Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Benjamin L, MD
Imeboreshwa:
13 Julai 2025, 10:36:47

Muwasho njia ya haja kubwa: Chanzo, Dalili, na Matibabu
Swali la msingi
“Daktari, nimekuwa nikisumbuliwa na muwasho mkali sehemu ya haja kubwa kwa takribani wiki mbili sasa. Muwasho huwa mbaya zaidi usiku, hadi wakati mwingine najikuna bila kujua nikiwa nimelala. Sina maumivu makali wala damu, lakini nahisi harufu mbaya isiyo ya kawaida na ngozi inakuwa kama imechubuka. Nimejaribu kuosha kwa sabuni lakini hakuna nafuu. Nini kinasababisha hali hii na je, naweza kujitibu nyumbani bila kuja hospitali mara moja?”
Majibu
Muwasho kwenye njia ya haja kubwa ni hali ya kawaida lakini yenye usumbufu mkubwa. Huathiri wanaume na wanawake wa rika zote. Ingawa mara nyingi si hatari, inaweza kuwa ishara ya tatizo linalohitaji uangalizi zaidi.
Dalili zinazoweza kuambatana na muwasho njia ya haja kubwa
Muwasho wa mara kwa mara au wa muda mrefu sehemu ya haja kubwa
Kuchubuka au maumivu madogo wakati wa kujikuna
Harufu isiyo ya kawaida
Ngozi kuwa kavu, nyekundu au kuwa na mipasuko midogo
Kutokwa na ute au uchafu mdogo kwenye chupi
Kuwashwa zaidi usiku au baada ya kujisaidia
Visababishi vya kuwashwa njia ya haja kubwa
Muwasho unaweza kusababishwa na sababu nyingi. Zifuatazo ni sababu kuu:
Kundi la Skisababishi | Mfano wa kisababishi | Maelezo |
1. Usafi wa kupitiliza au usiofaa | - Kuosha sana kwa sabuni kali - Kuacha mabaki ya kinyesi | Sabuni kali huondoa mafuta ya asili ya ngozi na kusababisha ukavu. Mabaki ya kinyesi huweza kuchokoza ngozi. |
2. Maambukizi ya vimelea | - Minyoo (Enterobius vermicularis) - Fangasi (kandida) - Magonjwa ya zinaa (kisonono, kaswende, herpes) | Minyoo husababisha muwasho usiku. Fangasi hujitokeza hasa kwa watu wa kisukari. Magonjwa ya zinaa huambatana na vidonda, malengelenge au muwasho mkali. |
3. Magonjwa ya ngozi | - Izima(pumu ya ngozi) - Soriasis - Demataitizi ya mguzo (mzio wa mguso) - Liken sklerosas | Haya ni magonjwa ya ngozi yanayoathiri maeneo yenye unyevu. Huambatana na wekundu, upele, au ngozi kukauka. |
4. Magonjwa ya njia ya haja kubwa | - Bawasiri - Fistula - Mpasuko(mchaniko) - Saratani ya njia ya haja | Haya husababisha maumivu, kutokwa damu au majimaji, na muwasho unaoendelea karibu na mkundu. |
5. Lishe | - Pilipili nyingi - Pombe - Kahawa - Vyakula vyenye tindikali (machungwa, nanasi) | Vyakula hivi huongeza asidi kwenye kinyesi au kuchokoza ngozi ya mkundu baada ya haja. |
6. Mzio | - Kondomu - Sabuni zenye harufu - Nepi zenye kemikali - Dawa za uzazi wa mpango (kwa wenza) | Hupatikana kutokana na bidhaa zinazogusa ngozi ya sehemu za siri, husababisha muwasho au upele. |
7. Dawa na matibabu | - Antibayotiki - Dawa za kuharisha - Tiba mionzi | Matibabu haya huathiri usawazishaji wa bakteria kwenye ngozi au ndani ya njia ya haja na kuongeza uwezekano wa maambukizi ya sekondari. |
8. Msongo wa mawazo | - Hofu - Aibu ya kwenda choo mahali fulani | Msongo unaweza kuongeza hisia za mwili, hata bila ugonjwa halisi wa ngozi. |
9. Mazingira ya kimwili | - Joto kali - Kutokwa jasho - Mavazi ya ndani yasiyopitisha hewa | Unyevu mwingi hutengeneza mazingira ya fangasi na kuchokoza ngozi ya eneo la haja kubwa. |
10. Sababu zisizojulikana | - Hakuna ugonjwa wa msingi unaogundulika | Hali hii huonekana kwa 25–50% ya wagonjwa, ambapo chanzo hakibainiki hata baada ya uchunguzi. |
Matibabu ya nyumbani kwa muwasho wa njia ya kubwa
Matibabu ya nyumbani hulenga kupunguza muwasho, kulinda ngozi ya eneo hilo, na kuzuia visababishi vinavyoweza kurudia. Yafuatayo ni hatua muhimu na salama ambazo unaweza kuchukua ukiwa nyumbani:
1. Usafi wa taratibu kila baada ya kujisaidia
Safisha sehemu ya haja kubwa kwa maji ya uvuguvugu, bila kutumia sabuni zenye harufu au kemikali kali.
Epuka kutumia wipes zenye spiriti au manukato.
Baada ya kusafisha, kausha kwa kitambaa laini au tishu zisizo na manukato kwa kupangusa taratibu badala ya kusugua.
Ikiwezekana, tumia maji badala ya karatasi ya kuchambia tu (kama unatumia choo cha kukalia).
Lengo: kuondoa mabaki ya kinyesi bila kuharibu ngozi nyeti ya eneo hilo.
2. Kupaka mafuta laini au krimu za kinga na kutuliza
Unaweza kutumia bidhaa salama kwa ngozi hii nyeti: Mafuta/krimu za kupaka ni pamoja na;
Petroleum jelly (Vaseline): Huzuia msuguano na kulainisha ngozi.
Krimu ya Zinc oxide (kama zinazotumiwa kwa vipele vya watoto): Huunda tabaka la ulinzi na kutuliza muwasho.
MAfuta ya A&D au krimu za kutibu mzio wa mguso pia zinaweza kusaidia.
Ikiwa kuna kuwasha sana:
Kirmu ya Hydrocortisone 1% : Tumia kwa muda mfupi (siku 3–5) tu kupunguza uvimbe na muwasho.
Usitumie zaidi ya siku 5 bila ushauri wa daktari – inaweza kufanya ngozi iwe nyembamba.
3. Lishe bora ili kuepuka haja ngumu
Mara nyingi, choo kigumu au kushinda kujisaidia husababisha kuchubuka na hivyo muwasho. Hivyo ni muhimu kufanya choo kuwa laini kwa njia zifuatazo:
Kula vyakula vyenye nyuzinyuzi: mboga za majani, matunda (hasa papai, ndizi mbivu, embe), nafaka kamili, na mbegu kama chia.
Kunywa maji mengi – angalau glasi 6 hadi 8 kwa siku.
Epuka vyakula vinavyochokoza: pilipili kali, kahawa, pombe, na vyakula vyenye tindikali kama vile machungwa (ikiwa vinakuletea muwasho).
4. Epuka kujikuna au kusugua sehemu ya haja kubwa
Ingawa muwasho unaweza kushawishi kujikuna, jichukulie kwa uvumilivu.
Kujikuna huongeza muwasho na kusababisha maambukizi ya pili.
Ukiwa umelala usiku, vaa nguo za ndani laini na ndefu ili kupunguza hatari ya kujikuna bila kujua.
5. Chagua mavazi sahihi
Va nguo za ndani za pamba – zinapumua vizuri.
Epuka chupi zinazobana sana au nguo za nailoni – husababisha joto na unyevu unaochochea muwasho.
Badilisha chupi kila siku na mara moja ikiwa unavuja jasho au unahisi unyevu.
6. Epuka sabuni, dawa au krimu zisizoeleweka
Usitumie dawa au krimu za dukani ambazo hazikuandikwa kutumika sehemu za siri.
Usitumie dawa za mitishamba za kupaka au kusafisha bila ushauri wa daktari.
Epuka kuweka kitu chochote ndani ya haja kubwa (suppository au vipakachini) bila maagizo.
7. Tiba ya Minyoo (ikiwa unahisi hujajitibu kwa muda)
Kama kuna uwezekano wa minyoo (hasa ikiwa kuna muwasho zaidi usiku), tumia Albendazole 400mg dozi moja, au dawa nyingine za kuua minyoo.
Rudia dozi baada ya wiki mbili ikiwa unaishi mazingira yenye uwezekano mkubwa wa maambukizi.
8. Pumzisha ngozi
Baada ya kuosha na kukausha, kaa bila chupi kwa dakika 15–30 ukiwa faragha nyumbani ili kuruhusu ngozi "kupumua".
Hii husaidia kupona kwa haraka na kupunguza unyevu unaochangia muwasho.
Kumbuka:
Matibabu haya ya nyumbani hutegemea chanzo cha muwasho. Ikiwa hutambui sababu au hali inaendelea zaidi ya siku 5 hadi 7, ni muhimu kumwona mtaalamu wa afya kwa uchunguzi zaidi.
Ni wakati gani umwone daktari?
Muone daktari haraka kama:
Muwasho haupungui baada ya kujitibu nyumbani kwa wiki 1
Kuna damu kwenye choo au chupi
Kuna uvimbe, maumivu makali au usaha
Unahisi uchovu mwingi au kupungua uzito bila sababu
Jinsi ya kuzuia muwasho kurudi tena
Kunywa maji ya kutosha
Kula matunda na mboga zenye nyuzinyuzi kusaidia choo kuwa laini
Epuka sabuni zenye kemikali kali
Osha vizuri baada ya kujisaidia na kausha
Va nguo za ndani zilizotengenezwa kwa pamba na zisizobana
Hitimisho
Muwasho sehemu ya haja kubwa unaweza kuwa wa muda mfupi au wa muda mrefu, lakini mara nyingi unatibika vizuri nyumbani. Hata hivyo, ukiona dalili zisizo za kawaida, ni muhimu kumwona mtaalamu wa afya kwa uchunguzi na matibabu sahihi.
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
Imeandikwa,
13 Julai 2025, 10:17:10
Rejea za mada hii
Surawicz CM, Aron DC. Anal and rectal disorders. In: McPhee SJ, Papadakis MA, editors. Current Medical Diagnosis & Treatment 2022. 61st ed. New York: McGraw-Hill Education; 2022. p. 681–4.
Wald A. Pruritus Ani. In: Feldman M, Friedman LS, Brandt LJ, editors. Sleisenger and Fordtran's Gastrointestinal and Liver Disease. 11th ed. Philadelphia: Elsevier; 2020. p. 2097–9.
Blake T, Kirsner RS. Pruritus ani: diagnosis and management. Clin Colon Rectal Surg. 2011 Dec;24(4):167–71. doi:10.1055/s-0031-1295685
Perry C. Anal pruritus: what causes it and how to relieve it. BMJ. 2016;352:h6991. doi:10.1136/bmj.h6991
NHS. Anal itching (itchy bottom) [Internet]. NHS.uk; 2021 [cited 2025 Jul 13]. Available from: https://www.nhs.uk/conditions/itchy-bottom/
