top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

ULY CLINIC

Dkt. Sospeter B, MD

3 Novemba 2026, 16:12:07

Shahawa kuwa nyepesi kama maji: Visababishi, Vipimo na Tiba

Shahawa hutoka zikiwa nzito kama jeli kisha huyeyuka kuwa majimaji ndani ya dakika 15 hadi 60, kwa hiyo kuona majimaji baada ya muda ni kawaida. Shahawa nyepesi tangu zinapotoka, kwa siku chache, mara nyingi hutokana na kumwaga mara nyingi kwa siku kadhaa mfululizo, na hurudi kawaida baada ya kupumzika siku 2 hadi 3.


Visababishi vingine ni mbegu chache au kutokuwepo kwa mbegu, upungufu wa homoni ya testosteroni (mara nyingi kwa kutumia testosteroni au dawa za kuongeza misuli), maambukizi ya tezi dume, kuziba kwa mirija ya shahawa, kisukari, pombe, sigara, bangi na lishe duni. Unene wa shahawa peke yake hauonyeshi uwezo wa kuzaa; kipimo cha mbegu ndicho kinachoonyesha.


Swali la msomaji


"Habari daktari, mimi ni mwanaume wa miaka 29. Kwa wiki moja sasa nimegundua kuwa kila ninapomwaga, shahawa zangu zinakuwa nyepesi sana kama maji. Hali hii inanitia wasiwasi kwa sababu zamani zilikuwa nzito na za kawaida. Hii inaweza kuwa tatizo gani, na nifanyeje?"


Asante kwa swali muhimu. Mabadiliko ya muonekano wa shahawa yanaweza kushtua, lakini mara nyingi ni ya muda mfupi. Hapa chini tunaeleza shahawa za kawaida zinavyokuwa, visababishi vya kuwa nyepesi, vipimo na unachoweza kufanya.


Shahawa za kawaida zinapaswa kuwa na sifa gani?


Sifa

Kawaida kwa mujibu wa WHO

Rangi

Nyeupe hadi kijivu hafifu, au njano kidogo

Muonekano mara zinapotoka

Nzito kama jeli

Muda wa kuyeyuka

Dakika 15 hadi 60

Kiasi

Takribani kijiko kidogo kimoja au zaidi; chini ya mililita moja na nusu huhesabiwa kidogo

Idadi ya mbegu

Milioni 16 au zaidi kwa kila mililita moja

Harufu

Ya kipekee isiyo kali


Mabadiliko ya rangi kama damu, harufu mbaya au maumivu wakati wa kumwaga yanahitaji kuonwa na mtoa huduma.


Visababishi vya shahawa kuwa nyepesi kama maji


1. Kujamiana mara kwa mara


Wanaume wanaofanya tendo la ndoa au kujichua mara nyingi kwa siku au kwa siku mfululizo, hupunguza muda wa tezi za uzazi (tezi dume na vifuko vya shahawa) kutengeneza shahawa yenye ubora wa kawaida. Matokeo yake, manii hutoka nyepesi kama maji kwa sababu mwili haujapata muda wa kutengeneza sehemu ya ute mzito wa shahawa.


2. Upungufu wa Virutubishi


Virutubisho kama zinki, selenium, vitamini B12, na asidi ya foliki ni muhimu katika kutengeneza shahawa zenye ubora. Ukosefu wake unaweza kuathiri muundo na kiasi cha shahawa.


3. Upungufu wa maji mwilini


Maji ni sehemu muhimu ya shahawa. Ukikosa kunywa maji ya kutosha, shahawa huweza kuwa chache na nyepesi kupita kawaida.


4. Maambukizi ya tezi tezi dume au vifuko vya shahawa


Maambukizi kwenye tezi ya uzazi yanaweza kuharibu utengenezaji wa ute mzito wa shahawa. Wakati mwingine hii huambatana na maumivu ya nyonga, kiuno au maumivu wakati wa kukojoa.


5. Matatizo ya homoni (Upungufu wa Testosteroni)


Homoni ya testosteroni inahusika katika kudhibiti uzalishaji wa shahawa. Ikiwa kiwango chake ni kidogo, muundo wa shahawa unaweza kuathirika.


6. Upungufu wa mbegu (Oligospemia au Azuspemia)


Wanaume wenye kiwango kidogo cha mbegu au kutokuwa na mbegu kabisa, mara nyingi hutokwa na shahawa nyepesi. Hili huwa halionekani kwa macho lakini hupimwa kwa kipimo maalum cha uchunguzi wa manii.


7. Magonjwa ya muda mrefu au msongo wa mawazo


Magonjwa sugu kama kisukari, shinikizo la damu au msongo wa mawazo huathiri utendaji wa homoni na mzunguko wa damu katika via vya uzazi, na hivyo kubadilisha sifa za shahawa.


8. Matumizi ya pombe, sigara au madawa ya kulevya


Vitu hivi hupunguza ubora wa shahawa na kusababisha kuwa nyepesi au kupungua kwa mbegu.


9. Matatizo ya kuziba kwa mirija ya shahawa


Kuziba kwa mirija inayopitisha shahawa huweza kufanya idadi ya mbegu iwe ndogo au kutokuwepo kabisa.


Kwa idadi ndogo ya mbegu soma Upungufu wa manii: dalili, vipimo na matibabu, na kwa shahawa nzito soma Shahawa kuwa nzito na mabonge mabonge, ni kawaida?.


Wakati gani ni muhimu kumwona daktari?


Ni muhimu kumwona daktari endapo:


  • Shahawa zinaeendelea kuwa nyepesi kwa zaidi ya wiki mbili

  • Unapata maumivu unapomwaga

  • Shahawa ina harufu mbaya au damu

  • Umekuwa na matatizo ya nguvu za kiume au kushindwa kumpa mwenza mimba

  • Una dalili nyingine kama homa, maumivu ya nyonga, kiuno au sehemu za siri


Vipimo na uchunguzi


  • Kipimo cha mbegu: kipimo kikuu; hupima kiasi, muda wa kuyeyuka, idadi, mwendo na umbo la mbegu.

  • Vipimo vya homoni: testosteroni, FSH, LH na prolaktini.

  • Ultrasound ya korodani na tezi dume: varikosili, uvimbe au kuziba kwa mirija.

  • Vipimo vya maambukizi: mkojo, magonjwa ya zinaa.

  • Kipimo cha sukari kwa kisukari.

  • Kipimo cha mkojo baada ya kumwaga kama kiasi ni kidogo sana: kuangalia shahawa kurudi kibofuni.


Tiba na ushauri


Tiba hutegemea chanzo cha tatizo. Baadhi ya hatua ni:


  • Kupunguza kujichua au tendo la ndoa mara kwa mara bila kupumzika

  • Kunywa maji ya kutosha kila siku

  • Kula lishe bora yenye protini, matunda, mboga na virutubisho kama zinc, selenium, vitamini C na E

  • Matibabu ya maambukizi iwapo yamegundulika

  • Ushauri wa kitaalamu wa uzazi kwa tatizo sugu au la muda mrefu


  • Kuacha testosteroni na dawa za kuongeza misuli zisizoandikwa na daktari.

  • Kutibu varikosili au kuziba kwa mirija kwa upasuaji inapohitajika.


Matibabu ya nyumbani


1. Fanya mapenzi kwa mpangilio


  • Epuka kujichua au kushiriki tendo mara nyingi sana kwa siku au siku mfululizo.

  • Mpe mwili muda wa kutengeneza shahawa zenye ubora kwa kupumzika angalau siku 2–3 kabla ya tendo jingine.


2. Kunywa maji ya kutosha kila siku


  • Shahawa huundwa kwa zaidi ya asilimia 90 na maji.

  • Lenga kunywa angalau glasi 8 za maji kwa siku, hasa kama unafanya kazi kwenye joto au unapoteza maji mengi kwa jasho.


3. Kula lishe bora inayosaidia afya ya uzazi


Vyakula vya kusaidia shahawa bora ni pamoja na:


  • Karanga na mbegu kama chia, alizeti, mbegu za maboga

  • Mayai na samaki wenye mafuta mengi kama sardine na salmon

  • Mboga za kijani kibichi (mchicha, matembele)

  • Matunda kama parachichi, machungwa, tikiti, ndizi

  • Vyakula vyenye zinki (nyama ya ng’ombe, maini, maharage)


4. Punguza msongo wa mawazo


  • Fanya mazoezi mepesi ya kupumua, tembea jioni, sikiliza muziki wa kutuliza au fanya ibada zako kwa utulivu.

  • Msongo wa mawazo unapungua, homoni za uzazi huongezeka na shahawa huboreka.


5. Jitahidi kupata usingizi wa kutosha


  • Lala kwa saa 7 hadi 8 kwa usiku ili kusaidia mwili wako kuzalisha homoni za testosterone.

  • Kuweka ratiba ya kulala na kuamka kwa wakati mmoja kila siku husaidia sana.


6. Epuka tabia zinazoharibu ubora wa shahawa


  • Usivute sigara wala bangi

  • Epuka pombe kupita kiasi

  • Punguza matumizi ya dawa au virutubisho visivyo na ushauri wa daktari


7. Fanya mazoezi ya mwili angalau mara 3 kwa wiki


  • Mazoezi kama kutembea kwa haraka, kuruka kamba au kuogelea husaidia mzunguko wa damu kwenye via vya uzazi na kuboresha uzalishaji wa shahawa.


Kumbuka:


Matibabu ya nyumbani ni kwa hali nyepesi tu. Ukiona hakuna mabadiliko, au kuna dalili za kuashiria tatizo la ndani kama maumivu, damu, kushindwa kumpa mwenza mimba, au kushuka kwa nguvu za kiume — tafadhali muone daktari mapema.


Maswali mengine yanayoulizwa na wasomaji


Kwanini shahawa yangu huwa tofauti kila ninapomwaga?


Ni kawaida kwa mwanaume kubadilika-badilika muundo wa shahawa kulingana na lishe, hali ya mwili, msongo wa mawazo, au hata muda uliopita toka mara ya mwisho kujamiiana. Kama mara moja ni nzito, siku nyingine nyepesi — si lazima iwe tatizo. Tatizo linakuwepo pale hali inapojirudia mara nyingi bila kubadilika.


Je, kukojoa mara kwa mara au usiku kunaweza kuathiri ubora wa shahawa?


Inaweza, hasa kama kukojoa mara kwa mara kunaambatana na maambukizi au shida kwenye tezi ya prostate. Hali kama hii inaweza kuathiri uzalishaji wa shahawa na kuifanya kuwa nyepesi. Ni vizuri kufanya uchunguzi wa mkojo na tezi ya uzazi unapokuwa na hali kama hiyo.


Ni kweli kwamba mtu akiwa hajakula vizuri kwa siku kadhaa shahawa yake inaweza kubadilika?


Inaweza kubadilika. Mwili unapokuwa hauna virutubishi vya kutosha, kama vile protini na madini ya zinki, hupunguza ubora wa shahawa. Kwa muda mrefu, lishe duni inaweza kufanya shahawa kuwa chache na mbegu kuwa na ubora mdogo; siku chache za kula vibaya mara nyingi hazileti mabadiliko makubwa. Lishe bora ni sehemu ya msingi wa afya ya uzazi.


Shahawa yangu huwa kama maji kabisa lakini bado naweza kumpa mwenza mimba?


Inawezekana, lakini sio uhakika. Maji ni sehemu kubwa ya shahawa, lakini kama shahawa ni nyepesi kupita kiasi inaweza kuashiria upungufu wa mbegu au ubora wa mbegu duni. Uchunguzi wa maabara (Uchunguzi wa shahawa) ndio njia pekee ya kupata majibu sahihi.


Nimegundua shahawa yangu haina harufu kabisa. Je, hiyo ni kawaida?


Shahawa kawaida huwa na harufu ya kipekee, siyo kali. Kukosa harufu kabisa siyo tatizo moja kwa moja, lakini mabadiliko ya ghafla katika harufu (iwe kupotea au kuwa kali) yanaweza kuashiria mabadiliko ya kemikali au maambukizi. Zingatia mabadiliko mengine pia.


Je, kuna mazoezi ya mwili yanayosaidia kuboresha muonekano wa shahawa?


Mazoezi ya wastani kama kutembea kwa kasi, mazoezi ya misuli ya sakafu ya nyonga, na kuacha maisha ya kukaa muda mrefu husaidia kuboresha mzunguko wa damu na viwango vya testosterone, ambavyo vinaathiri moja kwa moja ubora wa shahawa.


Naweza kutumia dawa za kienyeji kuongeza uzito wa shahawa?


Tahadhari sana! Baadhi ya dawa za kienyeji zinaweza kuwa na viambato visivyo salama au visivyo na ushahidi wa kitaalamu. Unapohitaji kuboresha shahawa zako, chaguo salama ni lishe bora, virutubisho vilivyothibitishwa, na ushauri wa daktari au mtaalamu wa afya ya uzazi.


Kuna uhusiano gani kati ya usingizi na ubora wa shahawa?


Usingizi wa kutosha (saa 7–8 kwa usiku) husaidia mwili kuzalisha homoni muhimu za uzazi. Kukosa usingizi kunaweza kupunguza testosteroni na kuongeza homoni msongo (kotisol), hali inayoweza kuharibu ubora wa shahawa.


Ni kweli kwamba kufikiria sana au hofu huathiri shahawa?


Msongo wa mawazo huathiri homoni na hata mzunguko wa damu kwenda kwenye via vya uzazi. Matokeo yake ni kushuka kwa ubora wa shahawa, kupungua kwa nguvu za kiume, au hata tatizo la kumwaga mapema.


Je, kuna kipindi fulani cha siku au mzunguko ambapo shahawa huwa bora zaidi?


Kwa kawaida, shahawa huwa bora zaidi asubuhi baada ya kupata usingizi wa kutosha, na baada ya kujizuia kujamiiana kwa siku 2–3. Hii inaruhusu mwili kutengeneza manii ya kutosha zenye ubora wa juu.


Maswali yanayoulizwa mara kwa mara


1. Je, ni kawaida shahawa kuwa nzito kisha kugeuka maji?

Shahawa hutoka zikiwa nzito kama jeli, kisha huyeyuka kuwa majimaji ndani ya dakika 15 hadi 60 kwa sababu ya vimeng'enya vya tezi dume. Hii ni kawaida kabisa na husaidia mbegu kuogelea. Kwa hiyo kuona shahawa zimekuwa maji baada ya muda si dalili ya ugonjwa; kinachojalisha ni jinsi zilivyo mara tu zinapotoka.

2. Je, shahawa nyepesi inamaanisha siwezi kumpa mke mimba?

Unene wa shahawa peke yake hauonyeshi uwezo wa kuzaa. Wanaume wengi wenye shahawa nyepesi wana mbegu za kutosha, na wengine wenye shahawa nzito wana mbegu chache. Njia pekee ya kujua ni kipimo cha mbegu kwenye maabara, kinachopima idadi, mwendo na umbo la mbegu. Kama mmejaribu kwa mwaka mmoja bila mimba, fanya kipimo hiki.

3. Kumwaga mara nyingi kunafanya shahawa ziwe nyepesi?

Kumwaga mara kadhaa kwa siku moja au siku mfululizo hupunguza kiasi cha shahawa na kuzifanya nyepesi kwa muda, kwa sababu tezi hazijapata muda wa kujaza akiba. Hii si hatari na hurudi kawaida baada ya siku 2 hadi 3 za kupumzika. Kwa wanaotafuta mimba, tendo kila baada ya siku 1 hadi 2 katika siku za rutuba bado ni bora.

4. Je, dawa za kuongeza misuli au testosteroni zinaathiri shahawa?

Testosteroni ya kudungwa au kumeza na dawa za kuongeza misuli hufanya ubongo usimamishe homoni zinazoamrisha korodani kutengeneza mbegu, hivyo mbegu hupungua au kukosekana kabisa, na korodani husinyaa. Shahawa zinaweza kuwa nyepesi. Hali hii mara nyingi hurudi baada ya kuacha, lakini inaweza kuchukua miezi hadi zaidi ya mwaka.

5. Kipimo cha mbegu hufanywaje?

Kipimo hufanywa kwa kutoa shahawa kwenye kikombe safi kwa kujichua, baada ya kukaa siku 2 hadi 7 bila kumwaga, na sampuli kufika maabara ndani ya saa moja ikiwa na joto la mwili. Maabara hupima kiasi, muda wa kuyeyuka, idadi, mwendo na umbo la mbegu. Kipimo kimoja kisicho cha kawaida hurudiwa baada ya wiki kadhaa.

6. Lishe gani husaidia ubora wa shahawa?

Lishe yenye mboga, matunda, nafaka zisizokobolewa, samaki, karanga na mbegu, pamoja na virutubisho kama zinki, folate na vitamini C, huhusishwa na ubora bora wa mbegu katika tafiti za uchunguzi. Kupunguza nyama zilizosindikwa, pombe, sigara na bangi, na kudumisha uzito unaofaa husaidia zaidi kuliko vidonge vya virutubisho peke yake.

Imeandikwa:

2 Aprili 2026, 19:07:10

ULY CLINIC inashauri usitegemee au kufuata ushauri wowote uliyoona kwenye makala hii bila kuwasiliana kwanza na daktari wako. Kabla ya kuchukua hatua yoyote ya matibabu, hakikisha umepata ushauri rasmi kutoka kwa daktari wako ili kuepuka madhara yoyote yanayoweza kutokea.

​

Makala hii ni ya kielimu tu na haitumiki kama mbadala wa matibabu ya daktari.

Rejea za mada hii:

  1. World Health Organization. WHO laboratory manual for the examination and processing of human semen. 6th ed. Geneva: WHO; 2021.

  2. Schlegel PN, Sigman M, Collura B, et al. Diagnosis and treatment of infertility in men: AUA/ASRM guideline part I. J Urol. 2021;205(1):36–43.

  3. Agarwal A, Mulgund A, Hamada A, Chyatte MR. A unique view on male infertility around the globe. Reprod Biol Endocrinol. 2015;13:37.

  4. Salas-Huetos A, Bulló M, Salas-Salvadó J. Dietary patterns, foods and nutrients in male fertility parameters and fecundability: a systematic review of observational studies. Hum Reprod Update. 2017;23(4):371–89.

  5. Rahnema CD, Lipshultz LI, Crosnoe LE, Kovac JR, Kim ED. Anabolic steroid-induced hypogonadism: diagnosis and treatment. Fertil Steril. 2014;101(5):1271–9.

bottom of page