top of page

Mwandishi:

Mhhariri

ULY CLINIC

ULY CLINIC

Imeboreshwa:

21 Julai 2026, 05:20:41

Maambukizi kwenye mfumo wa mkojo

Maambukizi kwenye mfumo wa mkojo

Maambukizi kwenye mfumo wa mkojo au maambukizi kwenye njia ya mkojo (Urinary Tract Infection - UTI) ni mojawapo ya magonjwa yanayotokea mara nyingi kwa binadamu. Ingawa wanawake huathirika zaidi kutokana na maumbile yao, ugonjwa huu unaweza pia kuwapata wanaume, watoto na wazee.


UTI hutokea pale bakteria au vijidudu vingine vinapoingia kwenye mfumo wa mkojo na kuanza kuzaliana. Mara nyingi maambukizi huanzia kwenye kibofu cha mkojo, lakini yanaweza kuenea hadi kwenye figo ikiwa hayatatibiwa mapema.


Kwa wanawake, mrija unaotoa mkojo (yurethra) ni mfupi kuliko wa wanaume. Hali hii hurahisisha bakteria kufika kwenye kibofu kwa urahisi zaidi. Hata hivyo, wanaume pia wanaweza kupata UTI, hasa wanapokuwa na matatizo ya tezi dume, mawe kwenye njia ya mkojo, kuziba kwa mkojo au matumizi ya muda mrefu ya mpira wa mkojo (katheta).


Kwa watoto, UTI inaweza kuwa ishara ya tatizo la kuzaliwa nalo kwenye mfumo wa mkojo, hivyo ni muhimu kufanyiwa uchunguzi wa kina, hasa ikiwa maambukizi yanajirudia.


Mfumo wa mkojo una sehemu gani?

Mfumo wa mkojo unaundwa na viungo vinne vikuu:

  • Figo mbili zinazochuja damu na kutengeneza mkojo.

  • Mirija miwili ya yureta inayosafirisha mkojo kutoka figoni kwenda kwenye kibofu.

  • Kibofu cha mkojo kinachohifadhi mkojo.

  • Yurethra, ambao ni mrija unaotoa mkojo kutoka kwenye kibofu kwenda nje ya mwili.

Kwa kawaida mfumo huu huwa hauna bakteria. Lakini bakteria wanapoingia na kushinda kinga ya mwili, husababisha maambukizi.


UTI inaweza kutokea sehemu gani?

Madaktari hugawanya UTI katika aina mbili kuu.


1. Maambukizi ya mfumo wa chini wa mkojo

Haya huhusisha:

  • Kibofu cha mkojo (sistaitisi)

  • Yurethra (yurethraitisi)

Hii ndiyo aina inayotokea mara nyingi zaidi.


2. Maambukizi ya mfumo wa juu wa mkojo

Haya huhusisha:

  • Yureta

  • Figo (payelonephraitisi)

Aina hii ni hatari zaidi kwa sababu inaweza kuharibu figo ikiwa haitatibiwa mapema. Wakati mwingine maambukizi yanaweza kwenda kwenye damu na kuamsha mwitikio wa kinga ya mwili dhidi ya maambukizi unaoanza kuharibu tishu na viungo vya mwili wenyewe(sepsisi), hali hii ni dharura ya kitabibu.


UTI hutokeaje?

Katika hali ya kawaida, mwili una njia nyingi za kujikinga dhidi ya maambukizi.

  • Mkojo wenyewe husaidia kusafisha bakteria wanaoingia kwenye njia ya mkojo.

  • Pia mkojo una kemikali zinazozuia baadhi ya bakteria kuongezeka.

  • Zaidi ya hayo, kinga ya mwili hufanya kazi ya kuharibu vijidudu vinavyojaribu kuingia kwenye mfumo wa mkojo.

  • Lakini wakati mwingine bakteria wanaweza kushinda ulinzi huu. Wanaweza kushikamana kwenye ukuta wa kibofu, kuanza kuzaliana na kusababisha maambukizi.

  • Ikiwa hawatatibiwa mapema, wanaweza kupanda kupitia ureta hadi kwenye figo.


Kwa nini baadhi ya watu hupata UTI mara kwa mara?

Baadhi ya watu hupata UTI mara nyingi kuliko wengine. Hii inaweza kusababishwa na:

  • bakteria wenye uwezo mkubwa wa kushikamana kwenye kibofu;

  • kinga ya mwili kuwa dhaifu;

  • kutokumaliza dozi ya antibiotiki;

  • matumizi ya antibiotiki yasiyo sahihi ambayo husababisha usugu wa bakteria;

  • matatizo ya kuzaliwa nayo kwenye mfumo wa mkojo;

  • mawe kwenye figo au kibofu;

  • kuziba kwa njia ya mkojo;

  • kisukari kisichodhibitiwa;

  • matumizi ya muda mrefu ya catheter.

Kwa wanawake wengine, UTI inaweza kujirudia baada ya kushiriki tendo la ndoa. Kwa wazee, matatizo ya kutokumaliza kutoa mkojo huongeza hatari ya maambukizi.


Ni vimelea gani husababisha UTI?

Zaidi ya asilimia 70 hadi 90 ya UTI husababishwa na bakteria aitwaye Escherichia coli (E. coli).

Bakteria huyu huishi kwa kawaida kwenye utumbo bila kusababisha madhara. Tatizo hutokea anapoingia kwenye njia ya mkojo.

Bakteria wengine wanaoweza kusababisha UTI ni:

  • Klebsiella species

  • Proteus species

  • Enterococcus faecalis

  • Staphylococcus saprophyticus

  • Enterobacter species

  • Pseudomonas aeruginosa (hasa hospitalini)


Mara chache UTI inaweza kusababishwa na fangasi kama Candida, hasa kwa wagonjwa wenye kisukari, wanaotumia catheter kwa muda mrefu au wenye kinga dhaifu.


Bakteria hawa huingiaje kwenye mfumo wa mkojo?

Njia kuu ni kupanda kutoka sehemu za siri kwenda kwenye yurethra. Kwa wanawake, bakteria wanaweza kutoka eneo la haja kubwa na kufika karibu na uke au yurethra. Ndiyo maana wataalamu wa afya hushauri kujisafisha kutoka mbele kwenda nyuma baada ya kujisaidia ili kupunguza uwezekano wa kusafirisha bakteria.


Kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini, bakteria wanaweza kuingia kupitia catheter ikiwa haitatunzwa vizuri au ikiwa itawekwa bila kufuata kanuni za usafi.


Nani yuko kwenye hatari kubwa ya kupata UTI?

Mtu yeyote anaweza kupata UTI, lakini hatari huwa kubwa zaidi kwa:

  • wanawake;

  • wajawazito;

  • watoto wadogo;

  • wazee;

  • wagonjwa wa kisukari;

  • watu wenye mawe kwenye figo au kibofu;

  • watu wenye kuziba kwa njia ya mkojo;

  • wanaotumia catheter;

  • waliopandikizwa figo;

  • wanaotumia dawa zinazoshusha kinga ya mwili;

  • wenye matatizo ya kuzaliwa nayo kwenye mfumo wa mkojo.

Kwa wanaume wenye umri mkubwa, kuvimba kwa tezi dume (prostate) kunaweza kuzuia mkojo kutoka vizuri na kuongeza hatari ya UTI.


Je, UTI huambukizwa kwa kufanya ngono?

UTI si ugonjwa wa zinaa, hata hivyo, kushiriki tendo la ndoa kunaweza kuongeza uwezekano wa bakteria kusukumwa kuelekea kwenye yurethra, hasa kwa wanawake. Ndiyo maana baadhi ya wanawake hupata UTI baada ya kufanya ngono.


Ikiwa mtu ana dalili kama kutokwa na usaha ukeni au kwenye uume, vidonda sehemu za siri au maumivu makali wakati wa kujamiiana, daktari anaweza kufikiria pia uwezekano wa magonjwa ya zinaa badala ya UTI pekee.


Je, UTI inaweza kuambukiza kutoka mtu mmoja kwenda mwingine?

Kwa kawaida hapana, huwezi kupata UTI kwa kushikana mikono, kukumbatiana, kutumia choo kimoja au kula chakula pamoja.


Kinachotokea ni kwamba bakteria wanaoishi mwilini mwa mtu mwenyewe huingia kwenye mfumo wa mkojo na kusababisha maambukizi.


Bakteria kwenye mkojo bila dalili ni nini?

Wakati mwingine vipimo vinaweza kuonyesha bakteria kwenye mkojo lakini mgonjwa hana dalili zozote.

Hali hii huitwa bakteria kwenye mkojo bila dalili. Kwa watu wengi, hali hii haihitaji antibiotiki. Hata hivyo, kwa wanawake wajawazito na baadhi ya wagonjwa wanaotarajiwa kufanyiwa upasuaji kwenye mfumo wa mkojo, hali hii hutibiwa kwa sababu inaweza kuongeza hatari ya kupata matatizo makubwa.


Dalili za UTI ni zipi?

Dalili hutegemea sehemu ya mfumo wa mkojo iliyoathirika. Watu wengi wenye maambukizi kwenye kibofu hupata dalili za ghafla ambazo huanza ndani ya saa chache au siku moja hadi mbili.

Dalili zinazojitokeza mara nyingi ni:

  • Maumivu au kuwaka wakati wa kukojoa.

  • Kukojoa mara kwa mara hata kama mkojo ni kidogo.

  • Kuhisi kubanwa na mkojo muda wote.

  • Kushindwa kujizuia mkojo.

  • Maumivu chini ya kitovu au kwenye kibofu.

  • Mkojo kuwa na harufu kali isiyo ya kawaida.

  • Mkojo kuwa wa mawingu au wenye ukungu.

  • Wakati mwingine damu inaweza kuonekana kwenye mkojo.

Baadhi ya wagonjwa hupata dalili chache tu, huku wengine wakipata dalili nyingi kwa wakati mmoja.


Dalili za UTI iliyofika kwenye figo

Maambukizi yanapofika kwenye figo huwa makubwa zaidi kuliko yale ya kwenye kibofu.

Dalili zinaweza kujumuisha:

  • Homa kali.

  • Kutetemeka.

  • Maumivu makali pembeni mwa mgongo chini ya mbavu.

  • Kichefuchefu.

  • Kutapika.

  • Mwili kuchoka sana.

  • Kizunguzungu.

Mtu mwenye dalili hizi anapaswa kufika hospitali haraka kwa sababu anaweza kuhitaji matibabu ya haraka na wakati mwingine kulazwa.


Dalili za UTI kwa watoto

Kwa watoto wachanga na walio chini ya miaka miwili, UTI inaweza isiwe na dalili zinazofanana na za watu wazima.

Mtoto anaweza kuwa na:

  • Homa bila sababu inayoeleweka.

  • Kukataa kunyonya au kula.

  • Kulia sana.

  • Kutapika.

  • Kushindwa kuongeza uzito.

  • Kusinzia kupita kiasi.


Kwa watoto wakubwa zaidi unaweza kuona:

  • Maumivu wakati wa kukojoa.

  • Kukojoa kitandani ghafla baada ya kuwa ameacha tabia hiyo.

  • Kukojoa mara kwa mara.

  • Maumivu ya tumbo.

  • Harufu kali ya mkojo.

Kwa mtoto mwenye homa isiyoeleweka, daktari anaweza kuagiza kipimo cha mkojo ili kutafuta UTI.


Dalili za UTI kwa wanaume

Ingawa UTI si ya kawaida kwa wanaume, ikitokea mara nyingi huhitaji uchunguzi wa kina kutafuta sababu.

Dalili zinaweza kuwa:

  • Maumivu wakati wa kukojoa.

  • Kukojoa mara kwa mara.

  • Kukojoa usiku mara nyingi.

  • Maumivu chini ya kitovu.

  • Damu kwenye mkojo.

  • Homa ikiwa maambukizi ni makubwa.

Kwa wanaume wenye umri mkubwa, UTI inaweza kuhusiana na kuvimba kwa tezi dume au kuziba kwa njia ya mkojo.


Je, harufu mbaya ya mkojo pekee inamaanisha una UTI?

Si lazima, harufu ya mkojo inaweza kubadilika kutokana na:

  • kunywa maji kidogo;

  • kula vyakula fulani kama asparagus;

  • kutumia baadhi ya vitamini;

  • dawa mbalimbali.

Ikiwa harufu mbaya inaambatana na maumivu wakati wa kukojoa, homa au kukojoa mara kwa mara, kuna uwezekano mkubwa wa kuwa na maambukizi.


Je, mkojo wenye rangi ya mawingu ni dalili ya UTI?

Unaweza kuwa ndiyo, lakini si kila wakati.

Mkojo unaweza kuwa wa mawingu kutokana na:

  • bakteria;

  • chembechembe nyeupe za damu;

  • chumvi mbalimbali kwenye mkojo;

  • upungufu wa maji mwilini.

Kwa hiyo kipimo cha mkojo ndicho huthibitisha sababu.


Ni wakati gani unapaswa kuwahi hospitalini?

Usisubiri kuona kama dalili zitapungua zenyewe ikiwa una mojawapo ya dalili hizi:

  • Homa kali.

  • Kutetemeka.

  • Kutapika mara kwa mara.

  • Maumivu makali ya ubavu au mgongo.

  • Kushindwa kukojoa kabisa.

  • Damu nyingi kwenye mkojo.

  • UTI wakati wa ujauzito.

  • Mtoto mchanga mwenye homa.

  • Mzee anayechanganyikiwa ghafla na kupata homa.

Dalili hizi zinaweza kuashiria maambukizi makubwa yanayohitaji matibabu ya haraka.


Vipimo vya UTI vinafanywaje?

Baada ya daktari kuchukua historia ya ugonjwa na kukuchunguza, anaweza kuagiza vipimo mbalimbali.

Vipimo vinavyoombwa hutegemea umri wa mgonjwa, dalili alizonazo na ukubwa wa maambukizi.


1. Kipimo cha mkojo (Urinalisisi)

Hiki ndicho kipimo kinachofanyika mara nyingi.

Huangalia:

  • chembe nyeupe za damu;

  • damu;

  • nitrite;

  • bakteria;

  • protini;

  • sukari;

  • vitu vingine vinavyoweza kuonyesha ugonjwa.


2. Kuotesha mkojo na kuangalia mwitikio kwenye dawa

Hiki ndiyo kipimo bora zaidi cha kuthibitisha bakteria aliyesababisha UTI.

Pia huonyesha antibiotiki zipi zinaweza kumuua bakteria huyo na zipi hazifanyi kazi kutokana na usugu.

Kipimo hiki ni muhimu hasa kwa:

  • UTI zinazojirudia;

  • wajawazito;

  • wanaume;

  • watoto;

  • wagonjwa waliolazwa hospitalini;

  • wagonjwa wasiopona baada ya kutumia antibiotiki.


3. Vipimo vya damu

Kwa wagonjwa wenye maambukizi makubwa, daktari anaweza kuagiza:

  • Picha kamili ya damu (FBC)

  • Kipimo cha utendaji kazi wa figo (Creatinine na Urea)

  • Kimimo cha elekrolaiti

  • Kuotesha damu ikiwa kunashaka maambukizi yameingia kwenye damu.


4. Ultrasound

Ultrasound inaweza kuhitajika ikiwa:

  • UTI zinajirudia mara kwa mara.

  • Kuna mawe kwenye figo.

  • Kuna shaka ya kuziba kwa njia ya mkojo.

  • Kuna uvimbe.

  • Mgonjwa haponi licha ya matibabu.


5. CT Scan

CT scan hutumika kwa wagonjwa wachache wenye:

  • jipu kwenye figo;

  • mawe makubwa;

  • kuziba kwa mfumo wa mkojo;

  • maambukizi makubwa yasiyoeleweka.


Matibabu ya UTI

Matibabu hutegemea:

  • umri;

  • jinsia;

  • ujauzito;

  • ukubwa wa maambukizi;

  • bakteria aliyesababisha ugonjwa;

  • usugu wa antibayotikikatika eneo husika.

Ndiyo maana si wagonjwa wote hupewa dawa zinazofanana.


Je, kila mtu mwenye UTI hupewa antibayotiki zilezile?

Hapana, antibayotiki huchaguliwa kulingana na:

  • aina ya bakteria;

  • eneo la maambukizi;

  • ujauzito;

  • mzio wa dawa;

  • kazi ya figo;

  • matokeo ya kipimo cha kuotesha mkojo ikiwa yamepatikana.

Kutumia antibayotiki bila ushauri wa daktari kunaweza kuongeza usugu wa bakteria na kufanya UTI iwe ngumu kutibu baadaye.


Kwa nini ni muhimu kumaliza dozi ya dawa?

Baadhi ya watu huacha kutumia dawa mara wanapojisikia vizuri.

Hili ni kosa.

Kuacha dawa mapema kunaweza:

  • kurudisha maambukizi;

  • kufanya bakteria wasife wote;

  • kuongeza usugu wa antibayotiki.

Hivyo, maliza dawa kama ulivyoelekezwa hata kama dalili zimekwisha.


UTI wakati wa ujauzito

UTI ni mojawapo ya maambukizi yanayotokea mara nyingi kwa wajawazito.

Mabadiliko ya homoni pamoja na kukua kwa mfuko wa uzazi hufanya mkojo utoke polepole zaidi, hali inayorahisisha bakteria kuzaliana.

Ikiwa haitatibiwa, UTI kwa mjamzito inaweza kuongeza hatari ya:

  • maambukizi ya figo;

  • uchungu wa kujifungua kabla ya wakati;

  • mtoto kuzaliwa na uzito mdogo.

Ndiyo sababu wajawazito wengi hupimwa mkojo mara kwa mara wanapohudhuria kliniki hata kama hawana dalili.


Je, UTI inaweza kupona yenyewe?

Kwa baadhi ya wanawake wenye maambukizi madogo sana, dalili zinaweza kupungua bila antibayotikii.

Hata hivyo, haiwezekani kujua ni nani atakayepata nafuu bila matibabu na nani atapata madhara makubwa.

Kwa hiyo, mtu mwenye dalili za UTI anashauriwa kufika kwenye kituo cha afya ili apimwe na kupata ushauri sahihi badala ya kusubiri ugonjwa ujiponye wenyewe.


Madhara ya UTI isipotibiwa

Watu wengi hudhani kuwa UTI ni ugonjwa mdogo unaoweza kupotea wenyewe. Ingawa baadhi ya maambukizi yanaweza kuwa mepesi, UTI isipotibiwa kwa wakati inaweza kusababisha matatizo makubwa, hasa kwa watoto, wajawazito, wazee na watu wenye kinga dhaifu.


Bakteria wanaweza kuendelea kuzaliana kwenye kibofu na baadaye kupanda kupitia mirija ya ureta hadi kwenye figo. Maambukizi yakifika kwenye figo huwa makubwa zaidi na yanaweza kuharibu tishu za figo ikiwa hayatadhibitiwa mapema.


Kwa wagonjwa wengine, bakteria wanaweza kuingia kwenye damu na kusababisha hali hatari iitwayo sepsisi, ambayo inaweza kuhatarisha maisha na kuhitaji matibabu ya haraka hospitalini.


Matatizo yanayoweza kutokea kutokana na UTI

UTI isipotibiwa au ikitokea mara kwa mara inaweza kusababisha:

  • Maambukizi ya figo (Payelonephraitisi).

  • Jipu ndani ya figo, ingawa ni nadra.

  • Maambukizi kuingia kwenye damu (Sepsisi).

  • Uharibifu wa kudumu wa figo kwa baadhi ya wagonjwa wenye maambukizi makubwa au yanayojirudia.

  • Kujifungua kabla ya wakati kwa wajawazito.

  • Mtoto kuzaliwa na uzito mdogo.

  • Kurudiarudia kwa UTI.

  • Kuongezeka kwa usugu wa bakteria dhidi ya antibayotiki kutokana na matumizi mabaya ya dawa.

Kwa watoto, maambukizi ya figo yanayojirudia yanaweza kuongeza hatari ya kupata makovu kwenye figo, ndiyo maana ni muhimu kutibu UTI mapema.


UTI inayojirudia ni nini?

Mtu husemwa ana UTI inayojirudia ikiwa:

  • anapata UTI mara mbili au zaidi ndani ya miezi sita, au

  • anapata UTI mara tatu au zaidi ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Kwa wanawake, hali hii hutokea mara nyingi zaidi kuliko kwa wanaume.

Ikiwa UTI inajirudia mara kwa mara, daktari anaweza kupendekeza vipimo vya ziada ili kutafuta sababu ya msingi badala ya kuendelea kutumia antibayotiki kila mara.


Sababu zinazoweza kufanya UTI ijirudie

Baadhi ya sababu ni:

  • Kutokumaliza dozi ya antibayotiki.

  • Kutumia antibayotiki bila ushauri wa daktari.

  • Kisukari kisichodhibitiwa.

  • Mawe kwenye figo au kibofu.

  • Kuziba kwa njia ya mkojo.

  • Matatizo ya kuzaliwa nayo kwenye mfumo wa mkojo.

  • Kuwa na mkojo unaobaki kwenye kibofu baada ya kukojoa.

  • Matumizi ya muda mrefu ya catheter.

  • Kushuka kwa kinga ya mwili.

Kwa wanawake waliokoma hedhi, kupungua kwa homoni ya estrojeni kunaweza kubadilisha mazingira ya uke na kuongeza uwezekano wa kupata UTI mara kwa mara.


Je, kunywa maji mengi husaidia?

Kunywa maji ya kutosha husaidia kuongeza kiasi cha mkojo kinachotolewa. Hii inaweza kusaidia kusafisha baadhi ya bakteria waliopo kwenye njia ya mkojo kabla hawajashikamana na ukuta wa kibofu.

Hata hivyo, kunywa maji pekee hakuponyi UTI iliyokwisha kusababisha maambukizi. Ikiwa una dalili za UTI, unapaswa kufika hospitalini kwa uchunguzi na matibabu sahihi.


Kiasi cha maji anachohitaji mtu hutegemea umri, hali ya afya, hali ya hewa na shughuli anazofanya. Watu wenye magonjwa ya figo au moyo wanapaswa kufuata ushauri wa daktari kuhusu kiwango cha maji wanachopaswa kunywa.


Je, juisi ya cranberry inaweza kutibu UTI?

Juisi au bidhaa za cranberry si tiba ya UTI. Baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa cranberry inaweza kusaidia kupunguza hatari ya kurudia kwa UTI kwa baadhi ya watu, hasa wanawake wanaopata maambukizi mara kwa mara. Hata hivyo, ushahidi si wa kutosha kusema kuwa kila mtu atanufaika nayo.

Ikiwa tayari una UTI, usitegemee cranberry badala ya matibabu yaliyopendekezwa na daktari.


Je, vitamini C huzuia UTI?

Hakuna ushahidi wa kutosha unaothibitisha kuwa vitamini C huzuia au kutibu UTI kwa watu wote.

Ingawa vitamini C ni muhimu kwa afya ya mwili na kinga, haitakiwi kutumiwa kama mbadala wa antibayotiki au matibabu mengine yaliyothibitishwa.


Je, probayotiki zina nafasi gani?

Probayotiki ni bakteria wazuri wanaopatikana kwenye baadhi ya vyakula na virutubisho. Baadhi ya tafiti zinaonyesha zinaweza kusaidia kurejesha uwiano wa bakteria kwenye uke kwa baadhi ya wanawake, lakini bado ushahidi haujathibitisha kuwa zinazuia UTI kwa kila mtu. Kwa hiyo, matumizi yake yanapaswa kuzingatia ushauri wa mtaalamu wa afya.


Njia za kujikinga na UTI

Ingawa si UTI zote zinaweza kuzuilika, hatua zifuatazo zinaweza kusaidia kupunguza hatari:

  • Kunywa maji ya kutosha kila siku.

  • Usizuie mkojo kwa muda mrefu bila sababu.

  • Kukojoa unapohisi haja.

  • Kudumisha usafi wa sehemu za siri.

  • Kwa wanawake, kujisafisha kutoka mbele kwenda nyuma baada ya kujisaidia.

  • Kubadilisha pedi au nepi mara kwa mara.

  • Kudhibiti kisukari vizuri.

  • Kutumia catheter pale inapokuwa lazima tu na kuitunza kwa usahihi.

  • Kufuata maelekezo ya daktari unapopewa antibayotiki.

Kwa wanawake wanaopata UTI mara kwa mara baada ya kushiriki tendo la ndoa, kukojoa baada ya tendo kunaweza kusaidia kupunguza uwezekano wa bakteria kubaki kwenye yurethra, ingawa si kinga ya asilimia 100.


Mambo ambayo hayajathibitishwa kusababisha UTI

Kuna imani nyingi zinazosambaa mitandaoni ambazo hazijathibitishwa kisayansi.

Kwa mfano:

  • Kukaa kwenye sakafu baridi pekee hakusababishi UTI.

  • Kunywa soda hakusababishi moja kwa moja UTI.

  • Kutokunywa juisi ya cranberry hakusababishi UTI.

  • Kula pilipili si sababu ya UTI.

  • Uchawi hauhusiki na chanzo cha UTI.

UTI husababishwa na vijidudu, hasa bakteria, na si mambo hayo.


Makosa ambayo watu wengi hufanya

Makosa yanayoweza kufanya UTI kuwa ngumu kutibu ni pamoja na:

  • Kununua antibayotiki bila kupimwa.

  • Kutokumaliza dozi ya dawa.

  • Kutumia dawa zilizobaki nyumbani.

  • Kutumia dawa za mtu mwingine.

  • Kurudia antibayotiki ileile kila unapohisi dalili bila ushauri wa daktari.

  • Kutokwenda hospitali dalili zinaposhindikana kuisha.

Tabia hizi zinaongeza usugu wa bakteria na kufanya matibabu ya baadaye kuwa magumu zaidi.


Je, UTI inaweza kuzuilika kabisa?

Hakuna njia inayoweza kuzuia UTI kwa asilimia 100. Hata hivyo, kufuata kanuni za usafi, kunywa maji ya kutosha, kutibu magonjwa yanayoongeza hatari kama kisukari, na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya kunaweza kupunguza uwezekano wa kupata maambukizi.


Kwa watu wanaopata UTI mara kwa mara, daktari anaweza kupendekeza mikakati maalumu ya kinga kulingana na sababu ya maambukizi yao.


Hitimisho

Maambukizi kwenye mfumo wa mkojo ni ugonjwa unaoweza kumpata mtu wa umri wowote, ingawa wanawake huathirika zaidi kutokana na maumbile yao. Dalili kama maumivu wakati wa kukojoa, kukojoa mara kwa mara na kuhisi kubanwa na mkojo hazipaswi kupuuzwa, kwani zinaweza kuwa ishara ya UTI.

Habari njema ni kwamba UTI nyingi hupona vizuri zikigunduliwa mapema na kutibiwa kwa dawa sahihi. Kuepuka kujitibu bila ushauri wa mtaalamu, kumaliza dozi ya antibayotiki na kufuata njia za kujikinga kunaweza kupunguza hatari ya maambukizi na madhara yake.


Maswali yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu maambukizi kwenye mfumo wa mkojo (UTI)

1. Je, UTI inaweza kupona bila kutumia antibayotiki?

Hili ni swali ambalo huulizwa mara nyingi sana. Ukweli ni kwamba si kila mtu mwenye dalili za UTI atahitaji matibabu yanayofanana, lakini kwa watu wengi wenye UTI iliyothibitishwa kusababishwa na bakteria, antibayotiki ndiyo tiba kuu. Watu wengine huona maumivu yanapungua baada ya kunywa maji mengi au kupumzika na kudhani wamepona, ilhali bakteria bado wapo kwenye mfumo wa mkojo. Hali hii inaweza kufanya ugonjwa urudi baada ya muda mfupi au kuendelea kuharibu mfumo wa mkojo bila mgonjwa kujua.


Kwa baadhi ya wanawake wenye dalili nyepesi sana, mwili unaweza kuondoa maambukizi wenyewe. Hata hivyo, haiwezekani kutambua nyumbani ni nani atakayepata nafuu bila dawa na nani atakayepata maambukizi makubwa yanayofika kwenye figo. Ndiyo maana wataalamu wa afya hushauri mtu mwenye dalili za UTI afanyiwe uchunguzi kabla ya kuamua kutotumia antibayotiki.


Ikiwa una homa, maumivu makali ya mgongo, kutapika, ujauzito, kisukari au unaona damu nyingi kwenye mkojo, usisubiri kuona kama ugonjwa utapona wenyewe. Hali hizi zinahitaji uchunguzi na matibabu ya haraka ili kuzuia madhara makubwa.

2. Kwa nini napata UTI kila mwezi licha ya kutumia dawa kila ninapougua?

Kupata UTI mara kwa mara si kawaida, na mara nyingi huwa kuna sababu inayochangia. Baadhi ya watu hutibiwa kila wanapougua lakini hawafanyi uchunguzi wa kutafuta chanzo cha maambukizi yanayorudi. Sababu zinaweza kuwa mawe kwenye figo, kisukari kisichodhibitiwa, matatizo ya mfumo wa mkojo, bakteria waliopata usugu wa dawa au kutokumaliza dozi ya antibayotiki.


Kwa wanawake, UTI inaweza kujirudia baada ya kushiriki tendo la ndoa, hasa kama tayari wana historia ya maambukizi ya mara kwa mara. Kwa wanaume, UTI inayorudia inaweza kuwa ishara ya tatizo la tezi dume, kuziba kwa njia ya mkojo au maambukizi kwenye tezi hiyo. Kwa watoto, UTI inayorudia inaweza kuashiria tatizo la kuzaliwa nalo kwenye mfumo wa mkojo ambalo linahitaji uchunguzi wa kina.


Ikiwa umeshapata UTI mara tatu au zaidi ndani ya mwaka mmoja, ni muhimu kumwona daktari kwa uchunguzi zaidi. Unaweza kuhitaji kipimo cha kuotesha mkojo, picha za mfumo wa mkojo au vipimo vingine ili kubaini chanzo halisi badala ya kuendelea kutumia antibayotiki kila unapopata dalili.

3. Je, kufanya mapenzi mara nyingi husababisha UTI?

Kufanya mapenzi si chanzo cha moja kwa moja cha UTI, lakini kunaweza kuongeza uwezekano wa bakteria kufika kwenye mrija wa mkojo, hasa kwa wanawake. Wakati wa tendo la ndoa, msuguano unaweza kusogeza bakteria waliopo karibu na sehemu za siri kuelekea kwenye yurethra, ambapo wanaweza kuingia kwenye kibofu na kusababisha maambukizi.


Hii haimaanishi kwamba mtu anapaswa kuacha kushiriki tendo la ndoa kwa sababu ya kuogopa UTI. Badala yake, ni muhimu kufuata kanuni za usafi, kukojoa baada ya tendo la ndoa ikiwa inawezekana na kunywa maji ya kutosha. Hatua hizi zinaweza kusaidia kupunguza hatari kwa baadhi ya watu, ingawa hazitoi kinga ya asilimia 100.


Ikiwa kila unaposhiriki tendo la ndoa unapata dalili za UTI, usiishie kununua dawa kila mara. Muone daktari ili afanye uchunguzi na kubaini kama kweli ni UTI au kuna tatizo jingine kama maambukizi ya uke, magonjwa ya zinaa au hali nyingine inayofanana na UTI.

4. Je, UTI inaweza kusababisha ugumba?

Kwa ujumla, UTI ya kawaida haihesabiwi kuwa sababu ya ugumba kwa wanawake au wanaume. Maambukizi mengi yanayohusisha kibofu cha mkojo hupona vizuri yakitibiwa mapema na hayaathiri uwezo wa kupata watoto.


Hata hivyo, watu wengi huchanganya UTI na magonjwa ya zinaa au maambukizi ya mfumo wa uzazi. Magonjwa kama kisonono na klamidia yasipotibiwa yanaweza kusababisha ugonjwa wa uvimbe kwenye nyonga (PID) kwa wanawake, ambao unaweza kuharibu mirija ya uzazi na kuongeza hatari ya ugumba.


Kwa wanaume, baadhi ya maambukizi yanaweza kuathiri korodani au sehemu nyingine za mfumo wa uzazi.

Kwa hiyo, ikiwa una maumivu wakati wa kukojoa yanayoambatana na usaha kutoka ukeni au kwenye uume, vidonda sehemu za siri au maumivu wakati wa tendo la ndoa, ni muhimu kupimwa ili kubaini kama tatizo ni UTI pekee au kuna maambukizi mengine yanayohitaji matibabu tofauti.

5. Je, kunywa maji mengi kunaweza kuondoa kabisa bakteria wanaosababisha UTI?

Kunywa maji ya kutosha ni tabia nzuri kwa afya ya mfumo wa mkojo. Maji huongeza kiasi cha mkojo kinachotolewa na hivyo kusaidia kusafisha njia ya mkojo. Hata hivyo, maji hayana uwezo wa kuua bakteria waliokwisha kusababisha maambukizi ndani ya kibofu au figo.


Watu wengine huchelewa kwenda hospitalini wakiamini kuwa kunywa lita nyingi za maji kutatosha kuponya UTI. Wakati mwingine dalili zinaweza kupungua kwa muda, lakini bakteria wanaweza kuendelea kuwepo na baadaye kusababisha maambukizi makubwa zaidi. Hii ni hatari hasa kwa wajawazito, watoto na watu wenye kisukari.


Maji yanapaswa kuonekana kama sehemu ya kusaidia afya ya mfumo wa mkojo, si mbadala wa matibabu. Ikiwa una dalili za UTI, kunywa maji kunaweza kusaidia mwili, lakini bado ni muhimu kupata uchunguzi na matibabu sahihi kulingana na ushauri wa mtaalamu wa afya.

6. Je, kunywa soda, pombe au vinywaji vya kuongeza nguvu husababisha UTI?

Hili ni swali linaloulizwa sana, hasa pale mtu anapopata UTI baada ya kunywa soda au pombe. Ukweli ni kwamba hakuna ushahidi wa kisayansi unaoonyesha kuwa soda, pombe au vinywaji vya kuongeza nguvu husababisha UTI moja kwa moja. Chanzo kikuu cha UTI ni bakteria wanaoingia kwenye mfumo wa mkojo, si aina ya kinywaji unachokunywa.


Hata hivyo, baadhi ya vinywaji vinaweza kufanya dalili za UTI ziwe kali zaidi. Kwa mfano, pombe, kahawa, chai yenye kafeini na baadhi ya soda vinaweza kukera kibofu cha mkojo kwa baadhi ya watu. Mtu mwenye UTI anaweza kuhisi maumivu zaidi wakati wa kukojoa au kuhisi haja ya kukojoa mara kwa mara baada ya kutumia vinywaji hivi. Hii haimaanishi kuwa ndivyo vilivyosababisha maambukizi, bali vinaweza kuongeza usumbufu wa dalili zilizopo.


Ikiwa una UTI, ni vyema kunywa maji ya kutosha na kupunguza matumizi ya pombe au vinywaji vyenye kafeini hadi utakapopona. Endapo dalili zinaendelea licha ya kufanya hivyo, ni muhimu kufika hospitalini kwa uchunguzi na matibabu sahihi badala ya kuamini kuwa kubadilisha aina ya kinywaji pekee kutamaliza tatizo.

7. Je, UTI inaweza kuambukizwa kwa mwenzi wakati wa tendo la ndoa?

UTI yenyewe si ugonjwa wa zinaa, hivyo kwa kawaida haiambukizwi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine wakati wa kufanya mapenzi. Maambukizi mengi ya UTI husababishwa na bakteria wanaotoka kwenye utumbo wa mtu mwenyewe na kuingia kwenye njia ya mkojo. Hivyo, kupata UTI haimaanishi kuwa umeambukizwa na mwenzi wako.


Hata hivyo, tendo la ndoa linaweza kuongeza uwezekano wa bakteria kuingia kwenye mrija wa mkojo, hasa kwa wanawake. Ndiyo maana baadhi ya wanawake hupata UTI baada ya kushiriki tendo la ndoa, ingawa hawajaambukizwa na mwenzi wao. Ikiwa mtu ana maambukizi ya zinaa kama kisonono au klamidia, dalili zake zinaweza kufanana na UTI, jambo linaloweza kuleta mkanganyiko.


Kama wewe au mwenzi wako mna maumivu wakati wa kukojoa yanayoambatana na usaha, vidonda sehemu za siri, kutokwa na uchafu usio wa kawaida au maumivu wakati wa tendo la ndoa, ni muhimu kupimwa magonjwa ya zinaa pamoja na UTI. Hii itasaidia kupata matibabu sahihi na kuzuia maambukizi kuendelea kuenea.

8. Je, UTI inaweza kuchelewesha hedhi?

Hakuna ushahidi unaothibitisha kuwa UTI ya kawaida husababisha hedhi kuchelewa. Mfumo wa mkojo na mfumo wa uzazi ni mifumo tofauti, ingawa viungo vyake vipo karibu. Kwa hiyo, maambukizi kwenye kibofu cha mkojo kwa kawaida hayaathiri mzunguko wa hedhi.


Hata hivyo, mwanamke anaweza kupata UTI na wakati huo huo akachelewa kupata hedhi kutokana na sababu nyingine. Sababu hizo zinaweza kuwa ujauzito, msongo wa mawazo, mabadiliko ya homoni, kupungua au kuongezeka kwa uzito, matumizi ya baadhi ya dawa au magonjwa yanayoathiri homoni. Wakati mwingine maumivu ya nyonga yanayotokana na UTI yanaweza kumfanya mtu afikiri kuchelewa kwa hedhi kunahusiana na maambukizi hayo, ilhali chanzo ni tofauti.


Ikiwa hedhi imechelewa kwa siku kadhaa na umeshiriki tendo la ndoa bila kutumia njia madhubuti ya uzazi wa mpango, ni muhimu kufanya kipimo cha ujauzito. Pia, kama una maumivu makali ya tumbo, kutokwa na damu isiyo ya kawaida au dalili nyingine zinazokusumbua, muone mtaalamu wa afya ili kubaini chanzo halisi.

9. Kwa nini nina maumivu wakati wa kukojoa lakini vipimo vinaonyesha sina UTI?

Maumivu wakati wa kukojoa si dalili inayosababishwa na UTI pekee. Wakati mwingine mtu hupimwa mkojo na vipimo vinaonyesha hakuna bakteria wanaosababisha UTI, lakini bado anaendelea kupata maumivu. Hali hii inaweza kuchanganya na kuwafanya baadhi ya watu kudhani vipimo vimekosea, ilhali kuna sababu nyingine inayohitaji kutafutwa.


Sababu nyingine zinazoweza kusababisha maumivu wakati wa kukojoa ni pamoja na maambukizi ya uke, fangasi ukeni, magonjwa ya zinaa kama kisonono au klamidia, mawe kwenye njia ya mkojo, kuwashwa kwa ngozi kutokana na sabuni au kemikali, kuvimba kwa tezi dume kwa wanaume, au ugonjwa wa kibofu wenye maumivu ya muda mrefu (sistaitisi ya misuli ya kibofu). Kwa hiyo, daktari anaweza kuagiza vipimo vingine kulingana na historia na dalili zako.


Usiendelee kutumia antibayotiki kila unapohisi maumivu wakati wa kukojoa bila kuthibitisha kuwa una UTI. Kutumia dawa zisizohitajika kunaweza kuongeza usugu wa bakteria na pia kuchelewesha kugundua ugonjwa halisi unaokusumbua.

10. Je, mtoto anaweza kupata UTI bila kulalamika maumivu wakati wa kukojoa?

Ndiyo. Hii hutokea mara nyingi kwa watoto wachanga na watoto wadogo ambao bado hawawezi kueleza wanachohisi. Badala ya kulalamika maumivu wakati wa kukojoa, mtoto anaweza kuonyesha dalili zisizo maalumu kama homa, kulia sana, kukataa kula, kutapika, kusinzia kupita kiasi au kushindwa kuongeza uzito vizuri. Ndiyo maana madaktari hufikiria uwezekano wa UTI kwa mtoto mwenye homa isiyoeleweka.


Kwa watoto wakubwa, dalili zinaweza kujumuisha kukojoa mara kwa mara, kukojoa kitandani baada ya kuwa ameacha tabia hiyo, maumivu ya tumbo, harufu kali ya mkojo au maumivu wakati wa kukojoa. Wazazi hawapaswi kupuuza dalili hizi, hasa kama zinajirudia au zinaambatana na homa.


Ikiwa mtoto atapatwa na UTI mara kwa mara, daktari anaweza kupendekeza vipimo vya ziada ili kuchunguza kama kuna tatizo la kuzaliwa nalo kwenye mfumo wa mkojo, mawe kwenye figo au sababu nyingine zinazoongeza hatari ya maambukizi. Kugundua tatizo mapema husaidia kuzuia madhara ya muda mrefu kwenye figo na kuboresha afya ya mtoto.


Imeandikwa:

12 Septemba 2023, 19:11:12

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kitiba baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kubofya 'Pata Tiba,  au ''mawasiliano yetu' chini ya tovuti hii

bottom of page