top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Benjamin L, MD

Imeboreshwa:

5 Desemba 2025, 09:45:16

Mtoto wa miaka 2 hajaanza kuongea: Sababu, Uchunguzi na Mambo ya Kuzingatia

Mtoto wa miaka 2 hajaanza kuongea: Sababu, Uchunguzi na Mambo ya Kuzingatia

Swali la msingi

“Daktari, mtoto wangu ana miaka 2, hajaanza kuongea maneno, na wasiwasi wangu ni kwamba labda kuna tatizo. Naomba kujua sababu na nifanye nini?”


Majibu

Kuchelewa kuongea kwa mtoto wa miaka 2 kunaweza kuwa dalili ya matatizo mbalimbali ya maendeleo ya ubongo, kusikia au mazingira. Makala hii inaeleza sababu, uchunguzi, ushauri na hatua za kuchukua kwa mzazi au mlezi.


Umri wa kuongea kwa watoto

Watoto wengi hufikia hatua za kuongea kati ya miezi 12 hadi 24. Hata hivyo, si watoto wote hufuata ratiba hiyo. Wakati mwingine kuchelewa kuongea huweza kuwa sehemu ya ukuaji wa kawaida, lakini wakati mwingine ni ishara ya changamoto ya kiafya inayohitaji uchunguzi wa kitaalamu.


Mzazi anaweza kuwa na wasiwasi endapo mtoto wake wa miaka 2 hajaanza kuzungumza au kutumia maneno yanayoeleweka.


Visababishi vya mtoto kuchelewa kuongea

Aina ya kisababishi

Maelezo

Changamoto ya kusikia(Tatizo la kusikia)

Mtoto anaweza kuwa na matatizo ya kusikia ambayo yanamzuia kujifunza au kuiga maneno. Hii inaweza kusababishwa na maambukizi ya mara kwa mara ya sikio (Maambukizi kwenye sehemu ya kati ya sikio), ulemavu wa kusikia wa kuzaliwa nao au sababu nyingine za kitabibu.

Mazingira duni ya mawasiliano

Watoto wanaoishi kwenye eneo lenye kiasi kidogo cha mazungumzo, michezo ya kuigiza, au kusomewa vitabu nyumbani, au kuwa na watoto wenzake karibu wanaweza kuchelewa kujifunza kuzungumza.

Ucheleweshwaji wa kawaida wa lugha (Kuchelewa kuzungumza)

Baadhi ya watoto huchelewa kwa kawaida bila kuwa na tatizo jingine la kimsingi. Hii mara nyingi hujirekebisha kadri wanavyoendelea kukua.

Matatizo ya neva (Ukuaji wa mfumo wa neva)

Hii ni pamoja na matatizo kama vile madhaifu ya lugha, ugonjwa wa akili kama Usonji (Autism), au mtindio wa ubongo.

Ugonjwa wa akili au kisaikolojia

Wakati mwingine msongo wa kisaikolojia, msiba, au ukatili unaweza kuchangia kuchelewa kuongea.

Kuchelewa kwa ukuaji kwa ujumla

Mtoto huyu pia atakuwa anaonyesha kuchelewa kwa hatua nyingine kama kukaa, kutembea, au kujifunza kujitegemea.


Dalili za tahadhari

Ikiwa mtoto wa miaka 2 na ana dalili zifuatazo zinapaswa kufuatiliwa kwa karibu, ni muhimu kumwona daktari mara moja;

  • Hasemi hata neno moja lenye maana (kama mama, baba, hapana)

  • Hatumii ishara au sauti kuelezea mahitaji yake

  • Haonyeshi nia ya kuwasiliana (hata kwa macho au ishara)

  • Haelewi maagizo rahisi (kama "lete mpira", "kaa chini")

  • Hatoi sauti au hutumia sauti zisizoeleweka tu

  • Haonyeshi ushirikiano wa kijamii (kama kucheka, kuangalia watu usoni)

  • Alikuwa anasema baadhi ya maneno lakini sasa ameacha kabisa



Vipimo na uchunguzi

Kwa mtoto aliyechelewa kuongea, uchunguzi ufuatao hushauriwa kufanyika

Aina ya Uchunguzi

Maelezo

Upimaji wa kusikia

Ili kuhakikisha kuwa mtoto anasikia vizuri au la.

Tathmini ya maendeleo ya mtoto

Kuangalia ikiwa mtoto anaendelea vizuri kwenye nyanja nyingine za ukuaji kama utembeaji, uchezaji, au kuelewa maelekezo.

Tathmini ya mtaalamu wa lugha na mawasiliano

Hupima uwezo wa mtoto kuwasiliana na kueleza hisia au mahitaji.

Tathmini ya magonjwa ya akili ya utotoni (Magonjwa ya mfumo wa ukuaji wa neva)

Inahusisha wataalamu kama madaktari wa magonjwa ya akili ya watoto au daktari wa mishipa ya fahamu kwa watoto.


Matibabu

Matibabu hutegemea chanzo cha kuchelewa kuongea:

  • Mazoezi ya lugha (Tiba lugha): Ni tiba kuu kwa watoto walio na tatizo la kuongea.

  • Huduma za kusaidia kusikia: Ikiwa kuna tatizo la kusikia, vifaa vya kusaidia kusikia au upasuaji wa masikio unaweza kupendekezwa.

  • Elimu ya wazazi: Mafunzo ya jinsi ya kuongeza mwingiliano wa mazungumzo na mtoto.

  • Tiba ya kitabia kwa watoto wenye Usonji: Kama ABA (Uchambuzi wa tabia ya mtoto).

  • Vikundi vya michezo ya mawasiliano: Huwasaidia watoto kwa njia ya michezo na mwingiliano na watoto wenzao.


Namna ya kumsaidia mtoto kuongea nyumbani

  • Ongea mara kwa mara na mtoto hata kama hajibu

  • Tumia vitabu vya picha, nyimbo na michezo ya sauti

  • Mpe nafasi ya kuchagua na kuelezea (kwa kutumia maneno au ishara)

  • Usimtishe au kumtania kuhusu kuchelewa kwake kuongea

  • Tumia lugha moja au mbili tu nyumbani kwa uwazi (usiweke mkanganyiko wa lugha nyingi kwa wakati mmoja)

  • Weka mazingira ya utulivu na ya mwingiliano

  • Mruhusu acheze na watoto wa rika lake


Wakati gani wa kumwona daktari haraka?

  • Ikiwa mtoto ana umri wa miaka 2 na hasemi hata neno moja

  • Ikiwa mtoto alikuwa anasema maneno kisha akaacha ghafla

  • Ikiwa mtoto haonekani kuelewa maelekezo rahisi

  • Ikiwa kuna historia ya matatizo ya kusikia, kifafa, au matatizo ya ukuaji


Hitimisho

Kuchelewa kuongea kwa mtoto wa miaka 2 si jambo la kubeza. Inaweza kuwa sehemu ya maendeleo ya kawaida, lakini pia inaweza kuwa dalili ya tatizo la kiafya linalohitaji msaada wa haraka. Uchunguzi wa mapema na msaada kutoka kwa wataalamu unaweza kusaidia mtoto kupata maendeleo bora na maisha ya kawaida.


Maswali yanayoulizwa mara kwa mara

1. Je, kuchelewa kuongea kunamaanisha mtoto ana ulemavu wa akili?

Si lazima. Watoto wengi wenye kuchelewa kuongea hukua kawaida baada ya matibabu. Lakini kuchelewa kwa muda mrefu bila msaada kunaweza kuathiri maendeleo mengine.

2. Je, kuna dawa za kuongeza uwezo wa kuzungumza?

Hakuna dawa ya kuongeza lugha. Suluhisho ni mazoezi ya mawasiliano, tiba lugha, na kutibu tatizo la msingi kama kusikia vibaya.

3. Je, mtoto wangu anaweza kuanza kuongea ghafla baada ya kuchelewa?

Ndiyo, kwa baadhi ya watoto hutokea, lakini haitabiriki. Uchunguzi na mazoezi ya mapema ni bora.

4. Ni lini nimpeleke mtoto hospitali?

Iwapo ana miaka 2 na hajaanza kusema maneno yoyote, haitiki jina, au haelewi maelekezo rahisi.

5. Je, TV na simu zinasaidia mtoto kujifunza kuongea?

Hapana. Mtoto hujifunza kupitia mawasiliano ya ana kwa ana, si TV au simu.

6. Je, kuchelewa kuongea ni dalili ya Usonji?

Inaweza kuwa, lakini si kila mtoto wa kuchelewa kuongea ana Usonji. Dalili zingine za usaonji lazima zipatikane, kama kuepuka kukuangalia machoni na kutopenda kucheza na watoto wenzake.

7. Mtoto akipata tiba lugha, ataongea baada ya muda gani?

Hutegemea chanzo cha tatizo, umri wa mtoto, na juhudi za mzazi. Mara nyingi, matokeo huanza kuonekana baada ya miezi kadhaa ya mazoezi.

8. Je, upungufu wa lishe husababisha kuchelewa kuongea?

Ndiyo, upungufu wa madini kama madini chuma na madini joto ( iodine) kunaweza kuathiri ukuaji wa ubongo, lakini mara nyingi si sababu pekee.

9. Je, mtoto mwenye masikio mazuri anaweza kuchelewa kuongea?

Ndiyo. Mazingira duni ya mawasiliano, matatizo ya neva au usonji yanaweza kusababisha kuchelewa kuongea hata bila tatizo la kusikia.

10. Je, mtoto wa kiume huchelewa kuongea kuliko wa kike?

Utafiti unaonyesha watoto wa kiume huchelewa kidogo kulinganisha na wa kike, lakini tofauti si kubwa sana.

11. Mtoto wangu wa kiume mwenye umri wa miaka 2 na miezi 3 anaelewa vizuri, anacheza, anatumia ishara kwa zaidi ya 80% na hufuata maelekezo. Hata hivyo, anashindwa kutamka maneno na hutumia zaidi ishara kuwasilisha. Je, tatizo linaweza kuwa nini na nishauriwe nini?

Mtoto wa umri wa miaka 2 na miezi 3 anayetumia ishara nyingi (>80%), anaelewa vizuri, hufuata maelekezo na kushiriki michezoni, lakini bado hajatamka maneno vizuri, anaweza kuwa na kuchelewa kwa maendeleo ya Lugha  bila kuwa na tatizo la kusikia au la ukuaji wa akili.


Kwa kawaida, mtoto wa umri huu huwa na uwezo wa:

  • Kutamka angalau maneno 20–50

  • Kuunganisha maneno 2 (mf. "mama njoo")

  • Kujaribu kurudia maneno anayosikia


Kwa kuwa mtoto wako anasikia vizuri, anacheza, anaelewa maelekezo, anacheza muziki na anaonyesha mawasiliano kupitia ishara, uwezo wake wa kushirikiana na jamii na uelewa uko vizuri—hii ni dalili nzuri sana.


Hata hivyo, ukitumia ishara nyingi kuliko maneno kunaweza kuonyesha kuwa sehemu ya uzalishaji wa maneno (kutamka sauti/maneno) bado haijakomaa.


Mambo yanayosababisha kuchelewa kuongea yanaweza kuwa:

  • Kuchelewa kukua sehemu ya ubongo inayohusika na hotuba (Uwezo wa kuongea kawaida)

  • Kuweka mazingira ya mawasiliano yasiyochochea matumizi ya maneno (mtoto kutumiwa ishara mara nyingi)

  • Kuwepo kwa tatizo dogo la misuli midogo ya mdomo/taya

  • Kurithi (kurithi tatizo la kuchelewa kuongea)

  • Kukaa mazingira ya kumfanya asifahamu maneno na kuongea- mfano kutokaa na watoto wenzake


Ushauri kwa sasa:

  1. Endelea kuzungumza naye mara kwa mara kwa maneno wazi na mafupi.

  2. Punguza kumuelewesha kila anachoashiria — mhamasishe kusema neno kwanza kabla ya kumpa kitu. Mfano: Akiashiria maji, sema: “Sema maji”, hata kama atatoa sauti isiyoeleweka.

  3. Mtazame moja kwa moja usoni ukiwa unaongea  naye.

  4. Soma vitabu vya picha na uliza maswali rahisi kama "hii ni nini?

  5. Cheza michezo ya kuiga sauti mfano: “ba-ba”, “ta-ta”, “ma-ma”.

  6. Epuka muda mwingi wa TV/simu, kwani hupunguza mawasiliano ya ana kwa ana.

  7. Mwone mtaalamu wa hotuba (speech therapist) kwa uchunguzi zaidi — hata bila dalili za hatari, inasaidia sana kuanza mapema.


Dalili zinazohitaji ushauri wa daktari haraka:

  • Kama mtoto hasemi hata neno moja

  • Kama hawezi kuiga sauti

  • Kama haonyeshi ishara, tabasamu au social interaction

  • Kama haelewi maelekezo rahisi


Kwa maelezo yako, hali yake inaonekana kuwa Speech Delay ya kawaida, na watoto wengi hupiga hatua haraka wanapopewa mazoezi sahihi.


Unaweza mpeleka mtoto kwa:

  • Daktari wa watoto

  • Daktari wa lugha kwa watoto (kama yupo)

  • Hospitali ya rufaa ya mkoa (wanayo huduma ya uchunguzi wa Masikio kinywa na koo na wataalamu wengine)


ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

Imeandikwa,

16 Julai 2025, 15:05:45

Rejea za mada hii

  1. American Academy of Pediatrics. Language Delay: When to Worry [Internet]. HealthyChildren.org; 2022.

  2. Nelson Textbook of Pediatrics. 21st ed. Kliegman RM, St Geme JW. Philadelphia: Elsevier; 2020.

  3. Paul R, Norbury CF, Gosse C. Language Disorders from Infancy Through Adolescence. 5th ed. Elsevier; 2018.

  4. World Health Organization. Developmental difficulties in early childhood: prevention, early identification, assessment and intervention in low- and middle-income countries. WHO; 2012.

  5. Bishop DV. Which neurodevelopmental disorders get researched and why? PLoS One. 2010;5(11):e15112.

  6. Shevell M. Clinical spectrum and diagnostic evaluation of developmental delay. Pediatr Clin North Am. 2008;55(6):1255-68.

  7. Speech-Language & Audiology Canada. Late Talkers: Information for Parents. SAC; 2021.

  8. Zubrick SR, Taylor CL, Rice ML, Slegers DW. Late language emergence at 24 months: an epidemiological study of prevalence, predictors, and covariates. J Speech Lang Hear Res. 2007;50(6):1562-92.

  9. Rescorla L. Late talkers: do good predictors of outcome exist? Dev Disabil Res Rev. 2011;17(2):141–50.

  10. Johnson CP, Myers SM. Identification and evaluation of children with autism spectrum disorders. Pediatrics. 2007;120(5):1183-215.

bottom of page