Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Benjamin L, MD
Imeboreshwa:
12 Agosti 2025, 06:30:32

Dawa ya kuwashwa ukeni
Kuwashwa ukeni ni moja ya malalamiko ya mara kwa mara kwa wanawake wa rika zote. Hali hii inaweza kuwa ya muda mfupi au kudumu, na mara nyingi huambatana na maumivu, uchafu ukeni, au harufu isiyo ya kawaida. Ingawa wengi hujaribu kujitibu nyumbani, kutumia dawa bila kufahamu chanzo sahihi cha tatizo kunaweza kusababisha matatizo makubwa zaidi kama maambukizi ya muda mrefu au kupoteza uwezo wa kuzaa.
Makala hii inaeleza kwa kina kuhusu chanzo cha kuwashwa ukeni, dawa zinazotumika kutibu, na hatua za kujikinga na hali hii.
Visababishi vya kuwashwa ukeni
Kuwashwa ukeni kunaweza kusababishwa na moja au zaidi ya sababu zifuatazo;
Chanzo | Maelezo Mafupi |
Fangasi (Kandidiasis) | Huambatana na uchafu mweupe mzito kama jibini, kuwashwa sana, na wekundu ukeni. Husababishwa na fangasi wa Kandida albikani. |
Bakteria (Vajinosisi ya bakteria) | Huambatana na uchafu mweupe au kijivu, harufu ya samaki, na kuwashwa. |
Magonjwa ya zinaa | Kama Trikomoniasis, Herpes ya sehemu za siri, Klamidia au Gonorea — husababisha kuwashwa, vidonda, au uchafu wa njano/kijani. |
Mzio (Mwitikio kwenye vichochea mzio) | Kutokana na sabuni, poda, barakoa, kondomu au nguo za ndani — husababisha muwasho na wekundu. |
Ukavu wa uke (Kusinyaa kwa uke) | Huonekana hasa baada ya kukoma hedhi — ukavu huleta muwasho na maumivu wakati wa tendo la ndoa. |
Dawa ya kuwashwa ukeni kulingana na chanzo
1. Dawa za fangasi (Kandidiasis)
Krimu za kupaka ukeni:
Clotrimazole
Miconazole
Vidonge vya antifungus:
Fluconazole (ya kumeza)
Muda wa matibabu: Siku 1–7 kulingana na dawa
Tahadhari: Tumia dawa hizi baada ya kipimo au ushauri wa daktari ili kuhakikisha tatizo ni fangasi.
2. Dawa za maambukizi ya bakteria (Vajinosisi ya bakteria)
Antibiotic ya kumeza au kupaka ukeni:
Metronidazole
Krimu ya Clindamycin
Tahadhari: Epuka kunywa pombe wakati wa kutumia metronidazole.
3. Dawa za magonjwa ya zinaa
Trikomoniasis:
Metronidazole au Tinidazole
Klamidia:
Doxycycline au Azithromycin
Herpes ya shemu za siri
Acyclovir au Valacyclovir
Muhimu:
Fanya kipimo cha magonjwa ya zinaa kabla ya matibabu
Tibu pia mwenza wa ndoa
Epuka kujamiiana hadi matibabu yawe yamekamilika
4. Dawa za mzio au ukavu wa uke
Kundi la antihistamine:
Loratadine, Cetirizine (kwa muwasho wa mzio)
Krimu ya Estrogen (kwa ukavu baada ya hedhi):
Kirumu ya uke ya Estriol
Hatua zingine:
Epuka sabuni zenye harufu
Vaa chupi za pamba
Tumia maji pekee kusafisha uke
Je, ni lini uonane na daktari haraka?
Tafadhali nenda hospitali haraka ikiwa:
Kuwashwa kunaambatana na uchafu usio wa kawaida
Kuna harufu kali ukeni
Una vidonda au malengelenge
Una homa au maumivu ya tumbo la chini
Unajihisi kuchoka sana au una maumivu wakati wa kujamiiana
Jinsi ya kujikinga na kuwashwa ukeni
Tumia sabuni isiyo na kemikali kali
Badilisha chupi kila siku na tumia zile za pamba
Kausha uke vizuri baada ya kuoga
Epuka kutumia dawa au krimu za kupaka bila ushauri wa daktari
Tumia kondomu unapofanya ngono na mwenza mpya
Fanya uchunguzi wa mara kwa mara wa afya ya uke na magonjwa ya zinaa
Hitimisho
Kuwashwa ukeni si hali ya kawaida inayoepuika. Ingawa dawa za kupunguza muwasho zipo, tiba sahihi hutegemea chanzo halisi cha tatizo. Kujitibu bila kipimo kunaweza kuharibu mazingira ya uke au kuzidisha tatizo. Ni muhimu kuonana na mtaalamu wa afya kwa uchunguzi na ushauri wa matibabu unaofaa.
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
Imeandikwa,
11 Julai 2025, 10:11:06
Rejea za mada hii
Workowski KA, Bachmann LH, Chan PA, et al. Sexually transmitted infections treatment guidelines, 2021. MMWR Recomm Rep. 2021;70(4):1–187.
Sobel JD. Vulvovaginal candidosis. Lancet. 2007;369(9577):1961–71.
Bradshaw CS, Sobel JD. Current treatment of bacterial vaginosis: limitations and need for innovation. J Infect Dis. 2016;214(Suppl 1):S14–20.
Nyirjesy P. Management of women with chronic recurrent vulvovaginitis. Curr Infect Dis Rep. 2001;3(6):546–52.
Marrazzo JM, Martin DH. Management of women with cervicitis. Clin Infect Dis. 2007;44(Suppl 3):S102–10.
ACOG Practice Bulletin No. 215: Vaginitis in Nonpregnant Patients. Obstet Gynecol. 2020;135(1):e1–17.
Centers for Disease Control and Prevention (CDC). Trichomoniasis – CDC Fact Sheet. 2021.
Donders GGG, Bellen G, Rezeberga D. Aerobic vaginitis in pregnancy. BJOG. 2011;118(10):1163–70.
Cribby S, Taylor M, Reid G. Vaginal microbiota and the use of probiotics. Interdiscip Perspect Infect Dis. 2008;2008:256490.
Fischer G, Bradford J, Esser M. Vulvar disease in prepubertal girls: a clinical review. J Paediatr Child Health. 2004;40(11):660–5.
