Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
ULY CLINIC
Imeboreshwa:
12 Julai 2025, 12:14:29

Je, ni kwa nini mtoto wa miezi 11 anajisaidia kinyesi cheusi?
Swali la msingi
“Habari Daktari, mimi natokea Tabora. Mtoto wangu ana miezi 11 na juzi niliona kinyesi chake kimetoka cheusi kabisa na chenye harufu kali sana. Hana homa wala kutapika, lakini mimi na mume wangu tumeingiwa na hofu kubwa. Je, hali hii ni ya kawaida au kuna tatizo kubwa linaendelea? Tafadhali tusaidie kuelewa.”
Majibu
Mabadiliko ya rangi ya kinyesi kwa mtoto yanaweza kuwa ya kawaida au kuashiria hali ya kiafya inayohitaji uangalizi wa haraka. Wazazi wengi huingiwa na hofu wanapoona mtoto wao anajisaidia kinyesi cheusi, hasa akiwa na umri kama wa miezi 11. Katika makala hii ya ULY Clinic, tutachambua sababu mbalimbali za kinyesi cheusi kwa mtoto, dalili zinazohitaji uangalizi wa haraka, na hatua unazoweza kuchukua kama mzazi.
Rangi ya kawaida ya kinyesi kwa mtoto wa miezi 11
Kwa kawaida, mtoto wa miezi 11 anayeanza kula vyakula vya kawaida pamoja na maziwa anaweza kuwa na kinyesi cha rangi ya hudhurungi, kijani hafifu au njano iliyochanganyika na kahawia. Rangi ya kinyesi inaweza kubadilika kulingana na aina ya chakula anachokula.
Visababishi vya kinyesi cheusi
Baadhi ya visababishi vya kinyesi cheusi kwa mtoto wa miezi 11 ni pamoja na;
1. Chakula au vinywaji alivyokula
Baadhi ya vyakula vinaweza kufanya kinyesi kuwa cheusi bila kuwa na tatizo la kiafya, kama:
Ndizi mbivu sana
Blueberries (zabibu za bluu)
Spinach au mboga za kijani kibichi nyingi(iliyokolea)
Vyakula vilivyo na rangi nyeusi kama biskuti za chocolate, uji wa dona
Mkaa wa dawa katika baadhi ya dawa za kukinga sumu
2. Madini chuma (Madini chuma ya nyongeza)
Watoto wanaopewa dawa au virutubisho vyenye madini chuma (iron) kwa ajili ya upungufu wa damu, mara nyingi hupata kinyesi cheusi au kijivu.
3. Damu katika mfumo wa juu ya mmeng’enyo wa chakula
Kinyesi cheusi chenye harufu kali sana kama ya kutu kinaweza kuashiria kuwa kuna damu inavuja kwenye tumbo au sehemu za juu ya tumbo. Hali kitiba huitwa melena.
Sababu za melena kwa mtoto zinaweza kuwa:
Vidonda vya tumbo
Kuwapo kwa maambukizi au uvimbe tumboni
Kumeza damu (kama mtoto aliumwa puani au mama mwenye chuchu zilizopasuka)
4. Kuwapo kwa maambukizi makali au fangasi
Maambukizi katika mfumo wa utumbo yanaweza kusababisha kinyesi kuwa na rangi isiyo ya kawaida ikiwa pamoja na kuwa cheusi, hasa kama yanaambatana na homa, kutapika au kuharisha.
Dalili zinazopaswa kukufanya kumpeleka mtoto hospitalini haraka
Kinyesi cheusi chenye harufu kali isiyo ya kawaida
Mtoto anatapika damu au kinyesi kinaonekana kama lami
Anaonekana dhaifu, mnyonge au kulala sana
Homa ya mara kwa mara au kupungua uzito
Hakula vizuri na amekuwa na choo kigumu sana au kuvimbiwa
Kinyesi cheusi kinaambatana na homa au ngozi kuwa ya njano
Vipimo vinavyoweza kufanyika hospitali
Picha kamili ya chembe kwenye damu (FBC) – kubaini kama kuna upungufu wa damu
Uchunguzi wa kinyesi – kuchunguza kama kuna damu au maambukizi
Kipimo cha damu iliyojificha kwenye kinyesi– kuangalia kama kuna damu kwenye kinyesi isiyoonekana kwa macho
Ultrasound ya tumbo – kutathmini hali ya ndani ya mfumo wa mmeng’enyo
Nifanye nini nyumbani kama mtoto anajisaidia kinyesi ceusi bila dalili nyingine?
Angalia aina ya chakula ulichompa – andika vyakula alivokula ndani ya siku 2–3 zilizopita
Angalia kama anatumia dawa au virutubishi vyenye madini chuma
Hakikisha mtoto anakunywa maji ya kutosha
Angalia kama anacheza, ana hamu ya kula, na analala vizuri
Kama hana dalili nyingine za hatari – mfuatilie kwa siku moja hadi mbili kabla ya kuamua kumuona daktari
Je, kinyesi cheusi ni tatizo la kudumu?
Hapana. Katika hali nyingi, kinyesi cheusi husababishwa na vyakula au dawa na hupita bila madhara. Lakini ikiwa inaambatana na dalili hatarishi, inahitaji uchunguzi wa haraka ili kuzuia madhara makubwa kwa afya ya mtoto.
Hitimisho
Kinyesi cheusi kwa mtoto wa miezi 11 si kila wakati ni ishara ya tatizo la kiafya. Inaweza kusababishwa na vyakula au virutubisho anavyotumia. Hata hivyo, ikiwa rangi hiyo inaambatana na dalili zingine za hatari kama kutapika damu, kuwa dhaifu au kinyesi kinachofanana na lami, ni muhimu sana kumpeleka mtoto hospitali kwa uchunguzi zaidi. Mama na baba, fahamu kuwa rangi ya kinyesi ni kiashiria kizuri cha afya ya mtoto wako – usipuuze mabadiliko yoyote makubwa.
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
Imeandikwa,
12 Julai 2025, 12:14:29
Rejea za mada hii
Walker WA, Durie PR. Pediatric gastrointestinal disease: pathophysiology, diagnosis, management. 6th ed. Shelton, CT: PMPH-USA; 2018.
Kliegman RM, St. Geme JW. Nelson Textbook of Pediatrics. 21st ed. Philadelphia: Elsevier; 2020.
World Health Organization. Pocket book of hospital care for children: guidelines for the management of common childhood illnesses. 2nd ed. Geneva: WHO; 2013.
Wyllie R, Hyams JS, Kay M. Pediatric gastrointestinal and liver disease. 6th ed. Philadelphia: Elsevier; 2021.
Bisset GS, Kirks DR. Gastrointestinal tract. In: Kirks' radiologic imaging of the gastrointestinal tract in infants and children. Philadelphia: Elsevier; 2015. p. 205–19.
Steiner MJ, DeWitt TG, Byerley JS. Is this child sick? Recognition of serious illness in children. Pediatr Clin North Am. 2019;66(5):831–45.
Lin CH, Lee HC, Lin CF, Hsu CH, Lee CL, Chang JH. Occult gastrointestinal bleeding in infants and children: a retrospective analysis. Pediatr Neonatol. 2017;58(3):250–6.
American Academy of Pediatrics. Iron supplementation for infants and children. Pediatrics. 2010;126(5):1040–50.
National Health Service (UK). Blood in your baby's stool. [Internet]. NHS; 2022 [cited 2025 Jul 12]. Available from: https://www.nhs.uk/conditions/blood-in-stool/
Mayo Clinic. Black or tarry stools: Causes and when to see a doctor. [Internet]. Mayo Foundation for Medical Education and Research; 2022 [cited 2025 Jul 12]. Available from: https://www.mayoclinic.org/symptoms/black-stools/basics/causes/sym-20050635
