top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Benjamin L, MD

5 Juni 2025, 11:12:33

Vichomi ukeni vya kuja na kupotea kwenye ujauzito wa miezi 9: Sababu na njia za kuthibiti nyumbani

Vichomi ukeni vya kuja na kupotea kwenye ujauzito wa miezi 9: Sababu na njia za kuthibiti nyumbani

Swali la msingi


Habari za kazi daktari, Sorry naomba nisaidie kunifahamisha Kama mjamzito wa miezi 9 anapata vichomi kwenye uke vya kuja na kupotea ni dalili za nini ?


Majibu

Asante kwa swali zuri. Kwa mjamzito aliye na ujauzito wa miezi 9, vichomi vya ghafla kwenye uke (vya kuja na kuondoka) vinaweza kuwa ni dalili ya kawaida ya mwili kujiandaa kwa kujifungua. Hapa chini nimeeleza kwa undani:


Maana ya vichomi vya kuja na kupotea kwenye uke miezi ya mwisho ya Ujauzito

1. Kushuka kwa kichwa cha mtoto

Kadri tarehe ya kujifungua inavyokaribia, kichwa cha mtoto huanza kushuka kuelekea kwenye nyonga na njia ya uzazi. Hii huongeza mgandamizo kwenye uke, na kinaweza kuhisiwa kama vichomi vya ghafla au kuchomachoma.

2. Kukunjuka na kuongezeka njia ya shingo ya kizazi

Mabadiliko haya huandaa mwili kwa ajili ya leba. Wakati mabadiliko haya yanaanza, unaweza kupata vichomi au mishtuko ya muda mfupi ukeni.

3. Kusogea au kucheza kwa mtoto tumboni

Harakati za mtoto, hasa anaposukuma au kugeuka, zinaweza kusababisha presha kwenye neva au misuli karibu na uke.

4. Leba ya uongo

Wakati mwingine, mama mjamzito hupata mikazo ya tumbo ya maandalizi ya kujifungua, na vichomi vinaweza kuwa sehemu ya hali hii.


Lini hali hii inahitaji kumwona daktari hharaka?

Ingawa vichomi vya ghafla vinaweza kuwa kawaida, unapaswa kumwona daktari haraka kama:

  • Vichomi vinaambatana na kutokwa damu au uchafu usio wa kawaida

  • Kuna maumivu makali ya tumbo au mgongo wa chini

  • Unapata uchungu wa leba wa kweli (maumivu ya kuja na kuondoka kwa mpangilio, na kuongezeka kwa nguvu)

  • Unahisi mtoto hachezi kama kawaida

  • Unaanza kupata maji kutoka ukeni (dalili ya kupasuka kwa chupa ya uzazi)


Mambo ya kufanya nyumbani

Mama mjamzito anaweza kufanya mambo kadhaa akiwa nyumbani ili kupunguza maumivu ya vichomi kwenye uke (hasa ikiwa ni dalili za kawaida za mwisho wa ujauzito). Haya ni baadhi ya mambo ya kusaidia:


Badilisha mkao wa mwili

Badilisha mkao kila baada ya muda mfupi – kama umekaa kwa muda mrefu, jaribu kusimama au kutembea kidogo. Ukiwa umesimama muda mrefu, jaribu kukaa au kulala kwa upande. Kulala upande wa kushoto ni bora kwa mzunguko wa damu na hupunguza presha kwenye kizazi na mishipa mikubwa.


Tembea polepole

Kutembea husaidia mtoto kushuka vizuri na pia kusaidia kuchochea uchungu wa kweli (kama umeanza). Tembea dakika 10–20 mara 2–3 kwa siku, kama huna matatizo ya kiafya yanayokuzuia.


Fanya mazoezi mepesi

Mazoezi kama kupiga magoti na mikono ardhini (position ya "cat-cow") husaidia kupunguza presha kwenye uke. Mazoezi ya kegeli pia yanaweza kusaidia kuimarisha misuli ya nyonga na kupunguza maumivu.


Tumia maji ya moto kwa njia salama

Kuoga maji ya uvuguvugu au kuweka kitambaa chenye joto (Au chupa maalumu ya maji moto ya kukanda tumbo) kwenye sehemu ya chini ya tumbo au mgongo kunaweza kusaidia kupunguza maumivu. Epuka maji ya moto sana (yasiyovumilika kwa ngozi).


Pumzika vya kutosha

Muda huu mwili unajitayarisha kwa kazi kubwa ya kujifungua, hivyo mama anatakiwa kupata usingizi wa kutosha na kupumzika mara kwa mara. Pumzika kwa kulala upande mmoja ukiwa umeegemea mto kati ya miguu au chini ya tumbo.


Pumua kwa utaratibu

Mafunzo ya kupumua taratibu (deep breathing) kama yale yanayofundishwa kwenye kliniki za wajawazito husaidia mama kutulia na kupunguza maumivu.


Hitimisho

Vichomi vya kuja na kuondoka kwenye uke kwa mjamzito wa miezi 9 ni jambo la kawaida linaloashiria kuwa mwili unaanza kujiandaa kwa leba. Hata hivyo, ikiwa kuna dalili za wasiwasi, ni busara kumwona daktari au mkunga kwa uchunguzi zaidi.

ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

Imeboreshwa,

5 Juni 2025, 11:12:33

Rejea za mada hii

  1. American College of Obstetricians and Gynecologists. Practice Bulletin No. 107: Induction of labor. Obstet Gynecol. 2009;114(2 Pt 1):386–97.

  2. Cunningham FG, Leveno KJ, Bloom SL, Spong CY, Dashe JS, Hoffman BL, et al. Williams Obstetrics. 25th ed. New York: McGraw-Hill Education; 2018.

  3. Royal College of Obstetricians and Gynaecologists. The investigation and management of the small-for-gestational-age fetus. Green-top Guideline No. 31. London: RCOG; 2013.

  4. Macones GA, Hankins GDV, Spong CY, Hauth J, Moore T. The 2008 National Institute of Child Health and Human Development workshop report on electronic fetal monitoring: update on definitions, interpretation, and research guidelines. J Obstet Gynecol Neonatal Nurs. 2008;37(5):510–5.

  5. World Health Organization. WHO recommendations: intrapartum care for a positive childbirth experience. Geneva: WHO; 2018.

  6. American Pregnancy Association. Braxton Hicks contractions [Internet]. 2020 [cited 2025 Jun 5]. Available from: https://americanpregnancy.org/labor-and-birth/braxton-hicks-contractions/

bottom of page