top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

ULY CLINIC

Dkt. Benjamin L, MD

6 Novemba 2026, 17:57:02

Maumivu ya Kichomi usawa wa Kitovu kwa Mjamzito: Sababu, Dalili hatari na Matibabu

Maumivu ya kichomi ubavuni usawa wa kitovu wakati wa ujauzito, hasa miezi 4 hadi 7, mara nyingi husababishwa na mishipa inayoshikilia kizazi (ligamenti duara) ikivutika kizazi kinapokua. Haya ni maumivu ya ghafla ya sekunde chache unapogeuka, kukohoa au kusimama haraka. Gesi, choo kigumu na misuli ya tumbo kunyooka pia huleta maumivu ya aina hii, na kwa kawaida si hatari.


Hata hivyo, maumivu ya mfululizo yanayoongezeka, au yanayoambatana na homa, damu ukeni, kutapika, maumivu ya kiuno au mikazo ya mpangilio, yanaweza kuwa maambukizi ya mkojo au figo, kidole tumbo, kondo kujitenga au uchungu wa mapema. Haya yanahitaji kuonwa hospitali mara moja.


Maumivu ya kichomi pembeni wakati wa ujauzito husababishwa na nini?


Kisababishi

Jinsi maumivu yalivyo

Je, ni hatari?

Mvutiko wa ligamenti duara

Ghafla, kama kuchomwa, upande mmoja au yote, sekunde hadi dakika chache; huongezeka ukigeuka, kukohoa au kucheka

Kawaida, si hatari

Kizazi kukua na kubana viungo

Kuvuta au kuchoma pembeni, misuli ya tumbo kunyooka

Kawaida

Gesi na kufunga choo

Kubana, tumbo kujaa; hupungua baada ya kutoa gesi au kujisaidia

Kawaida, lakini kitibiwe

Maambukizi ya mkojo au figo

Pamoja na kukojoa kwa maumivu, homa, maumivu ya kiuno

Inahitaji matibabu haraka

Kidole tumbo kuvimba

Upande wa kulia, huongezeka kwa saa, pamoja na kichefuchefu na homa

Dharura

Kondo kujitenga

Maumivu makali ya mfululizo, tumbo gumu, mara nyingi damu ukeni

Dharura

Uchungu wa mapema

Mikazo ya mpangilio, maumivu ya mgongo, maji au damu

Dharura kabla ya wiki 37


Kwa kukojoa kwa maumivu soma Kukojoa kwa maumivu.


Mvutiko wa ligamenti duara kwa undani


Ligamenti duara ni mishipa miwili inayoshikilia kizazi kutoka pande zake za juu hadi kwenye kinena. Kadri kizazi kinavyokua, mishipa hii hunyooka kama kamba ya mpira. Mwili ukibadilisha mkao ghafla, mishipa hukaza haraka na kuleta maumivu ya kuchoma upande mmoja, mara nyingi kulia.


  • Huanza zaidi miezi 4 hadi 6 ya ujauzito.

  • Huongezeka ukigeuka kitandani, kusimama ghafla, kukohoa, kupiga chafya au kucheka.

  • Hupungua kwa kupumzika, kujikunja kidogo kuelekea upande wenye maumivu, au kubadilisha mkao taratibu.

  • Haiambatani na homa, damu ukeni wala mikazo ya tumbo zima.


Dalili hatari unazopaswa kuzingatia


  • Maumivu makali yasiyopungua kwa kupumzika, au yanayoongezeka kwa saa.

  • Kutokwa na damu ukeni au maji kutoka ukeni.

  • Homa au kutetemeka.

  • Kichefuchefu kikali au kutapika pamoja na maumivu.

  • Mtoto kupunguza kucheza.

  • Maumivu wakati wa kukojoa au maumivu ya kiuno.

  • Mikazo ya mpangilio kabla ya wiki 37.

  • Kizunguzungu, kuzimia, maumivu makali ya kichwa au kuona vibaya.


Kwa maji kutoka mapema soma Kupasuka chupa ya uzazi kabla ya wakati, na kwa uvimbe wa miguu pamoja na kichwa kuuma soma Kuvimba miguu kwa mjamzito.


Vipimo vinavyoweza kufanyika


  • Uchunguzi wa tumbo kwa mkono na kupima shinikizo la damu na joto.

  • Kipimo cha mkojo na, inapohitajika, kipimo cha kuotesha mkojo.

  • Vipimo vya damu, ikiwemo wingi wa damu na chembe nyeupe.

  • Ultrasound ya mtoto, kondo na viungo vya tumbo.

  • Kusikiliza mapigo ya moyo wa mtoto na kufuatilia mikazo.


Namna ya kupunguza maumivu ya kichomi nyumbani


Ikiwa daktari amethibitisha kuwa maumivu yako si ya hatari (kama vile si appendisaitisi, maambukizi au uchungu wa kujifungua mapema), unaweza kutumia njia zifuatazo kupunguza maumivu kwa usalama ukiwa nyumbani:


Pumzika kwa mkao sahihi


Mkao wa mwili una mchango mkubwa katika kupunguza mvutano wa ligamenti na misuli ya tumbo.


Jinsi ya kufanya:


  • Lala kwa ubavu (hasa ubavu wa kushoto ili kuboresha mzunguko wa damu kwa mtoto).

  • Weka mto kati ya magoti ili kupunguza shinikizo kwenye nyonga.

  • Unaweza pia kuweka mto mdogo chini ya tumbo kwa msaada wa ziada.

  • Epuka kulala chali hasa katika miezi ya pili na ya tatu kwani kunaweza kubana mishipa mikubwa ya damu.


Kwa nini husaidia?


Mkao sahihi hupunguza mvutano wa ligamenti duara (round ligament) na hupunguza msukumo wa uterasi kwenye viungo vya ndani.


Tumia mkanda wa kusaidia tumbo


Mkanda maalum wa wajawazito husaidia kubeba uzito wa tumbo kadri ujauzito unavyoendelea.


Faida zake:


  • Hupunguza mvutano wa ligamenti

  • Husaidia mgongo wa chini

  • Hupunguza maumivu wakati wa kutembea au kusimama


Tahadhari:


  • Usivae kwa muda mrefu kupita kiasi (vaa wakati wa shughuli tu).

  • Hakikisha mkanda haukandamizi sana tumbo.


Fanya mazoezi mepesi ya wajawazito


Mazoezi husaidia kuimarisha misuli ya tumbo na nyonga na kupunguza maumivu.


Mazoezi salama ni pamoja na:


  • Kutembea taratibu kwa dakika 20–30

  • Prenatal stretching

  • Pelvic tilts

  • Yoga maalum ya wajawazito


Kwa nini ni muhimu?


Mazoezi huboresha mzunguko wa damu, hupunguza kukaza kwa misuli, na kusaidia mmeng'enyo wa chakula.


Epuka mazoezi makali au yanayohusisha kuruka.


Epuka kusimama au kukaa muda mrefu


Kusimama muda mrefu huongeza shinikizo kwenye tumbo na nyonga.


Ushauri wa vitendo:


  • Badilisha mkao kila baada ya dakika 30–60

  • Usikunjame ghafla

  • Tumia kiti chenye mgongo mzuri


Kunywa maji mengi na kula vyakula vyenye nyuzinyuzi


Kufunga choo na gesi ni chanzo kikubwa cha maumivu ya kuchoma tumboni wakati wa ujauzito.


Kula zaidi:


  • Matunda (papai, pera, parachichi)

  • Mboga za majani

  • Nafaka zisizokobolewa

  • Maharage na dengu


Kunywa maji angalau glasi 6–8 kwa siku.


Faida zake:


  • Huzuia kufunga choo

  • Hupunguza gesi

  • Hupunguza msongamano tumboni


Epuka harakati za ghafla


Harakati za kushtukiza zinaweza kuvuta ligamenti duara na kusababisha maumivu ya ghafla.


Mfano wa harakati za kuepuka:


  • Kusimama haraka kutoka kitandani

  • Kukohoa au kupiga chafya bila kushika tumbo

  • Kugeuka ghafla


Ushauri:


  • Inuka taratibu

  • Shika tumbo kwa mkono unapokohoa

  • Geuka kwa kutumia mwili mzima badala ya kupindisha kiuno


Tumia Joto la Wastani


Unaweza kuweka kitambaa cha uvuguvugu pembeni mwa tumbo kwa dakika 10–15.


Tahadhari:


  • Usitumie maji ya moto sana

  • Epuka kuweka joto moja kwa moja juu ya tumbo kwa muda mrefu


Joto husaidia kulegeza misuli iliyokaza.


Dawa salama kwa ushauri wa Daktari


Ikiwa maumivu ni makali kiasi, daktari anaweza kupendekeza paracetamol kwa kipimo sahihi. Usitumie dawa bila ushauri wa kitaalamu.


Maswali mengine yanayoulizwa na wasomaji


Je, maumivu ya kichomi pembeni wakati wa ujauzito ni dalili ya kuharibika kwa mimba?


Kwa kawaida maumivu ya kichomi pembeni mwa tumbo usawa wa kitovu si dalili ya kuharibika kwa mimba, hasa kama ni ya muda mfupi na hayana dalili nyingine. Mara nyingi husababishwa na mvutiko wa ligamenti duara (round ligament pain) au mabadiliko ya kawaida ya ujauzito.


Hata hivyo, kama maumivu yanaambatana na:


  • Kutokwa na damu ukeni

  • Maumivu makali ya tumbo la chini

  • Kizunguzungu au kuishiwa nguvu

  • Maumivu yanayoendelea bila kupungua


Ni muhimu kufika hospitali haraka kwa uchunguzi zaidi.


Maumivu ya round ligament huanza wiki ya ngapi?


Maumivu ya round ligament mara nyingi huanza katika trimester ya pili (wiki 13 hadi 28 za ujauzito) wakati uterasi inaanza kukua kwa kasi. Hata hivyo, baadhi ya wanawake wanaweza kuyahisi mapema kidogo au hata kuendelea kuyapata hadi trimester ya tatu.


Maumivu haya:


  • Huwa ya ghafla

  • Huuma upande mmoja

  • Huongezeka wakati wa kubadilisha mkao au kucheka


Je, maumivu upande wa kulia wakati wa ujauzito ni hatari zaidi?


Siyo lazima yawe hatari. Maumivu upande wa kulia mara nyingi ni round ligament pain. Lakini maumivu makali sana upande wa kulia yanaweza kuashiria:


  • Appendicitis (kidole tumbo)

  • Maambukizi ya njia ya mkojo

  • Tatizo la ini au kibofu cha nyongo


Ikiwa maumivu yanaongezeka kwa muda, yanaambatana na homa au kichefuchefu kikali, unapaswa kumuona daktari mara moja.


Je, gesi inaweza kusababisha maumivu makali ya kuchoma tumboni wakati wa ujauzito?


Gesi tumboni wakati wa ujauzito ni sababu ya kawaida ya maumivu ya kichomi. Homoni ya projesteroni hupunguza kasi ya mmeng’enyo wa chakula, na kusababisha:


  • Kujaa gesi

  • Kuvimba tumbo

  • Maumivu ya muda mfupi yanayohama kutoka sehemu moja kwenda nyingine


Maumivu haya mara nyingi hupungua baada ya kutoa hewa au kupata haja kubwa.


Je, maumivu ya kichomi yanaweza kuathiri mtoto tumboni?


Katika hali nyingi, maumivu ya kawaida ya ligamenti au gesi hayaathiri mtoto kabisa. Mtoto yuko salama ndani ya mfuko wa uzazi (kifuko cha maji ya ujauzito) unaomlinda dhidi ya mishtuko midogo ya nje.


Hata hivyo, kama maumivu yanahusiana na maambukizi au uchungu wa mapema, yanaweza kuwa na athari, hivyo uchunguzi wa mapema ni muhimu.


Je, kulala chali kunaweza kuongeza maumivu ya tumbo wakati wa ujauzito?


Kulala chali hasa baada ya miezi mitatu ya ujauzito kunaweza:


  • Kubana mshipa mkubwa wa damu (vena cava)

  • Kupunguza mzunguko wa damu kwa mama na mtoto

  • Kuongeza maumivu ya mgongo na tumbo


Inashauriwa kulala kwa ubavu, hasa ubavu wa kushoto.


Ni lini niende hospitali mara moja kwa maumivu ya kichomi wakati wa ujauzito?


Nenda hospitali haraka ikiwa una:


  • Maumivu makali yasiyovumilika

  • Kutokwa na damu ukeni

  • Homa

  • Kutapika sana

  • Kupungua kwa harakati za mtoto

  • Maumivu yanayoambatana na kukaza kwa tumbo mara kwa mara


Dalili hizi zinaweza kuashiria tatizo linalohitaji matibabu ya haraka.


Je, mazoezi yanaweza kusaidia kupunguza maumivu ya kichomi wakati wa ujauzito?


Mazoezi mepesi kama:


  • Kutembea taratibu

  • Yoga ya wajawazito

  • Pelvic tilt exercises


Husaidia kuimarisha misuli ya tumbo na nyonga, kuboresha mzunguko wa damu, na kupunguza mvutano wa ligamenti.


Epuka mazoezi makali au yanayoweza kusababisha kuanguka.


Je, maumivu haya yataisha baada ya kujifungua?


Maumivu yanayosababishwa na:


  • Mvutiko wa ligamenti

  • Ukuaji wa uterasi

  • Shinikizo la mimba


Hupungua au kuisha kabisa baada ya kujifungua kwa sababu uterasi hurudi katika ukubwa wake wa kawaida.


Maswali yanayoulizwa mara kwa mara


1. Maumivu ya mishipa inayoshikilia kizazi yanadumu muda gani?

Maumivu ya ligamenti duara kwa kawaida ni ya ghafla, kama kuchomwa, na hudumu sekunde chache hadi dakika chache, hasa unapogeuka, kusimama haraka, kukohoa au kucheka. Huanza mara nyingi miezi 4 hadi 6 ya ujauzito. Maumivu yanayodumu saa kadhaa, yanayoongezeka au yanayoambatana na homa au damu si ya ligamenti na yanahitaji uchunguzi.

2. Kidole tumbo kwa mjamzito huonyesha dalili gani?

Kwa mjamzito, kizazi kikubwa husukuma kidole tumbo juu, kwa hiyo maumivu yanaweza kuwa upande wa kulia usawa wa kitovu au juu yake, si chini tu. Huambatana na kichefuchefu, kupoteza hamu ya kula na homa, na maumivu huongezeka kwa saa. Ni dharura inayohitaji upasuaji, na kuchelewa huongeza hatari kwa mama na mtoto.

3. Je, ni salama kutumia dawa za maumivu nikiwa mjamzito?

Paracetamol kwa kipimo cha kawaida ni dawa ya maumivu inayotumika zaidi wakati wa ujauzito, kwa ushauri wa mtoa huduma. Dawa za jamii ya ibuprofen na diclofenac zinapaswa kuepukwa kuanzia wiki 20 za ujauzito, kwa sababu zinaweza kuathiri figo za mtoto na kiasi cha maji ya chupa. Usitumie dawa za mitishamba bila ushauri.

4. Maumivu ya kiuno pamoja na homa wakati wa ujauzito yanamaanisha nini?

Maumivu ya kiuno au ubavuni pamoja na homa, kutetemeka, kichefuchefu au kukojoa kwa maumivu yanaweza kuwa maambukizi ya figo. Kwa mjamzito, maambukizi haya yanaweza kuleta uchungu wa mapema na kudhuru mama, kwa hiyo yanahitaji kuonwa hospitali siku hiyo hiyo na mara nyingi antibiotiki za mshipa.

5. Nitajuaje kama ni mikazo ya uchungu wa mapema?

Mikazo ya uchungu huja kwa mpangilio, tumbo zima hukaza na kuwa gumu, kisha hulegea, na hujirudia mara nne au zaidi ndani ya saa moja. Huweza kuambatana na maumivu ya mgongo wa chini, shinikizo nyongani, kutokwa na maji au damu. Kama una mimba chini ya wiki 37 na mikazo hii, nenda hospitali mara moja.

6. Je, kufunga choo kunaweza kuleta kichomi tumboni wakati wa ujauzito?

Kufunga choo na gesi ni visababishi vya kawaida vya maumivu ya kuchoma au kubana tumboni wakati wa ujauzito, kwa sababu projesteroni hupunguza kasi ya utumbo na vidonge vya madini chuma hukausha choo. Maumivu hupungua baada ya kutoa gesi au kujisaidia. Kunywa maji ya kutosha, kula nyuzilishe na kutembea husaidia.

Imeandikwa:

2 Aprili 2026, 19:07:17

ULY CLINIC inashauri usitegemee au kufuata ushauri wowote uliyoona kwenye makala hii bila kuwasiliana kwanza na daktari wako. Kabla ya kuchukua hatua yoyote ya matibabu, hakikisha umepata ushauri rasmi kutoka kwa daktari wako ili kuepuka madhara yoyote yanayoweza kutokea.

​

Makala hii ni ya kielimu tu na haitumiki kama mbadala wa matibabu ya daktari.

Rejea za mada hii:

  1. American College of Obstetricians and Gynecologists. Round ligament pain and common discomforts of pregnancy (patient FAQ). Washington, DC: ACOG; 2023.

  2. World Health Organization. WHO recommendations on antenatal care for a positive pregnancy experience. Geneva: WHO; 2016.

  3. Cunningham FG, Leveno KJ, Dashe JS, et al. Williams Obstetrics. 26th ed. New York: McGraw-Hill; 2022.

  4. US Food and Drug Administration. FDA recommends avoiding use of NSAIDs in pregnancy at 20 weeks or later because they can result in low amniotic fluid. Silver Spring: FDA; 2020.

  5. Mourad J, Elliott JP, Erickson L, Lisboa L. Appendicitis in pregnancy: new information that contradicts long-held clinical beliefs. Am J Obstet Gynecol. 2000;182(5):1027–9.

  6. Ministry of Health, United Republic of Tanzania. Standard Treatment Guidelines and National Essential Medicines List (STG/NEMLIT), 7th edition. Dodoma: Ministry of Health; 2026.

bottom of page