Mwandishi:
Benjamin L, MD
Mhariri:
ULY CLINIC
31 Agosti 2025, 06:10:40

Mwasho wa mrija wa mkojo baaada ya tendo la ndoa: Sababu, Uchunguzi na Matibabu
Swali la msingi
"Habari daktari, nina umri wa miaka 25. Siku ya pili baada ya kufanya ngono bila ute wa kutosha, nilihisi mwasho kwenye urethra. Baada ya muda mfupi, dalili hizo zikatoweka na sasa ni miezi miwili sijapata tena usumbufu. Je, hali hii inaweza kuwa ishara ya maambukizi au kuna hatari nyingine ya kiafya inayoweza kujificha?"
Majibu
Urethra ni mrija unaobeba mkojo kutoka kwenye kibofu hadi nje ya mwili na hufahamika kama mrija wa mkojo. Kwa wanaume, pia hupitisha shahawa wakati wa kumwaga. Moja ya malalamiko ya kawaida baada ya tendo la ndoa ni muwasho au maumivu kwenye urethra. Dalili hii inaweza kuonekana mara moja au ndani ya masaa/hadi siku chache baadaye.
Kwa kawaida, mwasho wa muda mfupi unaweza kuwa wa mpito (mfano msuguano au ukavu wa uke), lakini pia unaweza kuashiria tatizo la kiafya linalohitaji uchunguzi zaidi, hasa kama unahusiana na magonjwa ya ngono.
Visababishi
Baadhi ya visababishi vikuu ni pamoja na;
Msuguano/Ukavu wa Uke
Tendo la ndoa bila majimaji ya kutosha (lubrication) linaweza kusababisha msuguano mkali.
Hii husababisha muwasho au maumivu ya muda mfupi kwenye urethra.
Urethraitis (Kuvimba kwa Urethra)
Husababishwa na vijidudu, mara nyingi kutoka kwenye magonjwa ya ngono.
Sababu za kawaida ni:
Chlamydia trachomatis
Neisseria gonorrhoeae (kisonono)
Mycoplasma genitalium
Virusi (HSV – Herpes simplex) mara chache.
Maambukizi ya njia ya mkojo (UTI)
Ingawa ni nadra kwa wanaume wasio na matatizo ya mkojo, maambukizi ya kibofu au urethra yanaweza kusababisha muwasho na maumivu ya kukojoa.
Uchokonozi (Sababu zisizo za maambukizi)
Sabuni zenye kemikali, dawa za kuua vijidudu ukeni, au kondomu zenye kemikali.
Magonjwa mengine ya sehemu za siri
Mawe kwenye kibofu au figo (rare, lakini yanaweza kusababisha muwasho na maumivu).
Prostataitis (kuvimba kwa tezi dume).
Dalili za kuangalia zaidi
Kuwashwa au kuchoma wakati wa kukojoa (dysuria).
Kutoka ute au usaha kwenye urethra.
Kukojoa mara kwa mara au mkojo wenye harufu mbaya.
Upele/vidonda kwenye uume au sehemu za siri.
Maumivu ya korodani au eneo la chini ya tumbo.
Uchunguzi unaoweza kufanywa hospitali
Kipimo cha mkojo (uchunguzi wa mkojo au kipimo cha kuotesha vimelea kwenye mkojo): kuchunguza kama kuna maambukizi ya UTI.
Kipimo cha PCR test: kugundua magonjwa ya ngono kama kisonono, klamidia, na mycoplasma.
Kipimo cha damu: kutathmini magonjwa ya ngono ya virusi (HIV, hepatitis, syphilis).
Matibabu
Matibabu hutegemea chanzo kilichothibitishwa:
Msuguano/ukavu wa uke → Hutulia wenyewe ndani ya siku chache; matumizi ya vilainishi (lubricants) wakati wa tendo husaidia.
Urethritis kutokana na magonjwa ya ngono → Inatibiwa kwa antibiotics sahihi (mfano doxycycline, azithromycin, au ceftriaxone kulingana na chanzo).
Maambukizi njia ya mkojo → Inatibiwa kwa antibiotics baada ya uchunguzi wa mkojo.
Uchokonozi → Epuka sabuni zenye kemikali kali, tumia kondomu salama.
Lini uonane na daktari haraka?
Unapaswa kuonana na daktari haraka ikiwa;
Kama mwasho ulidumu zaidi ya siku chache.
Kama unapata ute/usaha kutoka kwenye uume.
Kama kuna vidonda au upele sehemu za siri.
Kama unapata maumivu makali ya kukojoa au mkojo una damu.
Kama una mpenzi naye ana dalili.
Hitimisho
Muwasho wa ghafla kwenye urethra baada ya tendo la ndoa unaweza kuwa hali ndogo ya muda mfupi kutokana na msuguano. Hata hivyo, kwa sababu magonjwa ya ngono kama klamidia na kisonono ni ya kawaida na mara nyingine hayana dalili kali, ni muhimu sana kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu ili kujua chanzo na kupata tiba mapema.
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
Imeboreshwa,
31 Agosti 2025, 06:10:40
Rejea za mada hii
Workowski KA, Bachmann LH, Chan PA, Johnston CM, Muzny CA, Park I, et al. Sexually Transmitted Infections Treatment Guidelines, 2021. MMWR Recomm Rep. 2021;70(4):1–187.
Centers for Disease Control and Prevention. Gonococcal Infections Among Adolescents and Adults [Internet]. CDC; 2021 [cited 2025 Aug 31]. Available from: https://www.cdc.gov/std/treatment-guidelines/gonorrhea-adults.htm
Stamm WE, Holmes KK. Chlamydia trachomatis infections of the adult. In: Holmes KK, Sparling PF, Stamm WE, Piot P, Wasserheit JN, Corey L, et al., editors. Sexually Transmitted Diseases. 4th ed. New York: McGraw-Hill; 2008. p. 575–93.
Taylor SN, Manhart LE, Holmes KK. Mycoplasma genitalium—from Chrysalis to Multicolored Butterfly. Clin Infect Dis. 2018;67(5):731–3.
Flores-Mireles AL, Walker JN, Caparon M, Hultgren SJ. Urinary tract infections: epidemiology, mechanisms of infection and treatment options. Nat Rev Microbiol. 2015;13(5):269–84.
Sherrard J, Donders G, White D, Jensen JS. European (IUSTI/WHO) guideline on the management of non-gonococcal urethritis. Int J STD AIDS. 2011;22(8):424–9.
Schaeffer AJ, Nicolle LE. Urinary tract infections in older men. N Engl J Med. 2016;374(6):562–71.