top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

ULY CLINIC

ULY CLINIC

20 Desemba 2025, 16:43:42

Maumivu ya uke kwenye ujauzito wa miezi nane husababishwa na nini?

Maumivu ya uke kwenye ujauzito wa miezi nane husababishwa na nini?

Swali la msingi


Naomba kufahamu kwan mama mjamzito mwenye miezi nane anapata maumivu kama kuvuta ivi kwenye uke? Maumivu ni ya kuja na kuondoka hayadumu muda mrefu.


Majibu

Kwa kuwa maumivu ni ya muda mfupi na yanakuja na kuondoka, bila kuwa makali sana, kuna uwezekano mkubwa kuwa ni ya kawaida husababishwa na:

  • Mikazo ya maandalizi (uchungu wa uongo)

  • Shinikizo la kichwa cha mtoto kwenye uke na nyonga


Haya huwa ya kawaida kabisa katika ujauzito wa miezi nane. Ni njia ya mwili kujiandaa taratibu kwa ajili ya kujifungua, lakini siyo dalili ya uchungu wa kweli.


Dalili za kutofautisha:

Maumivu ya maandalizi (uchungu wa uongo)

Maumivu ya uchungu wa kweli

Hayana mpangilio maalumu

Yana mpangilio wa mara kwa mara

Hayaongezeki ukali

Yanazidi kuwa makali

Hutulia ukibadilisha mkao au kupumzika

Hayaishi hata ukibadilisha mkao

Hakuna kutokwa damu wala maji

Yanaweza kuambatana na kutokwa damu au maji

Visababishi vingine

Maumivu ya mishipa au neva:Mtoto anapokua, uzito wake unaweza kubana mishipa au neva (hasa 'nerve pudendal'), na hii inaweza kusababisha maumivu ya kuvuta kwenye uke au nyonga.


Kuongezeka kwa mtiririko wa damu kwenye eneo la nyonga:Ujauzito huongeza damu katika maeneo ya uke na nyonga, na wakati mwingine shinikizo hili huleta hisia ya kuvutwa au maumivu madogo.


Kupishana kwa viungo vya nyonga: Homoni ya relaxin huandaa nyonga kwa kujifungua kwa kulegeza mishipa na viungo, na hii inaweza kuleta hisia za kukaza au kuvutwa sehemu ya uke.


Namna ya kupunguza maumivu hayo
  • Pumzika kwa kulala upande wa kushoto

  • Kunywa maji mengi (kiwambo cha maji mwilini kikishuka huongeza mikazo)

  • Fanya mazoezi mepesi kama kutembea taratibu

  • Fanya mazoezi ya kupumua kwa kina

  • Fanya mazoezi ya sakafu ya nyonga


Kwa ujumla, hali unayoipitia inaonekana ni ya kawaida, ila ikiwa:

  • Maumivu yataanza kuwa ya mara kwa mara na kuongezeka kwa nguvu

  • Utatokwa na damu au maji

  • Atapata maumivu makali yasiyovumilika basi usisite kwenda hospitali.


Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake

1. Je, maumivu ya uke katika ujauzito wa miezi ya mwisho yanaweza kumdhuru mtoto?

Kwa ujumla hayamdhuru mtoto endapo ni ya muda mfupi, yanakuja na kuondoka, na hayana dalili hatarishi kama kutokwa damu au maji. Mara nyingi hutokana na mabadiliko ya kawaida ya mwili kujiandaa kwa kujifungua.

2. Mimi ni mjamzito wa wiki ya 38, napata maumivu makali ukeni hasa ninapolala muda wa kugeuka, hilo ni tatizo au ni kawaida?

Hali hii ni ya kawaida sana kwa wajawazito waliokaribia kujifungua. Mara nyingi husababishwa na:

  • Shinikizo la kichwa cha mtoto kwenye mishipa ya fahamu ya uke na nyonga

  • Kupishana kwa viungo vya nyonga

  • Kubanwa kwa mishipa ya fahamu wakati wa kugeuka.

Ikiwa hakuna damu, kutokwa na maji ukeni, au uchungu wa mpangilio maalumu, hali hii siyo hatari.

3. Kwa nini maumivu ya uke huongezeka zaidi usiku au wakati wa kugeuka kitandani?

Usiku:

  • Misuli huwa imetulia zaidi

  • Mtoto hubadilisha mkao

  • Uzito wa tumbo hubana nyonga zaidiHii husababisha maumivu ya ghafla kama kuchomwa au kuvutwa.

4. Je, maumivu haya yanaweza kuwa ishara ya kujifungua karibu?

Ndiyo, yanaweza kuashiria mwili unajiandaa, lakini si dalili ya moja kwa moja ya uchungu wa kujifungua, hasa kama hayana mpangilio wa muda na hayazidi nguvu kadri muda unavyopita.

5. Ni lini maumivu ya uke yanapaswa kunitia wasiwasi?

Unapaswa kumwona mtaalamu wa afya haraka ikiwa:

  • Maumivu yanakuwa ya mara kwa mara na kuongezeka

  • Kuna kutokwa damu au maji

  • Una homa

  • Mtoto hapigi au harakati zimepungua

6. Je, kufanya tendo la ndoa kunaweza kusababisha maumivu ya uke katika miezi ya mwisho ya ujauzito?

Ndiyo, kwa baadhi ya wajawazito:

  • Uke huwa laini na una damu nyingi zaidi

  • Shinikizo huongezekaHivyo maumivu madogo yanaweza kutokea, lakini tendo la ndoa ni salama kama daktari hajakukataza.

7. Je, maumivu ya uke yana uhusiano na kufunguka kwa mlango wa uzazi?

Wakati mwingine ndiyo, hasa wiki za mwisho. Kufunguka kwa mlango wa uzazi kunaweza kuleta hisia ya maumivu au kuvutwa, lakini kufunguka kamili huambatana na uchungu wa kweli.

8. Je, kuvaa mkanda wa tumbo (maternity belt) kunaweza kusaidia?

Ndiyo. Mkanda wa tumbo:

  • Hupunguza shinikizo kwenye nyonga

  • Husaidia mgawanyo wa uzito wa tumbo

  • Hupunguza maumivu ya uke na mgongo kwa baadhi ya wajawazito

9. Je, mazoezi ya sakafu ya nyonga (Kegel exercises) ni salama wakati wa ujauzito wa miezi ya mwisho?

Ndiyo, ni salama na yana faida:

  • Huimarisha misuli ya nyonga

  • Hupunguza maumivu

  • Huandaa mwili kwa kujifunguaLakini yafanywe kwa usahihi na kwa kiasi.

10. Je, maumivu ya uke yanaweza kuashiria maambukizi wakati wa ujauzito?

Inawezekana, lakini mara nyingi huambatana na dalili nyingine, kama:

  • Kuwashwa

  • Harufu mbaya ukeni

  • Uchafu wa ajabuMaumivu peke yake bila dalili hizo mara nyingi si maambukizi.


ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

Imeandikwa,

27 Aprili 2025, 13:58:40

Rejea za mada hii

  1. Cunningham FG, Leveno KJ, Bloom SL, Spong CY, Dashe JS, Hoffman BL, et al. Williams Obstetrics. 25th ed. New York: McGraw-Hill Education; 2018.

  2. Kilpatrick SJ, Gabbe SG. Signs and symptoms of labor. In: Gabbe SG, Niebyl JR, Simpson JL, Landon MB, Galan HL, Jauniaux ERM, et al., editors. Obstetrics: Normal and Problem Pregnancies. 7th ed. Philadelphia: Elsevier; 2017. p. 255–268.

  3. American College of Obstetricians and Gynecologists (ACOG). ACOG Practice Bulletin No. 222: Management of Preterm Labor. Obstet Gynecol. 2020;135(4):e106–e119.

  4. Norwitz ER, Robinson JN, Challis JR. The control of labor. N Engl J Med. 1999;341(9):660–6.

  5. Caughey AB, Cahill AG, Guise JM, Rouse DJ. Safe prevention of the primary cesarean delivery. Am J Obstet Gynecol. 2014;210(3):179–93.

bottom of page