top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

Dkt. Salome A, MD

Imeboreshwa:

18 Julai 2026, 10:31:28

Matibabu ya shinikizo la juu la damu

Matibabu ya shinikizo la juu la damu

Je kuna matibabu ya ugonjwa huu?

Presha ya kupanda ni ugonjwa wa muda mrefu unaoweza kudhibitiwa vizuri kwa kutumia dawa na kufanya mabadiliko ya mtindo wa maisha. Kwa watu wengi, matibabu huchukuliwa kwa muda mrefu na mara nyingi kwa maisha yote, isipokuwa kama daktari ataamua vinginevyo.


Lengo la matibabu ni kushusha shinikizo la damu hadi kiwango salama ili kupunguza hatari ya kupata kiharusi, mshtuko wa moyo, kushindwa kwa figo, kupoteza uwezo wa kuona na matatizo mengine yanayosababishwa na presha isiyodhibitiwa.


Ni muhimu kuelewa kuwa dawa za presha hazitibu ugonjwa moja kwa moja, bali husaidia kuudhibiti. Ndiyo maana watu wengi wanapaswa kuendelea kutumia dawa hata kama wanajisikia vizuri.


Daktari huchaguaje dawa ya presha?

Hakuna dawa moja inayofaa kwa kila mtu. Daktari huchagua dawa kulingana na mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na:

  • Kiwango cha shinikizo la damu.

  • Umri wa mgonjwa.

  • Uwepo wa kisukari.

  • Magonjwa ya figo.

  • Magonjwa ya moyo.

  • Historia ya kiharusi.

  • Ujauzito au mipango ya kupata ujauzito.

  • Madhara yaliyowahi kutokea kutokana na dawa nyingine.

Kwa baadhi ya wagonjwa dawa moja inaweza kutosha, lakini kwa wengine huenda zikahitajika dawa mbili au zaidi ili kufikia udhibiti mzuri wa presha.


Dawa zinazotumika kutibu presha ya kupanda

1. Dawa za kuongeza mkojo

Hizi husaidia mwili kutoa chumvi na maji ya ziada kupitia mkojo, hivyo kupunguza kiasi cha damu kinachozunguka mwilini na kushusha presha.

Mifano ni:

  • Hydrochlorothiazide

  • Chlorthalidone

  • Indapamide

Madhara yanayoweza kutokea ni pamoja na kukojoa mara kwa mara, kupungua kwa kiwango cha potasiamu na wakati mwingine kuongezeka kwa sukari au asidi ya uric.


2. Vizuia risepta za vibadili Angiotensi- ACE

Huzuia utengenezaji wa kemikali inayosababisha mishipa ya damu kubana.

Mifano ni:

  • Enalapril

  • Lisinopril

  • Ramipril

  • Perindopril

Dawa hizi ni muhimu sana kwa wagonjwa wenye kisukari au ugonjwa wa figo.

Baadhi ya watu hupata kikohozi kikavu kinachoendelea. Hazipaswi kutumiwa wakati wa ujauzito.


3. Vizuia risepta angiotensin-ARB

Hufanya kazi karibu sawa na ACE inhibitors lakini mara nyingi hazisababishi kikohozi.

Mifano ni:

  • Losartan

  • Valsartan

  • Telmisartan

  • Candesartan


4. Vizuia njia za kalisiamu

Husaidia mishipa ya damu kulegea ili damu ipite kwa urahisi.

Mifano ni:

  • Amlodipine

  • Nifedipine

  • Felodipine

Baadhi ya wagonjwa hupata uvimbe wa miguu, maumivu ya kichwa au mapigo ya moyo kwenda kasi.


5. VIzuia risepta Beta

Hupunguza kasi ya mapigo ya moyo na nguvu ambayo moyo unasukuma damu.

Mifano ni:

  • Atenolol

  • Bisoprolol

  • Metoprolol

  • Carvedilol

Hutumika zaidi kwa wagonjwa wenye magonjwa ya moyo kuliko kama dawa ya kwanza kwa kila mgonjwa wa presha.


6. Vizuia risepta Alpha

Hulegeza mishipa ya damu.

Mifano:

  • Prazosin

  • Doxazosin


7. Vipinzani vya Aldosterone

Mifano:

  • Spironolactone

  • Eplerenone

Hutumika zaidi kwa presha ambayo imekuwa ngumu kudhibiti.


Kwa nini wagonjwa wengine hupewa dawa mbili au tatu?

Wakati mwingine dawa moja haitoshi kushusha presha.

Kwa mfano mgonjwa anaweza kutumia:

  • Amlodipine pamoja na Losartan

  • Perindopril pamoja na Indapamide

  • Telmisartan pamoja na Amlodipine

Mchanganyiko huu unaweza kudhibiti presha vizuri zaidi kuliko kuongeza dozi kubwa ya dawa moja.


Ni muhimu kunywa dawa kila siku

Makosa yanayofanywa mara nyingi ni:

  • Kuacha dawa baada ya presha kushuka.

  • Kumeza dawa siku ambazo presha imepanda pekee.

  • Kutumia dawa za mtu mwingine.

  • Kubadilisha dawa bila ushauri wa daktari.

Haya yanaweza kufanya presha ipande tena na kuongeza hatari ya kupata kiharusi au mshtuko wa moyo.


Maswali 10 yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu matibabu ya presha ya kupanda

1. Nikianza kutumia dawa za presha nitazitumia maisha yote?

Kwa watu wengi, ndiyo. Presha ya kupanda ni ugonjwa wa muda mrefu unaohitaji kudhibitiwa kwa muda mrefu. Hata hivyo, baadhi ya watu wanaoweza kupunguza uzito, kupunguza matumizi ya chumvi, kufanya mazoezi mara kwa mara na kubadilisha mtindo wa maisha wanaweza kuhitaji dawa chache au dozi ndogo zaidi. Usiache dawa bila ushauri wa daktari.

2. Nimesikia nikianza dawa za presha sitaweza kuziacha. Je, ni kweli?

Si kwamba dawa "zinazoea mwili", bali zinadhibiti ugonjwa. Ukiziacha bila ushauri, presha inaweza kupanda tena kwa sababu chanzo cha ugonjwa bado kipo.

3. Nimesahau kunywa dawa leo nifanye nini?

Ukikumbuka ndani ya muda mfupi, meza dozi yako mara moja. Lakini ikiwa muda wa dozi inayofuata umekaribia, ruka dozi uliyosahau na endelea na ratiba yako ya kawaida. Usimeze dozi mbili kwa wakati mmoja isipokuwa umeelekezwa na daktari.

4. Je, nikiona presha imeshuka naweza kuacha dawa?

Hapana. Mara nyingi presha hushuka kwa sababu dawa zinafanya kazi. Kuacha dawa bila ushauri kunaweza kufanya presha ipande tena bila dalili zozote.

5. Mtindi (yoghurt) unaweza kusaidia presha ya kupanda kurudi kawaida baada ya kumeza dawa?

Mtindi ni sehemu ya lishe bora na unaweza kuwa na faida kwa afya ya moyo, hasa ikiwa ni mtindi usio na sukari nyingi na wenye mafuta kidogo. Baadhi ya tafiti zimeonyesha kuwa matumizi ya bidhaa za maziwa zisizo na mafuta mengi yanaweza kuchangia kushuka kidogo kwa shinikizo la damu kama sehemu ya lishe yenye matunda, mboga na ulaji mdogo wa chumvi.


Hata hivyo, mtindi si dawa ya kutibu presha, na hauwezi kushusha presha haraka baada ya kumeza dawa wala hauwezi kuchukua nafasi ya dawa ulizoandikiwa. Hakuna ushahidi wa kisayansi unaoonyesha kwamba kula mtindi baada ya kumeza dawa hufanya presha irudi kawaida mara moja.


Kwa hiyo, unaweza kula mtindi kama sehemu ya lishe yenye afya ikiwa huna sababu nyingine za kuuepuka, lakini endelea kutumia dawa zako kama ulivyoelekezwa na daktari.

6. Je, nikitumia dawa za presha naweza kunywa pombe?

Inashauriwa kupunguza au kuepuka pombe. Pombe inaweza kuongeza presha na pia kuingiliana na baadhi ya dawa za presha, hivyo kupunguza ufanisi wake au kuongeza madhara.

7. Dawa za presha zina madhara gani?

Madhara hutegemea aina ya dawa. Baadhi ya watu hupata kukohoa (kwa vizuia risepta za vibadili Angiotensin-ACE), uvimbe wa miguu (kwa amlodipine), kukojoa mara kwa mara (kwa diuretics), au kizunguzungu mwanzoni mwa matibabu. Usiache dawa bila kumwona daktari ikiwa utapata madhara.

8. Naweza kutumia dawa za mitishamba pamoja na dawa za presha?

Usifanye hivyo bila ushauri wa daktari. Baadhi ya dawa za mitishamba zinaweza kuongeza au kupunguza nguvu ya dawa za presha, na nyingine zinaweza kusababisha madhara au kuathiri figo.

9. Kwa nini presha yangu bado ipo juu wakati natumia dawa?

Sababu zinaweza kujumuisha kutotumia dawa kama ulivyoelekezwa, kutumia chumvi nyingi, unywaji wa pombe, uzito mkubwa, magonjwa mengine, au kuhitaji mchanganyiko tofauti wa dawa. Muone daktari ili kutathmini sababu na kurekebisha matibabu.

10. Je, ninaweza kuacha dawa nikipunguza uzito na kufanya mazoezi?

Kwa baadhi ya watu, mabadiliko makubwa ya mtindo wa maisha yanaweza kupunguza hitaji la dawa au dozi yake. Hata hivyo, uamuzi wa kupunguza au kuacha dawa unapaswa kufanywa na daktari baada ya kufuatilia vipimo vya presha kwa muda. Usiache dawa peke yako hata kama presha imeanza kuwa ya kawaida.


Imeandikwa;

10 Juni 2020, 17:51:11

ULY Clinic inakushauri siku zote usichukue hatua yoyote ile inayoathiri afya yako bila kuwasiliana na daktari wako. 

Wasiliana na daktari wa ULY CLinic kwa kubonyeza 'Pata Tiba' au kutumia namba za simu chini ya tovuti hii kwa elimu suhauri na Tiba

Rejea za mada hii,

​

  1. Beckett  NS, Peters  R, Fletcher  AE,  et al; HYVET Study Group.  Treatment of hypertension in patients 80 years of age or older.  N Engl J Med. 2008;358(18):1887-1898.PubMedGoogle ScholarCrossref. Imechukuliwa 09.06.2020

  2. SHEP Cooperative Research Group.  Prevention of stroke by antihypertensive drug treatment in older persons with isolated systolic hypertension: final results of the Systolic Hypertension in the Elderly Program (SHEP).  JAMA. 1991;265(24):3255-3264. ArticlePubMedGoogle ScholarCrossref. Imechukuliwa 09.06.2020

  3. Institute of Medicine.  Clinical Practice Guidelines We Can Trust. Washington, DC: National Academies Press; 2011. http://www.iom.edu/Reports/2011/Clinical-Practice-Guidelines-We-Can-Trust.aspx. Imechukuliwa 09.06.2020

  4. Staessen  JA, Fagard  R, Thijs  L,  et al; The Systolic Hypertension in Europe (Syst-Eur) Trial Investigators.  Randomised double-blind comparison of placebo and active treatment for older patients with isolated systolic hypertension.  Lancet. 1997;350(9080):757-764.PubMedGoogle ScholarCrossref. Imechukuliwa 09.06.2020

  5. Hsu  CC, Sandford  BA.  The Delphi technique: making sense of consensus.  Pract Assess Res Eval. 2007;12(10). http://pareonline.net/pdf/v12n10.pdf. Accessed October 28, 2013.Google Scholar. Imechukuliwa 09.06.2020

  6. Institute of Medicine.  Finding What Works in Health Care: Standards for Systematic Reviews. Washington, DC: National Academies Press; 2011. http://www.iom.edu/Reports/2011/Finding-What-Works-in-Health-Care-Standards-for-systematic-Reviews.aspx. Imechukuliwa 09.06.2020

  7. https://www.uptodate.com/contents/high-blood-pressure-in-adults-beyond-the-basics?topicRef=4415&source=see_link. Imechukuliwa 10.06.2020

  8. https://www.uptodate.com/contents/high-blood-pressure-diet-and-weight-beyond-the-basics.Imechukuliwa 10.06.2020

  9. Hypertension. https://jamanetwork.com/journals/jama/fullarticle/1791497. Imechukuliwa 11.06.2020

  10. Dash Diet- 365 Days of Low Salt, Dash Diet Recipes For Lower Cholesterol, Lower Blood Pressure and Fat Loss Without Medication ( PDFDrive.com )

bottom of page