top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Benjamin L, MD

Imeboreshwa:

21 Januari 2026, 09:34:56

Dalili za Kifua Kikuu (TB): Mwongozo kamili

Dalili za Kifua Kikuu (TB): Mwongozo kamili

Kifua Kikuu (Tuberculosis – TB) ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na bakteria aitwaye Mycobacterium tuberculosis. Ugonjwa huu huathiri zaidi mapafu, lakini pia unaweza kuathiri viungo vingine vya mwili kama ubongo, moyo, uti wa mgongo, mfumo wa uzazi na mkojo, mfumo wa chakula, na mitoki. Dalili za TB hutofautiana kulingana na umri, kinga ya mwili, uwepo wa magonjwa mengine (kama VVU), na sehemu ya mwili iliyoathirika.


Dalili za TB ya Mapafu (TB ya kawaida)

Hizi ndizo dalili zinazoonekana kwa watu wengi walio na TB ya mapafu:

  • Kukohoa mfululizo kwa zaidi ya wiki mbili

  • Kupata homa kwa muda mrefu (wiki kadhaa hadi mwezi)

  • Kutokwa na jasho jingi usiku (hadi kulowanisha mashuka)

  • Kupungua uzito bila sababu ya wazi

  • Kukohoa damu au makohozi yenye michirizi ya damu

  • Kupoteza hamu ya kula

  • Maumivu ya kifua au kushindwa kupumua vizuri

  • Mwili kuchoka na kukosa nguvu kwa muda mrefu


Dalili za TB kwa Watu Wenye HIV au Kinga ya Mwili ya Chini

Kwa watu wanaoishi na HIV au walio na kinga ya mwili iliyo dhaifu, dalili za TB zinaweza kuwa zisizo dhahiri:

  • Kupungua uzito kwa kasi

  • Homa ya muda mrefu au wakati mwingine kutokuwa na homa kabisa

  • Dalili zisizo maalum kama uchovu mwingi


Muhimu: Kwa kundi hili, kipimo cha makohozi kinaweza kuonyesha mtu hana TB ilhali anayo. Ndiyo maana vipimo vya kisasa kama GeneXpert na X-ray ya kifua hutumika kusaidia utambuzi.


Dalili za TB kwa Watoto na Wazee

Watoto na wazee mara nyingi hawaonyeshi dalili za wazi za TB kutokana na kinga ya mwili kuwa chini. Badala yake, wanaweza kuonyesha dalili kama:

  • Dalili za nimonia (pneumonia) isiyopona licha ya matibabu

  • Homa ya muda mrefu

  • Kushindwa kunenepa au kudhoofika


Dalili za TB iliyosambaa (TB ya nje ya kifua)


1. TB ya kuta ya nje ya Moyo (TB ya Perikadiamu)
  • Maumivu ya kifua

  • Kushindwa kupumua vizuri

  • Kushindwa kulala chali

  • Kuamka usiku kwa kukosa hewa


2. TB ya kuta za Ubongo(TB ya meninjezi)
  • Maumivu makali ya kichwa kwa wiki 2–3

  • Kuchanganyikiwa

  • Kupoteza fahamu

  • Degedege (kwa baadhi ya wagonjwa)


3. TB ya Uti wa Mgongo (Ugonjwa wa Pott)
  • Maumivu makali ya mgongo

  • Kukakamaa kwa uti wa mgongo

  • Kupinda kwa mifupa ya mgongo

  • Ganzi au kupooza kwa miguu endapo mishipa imeathirika


4. TB ya Mfumo wa Uzazi na Mkojo
  • Maumivu ya nyonga au chini ya mbavu

  • Kukojoa kwa maumivu au mara kwa mara

  • Kushindwa kukojoa vizuri

  • Kwa wanaume: kuvimba na maumivu ya mapumbu/korodani

  • Kwa wanawake: matatizo ya mfumo wa uzazi, ikiwemo ugumba


5. TB ya Mfumo wa Chakula
  • Vidonda vya mdomoni visivyopona

  • Ugumu wa kumeza

  • Maumivu ya tumbo yanayofanana na vidonda vya tumbo

  • Kuhara cha muda mrefu, wakati mwingine chenye damu


6. TB ya Mitoki (tezi limfu TB)
  • Kuvimba kwa mitoki bila maumivu makali

  • Mara nyingi huonekana shingoni, makwapani au kwenye nyonga


Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake

1. Je, TB huambukizwaje?

TB huambukizwa kupitia hewa pale mgonjwa mwenye TB ya mapafu anapokohoa, kupiga chafya au kuzungumza bila kujikinga.

2. Je, mtu anaweza kuwa na TB bila kukohoa?

Ndiyo. TB iliyoko nje ya mapafu inaweza kuwepo bila kukohoa kabisa.

3. Je, TB inatibika kabisa?

Ndiyo. TB inatibika kwa kutumia dawa maalum kwa kipindi cha miezi 6 au zaidi endapo mgonjwa atafuata maelekezo kikamilifu.

4. Kwa nini ni hatari kuacha dawa za TB kabla ya muda?

Kuacha dawa mapema kunaweza kusababisha TB sugu (drug-resistant TB) ambayo ni ngumu na gharama kubwa kutibu.

5. Je, TB na HIV vina uhusiano gani?

HIV hupunguza kinga ya mwili na kuongeza hatari ya mtu kupata TB au TB kuwa kali zaidi.

6. Je, mtu mwenye TB anaweza kuishi na familia bila kuwaambukiza?

Ndiyo, baada ya kuanza matibabu sahihi na kufuata ushauri wa daktari, hatari ya maambukizi hupungua sana.

7. Je, TB huathiri uwezo wa kupata watoto?

TB ya mfumo wa uzazi inaweza kuathiri uzazi endapo haitatibiwa mapema.

8. Je, TB ya mitoki ni hatari kama TB ya mapafu?

Ndiyo, ni hatari na inahitaji matibabu kamili sawa na TB ya mapafu.

9. Je, vipimo vya TB ni vipi vinavyopendekezwa kwa sasa?

GeneXpert, X-ray ya kifua, na vipimo vya maabara hutumika kulingana na dalili za mgonjwa.

10. Nifanye nini nikihisi dalili za TB?

Fika kituo cha afya haraka kwa uchunguzi. Usijitibu mwenyewe.


ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

Imeandikwa,

21 Januari 2026, 09:29:36

Rejea za mada hii

  1. World Health Organization. Tuberculosis fact sheet. WHO; 2023.

  2. Ministry of Health Tanzania. National Tuberculosis and Leprosy Guidelines. MoH; 2022.

  3. CDC. Tuberculosis (TB): Symptoms and Diagnosis. Centers for Disease Control and Prevention; 2023.

  4. Zumla A, et al. Tuberculosis. N Engl J Med. 2013;368(8):745–55.

  5. Lawn SD, Churchyard G. Epidemiology of HIV-associated tuberculosis. Curr Opin HIV AIDS. 2009;4(4):325–33.

bottom of page