top of page

Imeandikwa na daktari wa ULY Clinic

 

Dalili za uti kwa watu wazima Uti

Ni ugonjwa wa maambukizi katika mfumo wa mkojo. Mfumo wa mkojo unaundwa na mirija ya ureta, urethra, kibofu cha mkojo na figo.

Mfumo wa mkojo

Mfumo wa mkojo umegawanyika katika sehemu kuu mbili, mfumo wa mkojo wa chini na mfumo wa mkojo wa juu, mfumo wa chini umetengenezwa na mrija wa urethra, kibofu cha mkojo na mirija miwili ya ureta.

Mfumo wa juu wa mkojo umeundwa na figo ambazo huchuja maji mwilini na kutengeneza mkojo.

Maambukizi mfumo wa juu ya mkojo hutokea endapo maambukizi ya mfumo wa chini wa mkojo yamesambaa na kwenda kwenye figo. Maambukizi kwenye figo huwa hatari sana kwani yanaweza kusababisha bakteria kuingia kwenye damu kwa kuwa damu nyingi hupita kwenye figo kwa ajili ya kuchujwa. Hata hivyo maambukizi ya mfumo wa juu wa mkojo huleta dalili kali na hutishia uhai wa mtu.

 

Kazi kubwa ya mfumo wa mkojo ni kuondoa sumu, uchafu na maji ya ziada mwilini

Ni vimelea gani husababisha uti?

Uti kwa asilimia zaidi ya 90 husababishwa na bakteria ainayeitwa ya escherichia coli  ambaye hupatikana katika mfumo wa chakula. Bakteria wengine wanaoweza kusababisha uti ni pamoja na enterococcus faecalis, enterobacteriaceae na staphylococcus saprophyticus, na wakati mwingine uti inaweza kusababishwa na fangasi . Bakteria aina ya staphylococcus saprophyticus huleta  maambukizi kwa wasichana wadogo na dalili zake huamka haraka sana.

 

Dalili za uti ya mfumo wa chini wa mkojo kwa wanawake na wanaume

Dalili anazopata mwanamke ni sawa na zile anazopata mwanaume ambazo ni;

  • Maumivu wakati wa kukojoa

  • Maumivu ya tumbo haswa ya chini ya kitovu

  • Mkojo kutoa  harufu kali pamoja na kubadilika rangi ya mkojo na kuwa kama mawingu

  • Hisia za maumivu ya kuungua na mkojo wakati wa kukojoa

  • Kukojoa mara kwa mara

  • Kushikwa na hamu ya kukojoa ila mkojo unatoka kidogo

  • Homa

  • Uchovu wa mwili

  • Kichefuchefu na kutapika

 

 

Dalili za maambukizi mfumo wa juu wa mkojo zinaweza kuwa ni ;

  • Maumivu  nyuma ya mgongo chini ya mbavu, pande mmoja au pande zote mbili

  • Maumivu ya kiuno

  • Kutokwa na damu wakati wa kukojoa

  • Homa kali

  • Kichefuchefu na kutapika

  • Kutetemeka mwili

 

Endelea kusoma kuhusu UTI kwa kubonyeza hapa

 

Endapo umeona una dalili zilizotajwa hapo juu ni vema ukawasiliana na daktari wako kwa ushauri na tiba

Wasiliana na daktari wa ULY clinic kwa kupiga namba za simu chini ya tovuti hii kwa elimu ushauri na tiba. Au bonyeza hapa kupata tiba

Imeboreshwa 17.03.2020

Rejea

ULY-clinic mfumo wa mkojo
bottom of page