top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Benjamin L, MD

Imeboreshwa:

23 Desemba 2025, 13:16:48

Kutokwa jasho kupita kiasi Usoni: Visababishi, Dalili, Uchunguzi na Matibabu

Kutokwa jasho kupita kiasi Usoni: Visababishi, Dalili, Uchunguzi na Matibabu

Kutokwa na jasho ni utaratibu wa kawaida wa mwili unaosaidia kudhibiti joto na kuondoa sumu. Hata hivyo, pale jasho linapotoka kupita kiasi usoni, bila kuhusishwa na joto kali, mazoezi au homa, hali hii huleta usumbufu mkubwa wa kiafya, kijamii na kisaikolojia.


Kwa wagonjwa wengi, jasho la usoni huathiri kujiamini, kazi, mawasiliano ya kijamii na hata afya ya ngozi. Makala hii ya ULY Clinic inaeleza kwa undani mkubwa sababu zake kulingana na ushahidi wa tafiti, dalili, uchunguzi na njia za matibabu.


Kutokwa na Jasho Usoni Kupita Kiasi ni Nini?

Ni hali ambapo tezi za jasho (eccrine sweat glands) zilizopo usoni hutoa jasho kwa kiwango kikubwa kuliko mahitaji ya mwili. Jasho linaweza kuonekana:

  • Paji la uso

  • Mashavu

  • Pua

  • Mdomo wa juu

  • Kichwa (scalp)

  • Uso mzima kwa ujumla

Hali hii inaweza kuwa ya muda mfupi au ya kudumu.


Aina za kutokwa na jasho kupita kiasi


1.Aina ya awali ya kutoka na jasho
  • Haina ugonjwa mwingine wa msingi

  • Huanzia utotoni au ujana

  • Huchochewa na hisia

  • Mara nyingi huathiri uso, viganja, kwapa na nyayo


2. Aina ya pili ya kutokwa jasho jingi
  • Husababishwa na ugonjwa au hali nyingine ya kiafya

  • Huanzia ukubwani

  • Mara nyingi huathiri sehemu nyingi za mwili


Visababishi vya kutokwa na jasho kupita kiasi usoni


1. Msisimko kupita kiasi wa mfumo wa wa fahamu wa matendo yasiyo hiari
  • Mfumo wa fahamu wa sympathetiki unapokuwa na msisimko mkubwa

  • Husababisha tezi za jasho kutoa jasho bila sababu ya joto

  • Hii ndiyo chanzo kikuu cha awali cha kutoka jasho usoni


2. Mabadiliko ya homoni

a) Komahedhi

  • Kupungua kwa homoni ya estrojen

  • Husababisha mshiko wa jasho asubuhi na jasho la ghafla usoni

  • Jasho hutokea mchana au usiku

  • Ni sababu ya kawaida sana kwa wanawake wa miaka 45 na kuendelea


b) Ujauzito

  • Kuongezeka kwa homoni za projesterone na estrojen

  • Huongeza joto la mwili na jasho, hasa usoni


c) Baada ya Kujifungua

  • Mabadiliko ya ghafla ya homoni

  • Jasho huweza kuwa kali kwa wiki au miezi


3. Magonjwa ya Tezi shingo (thairoid)
  • Uzalishaji kupita kiasi wa homoni za tezi shingo huongeza kasi ya kimetaboliki

  • Dalili zake ni:

    • Jasho jingi

    • Mapigo ya moyo kwenda kasi

    • Kupungua uzito

    • Kutetemeka mikono


4. Msongo wa mawazo na magonjwa ya akili
  • Ugonjwa wa hofu kuu

  • Mshiko wa kutaharuki

  • Msongo wa mawazo

  • Hofu ya kuwa kwenye watu wengi


Msongo huamsha mfumo wa fahamu wa simpathetiki- jasho la usoni huongezeka hata bila joto.


5. Ugonjwa wa kisukari
  • Kiwango cha sukari kushuka (kwenye damu)

  • Magonjwa ya mishipa ya fahamu ya matendo yasiyohiari kutokana na kisukari

  • Jasho usoni huweza kuambatana na:

    • Kutetemeka

    • Kizunguzungu

    • Mapigo ya moyo kwenda kasi


6. Maambukizi na Magonjwa ya Muda Mrefu
  • Kifua kikuu

  • Maambukizi ya virusi vya UKIMWI(UKIMWI)

  • Maambukizi kwenye kuta ya ndani ya moyo

  • Homa sugu


Haya husababisha mwili kuwa katika hali ya uchochezi wa kudumu.


7. Dawa

Dawa zinazohusishwa na jasho la usoni ni pamoja na:

  • Dawa za magonjwa ya akili(SSRIs, TCAs)

  • Dawa za homoni

  • Dawa za shinikizo la damu

  • Dawa za maumivu (Jamii ya opioid)


8. Unene kupita kiasi
  • Huongeza uzalishaji wa joto mwilini

  • Huongeza mzigo kwa mfumo wa jasho


9. Matumizi ya vyakula na vinywaji fulani
  • Pombe

  • Kafeini (kama kutoka kwenye kahawa, soda n.k)

  • Vyakula vyenye pilipili kali

  • Vinywaji vya moto sana


10. Magonjwa ya mishipa ya fahamu
  • Ugonjwa wa Parkinson’s mara nyingi hutokea uzeeni

  • Kiharusi

  • Magonjwa ya mishipa ya fahamu ya matendo yasiyo hiari


Dalili zinazoambatana

  • Uso kuwa na unyevunyevu muda wote

  • Jasho kuanza ghafla bila sababu

  • Ngozi ya uso kupata vipele au fangasi

  • Aibu, hofu au kujitenga kijamii

  • Jasho kuongezeka wakati wa kuongea au kufikiria


Vipimo na Uchunguzi


1. Historia ya Kina ya Mgonjwa
  • Umri wa kuanza

  • Muda wa tatizo

  • Vichochezi

  • Dawa anazotumia


2. Uchunguzi wa Mwili
  • Kiasi na maeneo ya jasho

  • Dalili za homoni au magonjwa mengine


3. Vipimo vya Maabara

  • TSH, T3, T4

  • Sukari ya damu

  • Vipimo vya maambukizi

  • Vipimo vya homoni (kwa wanawake)


Matibabu ya kutokwa na Jasho usoni kupita kiasi


1. Matibabu ya kawaida
  • Dawa za kupunguza msongo (aluminum chloride)

  • Usafi wa ngozi kwa bidhaa zisizo kali


2. Dawa
  • Dawa za kuzuia uzalishaji wa homoni za mishipa ya fahamu (Kolijeni)

  • Dawa za kudhibiti wasiwasi

  • Dawa za homoni (kwa komahedhi, chini ya ushauri wa daktari)


3. Sindano za Botox
  • Huzuia mawasiliano ya neva na tezi za jasho

  • Athari hudumu miezi 4–6


4. Mabadiliko ya Mtindo wa Maisha
  • Kudhibiti msongo wa mawazo

  • Kupunguza uzito

  • Epuka pombe, kafeini na pilipili


5. Upasuaji

Ni nadra sana kufanyika kwa tatizo la kutoka jasho usoni


Wakati wa kumwona Daktari

  • Jasho linaanza ghafla

  • Linaambatana na kupungua uzito au mapigo ya moyo kwenda kasi

  • Linaharibu maisha ya kila siku


Hitimisho

Kutokwa na jasho usoni kupita kiasi ni tatizo linaloweza kusababishwa na msisimko wa neva, homoni (ikiwemo komahedhi), magonjwa ya ndani au dawa. Uchunguzi sahihi na matibabu husaidia kudhibiti dalili na kuboresha ubora wa maisha.


Maswali yanayoulizwa mara kwa mara na majibu yake

Je kutokwa na jasho usoni ni ugonjwa?

Ndiyo, endapo hutokea kupita kiasi bila sababu za kawaida, huchukuliwa kama tatizo la kiafya.

Je linaweza kuashiria ugonjwa wa tezi dume?

Ndiyo, hasa likifuatana na mapigo ya moyo kwenda kasi na kupungua uzito.

Je msongo wa mawazo unaweza kusababisha jasho usoni?

Ndiyo, ni moja ya sababu kuu kwa watu wengi.

Je wanaume huathirika zaidi kuliko wanawake?

Hapana, wote huathirika kwa kiwango sawa.

Je sindano ya Botox ni salama kwa uso?

Ndiyo, endapo itafanywa na mtaalamu aliyebobea.

Je hali hii hupona kabisa?

Inaweza kudhibitiwa vizuri, lakini baadhi ya watu huhitaji matibabu ya muda mrefu.

Je vipodozi vinaweza kuongeza tatizo?

Ndiyo, hasa vipodozi vizito vinavyofunga matundu ya ngozi.

Je jasho usoni linaweza kuashiria kisukari?

Katika baadhi ya hali, ndiyo, hasa likiambatana na dalili nyingine.

Je kunywa maji mengi husaidia?

Husaidia kudhibiti joto la mwili lakini hakutibu chanzo.

Ni lini ni lazima nimuone daktari?

Pale jasho linapoathiri maisha yako au linaanza ghafla bila sababu.


ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

Imeandikwa,

23 Desemba 2025, 13:16:48

Rejea za mada hii

  1. Hornberger J, et al. Recognition, diagnosis, and treatment of primary focal hyperhidrosis. J Am Acad Dermatol. 2004;51(2):274–286.

  2. Walling HW. Clinical differentiation of primary and secondary hyperhidrosis. J Am Acad Dermatol. 2011;64(4):690–695.

  3. Freedman RR. Menopause and hot flashes. Endocr Rev. 2001;22(3):347–363.

  4. Lear W, et al. Hyperhidrosis: management options. CMAJ. 2007;177(10):1205–1208.

  5. International Hyperhidrosis Society. Pathophysiology of hyperhidrosis.a

bottom of page