top of page

Mwandishi:

Mhariri:

ULY CLINIC

Dkt. Lugonda B, MD

4 Januari 2026, 04:55:47

Image-empty-state.png

Rhesus na ujauzito

Imeboreshwa:

Wakati wa ujauzito, mama hupimwa vipimo mbalimbali muhimu vinavyolenga kulinda afya yake na ya mtoto anayekua tumboni. Miongoni mwa vipimo hivyo ni kundi la damu (A, B, AB au O) na hali ya Rhesus (Rhesus chanya au hasi). Hali ya rhesus, ingawa wengi huihusisha kidogo, inaweza kuwa na madhara makubwa kwa ujauzito unaofuata endapo haitatambuliwa na kudhibitiwa mapema.


Rhesus ni nini?

Rhesus ni sifa ya kinasaba inayohusiana na uwepo au kutokuwepo kwa protini maalum inayoitwa D antijen kwenye chembe nyekundu za damu.

  • Rhesus chanya (+): Una protini ya D antijen

  • Rhesus hasi (−): Huna protini ya D antijen

Idadi kubwa ya watu duniani ni rhesus chanya, huku rhesus hasi ikiwa ndogo kwa idadi.


Rhesus hurithiwa vipi?

Hali ya rhesus hurithiwa kutoka kwa wazazi kupitia vinasaba. Mama mwenye rhesus hasi anaweza kupata mtoto mwenye rhesus chanya endapo baba ni rhesus chanya. Hapo ndipo tatizo la kutoshabihiana kwa rhesus huanza.


Rhesus huathirije ujauzito?

Tatizo hutokea pale ambapo:

  • Mama ni rhesus hasi

  • Mtoto ni rhesus chanya


Wakati wa kujifungua au kwenye matukio fulani ya ujauzito, damu ya mtoto inaweza kuchanganyika na damu ya mama. Mfumo wa kinga ya mwili wa mama hutambua damu hiyo kama ya kigeni na kuanza kutengeneza kingamwili (antibodi) dhidi yake.


Ujauzito wa kwanza mara nyingi huisha salama. Ujauzito unaofuata unaweza kuathirika vibaya kwa sababu kingamwili hizo huweza kuvuka kondo la nyuma (placenta) na kuharibu chembe nyekundu za damu za kijusi.


Madhara kwa kijusi

Kingamwili za mama zinaweza kusababisha:

  • Upungufu mkubwa wa damu kwa kijusi

  • Kifo cha kijusi tumboni

  • Mtoto kuzaliwa na manjano kali

  • Uhitaji wa kupewa damu kabla au baada ya kuzaliwa


Sindano ya Ant-D ni nini?

Ant-D (Anti-D immunoglobulin) ni dawa inayozuia mwili wa mama kutengeneza kingamwili hatarishi dhidi ya damu ya mtoto mwenye rhesus chanya.

Hufanya kazi kwa:

  • Kuharibu chembe za damu za mtoto zilizopita kwenda kwa mama

  • Kuzuia mfumo wa kinga wa mama “kujifunza” na kuhifadhi kumbukumbu ya damu ya mtoto


Ant-D huchomwa lini?

Mama mwenye rhesus hasi hupewa Ant-D:

  • Wiki ya 28 na 34 za ujauzito (au 28 na 30 kulingana na kliniki)

  • Ndani ya masaa 72 baada ya kujifungua mtoto rhesus chanya

  • Baada ya matukio hatarishi kama:

    • Kutokwa na damu ujauzito ukiwa zaidi ya wiki 20

    • Kupigwa tumboni

    • Ujauzito kutoka

    • Ujauzito nje ya mfuko wa kizazi

    • Amniosentesis au kuzungushwa kwa mtoto akae vema


Vipi kama mama tayari ana kingamwili?

Endapo vipimo vitaonyesha kuwa kingamwili tayari zipo:

  • Ant-D haitachomwa kwa sababu haitakuwa na msaada

  • Mama atahitaji uangalizi wa karibu na mtaalamu wa afya ya uzazi

  • Mtoto anaweza kufuatiliwa kwa vipimo maalum na kupewa damu akiwa tumboni endapo atakosa damu


Mtoto anapozaliwa hufanyiwa nini?

  • Damu ya kitovu hupimwa kujua kundi la damu na rhesus

  • Kama mtoto ni rhesus chanya, mama hupewa Ant-D ndani ya masaa 72

  • Kama mtoto ni rhesus hasi, Ant-D haitahitajika


Hitimisho

Rhesus na ujauzito ni suala la msingi linalohitaji uelewa, vipimo vya mapema na ufuatiliaji sahihi. Sindano ya Ant-D imeokoa maisha ya watoto wengi na kusaidia wanawake wengi kupata ujauzito salama. Elimu na huduma sahihi ni silaha muhimu dhidi ya madhara ya kutoshabihiana kwa rhesus.


Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara na majibu yake

1. Je rhesus hasi ni ugonjwa?

Hapana. Rhesus hasi si ugonjwa bali ni sifa ya kinasaba ya damu.

2. Je mwanamke rhesus hasi anaweza kupata watoto salama?

Ndiyo kabisa. Kwa ufuatiliaji sahihi na matumizi ya Ant-D, wanawake wengi hupata watoto salama bila matatizo.

3. Je baba wa mtoto ana mchango gani kwenye tatizo hili?

Baba mwenye rhesus chanya ndiye chanzo cha mtoto kuwa rhesus chanya, jambo linaloweza kusababisha mgongano wa rhesus.

4. Je mimba ya kwanza huwa hatarini?

Mara nyingi hapana. Hatari huongezeka zaidi kwenye mimba zinazofuata kama Ant-D haikutumika.

5. Je Ant-D ina madhara kwa mama au mtoto?

Ant-D ni salama sana. Madhara madogo kama maumivu ya sindano au homa ndogo yanaweza kutokea kwa nadra.

6. Kipi hutokea kama mama hakupata Ant-D kwa ujauzito uliopita?

Anaweza kuwa tayari ametengeneza kingamwili, hivyo ujauzito unaofuata huhitaji uangalizi wa karibu zaidi.

7. Kuna watu wengine wanachoma sindano ya Ant-D mara tatu, kwa nini?

Ndiyo. Hii hutokea endapo:

  • Mama alipata Ant-D ya kawaida wiki ya 28

  • Akapata tukio la kutokwa damu au ajali kabla ya kujifungua

  • Kisha akapewa Ant-D tena baada ya kujifunguaHii si kosa, bali ni ulinzi wa ziada kulingana na hatari iliyotokea.

8. Je Ant-D hupatikana hospitali zote?

Hospitali nyingi kubwa na kliniki za uzazi huwa nazo, lakini upatikanaji unaweza kutofautiana kulingana na eneo.

9. Je mwanamke rhesus chanya anahitaji Ant-D?

Hapana. Ant-D ni kwa mama rhesus hasi pekee.

10. Je vipimo vya rhesus hufanywa mara ngapi ujauzito?

Hufanywa mapema kabisa ujauzito unapoanza na hurudiwa wiki ya 28 ili kuhakikisha usalama.


ULY Clinic inakushauri uwasiliane na daktari wako siku zote kabla ya kufanya maamuzi yanayohusisha afya yako
Wasiliana na daktari wa  ULY Clinic kwa ushauri na Tiba au kuandikiwa dawa kwa kutumia namba za simu au Kubonyeza Pata tiba chini ya tovuti hii.

Imeandikwa:

5 Novemba 2021, 18:11:56

Rejea za dawa

  1. John Costumbrado, et al. Rh Incompatibility. https://www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK459353/. Imechukuliwa 5/11/2021

  2. Frequently asked questions. Pregnancy FAQ027. The Rh factor: How it can affect your pregnancy. American College of Obstetricians and Gynecologists. https://www.acog.org/Patients/FAQs/The-Rh-Factor-How-It-Can-Affect-Your-Pregnancy. Imechukuliwa 5/11/2021

  3. Moise KJ. Overview of Rhesus (Rh) alloimmunization in pregnancy. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 5/11/2021

  4. Moise KJ. Prevention of Rh (D) alloimmunization. https://www.uptodate.com/contents/search. Imechukuliwa 5/11/2021

  5. American College of Obstetricians and Gynecologists (ACOG) Committee on Practice Bulletins. Obstetrics. ACOG Practice Bulletin No. 192: Management of alloimmunization during pregnancy. Obstetrics & Gynecology. 2018;131:611.

  6. American College of Obstetricians and Gynecologists (ACOG) Committee on Practice Bulletins. Obstetrics. ACOG Practice Bulletin No. 181: Prevention of Rh D alloimmunization. Obstetrics & Gynecology. 2017;130:e57.

bottom of page