top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

ULY CLINIC

Imeboreshwa:

27 Februari 2026, 00:00:52

Maumivu ya mrija wa kutoa mkojo kwa wanaume

Maumivu ya mrija wa kutoa mkojo kwa wanaume

Maumivu ya mrija wa kutoa mkojo kwa wanaume ni hali inayohusisha hisia za kuwaka, kuchoma, kuuma au usumbufu kwenye mrija unaobeba mkojo kutoka kibofu cha mkojo hadi nje ya mwili. Kwa lugha ya kitabibu, hali hii mara nyingi huhusishwa na yurethraitisi (uvimbe wa yurethra) au maambukizi ya mfumo wa mkojo.


Dalili hii ni ya kawaida katika huduma za msingi na kliniki za magonjwa ya zinaa. Inaweza kuwa dalili rahisi inayotibika haraka au ishara ya tatizo kubwa zaidi kama maambukizi ya tezi dume au magonjwa ya zinaa.


Ufafanuzi na anatomia muhimu

Mrija wa yurethra kwa wanaume ni mrija mrefu unaopita ndani ya uume na pia hupitia kwenye tezi dume. Kazi zake ni:

  • Kupitisha mkojo kutoka kibofu

  • Kupitisha shahawa wakati wa kumwaga

Kwa sababu ya urefu na muundo wake, yurethra ya mwanaume inaweza kuathiriwa na maambukizi au uvimbe katika sehemu mbalimbali.


Dalili zinazoweza kuambatana

Mgonjwa anaweza kuwasilisha:

  • Maumivu au kuwaka wakati wa kukojoa (disiyuria)

  • Kuwasha au hisia ya kuchoma ndani ya uume

  • Kutokwa na uchafu kwenye uume (mweupe, wa manjano au wa kijani)

  • Maumivu wakati wa kumwaga shahawa

  • Kukojoa mara kwa mara

  • Homa (ikiwa maambukizi ni makali)

  • Maumivu ya chini ya tumbo au kwenye korodani


Dalili za maumivu ya Mrija wa Mkojo kwa Wanaume huonekana wakati gani?

Maumivu ya mrija wa kutoa mkojo kwa wanaume yanaweza kujitokeza katika nyakati tofauti kulingana na chanzo cha tatizo. Muda au hali ambayo maumivu hutokea husaidia sana kubaini sababu ya msingi. Jedwali namba 1 linamaelezo zaidi.


Jedwali 1 Wakati wa kuonekana kwa maumivu ya mrija wa kutoa mkojo kwa wanaume

Wakati wa kutokea kwa maumivu

Hisia za maumivu

Visababishi vinavyowezekana

Wakati wa kukojoa (Dysuria)

Kuwaka, kuchoma, maumivu yanayoanzia mwanzo au mwisho wa kukojoa

Urethritis, UTI, magonjwa ya zinaa kama Gono na klamidia

Wakati umekaa tu (bila kukojoa)

Maumivu ya kuchoma kidogo, kubana au kukereketa; huja na kupotea

Prostataitisi, uchokonozi wa yurethra, makovu kwenye yurethra, msongo wa misuli ya nyonga

Wakati wa kubana au kushika uume

Maumivu yanayoongezeka unapobonyeza au kushika

Uvimbe wa yurethra, maambukizi ya ndani ya mrija, jeraha au msuguano

Wakati wa kufanya ngono

Maumivu wakati wa kuingiza, msuguano au baada ya tendo

Urethritis, maambukizi ya zinaa, ukavu au msuguano mkali, jeraha la mrija

Wakati wa kufika kileleni (kumwaga shahawa)

Maumivu makali ndani ya mrija au nyonga, yanaweza kuendelea baada ya kumwaga

Prostatitis, urethritis, maambukizi ya mfumo wa uzazi, kuziba kwa mirija ya shahawa

Wakati wa kuanza kukojoa baada ya kushikilia muda mrefu

Kuwaka au maumivu ya ghafla mwanzoni mwa mkojo

Uvimbe wa yurethra, UTI, kuwashwa kwa ndani, mkojo wenye asidi zaidi


Vidokezo muhimu vya kitaalamu

  • Maumivu mwanzoni mwa kukojoa mara nyingi huhusiana na yurethra.

  • Maumivu mwisho wa kukojoa yanaweza kuashiria tatizo la kibofu cha mkojo.

  • Maumivu yanayoongezeka wakati wa kukaa muda mrefu mara nyingi huhusiana na tezi dume

  • Maumivu wakati wa kumwaga mara nyingi huashiria tatizo la tezi dume kuliko yurethra pekee.



Visababishi vya maumivu ya mrija wa mkojo kwa wanaume

Maumivu ya mrija wa kutoa mkojo kwa wanaume yanaweza kusababishwa na maambukizi au hali nyingine zisizo za maambukizi. Kutambua chanzo halisi husaidia kupanga matibabu sahihi na kuzuia madhara ya muda mrefu kama utasa au maambukizi kusambaa. Jedwali 2 linamaelezo zaidi kuhusu visababishi vikuu.



Jedwali 2: Visababishi vikuu vya maumivu ya mrija wa mkojo kwa wanaume

Kundi la kisababishi

Ugonjwa

Maelezo muhimu

Dalili kuu

Magonjwa ya zinaa

Gono

Husababishwa na bakteria Neisseria gonorrhoeae

Uchafu wa kijani/manjano, maumivu makali wakati wa kukojoa


Klamidia

Maambukizi ya bakteria yanayoweza kuwa na dalili hafifu

Kuwaka wakati wa kukojoa, uchafu mweupe

Maambukizi ya njia ya mkojo (UTI)

UTI kwa wanaume

Nadra kwa vijana, kawaida zaidi kwa wazee

Kuwaka wakati wa kukojoa, kukojoa mara kwa mara

Maambukizi ya tezi dume

Prostataitisi

Uvimbe au maambukizi ya tezi dume

Maumivu ya mrija, maumivu ya nyonga, homa, maumivu wakati wa kukaa


Watu walio kwenye hatari zaidi ya UTI:

  • Wazee

  • Wenye tezi dume iliyovimba

  • Wenye kisukari


Visababishi vingine vya maumivu ya mrija wa kutolea mkojo kwa wanaume

Jedwali 3 lina Hivi ni visababishi visivyo vya moja kwa moja vya maambukizi lakini vinaweza kuleta maumivu au muwasho kwenye yurethra.


Jedwali 3: Visababishi vingine vya Maumivu ya Mrija wa Mkojo kwa Wanaume

Kisababishi

Maelezo

Dalili zinazoweza kuonekana

Uchokonozi kwenye mrija yurethra kutokana na sabuni kemiklai n.k

Muwasho kutokana na sabuni, kemikali au vilainishi

Kuwaka bila uchafu

Jeraha la mrija

Msuguano mkali wakati wa ngono au kujichua

Maumivu yanayoongezeka unapobana uume

Kusinyaa kwa mrija yurethra

Mrija kuwa mwembamba kutokana na kovu

Mkojo kutoka kwa shida, maumivu

Jiwe kwenye njia ya mkojo

Jiwe kusogea kwenye yurethra

Maumivu makali ya ghafla

Msongo wa misuli ya nyonga

Misuli kukaza kupita kiasi

Maumivu ya ndani yanayokuja na kupotea

Kuingiziwa mpira wa mkojo

Kuwahi kuwekewa mpira wa mkojo

Kuwaka au muwasho wa muda

Vihatarishi

Vihatarishi ni hali au tabia zinazoongeza uwezekano wa kupata maambukizi au uvimbe wa mrija wa kutoa mkojo. Kwa wanaume wengi, vihatarishi hivi vinahusiana na maambukizi ya bakteria, hasa magonjwa ya zinaa na maambukizi ya njia ya mkojo.

Kihatarishi

Jinsi kinavyoongeza hatari

Ngono isiyo salama

Huongeza uwezekano wa maambukizi ya magonjwa ya zinaa

Wapenzi wengi

Huongeza hatari ya kuambukizwa na kuambukiza

Historia ya magonjwa ya zinaa

Huongeza uwezekano wa maambukizi kurudi au kovu

Kinga dhaifu

Maambukizi hutokea kwa urahisi na hudumu

Kisukari

Huchochea ukuaji wa bakteria na kupunguza kinga

Kutotibu mapema

Hupelekea maambukizi sugu na madhara ya muda mrefu


Uchunguzi wa Kitabibu


Kwa wagonjwa

Ni muhimu kumwona mtoa huduma wa afya mapema, hasa kama:

  • Kuna uchafu ukeni

  • Kuna homa

  • Maumivu yanaongezeka

  • Kuna damu kwenye mkojo


Kwa wataalamu wa Afya


Historia ya mgonjwa

  • Mwanzo wa dalili

  • Historia ya ngono

  • Matumizi ya kondomu

  • Dalili za mfumo mzima (fever, chills)


Uchunguzi wa Mwili

  • Angalia uchafu kwenye yurethra

  • Bonyeza yurethra kuona kama kuna uchafu unaotoka

  • Pima tezi dume kwa DRE kama inahitajika


Vipimo

  • Kipimo cha uchunguzi wa jumla wa mkojo

  • Kipimo cha kuotesha vimelea kutoka kwenye mkojo

  • Kipimo cha ute unaotoka kwenye uume kwa magonjwa ya zinaa

  • Kipimo cha NAAT kwa Gono na Klamidia


Matibabu

Matibabu hutegemea chanzo.


A. Magonjwa ya zinaa

Kwa kawaida hutibiwa kwa antibayotiki maalum kulingana na miongozo ya kitaifa. Wagonjwa wanapaswa:

  • Kumaliza dozi yote

  • Kumjulisha mwenzi wake

  • Kuepuka ngono hadi watakapomaliza matibabu


B. UTI

Antibiotiki kulingana na kipimo cha kuotesha vimelea na kuangalia dawa inayowadhuru.


C. Prostataitisi

  • Antibiotiki za muda mrefu (wiki 2–6 kulingana na aina)

  • Dawa za maumivu

  • Wakati mwingine dawa jamii ya vifunga alpha


D. Sababu zisizo za maambukizi

  • Epuka kemikali zinazosababisha muwasho

  • Tibu jiwe au kusinyaa kwa mrija wa mkojo kulingana na chanzo


Madhara yanayoweza kutokea

Ikiwa haitatibiwa mapema:

  • Kuenea kwa maambukizi hadi kwenye korodani (epididimaitisi)

  • Maambukizi kuingia kwenye damu

  • Kusinyaa kwa mrija wa mkojo

  • Utasa (hasa kwa magonjwa ya zinaa yasiyotibiwa)


Makundi maalum


Wazee

Maumivu yanaweza kuhusiana na kuvimba kwa tezi dume (Tezi dume au prostataitisi).


Wenye kisukari

Wapo kwenye hatari kubwa ya maambukizi sugu.



Vijana walio kwenye ngono hai

Chanzo kikubwa mara nyingi ni magonjwa ya zinaa.



Elimu kwa mgonjwa

Ili kupona haraka na kuzuia madhara au maambukizi kurudi, zingatia ushauri huu muhimu:

  • Tumia kondomu kila mara unapofanya ngono ili kujikinga na magonjwa ya zinaa kama Gono na Klamidia.

  • Epuka kujitibu bila vipimo. Dawa zisizofaa zinaweza kuficha dalili au kuongeza usugu wa antibiotiki.

  • Maliza dozi yote ya dawa hata kama maumivu yamepungua; kuacha njiani kunaweza kusababisha maambukizi kurudi.

  • Rudi hospitali ikiwa dalili hazipungui ndani ya siku 3–5 au zinaongezeka.

  • Epuka kufanya ngono hadi upone kabisa na, ikiwa ni maambukizi ya magonjwa ya zinaa, hakikisha mwenzi wako pia amepimwa na kutibiwa.

Kufuata ushauri huu husaidia kuzuia maambukizi sugu, utasa, na kuambukizana tena.


Dalili za hatari

Ingawa maumivu ya mrija wa kutoa mkojo mara nyingi husababishwa na maambukizi ya kawaida yanayotibika, kuna dalili fulani za hatari zinazoashiria uwezekano wa maambukizi makubwa au tatizo linaloweza kuhatarisha afya au hata maisha. Dalili hizi zinahitaji uchunguzi na rufaa ya haraka hospitalini.

  • Homa kali

  • Maumivu makali ya korodani

  • Damu kwenye mkojo

  • Kushindwa kukojoa

  • Maumivu makali ya nyonga

Hizi zinahitaji rufaa ya haraka.


Muhtasari wa kitaalamu (Kwa watoa Huduma)

Dalili ya hatari

Inaashiria nini

Hatua ya kuchukua

Homa kali

Maambukizi makali au kusambaa kwa sumu ya vimelea kwneye damu

Rufaa ya haraka, vipimo vya damu

Maumivu makali ya korodani

Epididymitis au torsion

Tathmini ya dharura

Damu kwenye mkojo

Jiwe, maambukizi au jeraha

Uchunguzi wa haraka

Kushindwa kukojoa

Retention ya mkojo

Kuwekewa mpira wa mkojo kwa dharura

Maumivu makali ya nyonga

Prostataitisa kali

Rufaa na antibiotiki za haraka


Hitimisho

Maumivu ya mrija wa kutoa mkojo kwa wanaume ni dalili muhimu inayoweza kuashiria maambukizi ya kawaida au tatizo kubwa zaidi. Uchunguzi wa mapema, vipimo sahihi na matibabu stahiki huzuia madhara ya muda mrefu kama utasa au maambukizi makali.



Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake

1. Maumivu ya mrija wa kutoa mkojo kwa wanaume husababishwa na nini?

Maumivu ya mrija wa kutoa mkojo kwa wanaume mara nyingi husababishwa na:

  • Maambukizi ya bakteria

  • Magonjwa ya zinaa kama Gono

  • Klamidia

  • Maambukizi ya njia ya mkojo (UTI)

  • Maambukizi ya tezi dume (prostataitisi)

  • Kuwashwa na kemikali au sabuni

  • Kuumia wakati wa ngono

Sababu kuu kwa wanaume vijana wenye ngono hai mara nyingi ni magonjwa ya zinaa.

2. Je, maumivu wakati wa kukojoa ni dalili ya ugonjwa wa zinaa?

Ndiyo, maumivu wakati wa kukojoa (disiyuria) yanaweza kuwa dalili ya ugonjwa wa zinaa, hasa kama yanaambatana na:

  • Uchafu kutoka kwenye uume

  • Kuwasha au kuungua

  • Maumivu wakati wa kumwaga shahawa

Hata hivyo, si kila maumivu ya kukojoa ni maambukizi ya magonjwa ya zinaa — yanaweza pia kuwa UTI au maambukizi kwenye tezi dume (prostataitisi). Vipimo ni muhimu kuthibitisha chanzo.

3. Nitajuaje kama nina yurethraitisi?

Dalili kuu za yurethraitisi (uvimbe wa mrija wa mkojo) ni:

  • Kuwaka au kuchoma wakati wa kukojoa

  • Kutokwa na uchafu kwenye uume

  • Kuwasha ndani ya mrija

  • Maumivu wakati wa kumwaga

Yurethraitisi mara nyingi husababishwa na gono au Klamidia, lakini pia inaweza kuwa isiyo ya maambukizi.

4. Je, maumivu ya mrija wa mkojo yanaweza kuisha yenyewe bila matibabu?

Wakati mwingine dalili zinaweza kupungua kwa muda, lakini ikiwa chanzo ni bakteria au ugonjwa wa zinaa, maambukizi hayawezi kuisha kabisa bila antibiotiki sahihi.

Kutotibu kunaweza kusababisha:

  • Maambukizi kusambaa hadi korodani

  • Urethra kuwa mwembamba (makovu kwenye mrija wa mkojo)

  • Utasa

Ni muhimu kufanyiwa vipimo kabla ya kutumia dawa.

5. Je, maumivu ya mrija wa mkojo bila uchafu yanaweza kuwa maambukizi ya magonjwa ya zinaa?

Ndiyo. Hasa kwa maambukizi ya Klamidia, dalili zinaweza kuwa hafifu au bila uchafu mkubwa.

Mtu anaweza kuwa na:

  • Kuwaka wakati wa kukojoa

  • Maumivu ya chini ya tumbo

  • Dalili chache sana

Hii ndiyo sababu vipimo vya maabara ni muhimu hata kama dalili ni ndogo.

6. Maumivu ya mrija wa mkojo yanaweza kusababisha utasa kwa mwanaume?

Ndiyo, ikiwa hayatatibiwa mapema. Maambukizi ya muda mrefu yanaweza kusababisha:

  • Epididimaitisi (uvimbe wa mirija ya mbegu)

  • Kuziba kwa njia ya mbegu

  • Uharibifu wa mfumo wa uzazi

Matibabu ya mapema hupunguza hatari ya utasa.

7. Ni lini niende hospitali kwa maumivu ya mrija wa mkojo?

Unapaswa kwenda hospitali mara moja ikiwa una:

  • Homa kali

  • Maumivu makali ya korodani

  • Damu kwenye mkojo

  • Kushindwa kukojoa

  • Maumivu makali ya nyonga

Hizi ni dalili za hatari zinazoweza kuashiria maambukizi makubwa.

8. Je, naweza kutumia antibayotiki bila vipimo kwa maumivu ya mrija wa mkojo?

Haishauriwi kutumia antibiotiki bila vipimo au ushauri wa daktari.

Sababu:

  • Unaweza kutumia dawa isiyofaa

  • Bakteria wanaweza kuwa sugu kwa dawa

  • Dalili zinaweza kuficha tatizo kubwa zaidi

Matumizi holela ya antibayotiki huongeza usugu wa vimelea kwenye dawa.

9. Je, mke au mwenzi wangu anapaswa kutibiwa pia kama ninapata matibabu ya maumivu ya mrija wa mkojo?

Ndiyo. Ikiwa chanzo ni ugonjwa wa zinaa kama gonorrhea au klamidia:

  • Wapenzi wote wanapaswa kupimwa

  • Wote watibiwe hata kama hawana dalili

  • Epuka ngono hadi wote mkamilishe matibabu

Hii huzuia kurudiana kwa maambukizi.

10. Nawezaje kuzuia maumivu ya mrija wa mkojo kwa wanaume?

Njia bora za kinga ni:

  • Kutumia kondomu kila mara

  • Kuwa na mwenzi mmoja mwaminifu

  • Kufanya vipimo vya maambukizi ya magonjwa ya zinaa mara kwa mara

  • Kuepuka kujitibu bila ushauri wa kitaalamu

  • Kutibu maambukizi mapema

Kinga ni rahisi na nafuu kuliko matibabu ya madhara ya muda mrefu.


ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

Imeandikwa,

26 Februari 2026, 13:16:12

Rejea za mada hii

  1. Workowski KA, Bachmann LH, Chan PA, Johnston CM, Muzny CA, Park I, et al. Sexually transmitted infections treatment guidelines, 2021. MMWR Recomm Rep. 2021;70(4):1–187.

  2. European Association of Urology (EAU). EAU Guidelines on Urological Infections 2023. Arnhem: EAU Guidelines Office; 2023.

  3. Schaeffer AJ, Nicolle LE. Urinary tract infections in older men. N Engl J Med. 2016;374(6):562–571.

  4. Krieger JN, Lee SWH, Jeon J, Cheah PY, Liong ML, Riley DE. Epidemiology of prostatitis. Int J Antimicrob Agents. 2008;31(Suppl 1):S85–S90.

  5. Taylor SN. Clinical presentation of urethritis in men. UpToDate. Waltham (MA): UpToDate Inc.; 2023.

  6. Horner PJ, Blee K, O’Mahony C, Muir P, Evans C, Radcliffe K. 2015 UK national guideline on the management of non-gonococcal urethritis. Int J STD AIDS. 2016;27(2):85–96.

  7. Lipsky BA. Prostatitis and urinary tract infection in men: What’s new; what’s true? Am J Med. 1999;106(3):327–334.

bottom of page