Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Lugonda B, MD
Imeboreshwa:
20 Oktoba 2025, 11:09:17

Kutokwa na jasho wakati wa usiku: Visababishi Uchunguzi na Tiba
Kutokwa na jasho ni njia ya kawaida ya mwili kupunguza joto na kudhibiti hali ya hewa ya ndani ya mwili. Hata hivyo, watu wengine hupata hali isiyo ya kawaida ambapo hutoka jasho jingi wakati wa usiku, mara nyingine bila hata joto au blanketi zito.Jasho hili linaweza kulowanisha mavazi na mashuka, na humuamsha mtu usingizini mara kadhaa. Wakati mwingine ni tatizo dogo, lakini pia linaweza kuwa ishara ya matatizo makubwa ya kiafya kama vile maambukizi, mabadiliko ya homoni au saratani fulani.
Tofauti kati ya jasho kawaida na jasho lisilo kawaida
Ni muhimu kutofautisha kati ya:
Jasho la kawaida: Hutokea unapolala kwenye mazingira ya joto, chumba kisicho na hewa, au umevaa nguo nzito.
Jasho la ugonjwa: Hutokea hata kama chumba ni baridi, na linaweza kuambatana na dalili nyingine za ugonjwa.
Dalili kuu za jasho la ugonjwa (lisilo la kawaida) ni pamoja na:
Jasho jingi linaloamsha usingizi,
Linatokea mara kwa mara (zaidi ya mara 2 kwa wiki),
Linahusiana na homa, kikohozi, au kupungua uzito,
Linahusiana na mapigo ya moyo kwenda kasi au wasiwasi mkali.
Visababishi
Sababu za kutokwa na Jasho usiku ni pamoja na;
1. Mabadiliko ya Homoni
Mabadiliko ya homoni mwilini yana athari kubwa kwenye joto na mzunguko wa damu.
Wanawake walio katika kipindi cha ukomo wa hedhi (Komahedhi) hupata jasho usiku kutokana na kushuka kwa homoni ya estrojeni. Hali hii inaweza kuambatana na hisia za moto ghafla (hot flashes).
Wanaume wenye upungufu wa homoni ya testosterone pia wanaweza kupata jasho la usiku.
Magonjwa ya tezi (hyperthyroidism) huongeza kasi ya metaboli na joto la mwili, hivyo kusababisha jasho jingi.
2. Maambukizi
Baadhi ya maambukizi ya muda mrefu husababisha mwili kuongeza joto ili kupambana na vimelea, jambo linalosababisha jasho usiku.Mifano ni:
Kifua kikuu (TB) – mojawapo ya sababu maarufu Afrika Mashariki; huambatana na kikohozi, homa, na kupungua uzito.
Virusi vya UKIMWI (HIV/AIDS) – husababisha jasho usiku katika hatua za awali na za baadaye.
Maambukizi ya bakteria sugu kama endokadaitiz (maambukizi ya moyo), osteomyelitis (maambukizi ya mifupa), na jipu la ndani.
Malaria sugu inaweza pia kuleta jasho usiku linalorudi-rudi.
3. Saratani na Magonjwa ya Damu
Baadhi ya aina za saratani hasa zile zinazohusisha mfumo wa damu huchochea jasho usiku.
Limphoma na Leukemia ni saratani zinazojulikana kwa kusababisha jasho jingi usiku, homa na kupungua uzito.
Wagonjwa wenye saratani ya mapafu, kongosho, au figo wanaweza pia kuonyesha dalili hii katika hatua za awali.
4. Dawa Zisizo na Madhara Makubwa Lakini Zinaweza Kuongeza Jasho
Baadhi ya dawa huathiri mfumo wa neva wa mwili unaodhibiti jasho. Mfano:
Dawa za antidepressant (hasa SSRIs na tricyclic antidepressants),
Aspirin, acetaminophen, na dawa za homa,
Dawa za kisukari kama insulin na sulfonylureas,
Dawa za steroid na opioid.Ikiwa umeanza kutumia dawa mpya na ukaanza kupata jasho usiku, ni muhimu kumjulisha daktari wako.
5. Sababu za kisaikolojia
Hisia kali na msongo wa mawazo (msongo, hofu, au ndoto za kutisha) huongeza homoni za adrenaline na kortisol mwilini, ambazo huchochea jasho hata ukiwa umelala. Watu wenye matatizo ya usingizi au ndoto za kutisha mara kwa mara wanaweza kupata hali hii.
6. Sababu nyingine za kawaida
Kula vyakula vyenye pilipili au viungo vikali kabla ya kulala,
Kunywa pombe au kafeini usiku,
Kuvuta sigara,
Unene uliopitiliza,
Kuvaa nguo nzito au kutumia mashuka mazito,
Matatizo ya usingizi kama sleep apnea (kupumua kukatakata wakati wa usingizi).
Dalili
Dalili zinazoweza kuambatana na jasho usiku hutegemea chanzo, unaweza kupata:
Homa na baridi kali,
Kupungua uzito bila sababu,
Kikohozi kisichoisha,
Maumivu ya kifua,
Mapigo ya moyo kwenda kasi,
Kichefuchefu au maumivu tumboni,
Uchovu mkubwa,
Hisia za wasiwasi au huzuni.
Uchunguzi wa tatizo
Daktari ataanza kwa kuchukua historia kamili ya afya yako na kufanya uchunguzi wa mwili. Vipimo vinaweza kujumuisha:
Vipimo vya damu – kupima wingi wa seli, kazi za ini na figo, na hali ya homoni.
X-ray ya kifua – kubaini kifua kikuu au saratani ya mapafu.
Vipimo vya tezi thairoid – kubaini kama kuna haipatharoidism.
Kipimo cha HIV na malaria kulingana na historia yako.
CT scan au ultrasound – iwapo kuna shaka ya saratani au jipu.
Matibabu
Matibabu yanategemea chanzo kilichosababisha tatizo:
1. Mabadiliko ya Mtindo wa Maisha
Lala katika chumba chenye hewa ya kutosha na joto la wastani.
Tumia mashuka na mavazi mepesi.
Epuka pombe, sigara, na vinywaji vyenye kafeini kabla ya kulala.
Punguza vyakula vyenye pilipili au mafuta mengi usiku.
Fanya mazoezi kwa utaratibu ili kupunguza msongo wa mawazo.
2. Matibabu ya ugonjwa wa msingi
Kifua kikuu → dawa kamili za TB kwa muda uliopendekezwa.
HIV → tiba ya ARVs na ufuatiliaji wa karibu.
Haipatharoidism → dawa za kudhibiti tezi (kama carbimazole) au matibabu ya mionzi.
Komahedhi → tiba ya homoni (HRT) au tiba asilia kama soya na flaxseed chini ya ushauri wa daktari.
Saratani → tiba ya mionzi, dawa au upasuaji kutegemea hatua.
3. Dawa za kudhibiti jasho
Kama hakuna chanzo kikubwa, daktari anaweza kupendekeza:
Dawa za antiperspirant zenye aluminium chloride,
Dawa za kupunguza shughuli za neva (anticholinergic),
Au tiba ya sindano ya Botox kwa jasho sugu (hutokea kwa nadra).
Wakati wa kumwona daktari haraka
Ni muhimu kupata msaada wa kitabibu ikiwa:
Unatoka jasho jingi kila usiku bila sababu inayoeleweka,
Unapoteza uzito au unapata homa mara kwa mara,
Una kikohozi kinachoendelea zaidi ya wiki mbili,
Unahisi uchovu uliokithiri au mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida,
Una historia ya saratani, TB, au HIV.
Madhara ya kupuuzia tatizo
Kupuuzia jasho la usiku kunaweza kusababisha:
Kupoteza maji mwilini,
Kukosa usingizi mzuri na uchovu wa kudumu,
Kuchelewesha utambuzi wa magonjwa makubwa kama TB au saratani,
Kuathiri afya ya akili kwa wasiwasi unaoendelea.
Namna ya kujitunza nyumbani
Kunywa maji ya kutosha mchana kutunza uwiano wa maji mwilini.
Epuka kula mara nyingi sana kabla ya kulala.
Hakikisha chumba ni safi, tulivu, na baridi kidogo.
Tumia matandiko ya pamba ambayo husaidia ngozi kupumua.
Epuka pombe na uvutaji sigara.
Fanya uchunguzi wa afya mara kwa mara.
Hitimisho
Kutokwa na jasho wakati wa usiku ni dalili, siyo ugonjwa. Wakati mwingine hutokana na mambo madogo kama joto au msongo wa mawazo, lakini pia linaweza kuwa ishara ya ugonjwa mkubwa kama kifua kikuu, saratani au matatizo ya homoni.Kama tatizo linaendelea au linaambatana na dalili zingine, usisite kumwona daktari. Tiba mapema inaweza kuokoa maisha na kuboresha usingizi wako.
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
Imeandikwa,
20 Oktoba 2025, 11:03:19
Rejea za mada hii
Mold JW, Holtzclaw BJ, Barton ED. Night sweats: a systematic review of the literature. J Am Board Fam Med. 2012;25(6):878–893.
Viera AJ, Bond MM. Diagnosis of night sweats. Am Fam Physician. 2015;91(11):736–741.
NHS. Night sweats. [Internet]. 2023 [cited 2025 Oct 20]. Available from: https://www.nhs.uk
Mayo Clinic. Night sweats: causes. [Internet]. 2024 [cited 2025 Oct 20]. Available from: https://www.mayoclinic.org
World Health Organization (WHO). Tuberculosis: symptoms and diagnosis. Geneva: WHO; 2023.
