top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Benjamin L, MD

Imeboreshwa:

10 Desemba 2025, 09:27:17

Kaswende isiyopona: Vipimo na Hatua Muhimu za Kuchukua

Kaswende isiyopona: Vipimo na Hatua Muhimu za Kuchukua

Kaswende  ni ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na bakteria Treponema pallidum. Mara nyingi ugonjwa huu hupata nafuu baada ya tiba sahihi, hasa penicillin. Hata hivyo, kuna baadhi ya watu ambao dalili zao huendelea au maambukizi hurudi licha ya kutumia matibabu. Hali hii huitwa kaswende isiyopona (kushindwa kwa matibabu) au kaswende inayoendelea (kaswende inayodumu), na ni suala linalohitaji uchunguzi wa kina.


Katika makala hii, tutajadili sababu, vipimo muhimu, na hatua za kuchukua pale kaswende inaposhindwa kupona.


Dalili za kaswende isiyopona zinazohitaji huduma ya dharura

  • Kupoteza uwezo wa kuona au kusikia

  • Maumivu makali ya kichwa

  • Ganzi au udhaifu wa viungo

  • Upele unaozidi kuenea

  • Maumivu makali ya nyonga au sehemu za siri

  • Homa ya mara kwa mara

  • Vidonda visivyopona


Visababishi vya kaswende isiyopona

Kuna sababu kadhaa zinazoweza kufanya mtu aendelee kuwa na dalili au vipimo kuendelea kuonyesha maambukizi baada ya matibabu:


1. Kutotumia dawa ipasavyo
  • Kutoshamaliza dozi

  • Kutozingatia muda sahihi wa sindano ya benzathine penicillin

  • Kukosa ufuatiliaji wa vipimo


2. Upinzani wa dawa (hutokea kwa nadra)

Ingawa T. pallidum mara nyingi haioti upinzani mkali kama bakteria wengine, kuna mazingira ambayo maambukizi hayaitikii tiba vizuri.


3. Kuambukizwa tena

Hili hutokea pale mwenza wa ngono akiwa bado ana kaswende na hajapimwa wala kutibiwa.


4. Maambukizi katika hatua ya mwisho

Kaswende ya muda mrefu (kaswende ya hatua za mwisho) au kaswende ya mfumo wa fahamu inaweza kuhitaji tiba maalumu tofauti na ya awali.


5. Kinga dhaifu ya mwili

Watu wenye VVU au kinga dhaifu hupona polepole au hupata maambukizi tena kwa urahisi.


Vipimo muhimu kwa kaswende isiyopona

Kwa mtu ambaye kaswende haiponi kama inavyotarajiwa, vipimo vifuatavyo hufanywa:


1. VDRL/RPR (Visivyogundua kimelea wa kaswende) – Ufuatiliaji wa matibabu

Vipimo hivi hutumika kupima wingi wa kingamwili (Dhidi ya kaswende).Ikiwa kingamwili hazipungui kwa kiwango kinachotarajiwa ndani ya miezi 6–12, kuna uwezekano wa kushindwa kwa matibabu.


2. TPHA/TPPA – Kipimo kinachodungua vimelea vya kaswende

Hutumika kuthibitisha maambukizi mapya au ya muda mrefu, au kuchunguza kama kuna kaswende sugu.


3. Uchunguzi wa maji ya uti wa mgongo

Kwa wale wanaoshukiwa kuwa na:

  • Kaswende ya mfumo wa fahamu

  • Upungufu wa kuona au kusikia

  • Maumivu au ganzi ya miguu

  • Kaswende isiyosikia dawa za kawaida


Kipimo cha maji ya uti wa mgongo (CSF) hutumika kutafuta VDRL-CSF, protini na chembe nyeupe za damu.


4. Vipimo vya VVU na magonjwa mengine ya zinaa

VVU huathiri kinga na uwezo wa mwili kupambana na T. pallidum. Kuzingatia pia magonjwa kama klamidia, gono na homaini ikiwa mtu ana hatari kubwa.


5. Uchunguzi wa kliniki wa mwili mzima

Daktari hutathmini:

  • Vidonda visivyopona

  • Michirizi ya upele

  • Uvimbe wa tezi

  • Dalili za mishipa ya fahamu


Hatua muhimu baada ya kupata matokeo


1. Kurudia matibabu

Kwa matokeo yanayoonyesha failure, matibabu ya kawaida ni Benzathine penicillin G uniti 2.4 million kila wiki kwa wiki 3 (Dozi tatu mfululizo). Ikiwa mtu ni allergic kwa penicillin, tiba mbadala hutolewa chini ya uangalizi.


2. Tiba ya kaswende ya mfumo wa fahamu (Kama inathibitishwa)

Aqueous crystalline penicillin G, kwa siku 10–14au Procaine penicillin + probenecid


3. Kuchunguza na kutibu wenza wa ngono

Ni muhimu sana wenza wote:

  • Wapimwe

  • Watibiwe

  • Waepuke ngono hadi daktari aseme salama


4. Ufuatiliaji wa vipimo

VDRL/RPR hurudiwa baada ya:

  • Miezi 3

  • Miezi 6

  • Mwaka 1


5. Kuepuka ngono bila kinga

Kutumia kondomu inapunguza hatari ya kuambukizwa mara nyingine.


6. Kuimarisha kinga ya mwili

Lishe bora, usingizi wa kutosha, kutibu magonjwa mengine, na kupunguza msongo wa mawazo.


Mambo ya kujiandaa kabla ya kumwona Daktari ukiwa na tatizo la kaswende isiyopona


Kwa wagonjwa wanaohisi kaswende imeshindikana kupona licha ya kutumia dawa mara kadhaa, ni muhimu kutoa taarifa sahihi na kamili kwa daktari. Hii humsaidia daktari kubadili mtazamo kutoka tiba za mazoea (empirical treatment) na kuchagua uchunguzi wa kina zaidi.


1. Toa Historia Kamili ya Dawa Zilizotumika Hapo Awali

Mgonjwa anapaswa kueleza:

  • Jina la dawa alizotumia (mfano Benzathine Penicillin, Doxycycline n.k.)

  • Kipimo alichopewa

  • Muda alitumia dawa (siku/ngapi)

  • Kama alipata dozi zote kikamilifu au alizikosa

Hii humsaidia daktari kutathmini kama tiba ilitolewa kwa usahihi au kukadiria uwezekano wa usugu au hitilafu ya matibabu.


2. Eleza dalili zilivyoanza, zimeendelea kwa muda gani, na kama zimewahi kupungua

Maelezo ya muda wa dalili ni muhimu sana:

  • Dalili zilianza lini?

  • Zimekuwa zikiongezeka au kupungua?

  • Je, zilirudi baada ya kupona?

  • Je, dalili zipo sehemu moja au zaidi (vidonda, vipele, maumivu ya misuli, kupoteza nywele, n.k.)?

Hii humsaidia daktari kubaini hatua ya kaswende (hatua ya awali, pili, au ya mwisho).


3. Toa historia ya vipimo ulivyowahi kufanya

Mgonjwa anapaswa kuonesha au kueleza:

  • Matokeo ya VDRL/RPR (pamoja na uwepo wa kinga mwili(antibodi) dhidi ya kaswende kama ipo)

  • TPHA/FTA-ABS

  • Kipimo cha Virusi vya UKIMWI

  • Vipimo vingine vya zinaa


Ikiwezekana, mgonjwa aende kliniki na:

  • Nakara za matokeo ya vipimo vya nyuma

  • Au picha za matokeo kwenye simu

Hii humwezesha daktari kuona mwenendo wa kingamwili dhidi ya kaswende (imepanda, imeshuka au haijabadilika).


4. Eleza idadi ya wenza wa ngono na kama wamewahi kupimwa/kutibiwa

Huu ni ukweli mgumu lakini muhimu:

  • Kama mwenza hajawahi kutibiwa au hawajamaliza tiba, mgonjwa atazidi kuambukizwa tena.

  • Daktari atahitaji kupendekeza tiba kwa wenza wote.


5. Eleza kama una historia ya mzio kwenye dawa Penicillin

Kwa sababu penicillin ndiyo tiba ya kwanza ya kaswende, daktari anahitaji kujua:

  • Kama mgonjwa ana mzio wa penicillin

  • Mzio ulijitokeza kwa namna gani (upele, kupumua kwa shida, n.k.)

Hii humsaidia kuchagua tiba mbadala kwa usalama.


6. Toa taarifa kuhusu magonjwa mengine unayougua

Hasa:

  • Virusi vya UKIMWI

  • Kisukari

  • Magonjwa ya kinga

  • Dawa unazotumia muda mrefu

  • Kipindi cha ujauzito (kwa wanawake)

Magonjwa haya yanaweza kuchelewesha kupona au kubadili tiba inayofaa.


7. Eleza kwa uwazi kama umewahi kupata matibabu ya mara kwa mara bila kufanya vipimo

Hii ni muhimu kumfanya daktari abadili mtazamo kutoka tiba ya mazoea kwenda uchunguzi wa kina:

  • Sema, “Nimekuwa nikipatiwa dawa bila kupimwa, lakini tatizo halijawahi kuisha.”

  • Omba vipimo vya uthibitisho kabla ya dawa nyingine kupewa.


8. Muombe Daktari afanye uchunguzi wa kina badala ya kutoa dawa moja kwa moja

Mgonjwa anapaswa kusema kwa heshima:

“Naomba tupime tena kwa undani ili tujue tatizo halisi, kwa sababu tatizo limedumu na nimetumia dawa kadhaa bila mafanikio.”

Hii humsaidia daktari kuzingatia:

  • Uchunguzi wa maji ya uti wa mgongo-CSF kama anashuku uwepo wa kaswende ya mfumo wa fahamu

  • Kufuata mwongozo wa WHO/CDC

  • Kufanya tathmini ya usugu wa dawa au maambukizi mchanganyiko.


Kwa nini haya ni muhimu?

Kwa kueleza mambo haya kwa uwazi:

  • Daktari hutathmini kwa haraka kama kaswende ni ya muda mrefu, imerudia, au kuna tatizo la usugu au maambukizi mengine

  • Hupunguza hatari ya kupewa dawa zisizofanya kazi

  • Huwezesha kupata tiba sahihi kulingana na hatua ya ugonjwa na historia binafsi ya mgonjwa


Maswali yaliyoulizwa Mara kwa Mara

1. Je, kaswende isiyopona ina maana kwamba nitakuwa nayo maisha yote?

Hapana. Kawaida kaswende isiyopona inamaanisha tu kwamba tiba ya awali haikufanya kazi au maambukizi yalirudi kutokana na kuambukizwa tena. Kwa matibabu sahihi, hata ikiwa ni kaswende ya mfumo wa fahamu, bado hupona. Kinachohitajika ni uchunguzi sahihi, ufuatiliaji wa karibu, na kuchagua tiba inayolingana na aina ya kaswende iliyoendelea.

2. Ndio maana matokeo yangu ya TPHA yameendelea kuwa chanya?

Ndiyo. Vipimo vya treponemal kama TPHA vinaweza kubaki chanya(kuonyesha kuwa maambukizi yapo) maisha yote, hata baada ya kupona. Hii haimaanishi una maambukizi ya sasa, bali inaonyesha kuwa uliwahi kuugua. Daktari hutumia VDRL/RPR kufuatilia kama maambukizi bado yapo.

3. Je, mtu anaweza kuishi na kaswende bila dalili kwa muda mrefu?

Ndiyo. Kaswende inaweza kukaa kimya kwa miaka (hatua ya kujificha) bila dalili yoyote. Hali hii ni hatari kwa sababu mtu anaweza kuonekana mzima lakini bacteria wanaendelea kuharibu mishipa ya fahamu, moyo, na viungo muhimu bila kugundulika.

4. Kaswende isiyopona inaweza kusababisha utasa?

Ndiyo, hasa kwa wanawake. Maambukizi ya muda mrefu yanaweza kusababisha:

  • Uvimbe wa via vya ndani ya nyonga (PID)

  • Kuziba mirija ya uzazi

  • Maambukizi ya muda mrefu kwenye shingo ya kizazi

Kwa wanaume, inaweza kuathiri mirija ya mbegu na kusababisha matatizo ya uzazi.

5. Je, penicillin ikishindwa kuna dawa nyingine?

Ndiyo, lakini kwa tahadhari. Doxycycline, ceftriaxone, au azithromycin hutumika kwa baadhi ya wagonjwa wasioweza kutumia penicillin. Hata hivyo, penicillin inabaki kuwa tiba bora zaidi, hasa kwa ujauzito na kaswende ya mfumo wa fahamu.

6. Je, kaswende inaweza kuathiri mtoto aliye tumboni?

Ndiyo. Kaswende ya mama ikishindwa kutibiwa inaweza kusababisha:

  • Mimba kuharibika

  • Mtoto kuzaliwa njiti

  • Mtoto kufariki tumboni

  • Kaswende ya kuzaliwa


Ndiyo maana upimaji wa mara kwa mara wakati wa ujauzito ni muhimu.

7. Nawezaje kujua kama nimeambukizwa tena?

Kuongezeka kwa kinga mwili za VDRL/RPR (kuongezeka mara nne zaidi) baada ya kushuka awali humaanisha umeambukizwa tena. Daktari pia huangalia dalili mpya kama upele, vidonda, au uvimbe wa tezi.

8. Je, kaswende isiyopona ni ya kawaida kwa watu wenye VVU?

Ndiyo, watu wenye VVU hupona polepole kutokana na kinga iliyodhoofika. Mara nyingi wanahitaji ufuatiliaji wa karibu, vipimo vya mara kwa mara, na wakati mwingine tiba ya muda mrefu zaidi.

9. Je, ukiachana na matibabu kwa muda mfupi kuna madhara?

Ndiyo. Kuchelewa kukamilisha dozi au kutokuhudhuria miadi ya sindano kunaongeza hatari ya:

  • Treatment failure

  • Kuendeleza kaswende ya mfumo wa fahamu

  • Kuambukiza wengine

  • Kuathiri viungo vya mwili visivyotibika

10. Nifanye nini nikiona dalili zimepotea lakini vipimo bado vinaongenya kinga mwili bado ni kubwa?

Hii inaweza kuwa " upo na kinga mwili nyingi dhidi ya kaswende," ambapo kingamwili hubaki juu kwa muda mrefu bila uwepo wa maambukizi hai. Daktari huchunguza mwenendo wa titre, si dalili peke yake. Mara nyingi hailinganishi dalili bali mabadiliko ya titre ndani ya miezi.


ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

Imeandikwa,

10 Desemba 2025, 08:44:26

Rejea za mada hii

  1. Workowski KA, Bachmann LH, Chan PA, et al. Sexually transmitted infections treatment guidelines, 2021. MMWR Recomm Rep. 2021;70(4):1–187.

  2. Ghanem KG. Syphilis. N Engl J Med. 2020;382:858–68.

  3. Hook EW, Marra CM. Acquired syphilis in adults. N Engl J Med. 1992;326:1060–9.

  4. ULY Clinic. Kaswende: Dalili, vipimo na matibabu. ULY Clinic Health Education Portal. 2025.

bottom of page