top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Mangwella S, B, MD

1 Juni 2025, 09:42:34

Dawa ya UTI inayoweza kuniponya

Dawa ya UTI inayoweza kuniponya

Swali la msingi


Habari daktari, nina swali, Je ni dawa gani ya UTI inayoweza kuniponya kabisa?


Majibu

Mara kwa mara, wagonjwa huuliza: "Daktari, ni dawa gani ya UTI inanifaa?" Ingawa swali hili linaonekana rahisi, jibu lake si la moja kwa moja. Hii ni kwa sababu maambukizi katika njia ya mkojo (Urinary Tract Infection UTI) yanaweza kusababishwa na bakteria mbalimbali, yanaweza kuwa katika sehemu tofauti za njia ya mkojo, na wagonjwa huonyesha mwitikio tofauti kwa dawa kulingana na hali ya afya na usugu wa bakteria.


UTI ni nini?

UTI ni maambukizi yanayotokea katika sehemu yoyote ya mfumo wa mkojo, ikiwemo kibofu cha mkojo, urethra, ureters au figo. Mara nyingi, bakteria waitwao Escherichia coli (E. coli) ndio chanzo kikuu, lakini si kila wakati.


Aina za UTI

  1. Maambukizi ya mfumo wa chini wa mkojo – kwenye kibofu (cystitis) au urethra.

  2. Maambukizi ya juu wa mkojo– kwenye figo, ambayo huwa makali zaidi na huhitaji matibabu ya haraka.


Kwa nini ni vigumu kutaja moja kwa moja dawa ya UTI bila vipimo?


Maambukizi ya njia ya mkojo (UTI) ni tatizo linaloathiri watu wengi, lakini utofauti wa visababishi na hali ya kiafya ya mgonjwa hufanya matibabu yake yawe ya kipekee kwa kila mtu. Hii ndiyo sababu kuu kwa nini si sahihi kuorodhesha dawa moja kwa moja kwa kila mgonjwa wa UTI.


1. Aina Tofauti za Bakteria

UTI husababishwa na bakteria mbalimbali kama Escherichia coli, Klebsiella, au Proteus. Aina ya bakteria wanaosababisha maambukizi hutofautiana kulingana na mazingira ya mgonjwa, jinsia, umri, na hali yake ya kiafya. Mfano, mwanamke mwenye afya njema anaweza kuwa na bakteria wa kawaida, lakini mtu mwenye kisukari, anayefanyiwa hemodialysis au aliye na kinga dhaifu anaweza kuwa na bakteria waliokomaa na sugu.


2. Usugu wa bkteria kwa dawa

Matumizi holela ya antibiotiki yamechangia kuibuka kwa vimelea waliokomaa na sugu. Wagonjwa wengi hununua dawa bila vipimo wala ushauri, hali inayosababisha bakteria kuendelea kuishi hata baada ya matibabu. Hii husababisha UTI kurudia mara kwa mara, na kufanya tiba kuwa ngumu zaidi.


3. Hitaji la vipimo maalum

Daktari anaweza kupendekeza kipimo cha “kuotesha vimelea” kwenye mkojo (urine culture) pamoja na kuchunguza mwitikio wa bakteria kwenye dawa mbalimbali (sensitivity test). Vipimo hivi hutambua kwa uhakika aina ya bakteria na dawa inayoweza kumuua. Bila vipimo hivi, matibabu hufanyika kwa kubahatisha (empirical treatment), ambavyo si salama kila mara.


4. Historia ya matumizi ya dawa kwa mgonjwa

Ikiwa mgonjwa amewahi kutumia dawa za UTI mara kadhaa, hasa bila kumaliza dozi au bila ushauri wa daktari, kuna hatari kubwa kwamba bakteria waliopo wamejenga kinga dhidi ya dawa nyingi. Hali hii huathiri uchaguzi wa dawa sahihi na hutaka daktari afahamu historia hiyo ili kuepuka kushindwa kwa tiba.


5. Hali maalum za kiafya za mgonjwa

Kuna hali zinazohitaji uangalizi maalum kabla ya kuamua dawa ya UTI. Kwa mfano, wanawake wajawazito hawaruhusiwi kutumia baadhi ya dawa kama ciprofloxacin kutokana na madhara kwa mimba. Vivyo hivyo, wagonjwa wenye kisukari au kinga dhaifu huhitaji matibabu ya tahadhari na ya muda mrefu, kwani maambukizi yao huwa na kasi ya kuenea hadi figo au damu.


Kwa nini hatupaswi kutumia dawa ya UTI pasipo vipimo?

Kuna ongezeko kubwa la usugu wa bakteria dhidi ya antibiotiki, hasa kwa sababu watu hutumia dawa kiholela, bila kupima mkojo wala kushauriwa na daktari. Hali hii huongeza ugumu wa matibabu, gharama, na madhara. Dawa ambazo zamani zilikuwa bora kama ciprofloxacin, trimethoprim au amoxicillin, sasa mara nyingine hazifanyi kazi tena kwa sababu bakteria wamezoea dawa hizo.


Dalili za UTI

  • Maumivu au kuchoma wakati wa kukojoa

  • Mkojo kuwa na harufu mbaya au rangi isiyo ya kawaida

  • Kuwashwa sehemu za siri

  • Kuhisi kukojoa kila mara

  • Maumivu ya chini ya tumbo au kiuno

  • Homa (kwa maambukizi ya juu ya figo)


Je, nini cha kufanya ukihisi una UTI?

  1. Fanya vipimo vya mkojo (Uchambuzi wa mkojo na kuotesha vimelea kwenye mkojo)

  2. Mtembelee daktari kwa uchunguzi

  3. Epuka kujitibu mwenyewe kwa dawa

  4. Kunywa maji mengi kusaidia kusafisha njia ya mkojo

  5. Tumia dawa kwa muda wote uliopangiwa hata kama dalili zitaisha mapema

  6. Usizuie mkojo kwa muda mrefu.

  7. Jisafishe vizuri, hasa wanawake, kuanzia mbele hadi nyuma.

  8. Usitumie sabuni zenye kemikali nyingi sehemu za siri.

  9. Wakati mwingine, maambukizi haya huambukizwa kwa ngono, ni muhimu kuzingatia afya ya mwenza pia.


Dawa zinazotumika kutibu UTI (kwa ujumla, bila ushauri wa moja kwa moja)

Dawa hizi huweza kusaidia kwa UTI zisizo kali, lakini hutolewa kwa ushauri wa daktari baada ya uchunguzi:

  • Nitrofurantoin – kwa maambukizi ya chini ya kibofu, hasa kwa wanawake.

  • Trimethoprim-sulfamethoxazole (Co-trimoxazole) – mara nyingi hutumika, lakini kuna usugu mkubwa.

  • Fosfomycin trometamol – dozi moja tu, mara moja, hufaa kwa maambukizi ya kawaida.

  • Ciprofloxacin – dawa ya kundi la fluoroquinolones, lakini haipendekezwi kutumiwa kiholela kwa sababu ya usugu wa vimelea kwenye dawa hii.

  • Cefixime au cephalexin – dawa za kundi la cephalosporins, hutumika kwa baadhi ya maambukizi.

Angalizo: Usitumie dawa yoyote bila vipimo, hasa kwa sababu usugu kwa dawa umetamalaki sana. Kunywa dawa bila mpangilio kunaweza kusababisha UTI ya mara kwa mara au maambukizi sugu.

Hitimisho

Swali la “ni dawa gani ya UTI?” halina jibu moja kwa moja bila uchunguzi wa kina. Dawa bora ni ile inayolengwa kulingana na aina ya bakteria waliogunduliwa kwenye kipimo cha mkojo na historia ya mgonjwa. Usugu wa dawa ni changamoto kubwa, hivyo ni muhimu kuepuka matumizi ya antibiotiki bila ushauri wa daktari. Kumbuka, afya yako ni bora zaidi ukiwa na taarifa sahihi na huduma sahihi za kitabibu.

ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

Imeboreshwa,

1 Juni 2025, 09:45:18

Rejea za mada hii

  1. Gupta K, Hooton TM, Naber KG, et al. International clinical practice guidelines for the treatment of acute uncomplicated cystitis and pyelonephritis in women: A 2010 update. Clin Infect Dis. 2011;52(5):e103-e120. doi:10.1093/cid/ciq257

  2. Flores-Mireles AL, Walker JN, Caparon M, Hultgren SJ. Urinary tract infections: epidemiology, mechanisms of infection and treatment options. Nat Rev Microbiol. 2015;13(5):269–284. doi:10.1038/nrmicro3432

  3. World Health Organization. Antimicrobial resistance: global report on surveillance. Geneva: WHO; 2014.

  4. Nicolle LE. Uncomplicated urinary tract infection in adults including uncomplicated pyelonephritis. Urol Clin North Am. 2008;35(1):1–12. doi:10.1016/j.ucl.2007.09.004

  5. Medina M, Castillo-Pino E. An introduction to the epidemiology and burden of urinary tract infections. Ther Adv Urol. 2019;11:1756287219832172. doi:10.1177/1756287219832172

  6. Foxman B. Epidemiology of urinary tract infections: incidence, morbidity, and economic costs. Am J Med. 2002;113 Suppl 1A:5S–13S. doi:10.1016/S0002-9343(02)01054-9

  7. Wagenlehner FM, Bartoletti R, Cek M, et al. Antibiotic resistance in uropathogens: a global perspective. Eur Urol Focus. 2020;6(1):6–20. doi:10.1016/j.euf.2019.07.009

  8. Flores-Mireles AL, Walker JN, Caparon M, Hultgren SJ. Urinary tract infections: epidemiology, mechanisms of infection and treatment options. Nat Rev Microbiol. 2015;13(5):269–284. doi:10.1038/nrmicro3432

  9. Gupta K, Bhadelia N. Management of urinary tract infections from multidrug-resistant organisms. Infect Dis Clin North Am. 2014;28(1):49–59. doi:10.1016/j.idc.2013.09.004

  10. Ventola CL. The antibiotic resistance crisis: part 1: causes and threats. P T. 2015;40(4):277–283. PMID: 25859123

bottom of page