top of page

Mwandishi:

Dkt. Benjamin L, MD,

Mhariri:

Dkt. James NL, MD

Imeboreshwa:

26 Septemba 2026, 08:44:23

Mgongo unauma kwenye kiuno, nilitumia dawa za hospital bila suluhu, tiba mbadala inaweza kuwa nini?

Matibabu mbadala inategemea kwanza kujua chanzo cha maumivu ya mgongo kwenye eneo la kiuno, kwa sababu si kila maumivu ya kiuno hutibiwa kwa dawa zilezile.


Maumivu yanaweza kutokana na:

  • Misuli au mishipa ya mgongo kuchoka/kukaza, hasa baada ya kubeba vitu vizito, kukaa muda mrefu au kufanya kazi inayohitaji kuinama.
  • Tatizo la pingili za mgongo, kama diski kubonyea na kubana mshipa.
  • Maambukizi ya njia ya mkojo au figo, hasa kama maumivu yanaambatana na homa, maumivu wakati wa kukojoa au mkojo kubadilika.
  • Mawe kwenye figo, ambayo mara nyingi yanaweza kusababisha maumivu makali upande wa mgongo/kiuno yanayoweza kwenda hadi tumboni au kinena.
  • Kwa wanawake, baadhi ya matatizo ya mfumo wa uzazi yanaweza pia kusababisha maumivu yanayohisiwa sehemu ya chini ya mgongo.

Kwa hiyo, kama dawa za hospitali hazijasaidia, si vizuri kuanza dawa za kienyeji au dawa nyingine bila kujua chanzo. Uchunguzi unaweza kuhusisha kuangalia historia ya maumivu, uchunguzi wa mwili na vipimo kama mkojo, damu au picha za mgongo/figo kulingana na dalili.


Wakati unasubiri uchunguzi, epuka kubeba vitu vizito na kukaa au kulala katika mkao unaoongeza maumivu.


Kama una udhaifu au ganzi miguuni, kushindwa kudhibiti mkojo/kubwa, homa, maumivu makali yanayoanza ghafla, au maumivu baada ya kuanguka/kupata jeraha, nenda hospitalini haraka.


Vipimo vinavyoweza kuhitajika ni:


  • Kipimo cha mkojo: kuangalia maambukizi ya njia ya mkojo au dalili zinazoweza kuashiria tatizo la figo.
  • Vipimo vya damu: kama kuna dalili za maambukizi au daktari anaona kuna sababu nyingine inayohitaji kuchunguzwa.
  • Ultrasound ya figo na njia ya mkojo: kama kuna dalili zinazofanya daktari ashuku mawe au tatizo la figo.
  • X-ray ya mgongo: inaweza kuhitajika katika baadhi ya hali, hasa kama kuna historia ya jeraha au tatizo la mifupa linaloshukiwa.
  • MRI ya mgongo: hufanyika zaidi kama kuna dalili za kubanwa kwa mishipa, kama maumivu yanayoshuka mguuni, ganzi au udhaifu, au kama maumivu yanaendelea licha ya matibabu.

Kwa hiyo, anza kwa kumuona daktari kwa uchunguzi wa mwili, kisha vipimo vitachaguliwa kulingana na dalili zako. Usifanye MRI au vipimo vyote bila sababu maalumu.

ULY CLINIC inakushauri uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ile baada ya kusoma majibu haya.

Kupata ushauri zaidi au tiba kutoka kwa daktari wa ULY CLINIC bofya hapa au tumia linki ya Pata tiba

Imeandikwa,

7 Septemba 2026, 23:41:18

​

bottom of page