top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Benjamin L, MD

Imeboreshwa:

22 Juni 2025, 18:07:21

Kutokwa damu baada ya usafishaji wa kizazi kufuatia kutoa mimba kwa dawa

Kutokwa damu baada ya usafishaji wa kizazi kufuatia kutoa mimba kwa dawa

Kutoa mimba kwa njia ya dawa ni njia inayotumika sana kwa mimba changa, hasa chini ya wiki 12. Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kuwa mwili unaweza kuendelea kutoa damu hata baada ya usafishaji kufanyika hospitalini. Katika makala hii, tunajadili sababu za kutoka damu baada ya kutoa mimba na hatua sahihi za kuchukua.


Kisa cha mgonjwa

Mwanamke alitoa mimba ya wiki mbili kwa kutumia dawa. Baada ya wiki moja, alikwenda hospitali kwa ajili ya kusafishwa mfuko wa mimba. Alitokwa damu kwa wiki moja, kisha damu ikasimama kwa siku nne. Baada ya hapo, damu ilianza kutoka tena. Hali hii inahitaji uchunguzi na ufuatiliaji wa karibu.


Visababishi

Sababu zinazowezek kuchangua kutokwa damu tena ni pamoja na;


1. Mabaki ya ujauzito

Mara nyingine, hata baada ya kusafishwa, kunaweza kubaki vipande vidogo vya ujauzito ndani ya mfuko wa mimba. Mwili hujaribu kuvisafisha kwa njia ya kutoka damu, na hali hii inaweza kudumu kwa siku au wiki kadhaa.


2. Maambukizi katika mfuko wa mimba

Ikiwa damu inaambatana na harufu mbaya, homa, au maumivu makali ya tumbo, huenda kuna maambukizi. Maambukizi haya huweza kutokea kutokana na mabaki au usafishaji usiokamilika.


3. Mzunguko wa hedhi kurudi mapema

Baada ya kutoa mimba ya wiki chache, homoni za uzazi huweza kurudi katika hali ya kawaida haraka. Kwa hiyo, damu ya pili inaweza kuwa hedhi ya kawaida ya kwanza baada ya kutoa mimba.


4. Mabadiliko ya homoni

Kutoa mimba kunaathiri kiwango cha homoni mwilini. Mabadiliko haya yanaweza kusababisha damu kutoka bila mpangilio hadi homoni zitakapowiana tena.


5. Matatizo ya kuganda kwa damu

Kama damu inaendelea kutoka kwa wingi au kwa muda mrefu isivyo kawaida, na hakuna mabaki wala maambukizi, basi matatizo ya kuganda kwa damu yanaweza kuwa chanzo. Hii ni pamoja na hali kama:

  • Upungufu wa chembe za kugandisha damu (thrombosaitopenia)

  • Ugonjwa wa Von Willebrand (ugonjwa wa kurithi unaosababisha damu kutoganda vizuri)

  • Mgando wa damu ulioenea ndani ya mishipa  (hali inayoweza kutokea baada ya mimba kutoka na mwili kupoteza udhibiti wa mgando)


Wanawake wenye historia ya kutokwa damu nyingi baada ya kuumia au upasuaji wanapaswa kufanyiwa uchunguzi wa damu ili kuthibitisha au kuondoa uwezekano huu.


Wakati gani wa kuonana na daktari haraka?

Ikiwa unaona dalili zifuatazo, unapaswa kumwona daktari mara moja:

  • Kutoka damu nyingi (kubadilisha pedi kila saa)

  • Maumivu makali ya tumbo yasiyopungua

  • Harufu mbaya kutoka ukeni

  • Homa au baridi kali

  • Kichefuchefu au kutapika kwa wingi


Hatua za kuchukua

  1. Fanya ultrasound: Ili kuangalia kama kuna mabaki ndani ya mfuko wa mimba.

  2. Pima damu: Vipimo vya homoni na kuangalia maambukizi pamoja na hali ya ugandaji wa damu

  3. Tumia dawa kwa usahihi: Ikiwa kuna maambukizi, daktari atakupa antibiotik.

  4. Epuka kujisafisha ndani ya uke  hadi upate ruhusa ya daktari.

  5. Pumzika na uepuke kufanya tendo la ndoa hadi daktari atakapothibitisha umepata nafuu.


Hitimisho

Kutoka damu baada ya kutoa mimba ni jambo la kawaida kwa muda mfupi. Hata hivyo, kutoka damu tena baada ya usafishaji kunahitaji kufuatiliwa kwa makini na mtaalamu wa afya. Mwanamke hapaswi kupuuzia dalili hizi kwa kuwa zinaweza kuashiria maambukizi au mabaki ya mimba. Uchunguzi wa kitaalamu ndio njia pekee ya kuhakikisha afya yake iko salama na anaweza kupata ujauzito salama siku zijazo.

ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

Imeandikwa,

22 Juni 2025, 18:06:17

Rejea za mada hii

  1. World Health Organization. Safe abortion: technical and policy guidance for health systems. WHO; 2022.

  2. Creinin MD, Gemzell-Danielsson K. Medical abortion in early pregnancy. N Engl J Med. 2019;380(1):64–70.

  3. Royal College of Obstetricians and Gynaecologists. Management of incomplete and missed abortion. Green-top Guideline No. 25; 2020.

  4. RCOG. Management of incomplete and missed abortion. Green-top Guideline No. 25; 2020.

  5. Hoffman BL, et al. Williams Gynecology. 3rd ed. McGraw-Hill; 2016.

  6. James AH. Bleeding disorders in pregnancy. Obstet Gynecol. 2010;115(5):1100–11.

bottom of page