Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Mangwella S, MD
Imeboreshwa:
10 Julai 2025, 14:58:09

Kujirudia kwa uchafu mweupe wenye harufu kali ukeni baada ya matibabu: Sababu, Uchunguzi na Tiba Madhubuti
Swali la msingi
Habari daktari, ninapata kutokwa na uchafu mweupe unaofanana na maziwa mtindi, ukihusishwa na majimaji yenye harufu kali. Nilipokea dawa za antibayotiki kama ceftriaxone na metronidazole, hali ikapungua lakini tatizo linarudi tena baada ya muda mfupi. Ni aina gani ya vipimo vya uchunguzi vinavyopaswa kufanywa ili kubaini chanzo halisi na kupata suluhisho madhubuti? Je, kuna sehemu fulani katika utambuzi au matibabu ambayo inaweza kuwa imeshindikana?
Majibu
Maambukizi ya uke ni hali ya kawaida inayowakumba wanawake wengi, na mara nyingine hujirudia hata baada ya matibabu. Mgonjwa anapotokwa na uchafu wa ukeni unaofanana na maziwa mtindi, wenye harufu kali na unyevu mwingi, mara nyingi huhusishwa na maambukizi ya fangasi aina ya Kandida albikani. Hata hivyo, maambukizi haya yanapojirudia mara kwa mara, yanaweza kuwa kiashiria cha sababu ya msingi isiyotibiwa ipasavyo, au hitilafu katika usafi, lishe, mfumo wa kinga, au mwenendo wa matumizi ya dawa.
Dalili za maambukizi yanayojirudia
Dalili Kuu | Maelezo |
Kutokwa na uchafu mweupe kama maziwa mtindi | Wenye harufu kali au ya kuchoma |
Kuwashwa ndani ya uke na maeneo ya sura ya uke (vulva) | Kwa muda mrefu au baada ya tendo la ndoa |
Maumivu wakati wa haja ndogo au kujamiiana | Inaweza kuashiria uvimbe au kuungua |
Kukojoa mara kwa mara au hisia ya kuungua | Dalili ya uambukizo wa mfumo wa mkojo pia |
Ngozi ya uke kuwa nyekundu, kuvimba au kuchubuka | Haswa kwa fangasi au maambukizi mchanganyiko |
Vipimo na uchunguzi unaoshauriwa
Uchunguzi wa kina unahitajika ili kubaini chanzo halisi cha maambukizi, aina ya vimelea vinavyosababisha, na kuchagua dawa sahihi.
Kipimo | Maelezo |
Kupima ute unaotoka ndani ya uke (HVS) | Hutumika kuchukua uchafu wa ukeni na kuupima kwa uangalifu kutambua aina ya vimelea |
Kuotesha vimelea kwenye ute ukeni na kuangalia dawa inayofaa | Husaidia kutambua dawa gani zinafanya kazi vizuri dhidi ya vimelea waliogunduliwa |
Uchunguzi wa ute mbichi kwa hadubini | Hupima uwepo kimelea Kandida, Trikomonas vaginalis au chembe ashiria za ugonjwa wa vajinosisi ya bakteria kwa haraka |
Kipimo cha pH ya uke | Fangasi kawaida hutokea kwenye uke wa pH ya chini (≤4.5), ilhali vajinosisi ya bakteria huongeza pH |
Gram stain | Hutambua aina ya bakteria au Kandida kwa kutumia darubini maalum |
Pap smia | Kwa dalili sugu au wasiwasi wa mabadiliko ya seli za shingo ya kizazi (saratani ya shingo ya kizazi) |
Visababishi vya kujirudia kwa maambukizi
Kisababishi | Maelezo |
Matibabu duni au yasiyokamilika | Kutotumia dawa kikamilifu au kutumia dawa isiyo sahihi au mchanganyiko usiojitosheleza |
Nguo za ndani zisizofaa | Nailoni au zinazobana sana huchochea unyevu na joto |
Kisukari kisichodhibitiwa | Hupunguza kinga na kuongeza hatari ya maambukizi ya fangasi aina ya Kandida |
Mabadiliko ya homoni | Hususani wakati wa ujauzito, hedhi au kutumia dawa za homoni(kama dawa za uzazi wa mpango) |
Sabuni zenye kemikali kali au kujisafisha ndani ya uke | Hubadilisha mazingira ya uke na kuua bakteria wema |
Mpenzi kuwa chanzo | Maambukizi huweza kujirudia kama mwenza hatibiwi pia ipasavyo. |
Kingamwili dhaifu (upungufu wa kinga) | Mfano: wagonjwa wa kisukari, VVU, au wanaotumia dawa za kupunguza kinga mwilini kama dawa jamii ya steroid |
Kutotumia dawa ya kuua fangasi | Kama ulikuwa na kandidiasis lakini ulitibiwa na antibayotiki tu, fangasi huendelea. |
Kutotambua maambukizi mchanganyiko | Kandidiasis + Vajinosisi ya bakteria wanaweza kuwepo pamoja. |
Matibabu ya kudhibiti maambukizi
(a) Fangasi (Kandida albikan):
Daktari anaweza kukuandikia dawa zifuatazo;
Dawa za ndani ya uke: Clotrimazole, Nystatin
Dawa za kumeza: Fluconazole mara moja, au kila wiki kwa matibabu ya muda mrefu
Fangasi sugu: Ketoconazole au Itraconazole, kwa ushauri wa daktari
(b) Maambukizi ya bakteria (Vajinosisi ya bakteria):
Daktari anaweza kukuandikia dawa zifuatazo kama anadhani ndio kisababishi;
Metronidazole mara mbili kwa siku kwa siku 7
Au: Clindamycin krimu ya kutumia ukeni usiku
(c) Maambukizi ya trikomonas
Daktari anaweza kukuandikia dawa zifuatazo;
Metronidazole dozi moja au dozi ndogo kwa siku 7
Mpenzi anapaswa kutibiwa pia
(d) Probiotiki
Daktari anaweza kukuandikia dawa za kufufua bakteria rafiki waishio ukeni kama Lactobacilli.
(e) Maambukizi mchanganyiko
Daktari anaweza kukuandikia dawa zote mbili – dawa za kuua fangasi na bakteria.
Unawezaje kudhibiti kujirudia kwa maambukizi?
Maliza dawa zote kama ulivyoelekezwa
Epuka sabuni zenye harufu, dawa za kusafisha ndani ya uke , na pedi za harufu kali(zenye manukato)
Vaa nguo za ndani za pamba zilizo pana
Kausha uke vizuri baada ya kuoga au kukojoa
Tumia kondomu kama maambukizi yamekuwa yakijirudia baada ya ngono
Punguza ulaji wa sukari mwingi (huchochea fangasi)
Fanya uchunguzi wa sukari (kipimo cha kisukari) kama tatizo ni la kurudi-rudi
Lini uonane na daktari haraka?
Wasiliana na daktari haraka endapo
Dalili zinarudi ndani ya wiki chache baada ya matibabu
Maumivu makali ya ndani ya uke au tumbo la chini
Kutokwa na damu isiyo ya hedhi
Mpenzi kuwa na dalili kama hizo
Kuwa mjamzito au kushukiwa kuwa na VVU
Hitimisho
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
Imeandikwa,
10 Julai 2025, 14:56:35
Rejea za mada hii
Sobel JD. Vulvovaginal candidosis. Lancet. 2007 Jun 2;369(9577):1961–71.
Koumans EH, Sternberg M, Bruce C, McQuillan G, Kendrick J, Sutton M, et al. The prevalence of bacterial vaginosis in the United States, 2001–2004; associations with symptoms, sexual behaviors, and reproductive health. Sex Transm Dis. 2007 Nov;34(11):864–9.
Workowski KA, Bachmann LH, Chan PA, Johnston CM, Muzny CA, Park I, et al. Sexually transmitted infections treatment guidelines, 2021. MMWR Recomm Rep. 2021 Jul 23;70(4):1–187.
Amsel R, Totten PA, Spiegel CA, Chen KC, Eschenbach D, Holmes KK. Nonspecific vaginitis: diagnostic criteria and microbial and epidemiologic associations. Am J Med. 1983 Jan;74(1):14–22.
Centers for Disease Control and Prevention. Bacterial vaginosis – CDC fact sheet. Atlanta (GA): CDC; 2021.
Donders GG, Bellen G, Rezeberga D. Aerobic vaginitis in pregnancy. BJOG. 2011 Oct;118(10):1163–70.
Marrazzo JM, Martin DH. Management of women with cervicitis. Clin Infect Dis. 2007 Jul 1;44 Suppl 3:S102–10.
Linhares IM, Witkin SS, Miranda SD, Fonseca AM, Pinotti JA, Ledger WJ. Differentiation between bacterial vaginosis and aerobic vaginitis by Gram stain and cultures. Am J Obstet Gynecol. 2011 Feb;204(2):e1–5.
Mendling W. Vaginal microbiota. Adv Exp Med Biol. 2016;902:83–93.
Bohbot JM, Sednaoui P. Major changes in the vaginal ecosystem. J Gynecol Obstet Biol Reprod (Paris). 2011 Apr;40(2):S1–8.
