Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
Dkt. Benjamin L, MD
Imeboreshwa:
28 Novemba 2025, 11:00:58

Nywele kukua ndani sehemu za siri: Sababu, Dalili na Tiba
Nywele kukua ndani ya ngozi ni hali inayotokea pale nywele inaposhindwa kuchomoza juu ya ngozi na badala yake inakua kuelekea upande wa ndani. Hali hii husababisha uvimbe mdogo kama upele, wekundu, maumivu, au usaha, hasa sehemu zinazonyolewa mara kwa mara kama sehemu za siri, makwapa na ndevu.
Kwa watu wengi, tatizo hili hurudia-rudia na husababisha usumbufu mkubwa, hasa pale uvimbe unapokuwa wenye maumivu au kuacha makovu.
Visababishi
Kunyoa karibu na ngozi: Kunyoa karibu mno na ngozi hufanya ncha ya nywele kuwa kali na kuingia ndani inapochomoza.
Nywele za kujikuja: Watu wenye nywele za kujikunja au zinazopinda mara nyingi hukumbana zaidi na tatizo hili.
Mavazi ya kubana: Suruali au chupi zinazobana huongeza msuguano na kuongoza nywele kurudi ndani.
Kuzuia tundu la nyweleKutokana na mafuta, jasho, seli zilizokufa au uchafu wa ngozi.
Maambukizi ya shina la ngozi: Maambukizi kwenye tundu la nywele yanaweza kufanya uvimbe kuwa mkubwa zaidi na kuhisi kama kipele chenye usaha.
Kuota nywele zaidi ya mara mbili: Mara nyingine nywele hukatika na kuanza kuota kama sehemu mbili, na hii huchochea kuota ndani.
Dalili kuu
Uvimbe mdogo kama upele
Kuwekundu (wakati mwingine joto juu ya uvimbe)
Maumivu au kuwashwa
Usaha au majimaji ya njano
Kuonekana kwa nywele nyeusi iliyojikunja ndani
Makovu au madoa ya giza baada ya kupona
Uchunguzi
Uchunguzi mara nyingi hufanywa kwa: Kuangalia kwa macho ambapo daktari anaweza kutambua kirahisi iwapo ni nywele iliyoota kwa ndani au maambukizi kwenye shina la nywele au jipu.
Mara chache hufanywa vipimo ikiwa:
Kuna maambukizi ya kurudia rudia
Uvimbe unakuwa mkubwa sana
Kuna dalili za fangasi au magonjwa mengine ya ngozi
Matibabu
Tiba ya hospitali
AntibiotikiHutolewa iwapo kuna dalili za maambukizi (wekundu mkali, maumivu, usaha).
Dawa za kupunguza uvimbeKama hydrocortisone cream (kwa muda mfupi tu).
Kutoa nywele iliyozamaDaktari hutumia kifaa maalumu kuondoa nywele bila kujeruhi ngozi.
Tiba za kuzuia kurudiaIkiwa tatizo linarudia mara nyingi, daktari anaweza kupendekeza tiba kama:
Kuondoa nywele kwa tekinolojia ya leza
Kupaka mafuta ya kuzuia ukuaji wa nywele
Matibabu ya nyumbani
Kukanda kwa maji ya uvuguvugu: Kufanya mara 2–3 kwa siku husaidia kufunguka kwa tundu la nywele.
Kusugua ngozi taratibu: Kwa kitambaa laini au mafuta ya nyenzo za kuondoa ngozi iliyokufa mara 2–3 kwa wiki ili kuondoa seli zilizokufa.
Epuka kubinya au kutumbua kwa nguvu: Kwa kuwa huongeza uwezekano wa maambukizi.
Tumia dawa za kupunguza maumivu: Mfano paracetamol kama kuna maumivu makali.
Epuka kunyoa kwa muda: Acha ngozi ipone kabla ya kuanza kunyoa tena.
Osha kwa sabuni isiyo na kemikali kaliIli kupunguza kuziba kwa vitundu vya nywele.
Jinsi ya kuzuia tatizo kujirudia
Tumia wembe mpya au mashine kila wakati.
Nyooa kwa kuelekea mwelekeo wa ukuaji wa nywele (si kinyume).
Usikandamize sana wakati wa kunyoa.
Tumia gel au povu la kunyoa kupunguza msuguano.
Vaeni nguo zisizobana hasa wakati wa kulala.
Fanya exfoliation mara kwa mara kuondoa seli zilizokufa.
Lini umuone daktari?
Onana na daktari ikiwa:
Uvimbe unauma sana au unaongezeka
Unatoka usaha mfululizo
Upele unarudia mara kwa mara
Kuna homa au mwili kuchoka
Uvimbe umegeuka jipu (abscess)
Una kisukari au kinga dhaifu
Hitimisho
Nywele kukua ndani sehemu za siri ni tatizo la kawaida linalotokea kutokana na mabadiliko ya ukuaji wa nywele, msuguano, au kunyoa kwa njia isiyo sahihi. Kwa bahati nzuri, linaweza kudhibitiwa kwa matibabu rahisi ya nyumbani na kubadilisha mbinu za kunyoa. Hata hivyo, ikiwa uvimbe unauma, una usaha au unarudia mara kwa mara, ni muhimu kumwona daktari ili kuzuia maambukizi au makovu ya kudumu.
ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.
Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba
Imeandikwa,
27 Novemba 2025, 12:57:54
Rejea za mada hii
James WD, Elston DM, Treat JR, Rosenbach MA, Neuhaus IM. Andrews’ Diseases of the Skin: Clinical Dermatology. 13th ed. Philadelphia: Elsevier; 2020.
Habif TP. Clinical Dermatology: A Color Guide to Diagnosis and Therapy. 6th ed. Philadelphia: Elsevier; 2016.
Burns T, Breathnach S, Cox N, Griffiths C, editors. Rook’s Textbook of Dermatology. 9th ed. Wiley-Blackwell; 2016.
Friedman PM, Skover GR, Payonk G, Geronemus RG, Kimyai-Asadi A. Treatment of pseudofolliculitis barbae with a pulsed diode laser: a controlled clinical trial. J Am Acad Dermatol. 2004;50(3): 465–9.
Ogunbiyi A. Pseudofolliculitis barbae; current diagnosis and management. Clin Cosmet Investig Dermatol. 2019;12: 241–7.
Callender VD, Wright DR, Davis EC, Taylor SC. Hair disorders in patients of African descent. J Am Acad Dermatol. 2011;64(2): 235–45.
Sperling LC, Cowper SE. An Atlas of Hair Pathology with Clinical Correlations. 2nd ed. Boca Raton: CRC Press; 2012.
