top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Mangwella S, MD

Imeboreshwa:

15 Julai 2025, 10:35:55

Kuwashwa wakati wa kukojoa kwa wanawake: Sababu, Tiba na Tahadhari

Kuwashwa wakati wa kukojoa kwa wanawake: Sababu, Tiba na Tahadhari

Swali la msingi

"Habari Daktari, mimi ni msichana wa miaka 22. Kwa miezi kadhaa sasa, kila nikikojoa nahisi kuwashwa sana ukeni hadi najikuna bila kujizuia na mwisho napata maumivu makali kwenye ngozi ya eneo hilo. Nimebadili sabuni, nimejaribu kujisafisha zaidi lakini hali bado haijabadilika. Sina uhakika kama ni maambukizi au tatizo jingine. Naomba msaada – je, hali hii inasababishwa na nini na naweza kupata tiba gani?"


Majibu

Kuwashwa au kujikuna wakati wa kukojoa ni dalili inayowasumbua wanawake wengi, hasa vijana. Inaweza kuwa ya muda mfupi au dalili ya maambukizi yanayohitaji matibabu. Makala hii inaeleza kwa lugha rahisi sababu zinazowezekana, tiba na wakati wa kumwona daktari.


Dalili hii inamaanisha nini?

Kuwashwa wakati wa kukojoa mara nyingi huashiria tatizo katika mfumo wa mkojo au maeneo ya uke na mashavu ya nje ya uke. Hali hii inaweza kuwa:

  • Ya muda mfupi (mfano baada ya kutumia sabuni yenye kemikali kali)

  • Ya kuashiria maambukizi (mfano UTI au fangasi)


Visababishi

Baadhi ya visababishi vikuu vinavyochangia ni kama vilivyoorodheshwa kwenye jedwali linalofuata;

Sababu

Maelezo

Maambukizi ya njia ya mkojo (UTI)

Sababu kubwa ya kuwashwa au kuchoma wakati wa kukojoa; huambatana na haja ndogo ya mara kwa mara

Fangasi ukeni (Kandida)

Kuwashwa mkali, uchafu mweupe kama jibini, na wekundu wa ngozi ya uke

Sabuni au kemikali kali

Sabuni za kusafisha ukeni au kubadilisha harufu huleta muwasho

Maambukizi ya magonjwa ya zinaa

Kama Klamidia, trikomoniasis au gonorea – husababisha muwasho na maumivu

Kukojoa mkojo wenye tindikali kali (asidi)

Mkojo mkali kutokana na vyakula, upungufu wa maji mwilini au kisukari

Mabadiliko ya homoni (hasa kwa vijana na wajawazito)

Huathiri unyevu wa uke na kuleta muwasho kwa urahisi


Dalili zinazoambatana

Dalili zinazoambatana na muwasho wakati w akukojoa mara nyingi huwa pomoja na;

  • Kuwashwa au kuchoma wakati wa kukojoa

  • Kujikuna hadi kupata michubuko

  • Harufu isiyo ya kawaida ukeni

  • Mkojo kuwa wa njano sana au na harufu kali

  • Kutokwa na uchafu ukeni (nyeupe, kijani au njano)

  • Maumivu ya tumbo la chini


Matibabu ya muwasho wakati wa kukojoa


Matibabu ya muwasho wakati wa kukojoa hutegemea kisababishi, baadhi yake yameandikwa kwenye jedwali linalofuata;

Sababu

Tiba inayopendekezwa

UTI

Dawa za antibaiotiki kama Nitrofurantoin au Ciprofloxacin (kwa maelekezo ya daktari)

Fangasi

Dawa za fangasi kama Fluconazole au krimu za Clotrimazole

Sabuni/kichocheo cha nje

Acha kutumia sabuni zenye manukato makali au dawa za kusafisha uke

Magonjwa ya zinaa

Dawa maalum kulingana na aina ya maambukizi na kama utakavyoandikiwa na daktari (kama azithromycin, metronidazole, ceftriaxon n.k)

Tindikali nyingi kwenye mkojo

Kunywa maji mengi, epuka vyakula vyenye asidi nyingi (soda, kahawa, pilipili)

Usitumie dawa bila kupima au kuagizwa na daktari. Unaweza kuzidisha tatizo au kuchelewesha tiba sahihi.

Lini umwone daktari haraka?

  • Maumivu au muwasho unazidi kila siku

  • Mkojo una damu

  • Kutokwa na uchafu wenye harufu kali

  • Una historia ya ngono bila kinga

  • Hali haibadiliki hata baada ya kujitibu nyumbani


Njia za kujikinga na kuwashwa wakati wa kukojoa

Hatua ya kinga

Maelezo

Kunywa maji ya kutosha

Husaidia kusafisha njia ya mkojo

Safisha uke kwa maji tu

Usitumie sabuni zenye manukato au vitakaso(viua bakteria)

Jisafishe kutoka mbele kwenda nyuma

Kuepuka kuhamisha bakteria kutoka haja kubwa kwenda kwenye uke

Vaa nguo za ndani zisizobana, zisizochochea joto

Vaa nguo safi, na za pamba

Epuka kufanya ngono bila kinga

Zuia maambukizi ya zinaa

Badili pedi au nguo za ndani mara kwa mara

Kuzuia unyevu na vijidudu

Hitimisho

Kuwashwa wakati wa kukojoa kwa binti au mwanamke si hali ya kawaida na mara nyingi huashiria maambukizi ya njia ya mkojo, fangasi au matumizi ya bidhaa zenye kemikali kali. Usisite kumwona daktari endapo hali hii inaendelea au inasababisha maumivu makali. Matibabu sahihi huanza na uchunguzi wa sababu.

ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

Imeandikwa,

15 Julai 2025, 10:35:55

Rejea za mada hii

  1. Hooton TM. Clinical practice: uncomplicated urinary tract infection. N Engl J Med. 2012;366(11):1028-37.

  2. Sobel JD. Vulvovaginal candidiasis. Lancet. 2007;369(9577):1961–71.

  3. Workowski KA, Bachmann LH, et al. Sexually transmitted infections treatment guidelines, 2021. MMWR Recomm Rep. 2021;70(4):1-187.

  4. Centers for Disease Control and Prevention. UTIs in Women. [Internet]. 2022.

  5. Mayo Clinic. Painful urination (dysuria) - causes. 2023.

  6. Gupta K et al. International clinical practice guidelines for the treatment of acute uncomplicated cystitis. Clin Infect Dis. 2011;52(5):e103–e120.

  7. American College of Obstetricians and Gynecologists. Vaginitis. 2020.

bottom of page