Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
ULY CLINIC
18 Juni 2025, 05:50:25

Je, mimba bado ipo kweli baada ya kuitoa kwa dawa na kutoka damu nyingi na matumizi ya antibiotics?
Swali la msingi
Habari za leo daktari, Je, mwanamke akitoa mimba damu ikatoka nyingi kupita kiasi then anapima tena inaonyesha ana mimba na pia alitumi antibiotics inaweza ikawa kweli mimba bado ipo?
Majibu
Ndiyo, inawezekana mimba bado ipo, hata kama mwanamke alitoa mimba na akapata damu nyingi baada ya hapo. Hii hutokea katika hali kama zifuatazo:
1. Mimba haikutoka yote
Damu nyingi inaweza kuwa sehemu ya mimba imetoka, lakini sehemu nyingine imebaki kwenye mji wa mimba.
Kipimo cha ujauzito kitaendelea kuonyesha kuwa ni mjamzito kwa sababu homoni ya mimba (β-hCG) bado ipo mwilini.
Hali hii ni hatari na inaweza kuleta maambukizi au kuvuja damu nyingi zaidi.
2. Mimba mpya baada ya ile ya awali
Iwapo mimba ya kwanza ilitoka kabisa, lakini tendo la ndoa lilifanyika bila kinga baada ya hapo, huenda mimba mpya imeanza. Hii hutokea kwa nadra sana kwa muda mfupi hivyo, lakini siyo jambo la kushangaza kabisa.
3. Homoni za mimba bado zipo mwilini
Kipimo cha mimba kinaweza kuonyesha mimba hata wiki 3–4 baada ya kutoa mimba, kwa sababu homoni ya hCG huisha taratibu kwenye damu. Hii siyo dalili ya mimba mpya wala kwamba mimba bado ipo—ni homoni tu iliyosalia.
Je, antibiotiki zinaathiri kipimo cha mimba?
Hapana. Antibiotiki hazibadilishi matokeo ya kipimo cha mimba. Matokeo ya kipimo bado ni sahihi hata kama mtu anatumia dawa.
Wakati gani wa kuonana na daktari haraka?
Ni muhimu kumwona daktari haraka endapo baada ya kutoa mimba au kuwa na dalili za ujauzito unakumbwa na mojawapo ya dalili zifuatazo:
Kutokwa na damu nyingi isiyoisha – ikiwa unabadili pedi kila baada ya saa moja au chini ya hapo kwa zaidi ya masaa 2 mfululizo.
Maumivu makali ya tumbo au nyonga – hasa yanayoendelea bila kupungua au yanayoongezeka.
Kichefuchefu kikali na kutapika kila kitu – hata maji, pamoja na kukosa hamu ya kula.
Dalili za homa – joto la mwili kupanda zaidi ya nyuzi joto 38°C, kutetemeka, kuchoka sana au kuhisi baridi kupita kiasi.
Kutokwa na usaha au harufu mbaya sehemu za siri – inaweza kuashiria maambukizi kwenye kizazi.
Dalili za mshtuko – kama vile mapigo ya moyo kwenda haraka, kushindwa kupumua vizuri, kizunguzungu au kuzimia.
Ikiwa baada ya kutoa mimba bado unapima na kuonekana una ujauzito – kuna uwezekano mimba haijatoka yote au kuna tatizo lingine la kiafya linalohitaji ufuatiliaji wa kitaalamu.
Utegemee nini ukifika hospitali?
Ukifika hospitali baada ya kutoa mimba na bado unapima una ujauzito, au unapata dalili hatarishi kama kutokwa damu nyingi, maumivu makali au homa, unaweza kutegemea huduma zifuatazo:
1. Uchunguzi wa awali wa mwili
Daktari atauliza historia ya afya yako, lini ulitoa mimba, ulitumia dawa gani, na kama una dalili kama kutokwa damu, maumivu au kichefuchefu.
Atafanya uchunguzi wa mwili na uchunguzi wa nyonga na sehemu za siri ili kutathmini hali ya kizazi na uke.
2. Vipimo vya kitabibu
Ultrasound ya fumbatio au ya uke: Kuangalia kama bado kuna mabaki ya mimba au mimba bado ipo.
Kipimo cha Beta-hCG (homoni ya ujauzito): Ili kuchunguza kama ujauzito unaendelea au unaisha.
Picha kamili ya damu (FBC): Kuangalia kiwango cha damu na kama kuna dalili za maambukizi.
Vipimo vya mkojo au damu vingine kulingana na dalili.
3. Matibabu kulingana na tatizo
Dawa ya kusafisha kizazi (misoprostol): Ikiwa mabaki bado yapo.
Antibiotiki: Ikiwa kuna dalili za maambukizi ya kizazi.
Kusafishwa kizazi kwa njia ya upasuaji mdogo: Kama damu nyingi na mabaki yapo.
Damu kuongezewa: Ikiwa umepoteza damu nyingi.
4. Ushauri na ufuatiliaji
Daktari atakushauri kuhusu afya ya uzazi kwa ujumla.
Utapewa ushauri kuhusu njia salama za kupanga uzazi baada ya afya yako kuimarika.
Utapangiwa tarehe ya kurudi kwa ufuatiliaji wa vipimo au hali yako.
Ushauri kwa muuliza swali
Fanya kipimo cha ultrasound (US) ya via ndani ya nyonga ili kujua kama kuna mabaki ya mimba.
Usitumie tena dawa za kutoa mimba bila usimamizi wa kitaalamu.
Onana na daktari
Hitimisho
Ndiyo, inawezekana mimba bado ipo au mabaki ya mimba yapo. Kipimo cha ujauzito kuwa chanya baada ya kutoa mimba si hakikisho la ujauzito mpya. Uchunguzi wa daktari ni muhimu kuthibitisha hali yako.
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
Imeboreshwa,
18 Juni 2025, 06:11:29
Rejea za mada hii
World Health Organization. Clinical practice handbook for safe abortion. Geneva: WHO; 2014.
American College of Obstetricians and Gynecologists. Early pregnancy loss: ACOG Practice Bulletin, Number 200. Obstet Gynecol. 2018;132(5):e197–e207.
Barnhart KT, Sammel MD, Rinaudo PF, Zhou L, Hummel AC, Guo W. Symptomatic patients with an early viable intrauterine pregnancy: hCG curves redefined. Obstet Gynecol. 2004;104(1):50–5.
Chen MJ, Creinin MD. Mifepristone with buccal misoprostol for medical abortion: A systematic review. Obstet Gynecol. 2015;126(1):12–21.
American Pregnancy Association. Incomplete miscarriage. [Internet]. 2020 [cited 2025 Jun 17]. Available from: https://americanpregnancy.org/
Schreiber CA, Creinin MD, Atrio J, Sonalkar S, Ratcliffe SJ, Barnhart KT. Mifepristone pretreatment for the medical management of early pregnancy loss. N Engl J Med. 2018;378(23):2161–70.
Wilcox AJ, Baird DD, Weinberg CR. Time of implantation of the conceptus and loss of pregnancy. N Engl J Med. 1999;340(23):1796–9.
Speroff L, Fritz MA. Clinical gynecologic endocrinology and infertility. 8th ed. Philadelphia: Lippincott Williams & Wilkins; 2010.