top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

ULY CLINIC

25 Aprili 2025, 06:32:10

Je, choo cha njano chenye kamasi husababishwa na nini?

Je, choo cha njano chenye kamasi husababishwa na nini?

Swali la msingi


Habari daktkari, napata choo cha njano chenye utelezi kikiambata na tumbo kuuma, siharishi, choo kipo kawaida na muda mwingine tumbo likiuma nikienda kujisaidia zinatoka kamasi tu kidogo. Mimi ni mwanamke, sina homa, wala kichefuchefu, dalili zimeanza jana(zina siku 2), shida inakua ni nini?


Majibu

Asante kwa maelezo yako ya kina. Kwa mujibu wa dalili ulizotaja:

  • Choo cha njano chenye utelezi

  • Tumbo kuuma

  • Wakati mwingine choo hakitoki isipokuwa kamasi kidogo

  • Hauharishi

  • Hakuna homa wala kichefuchefu


Visababishi vya magonjwa

Dalili hizi zinaweza kuashiria hali na magonjwa kadhaa, lakini sababu zinazowezekana zaidi ni pamoja na;


1. Maambukizi kwenye matumbo (bakteria au virusi)

Kamasi kwenye choo huashiria uwepo wa michomokinga kutokana na maambukizi ya bakteria au virusi. Maambukizi haya si lazima yaambatane na homa kila wakati. Maumivu ya tumbo na choo cha njano pia ni kawaida katika hali hii.


2. Amebiasis

Inasababisha maumivu ya tumbo (hasa ya chini kushoto), choo chenye kamasi au hata damu, na wakati mwingine kutojisaidia ipasavyo. Homa huweza kosekana, hasa mwanzoni. Maambukizi haya ni kawaida kutokea kwenye maeneo yenye usafi wa maji usio wa kuridhisha.


3. Muwasho wa matumbo

Husababisha maumivu ya tumbo yanayopungua baada ya kujisaidia, choo kinaweza kuwa na ute au kamasi na mara nyingine mtu huhisi haja lakini choo hakitoki au kinakuwa kidogo tu.


4. Maambukizi ya bakteria kama Shigella au Campylobacter

Ingawa mara nyingi huambatana na homa, hali si ya lazima. Huweza kusababisha maumivu ya tumbo makali, kamasi kwenye choo, au choo kilicho na utelezi.


Visababishi vya kawaida

Hali za kawaida tu zinaweza kusababisha dalili kama hizo bila kuwa na ugonjwa mkubwa. Hapa kuna baadhi ya sababu zisizo za hatari zinazoweza kueleza hali yako:


1. Mvurugiko wa tumbo (Kuvimbiwa)

Unaweza kupata maumivu ya tumbo, gesi, choo kuwa tofauti (kama chepesi au chenye ute). Huja mara baada ya kula chakula kisichoendana na tumbo lako (kama mafuta mengi, vyakula vibichi, au vyenye sukari nyingi).


2. Msongo wa mawazo au wasiwasi

Mfumo wa mmeng’enyo wa chakula unaathiriwa sana na akili. Msongo wa mawazo au hofu huweza kuleta maumivu ya tumbo na mabadiliko ya choo. Hali hii hufanana na ugonjwa wa muwasho wa matumbo


3. Mabadiliko ya mlo au ratiba ya kula

Ukibadilisha chakula ghafla au kula vyakula tofauti (kama vyenye viungo kwa wingi au vilivyohifadhiwa muda mrefu), tumbo linaweza kupatwa na mshtuko wa muda.


4. Kula chakula kilichoharibika kidogo

Hata bila kuumwa sana au kupata homa, chakula kilichoanza kuharibika huweza kuchokoza utumbo na kuleta dalili za muda mfupi.


Nini cha kufanya?

  • Kunywa maji mengi (hasa ikiwa choo kina utelezi au umetoka zaidi ya mara moja).

  • Epuka vyakula vya mafuta, vya viwandani, na vyenye pilipili kwa sasa.

  • Kama dalili zitaendelea zaidi ya siku 2–3, au

  • Maumivu yatazidi, au

  • Choo kitatoka na damu, au

  • Unapata homa

Ni vyema uende kituo cha afya kwa uchunguzi zaidi, ikiwemo kipimo cha choo kuangalia kama kuna vimelea (protozoa, bakteria, nk.).

ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

Imeboreshwa,

25 Aprili 2025, 07:20:55

Rejea za mada hii

  1. Guerrant RL, Walker DH, Weller PF. Tropical Infectious Diseases: Principles, Pathogens and Practice. 3rd ed. Philadelphia: Saunders; 2011.

  2. DuPont HL. Acute infectious diarrhea in immunocompetent adults. N Engl J Med. 2014;370(16):1532–40. doi:10.1056/NEJMra1301069

  3. Longstreth GF, Thompson WG, Chey WD, Houghton LA, Mearin F, Spiller RC. Functional bowel disorders. Gastroenterology. 2006;130(5):1480–91. doi:10.1053/j.gastro.2005.11.061

  4. Collins SM. A role for the gut microbiota in IBS. Nat Rev Gastroenterol Hepatol. 2014;11(8):497–505. doi:10.1038/nrgastro.2014.40

  5. Schiller LR. Diarrhea and malabsorption. In: Feldman M, Friedman LS, Brandt LJ, editors. Sleisenger and Fordtran's Gastrointestinal and Liver Disease. 10th ed. Philadelphia: Elsevier Saunders; 2016. p. 203–27.

bottom of page