Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
ULY CLINIC
Dkt. Helen L, M.D
2 Aprili 2026, 16:17:50

Soma tarehe ya mwisho wa matumizi kwa kila dawa unayonunua
Kufahamu tarehe ya mwisho wa matumizi ya dawa ni njia mojawapo ya kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza pamoja na usugu wa vimelea vya maradhi dhidi ya dawa hiyo. Jenga tabia ya kusoma mwisho wa matumizi wa kila dawa unayonunua.
Utambuzi wa tarehe ya mwisho wa matumizi ya dawa
Tarehe ya mwisho wa matumizi huandikwa na kiwanda kinachozalisha dawa au mtaalamu wa dawa. Alama ya tarehe ya mwisho wa matumizi ya dawa huandikwa kwa majina mbalimbali kama;
Exp
Exp date
Expires
Expiry
Expiry date
Use before
Use by
Isitumike baada ya
Tarehe ya kuisha muda wa matumizi
Tumia kwa siku baada ya kufungua
Maelezo ya ziada kuhusu tarehe ya mwisho wa matumizi ya dawa
Endapo dawa yako imeandikwa, 'tumia kabla' au 'tumia mpaka' au 'tarehe ya mwisho wa matumizi', hii humaanisha dawa hiyo haipaswi kutumika baada ya muda huo kuisha. Dawa pia huweza kuandikwa kwa lugha ya Kiingereza kwa kutumia maneno ambayo yameorodheshwa hapo juu.
Mfano 1
Endapo dawa imeandikwa, 'tumia mpaka Julai 2021', kwa lugha ya kiingereza ‘Use by July 2021’, hii inamaanisha, usitumie dawa hii kuanzia tarehe 31/7/2021 na kuendelea.
Mfano 2
Baadhi ya dawa za kimiminika zinazofunguliwa huandikwa, 'Tumia kwa siku 7 tu baada ya kufungua chupa ya dawa au kwa lugha ya kiingereza "discard 7 days after opening". Hii inamaanisha usitumie dawa hiyo siku 7 baada ya kufungua dawa hiyo, hata kama hujaimaliza na tarehe ya mwisho wa matumizi haijafika.
Muda wa dawa kuishi
Baadhi ya dawa zina muda mfupi wa matumizi, hivyo kuwa makini kusoma tarehe zinazoandikwa kwenye dawa hizo. Dawa za kimiminika kama dawa za kuweka machoni, masikioni, kunywa, n.k huwa na muda mfupi sana wa matumizi, takribani kuanzia siku saba hadi wiki nne tu tangu zimefunguliwa.
Dawa zenye asili ya vidonge vigumu au tembe huishi kwa muda mrefu na tarehe ya mwisho wa matumizi huweza kuwa takribani mwaka mmoja na kuendelea.
Kumbuka
Usitumie dawa za kwenye kopo ambazo hazionyeshi tarehe ya mwisho wa matumizi
Usitumie dawa zilizo kwenye karatasi ambazo hazina tarehe za kutengenezwa na tarehe ya kuisha muda wake
Usinunue dawa kwa wingi ambayo inakaribia kuisha muda wake
Imeandikwa:
2 Aprili 2026, 16:17:50
ULY CLINIC inashauri usitegemee au kufuata ushauri wowote uliyoona kwenye makala hii bila kuwasiliana kwanza na daktari wako. Kabla ya kuchukua hatua yoyote ya matibabu, hakikisha umepata ushauri rasmi kutoka kwa daktari wako ili kuepuka madhara yoyote yanayoweza kutokea.
​
Makala hii ni ya kielimu tu na haitumiki kama mbadala wa matibabu ya daktari.
