top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Sospeter B, MD/MMED

Imeboreshwa:

5 Desemba 2025, 09:11:52

Kukosa usingizi

Kukosa usingizi

Kukosa usingizi hufahamika pia kama insomnia ambalo ni neno lililotokana na Kilatini: in (kukosa) na somnus (usingizi). Kwa mara ya kwanza lilianza kutumika katika tiba karne ya 17, likimaanisha hali ya kukosa usingizi licha ya kuwa na muda na mazingira mazuri ya kulala.

Insomnia ni tatizo endelevu linalosababisha mtu:

  • Kushindwa kuanza kulala

  • Kushindwa kudumu usingizini

  • Kuamka mara kwa mara usiku

  • Au kuamka mapema kuliko kawaida


Mara nyingi watu wanaokosa usingizi huamka wakiwa hawajapumzika, jambo linalodhoofisha ufanisi wao wakati wa mchana. Usingizi ni muhimu kama chakula na mazoezi—ukikosekana, huathiri afya ya mwili, akili, na ubora wa maisha. Kwa kawaida, watu wazima huhitaji masaa 7–8 ya kulala.


Dalili za kukosa usingizi

Mtu mwenye insomnia anaweza kupata dalili zifuatazo:

  • Kushindwa kusinzia

  • Kuamka mara kwa mara usiku

  • Kuamka mapema sana

  • Kutohisi kuchangamka baada ya kulala

  • Uchovu au kusinzia mchana

  • Kukosa umakini na kumbukumbu

  • Ukali wa hasira, msongo au wasiwasi

  • Kuongezeka kwa makosa kazini/ shuleni

  • Maumivu ya kichwa

  • Usumbufu tumboni

  • Hofu au msongo kuhusu kulala


Utafahamika kuwa unashida ya kukosa usingizi endapo hali mojawapo kati ya zifuatazo zinatokea:

  • Kutumia dakika 30 au zaidi kupata usingizi

  • Kulala masaa 6 au pungufu yake

  • Hali hutokea mara 3 kwa wiki au zaidi

  • Hali inadumu kwa muda wa mwezi mmoja au zaidi


Visababishi


1. Msongo wa mawazo

Kuhusu kazi, familia, shule, afya, au matukio makubwa ya maisha kama msiba, talaka, kupoteza kazi n.k.


2. Wasiwasi

Wasiwasi wa kudumu husababisha kuamka mara kwa mara au kushindwa kulala.


3. Magonjwa ya mwili
  • Maumivu sugu

  • Shida za kupumua

  • Kuumwa kiungulia au kucheua tindikali (GERD)

  • Tezi kufanya kazi kupita kiasi

  • Saratani

  • Magonjwa ya moyo na mapafu

  • Ugonjwa wa Parkinson’s na Alzheimer’s

  • Kukojoa mara kwa mara


4. Mabadiliko ya ratiba
  • Safari ndefu (kama safari za ndege kuvuka mabara)

  • Kufanya kazi usiku

  • Kazi za zamu za usiku zinazobadilika mara kwa mara


5. Tabia zisizo rafiki kwa usingizi
  • Kutolala muda maalumu

  • Mazingira yasiyo tulivu

  • Kitanda kutumiwa kwa kazi nyingine (kutoa usingizi kwa ubongo)

  • Mazoezi mazito kabla ya kulala


6. Matumizi ya dawa

Hasa:

  • Dawa za sononeko

  • Dawa za presha/moyo

  • Antihistamine

  • Steroid

  • Viamsha mwili (mf. Ritalin)

  • Dawa za kupunguza uzito

  • Baadhi ya dawa za maumivu


7. Vilevi na viamsha ubongo
  • Kahawa, chai, kola

  • Nikotini

  • Pombe (husinzisha lakini huvuruga usingizi wa usiku)


8. Kula sana usiku

Husababisha kiungulia, gesi na uzito tumboni.


Kukosa usingizi kwa wazee

Wazee wako kwenye hatari zaidi kwa sababu:

  • Tabia ya usingizi hubadilika

  • Wanachoka mapema na kuamka mapema

  • Wanapunguza shughuli za kijamii na mazoezi

  • Wanahusika zaidi na maumivu sugu

  • Wanatumia dawa nyingi


Vihatarishi

  • Uwanamke (mabadiliko ya homoni, ujauzito, kukoma hedhi)

  • Umri > miaka 60

  • Magonjwa ya akili (mf. sononeko, wasiwasi)

  • Msongo mkali

  • Kufanya kazi usiku

  • Kusafiri umbali mrefu


Madhara ya kukosa usingizi

  • Ufanisi mdogo kazini / shuleni

  • Ajali kutokana na usingizi wakati wa kuendesha gari

  • Sononeko, wasiwasi

  • Kuzidi kwa uzito/kitambi

  • Ukali wa tabia

  • Hatari ya presha ya juu

  • Hatari ya magonjwa ya moyo

  • Hatari ya kisukari

  • Hatari ya ulevi


Vipimo

Vipimo hutegemea chanzo, na baadhi ya wagonjwa hupelekwa kwa mtaalamu wa usingizi. Vipimo hivyo baadhi yake vimeainishwa kwenye jedwali 2


Jedwali 2: Vipimo vya kukosa usingizi

Aina ya kipimo

Malengo ya kipimo

Historia ya ugonjwa

Kubaini dalili, muda wa tatizo, vihatarishi, msongo wa mawazo, dawa anazotumia.

Kipimo cha kimwili

Kuchunguza magonjwa yanayosababisha usingizi kama matatizo ya tezi, moyo, mapafu au maumivu sugu.

Ratiba ya kulala-Shajara ya usingizi) – siku 1–2 wiki

Kurekodi saa za kulala, kuamka, usingizi wa mchana, kahawa, pombe, dawa n.k.

Actigraphy

Kifaa kama saa mkononi kinachopima mzunguko wa kulala na kuamka kwa siku kadhaa.

Polysomnography

Kipimo cha hospitali kinachoangalia ubongo (EEG), pumzi, mapigo ya moyo, misuli na harakati usiku.

Epworth Sleepiness Scale

Kupima kiwango cha kusinzia mchana.

Vipimo vya damu (CBC, thyroid, sukari)

Kubaini magonjwa yanayoweza kusababisha insomnia kama hyperthyroidism, anemia, kisukari n.k.

Kipiomo cha afya ya akili

Kuchunguza kama kuna wasiwasi, sononeko au matatizo ya kiakili yanayochangia tatizo.


Matibabu

Kwa maelezo zaidi kuhusu matibabu ya kukosa usingizi soma makala ya dawa za kuleta usingizi haraka hapa


Matibabu ya kukosa usingizi

1. Matibabu yasiyo ya dawa (yanapendekezwa kwanza):

  • Kuunda ratiba ya kulala inayofanana kila siku

  • Kuepuka kahawa, tumbaku na pombe jioni

  • Kuepuka simu/TV saa 1 kabla ya kulala

  • Mazoezi ya kutuliza mwili (kupumzisha mwili na kupumua kwa kina)

  • Kuboresha mazingira ya usingizi (utulivu, giza, kitanda bora)

  • Tiba tabia (CBT-I)


2. Matibabu ya dawa (hutoa kwa ushauri wa daktari):

  • Dawa za muda mfupi za kusaidia kuleta usingizi

  • Antidepressants maalumu kwa ajili ya kukosa usingizi

  • Melatonin kwa matatizo ya mzunguko wa usingizi


3. Kutibu chanzo cha tatizo:

  • Kudhibiti maumivu sugu

  • Kutibu shida za tezi, pumu, GERD, matatizo ya tezi, wasiwasi au sononeko

  • Kubadilisha dawa zinazosababisha shida ya kulala


Kwa maelezo zaidi kuhusu matibabu soma makala ya dawa za kuleta usingizi haraka hapa

ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

Imeandikwa,

5 Desemba 2025, 09:11:40

Rejea za mada hii

  1. National Heart, Lung, and Blood Institute. What is insomnia? 2020.

  2. Office on Women’s Health. Insomnia fact sheet. U.S. Department of Health & Human Services; 2020.

  3. American Psychiatric Association. Diagnostic and Statistical Manual of Mental Disorders (DSM-5). 5th ed. Washington, DC; 2013.

  4. National Alliance on Mental Illness (NAMI). Sleep disorders: The connection between sleep and mental health. 2020.

  5. Bonnet MH, Arand DL. Clinical features and diagnosis of insomnia. UpToDate; 2020.

  6. Merck Manual Professional Version. Approach to the patient with sleep or wakefulness disorder. 2020.

  7. Natural Medicines. Insomnia. Therapeutic Research Center; 2020.

  8. National Institute on Aging. Sleep and aging. 2020.

  9. Kliger B, et al. Complementary/integrative therapies that work: A review of the evidence. Am Fam Physician.

bottom of page