Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Peter A, MD
Imeboreshwa:
19 Februari 2026, 07:47:43

Je, p2 ina madhara gani?
Postinor 2 (P2) ni dawa ya dharura ya kuzuia mimba isiyotakiwa baada ya kufanya tendo la ndoa bila kinga au endapo kinga imeshindikana (kondomu kupasuka, kusahau vidonge vya uzazi n.k).
Kwa ujumla, Postinor 2 ni dawa salama kwa wanawake wengi ikiwa itatumika kwa dozi sahihi na ndani ya muda uliopendekezwa (ndani ya saa 72 baada ya tendo la ndoa). Hata hivyo, kama ilivyo kwa dawa nyingine, inaweza kusababisha maudhi kwa baadhi ya watumiaji.
Maudhi ya Postinor 2 (P2)
Maudhi mengi ya P2 huwa ya muda mfupi na hutoweka yenyewe bila kuhitaji matibabu maalum. Maudhi hayo yanaweza kujumuisha:
1. Maudhi ya kawaida
Kichefuchefu
Kutapika
Maumivu ya kichwa
Kizunguzungu
Uchovu wa mwili
Kuharisha
2. Maumivu ya mwili
Maumivu ya tumbo (hasa sehemu ya chini ya tumbo)
Maumivu ya matiti
3. Mabadiliko ya mzunguko wa hedhi
Hedhi kuwa nzito kuliko kawaida
Hedhi kuwa nyepesi kuliko kawaida
Kuchelewa kwa hedhi
Kuona damu mapema kabla ya muda wa kawaida wa hedhi
Muhimu: Ikiwa hedhi yako itachelewa kwa zaidi ya siku 5, au ukiona dalili za ujauzito (kichefuchefu cha asubuhi, maumivu ya matiti yanayoendelea), fanya kipimo cha ujauzito au wasiliana na mtaalamu wa afya.
Wakati Gani Uwasiliane na Daktari Haraka?
Wasiliana na daktari au nenda kituo cha afya haraka iwapo utapata mojawapo ya dalili zifuatazo:
Maumivu makali ya tumbo la chini yanayoendelea
Dalili kali za mzio kama:
Ngozi kubadilika rangi au kupata melenge
Kuumwa na kuwasha mwili sana
Kuvimba midomo, uso au koo
Kutokwa na damu nyingi sana au isiyo ya kawaida
Kama una hofu au mashaka ya kuwa una ujauzito
Maswali yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu postinor 2 (P2)
1. Je, ukitumia P2 mara moja ina madhara gani?
Kwa kutumia P2 mara moja, madhara huwa madogo au hayapo kabisa kwa wanawake wengi. Unaweza kupata kichefuchefu, maumivu ya kichwa au mabadiliko madogo ya hedhi, lakini haya huwa ya muda mfupi na hupotea yenyewe.
2. Je, P2 inaweza kusababisha utasa?
Hapana. Hakuna ushahidi wa kisayansi unaothibitisha kuwa Postinor 2 husababisha utasa. Baada ya muda mfupi, mfumo wa uzazi hurudi katika hali yake ya kawaida.
3. Je, P2 inafanya kazi vipi kuzuia mimba?
P2 hufanya kazi kwa kuchelewesha au kuzuia yai kutoka kwenye ovari (uovuleshaji). Haitoi mimba iliyokwisha tungwa.
4. Je, P2 inaweza kutoa mimba?
Hapana. Postinor 2 si dawa ya kutoa mimba. Ikiwa mimba tayari imeshatungwa, P2 haitaiondoa wala kuiharibu.
5. Je, ninaweza kutumia P2 zaidi ya mara moja kwa mwezi?
Kitaalamu inawezekana, lakini haipendekezwi kuitumia mara kwa mara. Matumizi ya mara kwa mara huongeza maudhi na huvuruga mzunguko wa hedhi. Inashauriwa kutumia njia ya kudumu ya uzazi wa mpango.
6. Je, nikitapika baada ya kunywa P2 nifanye nini?
Ikiwa umetapika ndani ya saa 2 baada ya kunywa P2, unashauriwa kunywa dozi nyingine kwani dawa inaweza kuwa haijafanya kazi ipasavyo.
7. Je, P2 inalinda dhidi ya magonjwa ya zinaa?
Hapana. P2 hailindi dhidi ya magonjwa ya zinaa kama UKIMWI, kaswende au kisonono. Kondomu ndiyo njia bora ya kujikinga.
8. Je, ni lini P2 haifanyi kazi vizuri?
P2 hufanya kazi vizuri zaidi ikitumika mapema. Ufanisi hupungua kadri muda unavyoongezeka, hasa baada ya saa 72 tangu tendo la ndoa.
9. Je, P2 inaweza kuathiri uzito wa mwili?
Hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa P2 husababisha kuongezeka au kupungua kwa uzito. Mabadiliko ya muda mfupi yanaweza kutokana na mabadiliko ya homoni.
10. Je, nifanye nini baada ya kutumia P2?
Baada ya kutumia P2:
Fuata mzunguko wako wa hedhi
Tumia njia salama ya uzazi wa mpango kwa siku zijazo
Fanya kipimo cha ujauzito ikiwa hedhi itachelewa
Wasiliana na mtaalamu wa afya kama una wasiwasi wowote
11. Je, ni salama kutumia P2 mara mbili ndani ya siku moja au siku mbili mfululizo?
Ndiyo, ungeweza kutumia vidonge vya dharura (P2) mara ya pili ikiwa ulifanya tendo bila kinga tena ndani ya saa 24–48, lakini matumizi ya karibu karibu yanaweza kupunguza ufanisi wake na kusababisha mwili wako kupata madhara madogo kama kichefuchefu, kizunguzungu, maumivu ya tumbo, au mabadiliko ya hedhi.
P2 si hatari kwa afya kwa dozi hizo mbili, lakini si dawa ya kutumia mara kwa mara. Ni muhimu kutafuta njia ya uzazi wa mpango iliyo salama na ya kudumu zaidi, na pia usisite kumuona mtoa huduma ya afya ikiwa una wasiwasi au kama hedhi yako itachelewa zaidi ya wiki moja.
12. Je, kumeza P2 kwa siku mbili mfululizo kunaweza kuniletea madhara makubwa?
Kumeza P2 (kwa dharura) kwa siku mbili mfululizo kwa kawaida hakuletei madhara makubwa ya kudumu, lakini kunaweza kusababisha madhara ya muda kutokana na mabadiliko ya homoni. Madhara hayo yanaweza kujumuisha:
Kuchelewa au kutangulia kwa hedhi
Kichefuchefu
Kuumwa kichwa au tumbo
Kutokwa na damu kidogo isiyo ya kawaida
Kuchoka au kuhisi mwili kubadilika
P2 ni salama kwa matumizi ya dharura, lakini haitakiwi kutumiwa mara kwa mara au ndani ya siku kadhaa mfululizo kwa sababu haifanyi kazi vizuri ukitumia mara nyingi na inaweza kuleta mabadiliko makubwa ya hedhi.
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
Imeandikwa,
7 Novemba 2021, 09:02:45
Rejea za mada hii
Postinor. https://postinorpill.com/faq/#:~:text=Usually%20taking%20an%20POSTINOR%20pill,spotting%20until%20your%20next%20period. Imechukuliwa 07.11.2021
Edgren RA, et al. Nomenclature of the gonane progestins. Contraception. 1999 Dec;60(6):313.
Sitruk-Ware R: New progestagens for contraceptive use. Hum Reprod Update. 2006 Mar-Apr;12(2):169-78. Epub 2005 Nov 16.
Kahlenborn C, et al. Mechanism of action of levonorgestrel emergency contraception. Linacre Q. 2015 Feb;82(1):18-33. doi: 10.1179/2050854914Y.0000000026.
Kook K, et al. Pharmacokinetics of levonorgestrel 0.75 mg tablets. Contraception. 2002 Jul;66(1):73-6.
Sambol NC, etal. Pharmacokinetics of single-dose levonorgestrel in adolescents. Contraception. 2006 Aug;74(2):104-9. doi: 10.1016/j.contraception.2006.01.011. Epub 2006 Jun 16.
Natavio M, et al. Pharmacokinetics of the 1.5 mg levonorgestrel emergency contraceptive in women with normal, obese and extremely obese body mass index. Contraception. 2019 May;99(5):306-311. doi: 10.1016/j.contraception.2019.01.003. Epub 2019 Jan 28.
Shohel M, et al. A systematic review of effectiveness and safety of different regimens of levonorgestrel oral tablets for emergency contraception. BMC Womens Health. 2014 Apr 4;14:54. doi: 10.1186/1472-6874-14-54.
