Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Benjamin L, MD
Imeboreshwa:
30 Januari 2026, 13:43:04

Kipimo cha Mimba kwa Mkojo Baada ya Kutoa Mimba
Baada ya kutoa mimba, wanawake wengi hupima mimba mapema ili kujua kama ujauzito umetoka au la. Hata hivyo, kipimo cha mimba cha mkojo kinaweza kuonyesha majibu chanya (positive) kwa wiki kadhaa kutokana na uwepo wa homoni ya ujauzito inayofahamika kama hCG, hata kama mimba imeshatoka. Makala hii inaeleza kwa kina muda sahihi wa kupima, maana ya matokeo katika nyakati tofauti, na vipimo vya uhakika kama unahitaji kujiridhisha mapema.
Jinsi homoni ya hCG inavyopungua baada ya kutoa mimba
Baada ya ujauzito kusitishwa, mwili huanza kupunguza kiwango cha homoni ya hCG taratibu. Hii haifanyiki ghafla, ndiyo maana vipimo vinaweza kuendelea kuonyesha positive hata kama mimba imetoka.
Kwa ujumla:
Siku 1–7: hCG bado juu, vipimo vya mkojo vinaweza kusoma mimba ipo (positive)
Wiki 1–2: hCG inaendelea kushuka, kipimo kinaweza kutoa majibu chanya au hasi(negative- Mimba hamna)
Wiki 3–4: hCG inapaswa kushuka karibu sifuri → kipimo kinapaswa kuwa hasi kuashiria mimba haipo
Hii ndiyo sababu majibu mapema si ya kuaminika.
Wakati sahihi wa kufanya kipimo cha mimba kwa mkojo
Kwa matokeo yanayoaminika zaidi, kipimo cha mkojo kinapendekezwa kufanywa:
Baada ya wiki 3–4 tangu kutoa mimba.
Huu ndio muda ambao homoni ya hCG imepungua vya kutosha, na uwezekano wa positive ya uongo hupungua.
Maana ya kupata majibu chanya siku chache baada ya kutoa mimba
Kipimo kikisoma majibu chanya(mimba ipo) ndani ya siku 7–14 baada ya kutoa mimba ni kawaida kabisa. Hii haiashirii ujauzito unaoendelea, bali homoni ya hCG inayobaki mwilini wakati mwili unajisafisha.
Maana ya chanya baada ya wiki ya pili ya kutoa mimba
Kupata majibu chanya baada ya wiki 2 kunahitaji tahadhari zaidi, kwa sababu kuna uwezekano wa mambo mawili:
Mabaki ya ujauzito bado yapo kwenye kizazi
Kipimo kinaweza kubaki chanya ikiwa bado kuna tishu za ujauzito ambazo hazijatoka kikamilifu.Dalili zinazoweza kuandamana:
Kutokwa damu kunakoendelea muda mrefu
Maumivu ya tumbo yanayoendelea
Harufu isiyo ya kawaida ukeni
Homoni ya hCG bado haijapungua kikamilifu
Katika baadhi ya wanawake, hCG hushuka polepole zaidi. Hali hii haiwezi kutofautishwa kwa kipimo cha mkojo pekee. Kwa hiyo majibu chanya baada ya wiki 2 inahitaji uchunguzi zaidi kama haitaisha.
Wakati ambao kipimo kinapaswa kuwa hasi(kuonyesha mimba haipo)
Kama ujauzito umetoka kikamilifu:
Kipimo cha mkojo kinapaswa kuwa hasi ndani ya wiki 3–4.
Ikiwa bado positive baada ya muda huo, kuna uwezekano wa mabaki ya ujauzito au ujauzito unaoendelea, na ni muhimu kufanyiwa uchunguzi.
Jinsi ya kupata uhakika mapema zaidi
Ikiwa hutaki kusubiri wiki 3–4 ili kupata matokeo sahihi ya kipimo cha mkojo, njia hizi mbili ni za uhakika zaidi:
Kipimo cha damu cha β-hCG (kiwango)
Hiki ndicho kipimo sahihi zaidi kuthibitisha kama hCG inapungua kweney damu.
Kipimo hufanywa siku ya kwanza
Kinarudiwa baada ya siku 2–3
hCG ikionekana kuwa inapungua inaashiria mimba imetoka
hCG ikiwa juu au inaongezeka inaashiria kuwa kuna mabaki ya mimba au mimba inaendelea
Kipimo hiki ni gharama pia kufanyika
Ultrasound
Ultrasound huonyesha moja kwa moja:
Kama mfuko wa uzazi uko wazi
Kama kuna mabaki
Kama kuna ujauzito unaoendelea
Hiki ndicho kipimo cha uhakika kuliko vyote.
Kipimo hiki ni gharama pia na kinategemea uzoefu wa mpiga picha.
Je, kutokwa na damu kwa muda mrefu kunamaanisha mimba imetoka?
Kutokwa na damu nyingi au kwa muda mrefu hakuwezi kuthibitisha kwa uhakika kama mimba imetoka au bado ipo. Sababu ni kwamba:
Baada ya mimba kutoka (kwa dawa au kutoka yenyewe), mwili unaweza kuendelea kutoa damu kwa siku 7–14, wengine hadi wiki 3—bila kuashiria matatizo.
Wakati mwingine, mtu anaweza kuendelea kupata damu hata kama ujauzito bado haujatoka kikamilifu.
Kwa wengine, damu inaweza kuonekana nyingi lakini ujauzito tayari umeshatoka na mwili unamalizia kusafisha.
Kwa hiyo, idadi ya siku za kutokwa na damu peke au wingi wa damu si kigezo cha kupima mafanikio ya kutoa mimba.
Nini cha kufanya ukipata majibu chanya baada ya wiki ya pili
Usirudie kipimo hicho hicho mara nyingi bila mpango
Fanya kipimo cha damu cha β-hCG
Pinga ultrasound ya kizazi
Muone mtoa huduma ya afya kama hCG haishuki au kuna dalili zisizo kawaida
Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake
1. Je, ni kawaida kipimo cha mimba kuwa chanya siku chache baada ya kutoa mimba?
Ndiyo, ni kawaida kabisa kwa sababu hCG bado iko juu ndani ya wiki 1–2 baada ya kutoa mimba.
2. Majibu chanya baada ya wiki ya pili ina maana gani?
Inaweza kuashiria mabaki ya ujauzito au hCG kushuka polepole. Unapaswa kufanya kipimo cha damu au ultrasound.
3. Kipimo cha mimba kinapaswa kuwa negative baada ya muda gani?
Kwa kawaida ndani ya wiki 3–4. Ikiwa positive baada ya muda huo, unahitaji uchunguzi.
4. Naweza kupima mara ngapi baada ya kutoa mimba?
Kwa uaminifu wa matokeo, subiri wiki 3–4 kabla ya kutumia kipimo cha mkojo.
5. Je, chanya wiki ya tatu ina maana mimba haijatoka?
Inawezekana, lakini kipimo cha mkojo pekee hakitoshi. Thibitisha kwa kipimo cha damu.
6. Je, kipimo cha damu kinaonyesha mapema zaidi?
Ndiyo. β-hCG ndicho kipimo sahihi zaidi na kinaweza kuonyesha mabadiliko ndani ya siku.
7. Ultrasound inasaidia nini baada ya kutoa mimba?
Inaonyesha kama uterasi iko wazi, kama kuna mabaki, au kama ujauzito bado unaendelea.
8. Dalili za mabaki ya ujauzito ni zipi?
Kutokwa damu kwa muda mrefu, maumivu ya tumbo, harufu isiyo kawaida, au positive inayodumu zaidi ya wiki 4.
9. Je, naweza kupata hedhi kabla hCG kushuka?
Ndiyo. Hedhi inaweza kurudi ndani ya wiki 4–6 hata kabla hCG kutoweka kabisa.
10. Majibu chanya baada ya wiki 4 ina maana nini?
Mara nyingi inaonyesha mabaki ya ujauzito au tatizo lingine linalohitaji uchunguzi wa daktari.
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
Imeandikwa,
30 Januari 2026, 13:43:04
Rejea za mada hii
Schreiber CA. Postabortion follow-up and hCG levels. Contraception. 2017;95(3):211–217.
Haddad LB, Tocce K. Postabortion care: Clinical guidelines. Obstet Gynecol Clin North Am. 2020;47(2):357–372.
Chen MJ, Creinin MD. Mifepristone and misoprostol for early pregnancy loss and abortion. Obstet Gynecol. 2015;126(3):673–681.
World Health Organization. Clinical practice handbook for quality abortion care. WHO; 2022.
Royal College of Obstetricians and Gynaecologists. Post-abortion care guidelines. RCOG; 2020.
