top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Mangwella S, MD

Imeboreshwa:

7 Januari 2026, 08:53:28

Kutokwa na Damu kwenye Mkojo bila chanzo cha wazi: Nini kinaweza kuwa Tatizo?

Kutokwa na Damu kwenye Mkojo bila chanzo cha wazi: Nini kinaweza kuwa Tatizo?

Kutokwa na damu kwenye mkojo (hematuria) ni dalili inayoweza kumtia mtu hofu kubwa, hasa pale anapofanya vipimo mara kadhaa na kuambiwa kila kitu kiko sawa lakini damu bado inaendelea kutoka. Hali hii ni ishara muhimu ya kiafya inayohitaji uchunguzi wa kina zaidi, si kupuuzwa wala kujitibu.


Kutokwa na damu kwenye mkojo (Hematuria) ni nini?

Hematuria ni hali ya kuwepo kwa damu kwenye mkojo, ambayo inaweza:

  • Kuonekana kwa macho (mkojo mwekundu au wa kahawia)

  • Au kuonekana tu kwa kipimo cha maabara (hematuria isiyoonekana kwa macho)


Kwa nini mtu anaweza kukojoa damu lakini vipimo vya awali viko sawa?

Baadhi ya sababu hujitokeza baada ya vipimo vya kawaida kushindwa kubaini chanzo kama inavyoonekana kwenye jedwali 1.


Jedwali 1: Sababu Zinazowezekana za Damu Kuendelea Kutoka Kwenye Mkojo (Hematuria)

Sababu

Maelezo kwa ufupi

Dalili za kipekee

Hematuria isiyo na chanzo wazi

Damu huendelea kutoka bila maambukizi au mawe kuonekana; huhitaji ufuatiliaji wa karibu na vipimo maalum

Damu hujitokeza mara kwa mara bila maumivu au dalili nyingine wazi

Maambukizi sugu ya njia ya mkojo

Baadhi ya bakteria hawaonekani kirahisi; dawa zisizolenga kimelea sahihi hufanya tatizo kuendelea

Kukojoa mara kwa mara, kuungua wakati wa kukojoa, harufu mbaya ya mkojo

Mawe madogo ya figo/kibofu

Huenda yasionekane kwenye ultrasound ya kawaida; huchubua mishipa ya damu

Maumivu ya ghafla upande wa kiuno, damu kuongezeka baada ya kazi nzito

Magonjwa ya ndani ya figo (glomerular)

Mfano glomerulonephritis; mara nyingi hakuna maumivu makali; huhitaji vipimo maalum

Mkojo wenye povu, uvimbe wa miguu/uso, shinikizo la damu

Matatizo ya tezi dume (wanaume)

Prostatitis au kuvimba kwa tezi dume; husababisha damu kwenye mkojo au shahawa

Maumivu chini ya tumbo au kati ya miguu, kukojoa kwa shida

Athari za dawa au miti shamba

Baadhi ya dawa/mitishamba huathiri figo na kusababisha hematuria

Dalili huanza baada ya kuanza dawa fulani; kichefuchefu au uchovu

Saratani za njia ya mkojo

Nadra lakini muhimu kuondoa shaka; damu hutoka bila maumivu

Damu nyingi bila maumivu, kupungua uzito bila sababu, uchovu wa muda mrefu

Kumbuka: Dalili zinaweza kutofautiana kati ya mtu na mtu; vipimo vya daktari bingwa ni muhimu kuthibitisha chanzo halisi.

Ni vipimo gani vya kina vinahitajika endapo hali inaendelea?

Iwapo damu inaendelea licha ya matibabu ya awali, daktari bingwa anaweza kupendekeza:

  • Kipimo maalumu kwa kuchugnuza mkojo kwenye hadubini

  • Kuotesha mkojo

  • Kipimo cha kuangalia njia ya mkojo- CT Urogram

  • Sistoskopi (kuangalia ndani ya kibofu)

  • Vipimo vya figo (kipimo cha utendaji kazi wa figo)

  • Vipimo vya magonjwa ya kinga ya mwili (shambulio binafsi la kinga ya mwili)


Matibabu hutegemea nini?

Hakuna dawa moja kwa wote. Matibabu hutegemea chanzo halisi kama inavyoonekana kwenye jedwali 2.


Jedwali 2: Kisababishi cha damu kwenye mkojo na matibabu yake

Kisababishi

Matibabu yanayopendekezwa

Hematuria isiyo na chanzo wazi

Ufuatiliaji wa karibu wa kitabibu, vipimo vya mara kwa mara vya mkojo na damu, na uchunguzi wa kina (mf. uchunguzi wa kibofu kupitia kipimo cha sistoskopi au Njia za mkojo kupitia kipimo cha CT urogram) ili kubaini chanzo kilichojificha

Maambukizi sugu ya njia ya mkojo

Antibiotics maalum kulingana na majibu ya kuotesha vimelea kwenye mkojo, kuongeza maji mwilini, na kufuatilia tiba hadi maambukizi yatokomee kabisa

Mawe madogo ya figo/kibofu

Kunywa maji mengi, dawa za kusaidia mawe kutoka, dawa za maumivu; endapo hayashuki, hutumika matibabu ya kitaalamu kama ESWL au upasuaji mdogo

Magonjwa ya ndani ya figo (glomerula)

Matibabu ya figo chini ya daktari bingwa wa mkojo au figo (nephrologist), dawa za kupunguza kinga ya mwili, kudhibiti shinikizo la damu na lishe maalum

Matatizo ya tezi dume (wanaume)

Antibiotics (kama ni maambukizi), dawa za kupunguza uvimbe wa tezi dume, au matibabu ya kitaalamu endapo tatizo ni sugu

Athari za dawa au miti shamba

Kusitisha dawa/mitishamba inayosababisha tatizo, kufanyiwa tathmini ya figo, na kutumia dawa mbadala salama kwa ushauri wa daktari

Saratani za njia ya mkojo

Rufaa ya haraka kwa bingwa wa saratani; matibabu hutegemea hatua ya ugonjwa (upasuaji, mionzi au kemotherapia)

Tahadhari muhimu: Matibabu hutegemea chanzo halisi. Usijitibu au kuacha dawa bila ushauri wa daktari bingwa, hasa pale damu kwenye mkojo inapoendelea au kujirudia.

Nifanye nini kama damu inaendelea kutoka?

  • Usijitibu

  • Epuka kutumia dawa bila vipimo sahihi

  • Tafuta rufaa ya kuonana na daktari bingwa wa mfumo wa mkojo

  • Fuata vipimo hadi chanzo halisi kijulikane


Mambo ya kufanya nyumbani na mabadiliko ya mtindo wa maisha

Jedwali 3 linaonyesha hatua rahisi za kujitunza nyumbani na mabadiliko ya mtindo wa maisha yanayoweza kusaidia kupunguza hatari na kulinda afya ya njia ya mkojo. Hatua hizi husaidia mwili lakini hazibadilishi uchunguzi na matibabu ya daktari.


Jedwali 3: Mambo ya kufanya nyumbani na Mabadiliko ya mtindo wa maisha kwa mtu anayekojowa damu

Jambo la kufanya

Maelezo kwa ufupi

Kunywa maji ya kutosha

Lita 2–3 kwa siku husaidia kusafisha njia ya mkojo na kupunguza muwasho

Epuka kujizuia kukojoa

Kukojoa mara kwa mara huzuia bakteria kukaa muda mrefu kwenye kibofu

Punguza chumvi na vyakula vilivyosindikwa

Hulinda figo na kupunguza hatari ya mawe ya figo

Epuka dawa za maumivu bila ushauri

Dawa kama ibuprofen/diclofenac zinaweza kuharibu figo zikitumiwa mara kwa mara

Epuka miti shamba

Baadhi huathiri figo na kuongeza damu kwenye mkojo

Epuka pombe na sigara

Hupunguza uharibifu wa mishipa ya damu na hatari ya saratani

Dumisha usafi wa njia ya mkojo

Hupunguza maambukizi ya njia ya mkojo, hasa kwa wanawake

Dhibiti magonjwa sugu

Kudhibiti kisukari na shinikizo la damu hulinda figo

Pumzika, epuka kazi nzito

Husaidia kama damu huongezeka baada ya shughuli nzito

Fuata ushauri wa daktari

Mabadiliko ya maisha husaidia lakini hayabadilishi uchunguzi wa kitaalamu

Kumbuka: Jedwali hili ni msaada wa kujitunza, sio mbadala wa vipimo na matibabu ya daktari endapo damu inaendelea kutoka.

Hitimisho

Kutokwa na damu kwenye mkojo ni ishara muhimu ya kiafya. Endapo vipimo vya awali havijaonyesha chanzo lakini dalili inaendelea, uchunguzi wa kina zaidi ni lazima. Usikubali kuishi na dalili bila majibu sahihi.


Maswali yanayoulizwa mara kwa mara na majibu yake

1. Kukojoa damu bila maumivu kunaweza kumaanisha nini?

Damu bila maumivu mara nyingi huashiria tatizo linaloendelea polepole kama matatizo ya kibofu, figo au mishipa ya damu, na huhitaji uchunguzi wa haraka hata kama hakuna maumivu.

2. Ni muda gani kukojoa damu kunapaswa kumfanya mtu awahi hospitali?

Ikiwa damu inaendelea zaidi ya siku 2–3, inajirudia, au inaambatana na uchovu, kupungua uzito au mkojo kubadilika rangi sana, ni muhimu kumwona daktari mara moja.

3. Kichocho kinaweza kusababisha damu kwa muda mrefu hata baada ya matibabu?

Ndiyo. Kichocho kinaweza kuacha vidonda au uharibifu wa kudumu kwenye kibofu, hivyo damu inaweza kuendelea kutoka hata baada ya kimelea kuondoka.

4. Vipimo gani vinaweza kukosa kugundua chanzo cha damu kwenye mkojo?

Vipimo vya awali kama ultrasound ya kawaida au urine routine vinaweza kukosa mawe madogo, vidonda vya ndani ya kibofu au magonjwa ya figo ya ndani.

5. Je, mkojo wenye damu kila wakati ni maambukizi (UTI)?

Hapana. Ingawa UTI ni sababu ya kawaida, damu inaweza pia kusababishwa na figo, tezi dume, mishipa ya damu au hata dawa fulani.

6. Kukojoa damu kuna uhusiano gani na shinikizo la damu au kisukari?

Magonjwa haya huweza kuharibu mishipa midogo ya damu ya figo, na kusababisha damu kuvuja kwenye mkojo bila dalili nyingine za awali.

7. Je, mtu anaweza kukojoa damu bila kuhisi chochote kibaya?

Ndiyo. Baadhi ya watu hawahisi maumivu, homa wala kichefuchefu, lakini damu huonekana ghafla—hali hii ni ishara muhimu ya kuchunguzwa.

8. Dawa za kawaida kama za maumivu zinawezaje kuleta damu kwenye mkojo?

Matumizi ya muda mrefu ya dawa za maumivu huweza kuathiri figo au kusababisha michubuko midogo ya ndani, na hivyo kusababisha hematuria.

9. Kukojoa damu kunaweza kuhusiana na shughuli nzito au mazoezi makali?

Ndiyo, mazoezi makali au kazi nzito zinaweza kuchochea damu kutoka hasa kama kuna tatizo lililojificha kwenye figo au kibofu.

10. Ni lini rufaa kwa daktari bingwa inakuwa muhimu?


Ikiwa damu haijaisha baada ya matibabu ya awali, au inajirudia mara kwa mara, ni muhimu kumuona urologist au nephrologist kwa uchunguzi wa kitaalamu zaidi.


ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

Imeandikwa,

7 Januari 2026, 08:46:51

Rejea za mada hii

  1. Grossfeld GD, et al. Evaluation of asymptomatic microscopic hematuria in adults. J Urol. 2001;165(2):441–445.

  2. Davis R, et al. Hematuria: diagnosis and management. Am Fam Physician. 2012;85(11):1153–1160.

  3. Copley JB. Persistent hematuria: causes and evaluation. Clin Med. 2018;18(3):242–245.

  4. Johnson EK, et al. Imaging in hematuria. Radiol Clin North Am. 2017;55(2):327–345.

  5. Glassock RJ. Glomerular causes of hematuria. Clin J Am Soc Nephrol. 2010;5(3):441–448.

bottom of page