Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Mangwella S, MD
Imeboreshwa:
6 Desemba 2025, 05:08:40

Njia za kuzuia kutungwa kwa mimba
Njia za kuzuia mimba ni mbinu salama zinazotumiwa na wanawake na wanaume ili kuzuia mbegu ya mwanaume (manii) kukutana na yai la mwanamke (utungisho) au kuzuia kiinitete kujishikiza kwenye ukuta wa mji wa mimba. Njia hizi hutoa uhuru wa kupanga uzazi, kupunguza vifo vinavyotokana na mimba zisizotarajiwa, na kuboresha afya ya mama na familia.
Kuna njia za muda mfupi, muda mrefu, za kudumu, za homoni, zisizo za homoni, na njia za dharura. Kila njia ina namna inavyofanya kazi, faida na changamoto zake, hivyo ni muhimu kupatiwa ushauri kutoka kwa mtaalamu wa afya ili kuchagua njia inayofaa zaidi kwa afya na maisha yako.
Aina za njia za kuzuia mimba
Njia za kuzuia mimba zimeainishwa katika majedwali hapa chini;
Jedwali 1. Njia zinazozuia mbegu kukutana na yai (Kuzuia utungishaji)
Njia | Inavyofanya kazi | Faida | Hasara / Tahadhari |
Kondomu ya kiume | Huzuia mbegu kuingia ukeni | Inalinda pia dhidi ya magonjwa ya zinaa | Inaweza kuchanika, matumizi mabaya |
Kondomu ya kike | Huzuia mbegu kufika kwenye shingo ya uzazi | Inatoa udhibiti kwa mwanamke | Haitumiki sana, gharama juu |
Kiwamba shingo ya kizazi/Kofia ya shingo ya kizazi | Hufunika mlango wa kizazi kuzuia mbegu | Haina homoni | Inahitaji kufungwa vizuri; ufanisi mdogo ikiwa matumizi si sahihi |
Kiuamanii (spemisaidi) | Huuwa au kupunguza uwezo wa mbegu | Rahisi kutumia | Ufanisi mdogo bila kuchanganywa na njia nyingine |
Jedwali 2. Njia zenye homoni (Kuzuia uovuleshaji, Kuzuia mbegu, au kupunguza yai lililochavushwa kujipandikiza kwenye kuta za kizazi)
Njia | Kazi | Faida | Tahadhari / Madhara Madogo |
Vidonge vya uzazi wa mpango (OCPs) | Huzuia yai kupevuka | Mzunguko wa hedhi kuwa wa mpangilio | Maumivu ya kichwa, kichefuchefu kwa baadhi |
Sindano ya homoni (Depo-Provera) | Huzuia uovuleshaji hadi miezi 3 | Rahisi kwa watu wasio kumbuka vidonge | Hedhi kusimama au kuwa nzito, kuchelewa kupata mimba baada ya kuacha |
Njiti za mkono/Kipandikizi | Huzuia ovulation kwa miaka 3–5 | Nguvu, muda mrefu | Mabadiliko ya hedhi |
Pachi ya homoni | Hutoa homoni kupitia ngozi | Rahisi kutumia mara 1 kwa wiki | Inaweza kukera ngozi |
Kitanzi chenye homoni (Hormonal IUD) | Huondoa unene wa ukuta wa kizazi na kupunguza uwezekano wa yai kupandikizwa | Muda mrefu (5–7 yrs) | Maumivu wakati wa kuweka |
Jedwali 3. Njia za kuzuia yai lililochavushwa kujipandikiza moja kwa moja kwenye kuta ya kizazi
Njia | Jinsi Inavyofanya | Faida | Hasara / Tahadhari |
Kitanzi kisicho na homoni (Copper IUD) | Shaba huua mbegu na kuzuia yai kujipandikiza | Ufanisi mkubwa, hadi miaka 10 | Maumivu ya hedhi yanaweza kuongezeka |
Vidonge vya dharura vya uzazi wa mpango kama P2 n.k | Huzuia au kuchelewesha uovuleshaji; huwahi ukuta wa kizazi kuzuia implantation | Hutumika baada ya ngono bila kinga | Si ya matumizi ya mara kwa mara, ufanisi hupungua ukichelewa |
Jedwali 4. Njia za upasuaji (Njia za kudumu za uzazi wa mpango)
Njia | Kazi | Faida | Tahadhari |
Kufunga mirija ya kizazi kwa mwanamke | Huzuia mayai kupita kuelekea sehemu ya kukutana na mbegu | Njia ya kudumu | Haifai kwa mtu mwenye mpango wa kupata watoto baadaye |
Kufunga mirija ya uzazi kwa mwanaume | Huzuia mbegu kutoka kwenye korodani | Rahisi, salama | Ni ya kudumu, mwanaume anaweza kukosa uwezo wake wa kutundisha mimba kwa njia ya kujamiana |
Jedwali 5. Njia za kitamaduni kwa kuongeza uelewa wa mwili (Uelewa wa ishara na siku za hatari)
Njia | Kazi | Faida | Changamoto |
Kujua siku za hatari kwa kalenda | Kuepuka ngono siku yai linatarajiwa kutolewa (Siku ya uovuleshaji) | Bila dawa, rahisi | Uhitaji wa ufuatiliaji wa karibu |
Kupima joto la mwili (BBT) | Kubaini uovuleshaji kwa kuangalia mabadiliko ya joto la mwili wa mwanamke | Husaidia pia kupanga mimba | Haifai kwa watu wenye mizunguko ya hedhi isiyotabirika |
Kuchunguza ute wa uke | Kubaini siku za rutuba(Uovuleshaji) | Inafaa kwa wanandoa ambao hawataki kutumia njia za homoni | Magonjwa ya uke yanaweza kuathiri hali ya ute |
Ulinganisho wa njia za kuzuia mimba
Njia | Inavyofanya Kazi | Muda wa Ufanisi / Matumizi | Ufanisi (%) |
Kondomu ya kiume | Huzuia mbegu kuingia ukeni | Kila tendo la ngono | 85–98 |
Kondomu ya kike | Huzuia mbegu kufika shingoni | Kila tendo la ngono | 79–95 |
Vidonge vya uzazi wa mpango | Huzuia ovulation | Kila siku | 91–99 |
Sindano (Depo-Provera) | Huzuia ovulation | Kila wiki 8–12 | 94–99 |
Kitanzi chenye homoni (Hormonal IUD) | Huzuia ovulation + kuimarisha ute mzito | Miaka 3–7 | >99 |
Kitanzi cha shaba (Copper IUD) | Kuzuia urutubishaji + kujipandikiza kwa yai lililorutubishwa | Miaka 5–12 | >99 |
Vipandikizi / Njiti | Huzuia uovuleshaji | Miaka 3–5 | >99 |
Pachi ya homoni | Huzuia uovuleshaji kupitia ngozi | Kila wiki | 91–99 |
Pete ya uke (Vaginal ring) | Huzuia uovuleshaji | Kubadilishwa kila mwezi | 91–99 |
Vidonge vya dharura | Kuzuia uovuleshaji / kupunguza kujipandikiza kwa yai lililochavushwa | Matumizi ya mara moja | 58–85 |
Viuajimanii (Spermisaidi) | Huuwa au kupunguza uwezo wa mbegu | Kila tendo | 70–85 (nyingi hufanya kazi vizuri zikichanganywa na Kiwamba shingo ya kizazi/Kondomu) |
Kiwamba shingo ya kizazi /Kofia ya shingo ya kizazi | Kufunika shingo ya kizazi ili kuzuia mbegu kuingia kwenye kizazi | Kila tendo + Ongeza na kiua manii | 71–88 |
Kufahamu siku za hatari, ute, joto | Kuepuka tendo katika siku za rutuba | Kila siku, kufuatilia mzunguko | 76–88 (kwa matumizi sahihi hadi 95) |
Kufunga kizazi kwa mwanamke (BTL) | Kukata/kufunga mirija ya mayai | Kudumu | >99 |
Kufunga mirija ya uzazi kwa mwanaume | Kufunga njia ya mbegu kutoka korodani | Kudumu | >99.5 |
Faida za njia za kuzuia mimba
Kuzuia mimba zisizotarajiwa
Kupanga muda na nafasi kati ya watoto
Kuboresha afya ya mama na mtoto
Kupunguza vifo vinavyohusiana na mimba
Njia nyingine huimarisha afya ya hedhi
Madhara madogo yanayoweza kutokea
Kutokwa damu katikati ya hedhi
Kuongeza au kupunguza hedhi
Kichefuchefu (kwa vidonge)
Maumivu ya tumbo la chini (Vitanzi)
Kubadilika kwa hisia au ngozi
Nani hafai kutumia njia fulani?
Wanawake wenye shinikizo la damu lisilodhibitiwa – wanapaswa kupata ushauri kabla ya kutumia vidonge.
Wenye tatizo la damu kuganda haraka – wanapaswa kushauriwa kuhusu vipandikizi/homoni kabla ya kutumia
Wale wenye maambukizi kwenye kizazi au mirija – Wanapaswa kupata matibabu kabla ya kuwekewa kitanzi.
Wanawake wanaoshukiwa au wenye saratani ya titi – Hawapaswi kutumia homoni za uzazi wa mpango
Hitimisho
Kuna njia nyingi salama za kuzuia mimba ambazo zinaweza kumfaa mwanamke au mwanaume kulingana na mahitaji, afya, na mpango wa familia. Ni muhimu kushauriana na daktari ili kupata njia inayofaa mwili wako. Kumbuka: hakuna njia inayofaa kila mtu sawa, hivyo ushauri binafsi ni muhimu.
Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake
1. Je, ninaweza kubadilisha njia ya uzazi wa mpango mara nyingi?
Ndiyo. Unaweza kubadilisha kulingana na madhara unayopata au mabadiliko ya mahitaji ya uzazi. Hata hivyo, baadhi ya njia kama sindano hutakiwa kusubiri muda fulani kabla ya kuanza njia mpya.
2. Je, vidonge vya dharura vinaathiri uwezo wa kupata ujauzito baadaye?
Hapana. Vidonge vya dharura haviharibu uzazi wa baadaye; vinafanya kazi tu kwenye mzunguko wa hedhi wa wakati huo.
3. Je, kitanzi kinaweza kusogea au kupotea ndani ya mwili?
Ni nadra sana. Mara chache, kinaweza kusogea kidogo kutoka sehemu kilipowekwa, lakini huwa hakisafiri kwenda maeneo mengine ya mwili nje ya mji wa mimba.
4. Je, vipandikizi vinaweza kuathiri uzito?
Watu wengine hupata ongezeko dogo la uzito, lakini si wote. Mabadiliko haya hutokana na athari za homoni kwa hamu ya kula na uhifadhi wa maji mwilini.
5. Je, mwanamke akitumia njia za homoni kwa muda mrefu anaathirika?
Wengi hutumia kwa miaka mingi bila tatizo. Uchunguzi unaonyesha kuwa matumizi ya muda mrefu ya vidonge husaidia pia kupunguza hatari ya saratani ya ovari.
6. Je, wanaume nao wana njia za kuzuia mimba za muda mrefu?
Kihistoria hapana, zaidi ya kondomu na kufunga uzazi kwa mwanaume. Tafiti za vidonge kwa wanaume bado zinaendelea lakini hazijaanza kutumika kwa watu kwa wingi.
7. Je, ninaweza kupata mimba nikiwa kwenye kitanzi?
Uwezekano upo lakini ni mdogo sana (chini ya 1%). Ikiwa mimba imetokea, mara nyingi hupewa vipimo kuhakikisha si mimba ya nje ya kizazi.
8. Njia ya kalenda ni salama kiasi gani?
Ina ufanisi mdogo (75–85%). Mzunguko hutofautiana kwa wanawake wengi, hivyo ni rahisi kupata mimba bila kutarajia.
9. Je, vidonge vya uzazi wa mpango vinahitaji kipimo cha damu kabla ya kuanza?
Kwa wanawake wengi, hapana. Kinachohitajika zaidi ni historia ya afya na vipimo vya shinikizo la damu. Vipimo vingine hutolewa tu kwa wenye magonjwa maalumu.
10. Je, kifafa au magonjwa mengine sugu yanaathiri chaguo la njia ya uzazi wa mpango?
Ndiyo. Baadhi ya dawa za kifafa hupunguza ufanisi wa vidonge. Wagonjwa hawa hupewa njia zisizotegemea homoni fulani, kama kitanzi cha shaba au vipandikizi maalumu.
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
Imeandikwa,
6 Desemba 2025, 05:08:40
Rejea za mada hii
World Health Organization. Medical eligibility criteria for contraceptive use. 5th ed. WHO; 2015.
Trussell J. Contraceptive failure in the United States. Contraception. 2011;83(5):397–404.
American College of Obstetricians and Gynecologists. Long-Acting Reversible Contraception (LARC): Implants and Intrauterine Devices. Practice Bulletin No. 186. Obstet Gynecol. 2017;130:e251–e269.
Hubacher D, Trussell J. A definition of modern contraceptive methods. Contraception. 2015;92(5):420–421.
Cleland K, Zhu H, Goldstruck N, Cheng L, Trussell J. The efficacy of intrauterine devices for emergency contraception: a systematic review. Hum Reprod. 2012;27(7):1994–2000.
Glasier A. Emergency postcoital contraception. N Engl J Med. 1997;337:1058–1064.
Winner B, Peipert JF, Zhao Q, et al. Effectiveness of long-acting reversible contraception. N Engl J Med. 2012;366:1998–2007.
Hatcher RA, Nelson AL, Trussell J, et al. Contraceptive Technology. 21st ed. New York: Ayer Company Publishers; 2018.
Faculty of Sexual and Reproductive Healthcare (FSRH). UK Medical Eligibility Criteria for Contraceptive Use (UKMEC). FSRH; 2016.
Curtis KM, Tepper NK, Jatlaoui TC, et al. U.S. Medical Eligibility Criteria for Contraceptive Use. MMWR Recomm Rep. 2016;65(3):1–103.
Peterson HB. Sterilization. Obstet Gynecol. 2008;111(1):189–203.
Cook LA, Van Vliet H, Lopez LM, Pun A. Vasectomy occlusion techniques for male sterilization. Cochrane Database Syst Rev. 2014;(3):CD003991.
