Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Mangwella SB, MD
Imeboreshwa:
18 Desemba 2025, 09:09:27

Je, Mwanamke mwenye PID Anaweza kumwambukiza Mwanaume?
Pelvic Inflammatory Disease (PID) ni tatizo la kiafya linalowaathiri wanawake, hasa mfumo wa juu wa uzazi (mfuko wa uzazi, mirija ya uzazi na ovari). Wagonjwa wengi hujiuliza swali muhimu: Je, mwanamke mwenye PID anaweza kumwambukiza mwanaume? Makala hii imeandaliwa kwa lugha rahisi na ya kitaalamu kwa ajili ya wagonjwa, ili kuelewa ukweli wa kitabibu, hatari zinazohusika, na nini cha kufanya ili kujikinga.
PID ni nini kwa ufupi?
PID ni maambukizi ya mfumo wa uzazi wa mwanamke yanayotokea pale bakteria wanapopanda kutoka uke na shingo ya kizazi kwenda juu. Mara nyingi husababishwa na maambukizi ya magonjwa ya zinaa, hasa bakteria Chlamydia trachomatis na Neisseria gonorrhoeae, ingawa bakteria wengine pia wanaweza kuhusika.
Je, PID yenyewe huambukizwa?
Hapana. PID kama ugonjwa haumuambukizi mwanaume moja kwa moja. Lakini, bakteria wanaosababisha PID (hasa wale wa magonjwa ya zinaa) wanaweza kuambukizwa kupitia tendo la ndoa.
Hii ina maana kuwa:
Mwanamke hana uwezo wa “kumpa mwanaume PID”,
Lakini anaweza kumpa mwanaume maambukizi ya zinaa ambayo yamesababisha PID kwake.
Ni maambukizi gani yanaweza kuambukizwa kutoka kwa mwanamke mwenye PID?
Ikiwa PID imesababishwa na maambukizi ya zinaa, mwanaume anaweza kuambukizwa:
Kisonono
Klamidia
Maambukizi mengine ya bakteria wanaoishi kwenye uke au shingo ya kizazi
Kwa mwanaume, maambukizi haya yanaweza kuathiri:
Mrija wa mkojo (Husababisha maambukizi kwenye mfumo wa mkojo kwa jina jingine UTI)
Korodani au mfuko wa mbegu (Husababisha epididimaitis)
Tezi dume (husababisha prostaittis)
Dalili kwa mwanaume aliyeambukizwa
Mwanaume aliyeambukizwa bakteria hawa anaweza:
Kuwa hana dalili kabisa
Kupata maumivu au kuchoma wakati wa kukojoa
Kutokwa na usaha au majimaji kwenye uume
Kuumwa korodani
Kupata matatizo ya uzazi endapo hatatibiwa mapema
Kwa nini tiba ya wenza wote ni muhimu?
Iwapo mwanamke anatibiwa PID lakini mwanaume wake hatibiwi:
Mwanamke anaweza kuambukizwa tena
Maambukizi yanaweza kuendelea kusambaa kimya kimya
Hatari ya utasa, mimba nje ya mfuko wa uzazi, na maumivu ya muda mrefu ya nyonga huongezeka
Ndiyo maana, kitabibu, wanandoa au wapenzi wote wanashauriwa kupima na kutibiwa pamoja.
Nini cha kufanya kama mmoja wenu ana PID?
Sitisha ngono hadi matibabu yakamilike kwa wote
Pima magonjwa ya zinaa kwa wenza wote
Fuata matibabu kikamilifu kama yalivyoelekezwa
Tumia kinga (kondomu) baada ya kuruhusiwa kuanza ngono
Fanya uchunguzi wa ufuatiliaji kuhakikisha maambukizi yameisha
Je, PID inaweza kuzuilika?
Ndiyo. Njia kuu ni:
Kujikinga dhidi ya magonjwa ya zinaa
Kupima mara kwa mara endapo una mwenza zaidi ya mmoja
Kutibu mapema maambukizi ya uke au shingo ya kizazi
Kuepuka ngono zembe bila kinga
Hitimisho
PID haimumbukizwi kwa mwanaume moja kwa moja, lakini bakteria wanaosababisha PID wanaweza kuambukizwa kupitia ngono. Hivyo, PID ni ishara ya hatari kwa wanandoa wote wawili. Elimu, uchunguzi wa mapema na matibabu ya pamoja ni msingi wa kuzuia madhara makubwa ya kiafya. ULY Clinic inaendelea kusisitiza: Afya ya uzazi ni jukumu la wote wawili.
Maswali yanayoulizwa Mara kwa Mara na majibu yake
1. Je, mwanaume anaweza kuwa na maambukizi bila dalili kabisa?
Ndiyo. Wanaume wengi walioambukizwa klamidia au kisonono hawana dalili, lakini bado wanaweza kuwa chanzo cha maambukizi kwa wenza wao.
2. Je, PID inaweza kutokea bila mwanamke kuwa na Magonjwa ya zinaa?
Ndiyo. PID inaweza kusababishwa pia na bakteria wa kawaida wa uke, hasa baada ya kuingizwa Kitanzi cha uzazi uzazi wa mpango, kujifungua, au kutoa mimba bila usafi wa kutosha.
3. Je, kondomu huzuia kabisa hatari ya PID?
Kondomu hupunguza sana hatari ya maambukizi ya zinaa, lakini sio kinga ya asilimia 100, hasa kama haitumiki kwa usahihi.
4. Mwanaume anapaswa kupimwa nini kama mwenza ana PID?
Kwa kawaida hupimwa kisonono, klamidia, VVU, kaswende, na wakati mwingine maambukizi mengine kulingana na historia ya hatari.
5. Je, PID inaweza kurudia baada ya matibabu?
Ndiyo, hasa kama maambukizi ya awali hayakutibiwa kikamilifu au kama aliambukizwa tena kutoka kwa mwenza ambaye hakutibiwa.
6. Je, PID huathiri uwezo wa mwanaume kupata mtoto?
Si moja kwa moja, lakini maambukizi yanayoambukizwa kutoka kwa mwanamke yanaweza kusababisha matatizo ya mbegu kwa mwanaume endapo hayatatibiwa mapema.
7. Ni muda gani wa kusubiri kabla ya kuanza tena ngono baada ya PID?
Kwa kawaida ni baada ya kukamilisha dozi zote za dawa na kuthibitishwa kuwa maambukizi yameisha kwa wenza wote.
8. Je, PID inaweza kuathiri ndoa au mahusiano?
Ndiyo, hasa kama hakuna mawasiliano ya wazi, uelewa wa pamoja, na ushirikiano katika tiba. Elimu sahihi hupunguza migogoro isiyo ya lazima.
9. Je, mwanamke anaweza kupata PID akiwa mjamzito?
Ni nadra, lakini inawezekana. Hali hii ni hatari na huhitaji uangalizi wa karibu wa kitabibu.
10. Je, PID ni sawa na maambukizi ya uke ya kawaida?
Hapana. Maambukizi ya uke huathiri sehemu ya chini, wakati PID huathiri mfumo wa uzazi wa juu na ina madhara makubwa zaidi kama haitatibiwa.
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
Imeandikwa,
18 Desemba 2025, 09:09:27
Rejea za mada hii
Brunham RC, Gottlieb SL, Paavonen J. Pelvic inflammatory disease. N Engl J Med. 2015;372(21):2039–48.
Ross J, Guaschino S, Cusini M, Jensen J. 2017 European guideline for the management of pelvic inflammatory disease. Int J STD AIDS. 2018;29(2):108–14.
Workowski KA, Bachmann LH, Chan PA, et al. Sexually transmitted infections treatment guidelines, 2021. MMWR Recomm Rep. 2021;70(4):1–187.
Haggerty CL, Taylor BD. Mycoplasma genitalium: an emerging cause of pelvic inflammatory disease. Infect Dis Obstet Gynecol. 2011;2011:959816.
World Health Organization. Guidelines for the management of sexually transmitted infections. Geneva: WHO; 2003.
