upasuaji mdogo. Miti shamba haiwezi kuondoa makovu haya wala kubadili hali ya kushikana kwa kuta za uterasi. Ucheleweshaji wa matibabu sahihi unaweza kuathiri uwezo wa kupata ujauzito wa baadaye.

ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

Imeandikwa,

16 Julai 2025, 05:12:19

Rejea za mada hii

  1. March CM. Management of Asherman’s syndrome. Reprod Biomed Online. 2011;23(1):63–76.

  2. Yu D, Wong YM, Cheong Y, Xia E, Li TC. Asherman syndrome–one century later. Fertil Steril. 2008;89(4):759–79.

  3. Schenker JG, Margalioth EJ. Intrauterine adhesions: an updated appraisal. Fertil Steril. 1982;37(5):593–610.

  4. AAGL Practice Report: Practice Guidelines for management of intrauterine adhesions. J Minim Invasive Gynecol. 2010;17(1):1–7.

  5. American College of Obstetricians and Gynecologists. Diagnosis and Management of Asherman Syndrome. ACOG Practice Bulletin. 2022.

bottom of page