Maelezo ya majibu ya maswali mbalimbali ya kiafya

Je, unapoanguka chini unapaswa kuinuka mara moja?
Si kila wakati. Baada ya kuanguka, usikimbilie kuinuka. Tulia kwanza ujihakikishie kama umeumia au kama kuanguka kulitokana na tatizo la kiafya kama kuzimia, kiharusi au mshtuko wa moyo. Kuinuka haraka kunaweza kuongeza madhara ikiwa kuna jeraha la kichwa, kuvunjika kwa mfupa au majeraha ya ndani. Vivyo hivyo, usimnyanyue mtu aliyeanguka mara moja. Hakikisha kwanza yuko macho, hana maumivu makali, kizunguzungu au dalili za jeraha kubwa. Msaidie kuinuka taratibu tu ikiwa ni salama kufanya hivyo. Ukiwa na shaka yoyote, mwache atulie na tafuta huduma ya afya haraka.

Sekunde chache za kushika kipimo: Je, Quantum Analyzer Inaona Magonjwa Mengi au ni Madai Tu?
Kwa mujibu wa ushahidi wa kisayansi uliopo, hakuna uthibitisho wa kuaminika kwamba kushika kifaa hiki kwa dakika chache kunaweza kugundua magonjwa mengi kwa usahihi au kuchukua nafasi ya vipimo vya hospitali. Madai hayo hayajaungwa mkono na tafiti za kiwango cha juu. Daima thibitisha matokeo kwa uchunguzi na vipimo vya hospitali kabla ya kuanza matibabu.

Mbegu za Papai zinaweza kuzuia mimba? Tafisi zinasema nini hasa?
Tafiti za maabara na wanyama zinaonyesha kuwa mbegu za papai zina uwezo wa kupunguza uzazi kupitia athari zake kwa mbegu za kiume, homoni za uzazi na michakato mingine ya uzazi. Ingawa ushahidi wa kuaminika kwa binadamu bado ni mdogo, taarifa nyingi za uzoefu wa watumiaji zinaashiria kuwa mbegu za papai zinaweza kuwa na mchango katika kupunguza uwezekano wa kutungisha na kushika ujauzito, jambo linalohitaji tafiti zaidi za kisayansi kuthibitisha ufanisi na usalama wake.

Kwanini uweke dawa ya meno mbali na watoto?
Watoto wanaweza kuimeza kwa dawa kwa bahati mbaya na kusababisha kichefuchefu, kutapika, maumivu ya tumbo na kuongeza hatari ya meno yao kubadilika rangi. Kiasi sahihi kinachopendekezwa kwa watoto chini ya miaka 3 kiasi kinacholingana na punje ya mchele, watoto miaka 3–6 watumie kiasi cha punje ya njegere, na watu wazima watumie kiasi kidogo kinachofunika kichwa cha mswaki.

Je, Watu wenye Shinikizo la juu la Damu wanapaswa kuacha Chumvi kabisa?
Huhitaji kuacha chumvi kabisa ikiwa una shinikizo la juu la damu; badala yake, unahitaji kuitumia kwa kiasi kinachoshauriwa na wataalamu wa afya. Kwa ujumla, watu wazima wanashauriwa kutumia chini ya gramu 5 za chumvi kwa siku (sawa na kijiko kimoja kidogo cha chai) ili kusaidia kudhibiti presha na kulinda afya ya moyo. Hata hivyo, ni muhimu kufuata ushauri wa daktari wako, kwani mahitaji ya kiafya yanaweza kutofautiana kati ya mtu na mtu.

Je, Chumvi huongeza Shinikizo la Damu? Ushahidi kutoka Afrika
Tafiti mbalimbali barani Afrika zimeonyesha kuwa matumizi makubwa ya chumvi huongeza hatari ya shinikizo la damu. Kwa afya bora ya Moyo, wataalamu wa Afya wanapendekeza watu wazima kutumia chini ya gramu 5 za chumvi kwa siku (sawa na kijiko kimoja kidogo cha chai). Kupunguza chumvi kwenye chakula kunaweza kusaidia kupunguza hatari ya shinikizo la damu, kiharusi na magonjwa ya moyo.
