Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Benjamin M, MD
Imeboreshwa:
15 Februari 2026, 06:40:34

Dalili za PID ni zipi?
PID ni maambukizi ya viungo vya uzazi vya ndani (mfuko wa uzazi, mirija ya uzazi na ovari).Tatizo kubwa ni kwamba wagonjwa wengi hawatambui mapema kwa sababu dalili zake huiga magonjwa mengine kama UTI, appendicitis au maumivu ya kawaida ya hedhi. Kwa hiyo, utambuzi wa PID hutegemea sana kutambua dalili mapema hata kabla ya vipimo ili kuthibitisha na kuondoa visababishi vingine vinavyofanana dalili.
1) Dalili kuu (karibu wagonjwa wote)
Hizi ndizo dalili muhimu zaidi kitabibu. Zikitokea pamoja, daktari huanza matibabu hata bila majibu ya maabara.
Maumivu ya tumbo la chini
Dalili ya kwanza na ya kawaida zaidi
Huwa ya kuvuta au kubana
Huongezeka wakati wa kutembea, kusimama au tendo la ndoa
Mara nyingi hudhaniwa ni “maumivu ya hedhi”
Maumivu wakati wa tendo la ndoa
Maumivu ndani kabisa tumboni
Huongezeka kadri tendo linavyoendelea
Hupelekea baadhi ya wanawake kuogopa tendo la ndoa
Uchafu ukeni usio wa kawaida
Rangi: njano, kijani au kijivu
Mzito au wa usaha
Harufu kali isiyo ya kawaida
Maumivu wakati wa kubonyeza mfuko wa uzazi
Hii ni dalili ya uchunguzi wa daktari wakati anaangalia uwepo wa PID
Daktari akigusa shingo ya kizazi hutokea maumivu makali
Maumivu upande wa ovari
Maumivu upande mmoja au pande zote za nyonga
Huonyesha maambukizi yameshafika kwenye mirija ya uzazi
Dalili hizi peke yake zinatosha kuanza matibabu haraka ili kulinda uwezo wa kushika mimba.
2) Dalili za maambukizi
Huonyesha bakteria wameanza kuenea mwilini.
Homa (≥ 38°C)
Baridi kali mwilini
Kichefuchefu au kutapika
Uchovu mkali sana
Mapigo ya moyo kwenda kasi
Muhimu: wanawake wengi wenye PID hawapati homa — hivyo kukosa homa hakumaanishi uko salama.
3) Dalili za uke na hedhi
Hizi ndizo wagonjwa wengi hupelekea kliniki.
Kutokwa damu baada ya tendo la ndoa
Kutokwa damu katikati ya mzunguko
Hedhi kuwa nyingi au chungu kuliko kawaida
Kuwashwa uke
Harufu kali ya samaki ukeni (huweza kufanana na maambukizi ya vajinosisi ya bakteria)
4) Dalili za njia ya mkojo na utumbo
Ndiyo sababu PID huchanganywa sana na UTI au ugonjwa wa kidole tumbo(apendeksi)
Maumivu wakati wa kukojoa
Kukojoa mara kwa mara
Maumivu wakati wa haja kubwa
Kuvimba tumbo
Gesi nyingi tumboni
5) Dalili hatari
Ukiona dalili hizi nenda hospitali HARAKA
Maumivu makali upande mmoja wa tumbo
Kuzimia au kizunguzungu
Kutapika sana
Tumbo kuwa gumu kama ubao
Kushindwa kutembea kwa maumivu
Kutokuja hedhi + maumivu makali
Huashiria mimba nje ya mfuko
6) Dalili za PID sugu
Hapa wagonjwa wengi hawaelewi kabisa wana ugonjwa.
Maumivu ya nyonga kwa miezi
Kushindwa kupata mimba
Maumivu wakati wa ovulation
Maumivu ya mgongo wa chini
Tendo la ndoa kuwa chungu kila mara
Ukweli muhimu
Takribani asilimia 30–40 ya wanawake wenye PID hawana homa wala uchafu mwingi bali huwa na maumivu tu. Ndiyo maana PID ni chanzo kikubwa cha utasa kimya kimya.
Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake
1. Naweza kuwa na PID bila uchafu ukeni?
Ndiyo, unaweza kuwa na PID bila uchafu ukeni. Tafiti zinaonyesha kuwa sehemu kubwa ya wanawake wenye PID hupata maumivu ya nyonga pekee bila homa au uchafu mwingi. Hii huitwa subclinical PID (PID isiyo na dalili nyingi wazi).
Tatizo ni kwamba hali hii huchelewesha utambuzi, na maambukizi yanaweza kuendelea kuharibu mirija ya uzazi kimya kimya. Hivyo, maumivu ya chini ya tumbo yasiyoelezeka, hasa kwa mwanamke mwenye historia ya maambukizi ya zinaa, yanapaswa kuchukuliwa kwa uzito hata kama hakuna uchafu mwingi.
2. PID inauma wapi hasa?
PID huuma zaidi chini ya tumbo (pelvic area) — eneo lililo chini ya kitovu.
Maumivu yanaweza kuwa:
Pande zote mbili za nyonga
Upande mmoja (hasa kama kuna jipu la ovari)
Ya kuvuta au kubana
Yanayoendelea kwa siku kadhaa
Maumivu huongezeka wakati wa:
Tendo la ndoa (deep penetration)
Kutembea haraka
Kubonyeza chini ya tumbo
Wakati wa ovulation
Wakati mwingine maumivu husambaa hadi mgongo wa chini.
3. PID inaweza kufanana na UTI?
Ndiyo, PID mara nyingi huchanganywa na UTI (maambukizi ya njia ya mkojo).
Dalili zinazofanana ni:
Maumivu wakati wa kukojoa
Kukojoa mara kwa mara
Maumivu ya chini ya tumbo
Tofauti ni kwamba PID huambatana pia na:
Maumivu wakati wa tendo la ndoa
Maumivu ya ndani kabisa ya nyonga
Uchafu ukeni usio wa kawaida
Ikiwa dawa za UTI hazisaidii na maumivu yanaendelea, PID inapaswa kufikiriwa.
4. Naweza kupata PID bila homa?
Ndiyo. Wanawake wengi wenye PID hawapati homa kabisa.
Homa hutokea zaidi pale maambukizi yanapokuwa makali au yameanza kuenea mwilini. Lakini PID ya hatua za mwanzo mara nyingi huonyesha maumivu tu. Kutokuwepo kwa homa hakumaanishi hakuna maambukizi.
5. Maumivu ya hedhi yanawezaje kutofautiana na PID?
Hedhi yenye maumivu:
Huja kabla au siku za mwanzo za hedhi
Huisha baada ya siku chache
Hayahusiani sana na tendo la ndoa
Maumivu ya PID:
Huendelea hata baada ya hedhi kuisha
Huuma wakati wa tendo la ndoa
Huambatana na maumivu ya kubonyeza mfuko wa uzazi
Huwa ya muda mrefu au yanayorudia mara kwa mara
Ikiwa maumivu yanaongezeka tofauti na kawaida yako, tafuta uchunguzi.
6. PID husababisha utasa baada ya muda gani?
Uharibifu wa mirija ya uzazi unaweza kuanza ndani ya siku chache hadi wiki kama maambukizi hayatatibiwa.
Kila tukio la PID huongeza hatari ya:
Mirija kuziba
Mimba kutungwa nje ya mfuko wa uzazi
Utasa wa kudumu
Hata maambukizi ya kwanza yanaweza kusababisha madhara ya muda mrefu.
7. Kutokwa damu baada ya tendo la ndoa ni ishara ya PID?
Ndiyo, inaweza kuwa ishara ya PID, hasa ikiwa inaambatana na:
Maumivu ya nyonga
Uchafu wa rangi isiyo ya kawaida
Maumivu wakati wa tendo
Hii hutokea kwa sababu shingo ya kizazi huwa imevimba (Sevisaitisi).
8. PID inaweza kuisha yenyewe?
Hapana. Dalili zinaweza kupungua kwa muda, lakini bakteria wanaweza kubaki ndani ya mirija ya uzazi.
Bila antibayotiki sahihi:
Maambukizi yanaweza kuwa sugu
Uharibifu wa mirija huendelea kimya kimya
Hatari ya utasa huongezeka
PID inahitaji matibabu ya haraka kwa antibiotiki.
9. PID inaathiri ovulesheni?
Ndiyo. PID inaweza:
Kusababisha maumivu makali wakati wa uvulesheni
Kusababisha kovu kwenye mirija ya uzazi
Kuzuia yai kupita vizuri
Hii ndiyo sababu baadhi ya wanawake wenye PID hupata ugumu wa kushika mimba.
10. Ni lini niende hospitali haraka?
Nenda hospitali mara moja ukipata:
Maumivu makali ghafla upande mmoja wa tumbo
Kizunguzungu au kuzimia
Kutapika sana
Tumbo kuwa gumu
Kukosa hedhi + maumivu makali
Hii inaweza kuashiria mimba nje ya mfuko (ectopic pregnancy) au jipu la ovari lililopasuka — hali hatari zinazohitaji matibabu ya dharura.
11. Je kuchelewa kupata hedhi, maumivu ya mgongo na chini ya kitovu ni dalili ya PID?
Inaweza kuwa PID — lakini pia inaweza kuwa hali nyingine.
PID inaweza kusababisha:
Maumivu chini ya kitovu (kwenye via vya nyonga)
Maumivu ya mgongo wa chini
Hedhi kubadilika au kutokwa damu isiyo ya kawaida
Hata hivyo, kuchelewa hedhi pamoja na maumivu makali lazima kuchunguzwe haraka ili kuondoa uwezekano wa:
Mimba ya kawaida
Mimba nje ya mfuko
Mabadiliko ya homoni
Ikiwa kuna:
Maumivu makali upande mmoja
Kizunguzungu
Kutokwa damu isiyo ya kawaida
Hii ni dharura ya kitabibu.
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
Imeandikwa,
15 Februari 2026, 06:30:52
Rejea za mada hii
Workowski KA, Bachmann LH, Chan PA, Johnston CM, Muzny CA, Park I, et al. Sexually transmitted infections treatment guidelines, 2021. MMWR Recomm Rep. 2021;70(4):1–187.
Haggerty CL, Ness RB. Epidemiology, pathogenesis and treatment of pelvic inflammatory disease. Expert Rev Anti Infect Ther. 2006;4(2):235–47.
Brunham RC, Gottlieb SL, Paavonen J. Pelvic inflammatory disease. N Engl J Med. 2015;372(21):2039–48.
Ross J, Guaschino S, Cusini M, Jensen J, Moi H. 2017 European guideline for the management of pelvic inflammatory disease. Int J STD AIDS. 2018;29(2):108–14.
Sweet RL. Pelvic inflammatory disease: current concepts of diagnosis and management. Curr Infect Dis Rep. 2012;14(2):194–203.
Wiesenfeld HC, Sweet RL. Progress in the management of pelvic inflammatory disease. Clin Obstet Gynecol. 2015;58(2):321–33.
Paavonen J, Westrom L, Eschenbach D. Pelvic inflammatory disease. In: Holmes KK, Sparling PF, Stamm WE, Piot P, Wasserheit JN, Corey L, et al., editors. Sexually Transmitted Diseases. 4th ed. New York: McGraw-Hill; 2008. p. 1017–50.
Centers for Disease Control and Prevention (CDC). Pelvic inflammatory disease (PID) – 2021 STI treatment guidelines. Atlanta: CDC; 2021.
Simms I, Stephenson JM. Pelvic inflammatory disease epidemiology: what do we know and what do we need to know? Sex Transm Infect. 2000;76(2):80–7.
Tsevat DG, Wiesenfeld HC, Parks C, Peipert JF. Sexually transmitted diseases and infertility. Am J Obstet Gynecol. 2017;216(1):1–9.
