top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Mangwella S, MD

Imeboreshwa:

20 Juni 2025, 10:00:41

Je, ikiwa mtu mwenye VVU atakurushia mate kwenye jeraha, unaweza kuambukizwa UKIMWI?

Je, ikiwa mtu mwenye VVU atakurushia mate kwenye jeraha, unaweza kuambukizwa UKIMWI?

Maelezo ya msingi


Katika jamii zetu, kuna hofu kubwa kuhusu namna ambavyo Virusi vya UKIMWI (VVU) vinaweza kuambukiza. Swali linaloulizwa mara kwa mara ni: Je, ikiwa mtu mwenye VVU atakurushia mate kwenye jeraha, unaweza kuambukizwa UKIMWI? Hili ni swali la msingi, hasa kwa watu wanaohusiana karibu na watu wanaoishi na VVU. Makala hii ya ULY Clinic inalenga kueleza ukweli wa kitaalamu kuhusu suala hili.


Uwezekano wa maambukizi ya VVU kupitia mate

Kwa ujumla, mate hayachukuliwi kuwa njia kuu ya maambukizi ya VVU. Tafiti za kisayansi na miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) zimeonyesha kuwa mate yana kiwango kidogo sana cha virusi vya VVU kiasi kwamba haviwezi kusababisha maambukizi katika hali ya kawaida. Pia mate yana kemikali maalumu za kinga (antibodies navimeng'enya) vinavyosaidia kuua virusi hivyo.


Hii ina maana kuwa, hata kama mtu mwenye VVU atakurushia mate kwenye jeraha dogo, uwezekano wa kuambukizwa ni mdogo sana hadi kufikia karibu sifuri.


Hali zinazoongeza hatari ya maambukizi ya VVU kwa mate

Ingawa mate peke yake si hatari, kuna hali maalumu ambapo hatari ya maambukizi inaweza huongezeka ambazo ni;

  1. Kama mate yana damu kutoka kwa mtu mwenye VVU – hasa ikiwa ana vidonda au fizi zinazovuja damu.

  2. Jeraha lako ni kubwa na lina damu inayoonekana – yaani si jeraha dogo tu la juu juu.

  3. Kama kuna kiasi kikubwa cha virusi kwenye damu ya yule aliye na VVU (yaani ana mzigo mkubwa wa virusi ).

Katika mazingira hayo, VVU vinaweza kupenya mwilini kupitia jeraha kubwa, ingawa bado hali hii ni nadra sana kutokea.


Nini cha kufanya ukikumbwa na hali hii?

Iwapo umepatwa na hali kama hii na una hofu ya kuambukizwa, fuata hatua hizi:

  1. Osha jeraha kwa maji safi ya uvuguvugu na sabuni haraka iwezekanavyo.

  2. Usibane jeraha wala kulifunika bila kusafisha.

  3. Fika kituo cha afya mapema – ndani ya saa 72 – kupewa ushauri kuhusu kutumia dawa za kuzuia maambukizi (PEP – Kinga baada ya kujianika) kama kuna hatari ya kweli.

  4. Pima VVU baada ya siku 28 hadi 90 ili kupata majibu ya uhakika kama kulikuwa na maambukizi.


Hitimisho

Katika hali ya kawaida, mate ya mtu mwenye VVU hayawezi kusababisha maambukizi ya UKIMWI hata kama yakiingia kwenye jeraha dogo. Lakini endapo mate hayo yana damu na jeraha ni kubwa, basi ni busara kuchukua tahadhari kwa kufika kituo cha afya kwa ushauri na kupima.

ULY Clinic inaendelea kukuelimisha kwa lugha nyepesi na yenye uhalisia wa maisha ya kila siku – kwa afya bora ya jamii

ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

Imeandikwa,

20 Juni 2025, 09:11:11

Rejea za mada hii

  1. World Health Organization. HIV transmission through exposure to bodily fluids. Geneva: WHO; 2021.

  2. Centers for Disease Control and Prevention (CDC). HIV Transmission. Atlanta, GA: CDC; 2022.

  3. Fiebig EW, Wright DJ, Rawal BD, et al. Dynamics of HIV viremia and antibody seroconversion in plasma donors. J Infect Dis. 2003;188(2):219-229.

  4. Henderson DK. Management of needlestick injuries: a house officer who has a needlestick. JAMA. 2001;286(7):863-871.

  5. UNAIDS. HIV and AIDS transmission myths and facts. UNAIDS Fact Sheet; 2020.

bottom of page