top of page

Maelezo ya majibu ya maswali mbalimbali ya kiafya

Kisukari cha mazoezi

"Kisukari cha mazoezi" hapa humaanisha sukari kushuka (hypoglycaemia) wakati au baada ya mazoezi kwa mtu mwenye kisukari – hasa anayetumia insulini au vidonge vinavyoongeza insulini (sulfonylurea kama glibenclamide). Mazoezi ni dawa nzuri kwa kisukari: hupunguza sukari, huongeza uwezo wa mwili kutumia insulini, hulinda moyo, na husaidia uzito – ADA inashauri dakika 150 kwa wiki za mazoezi ya wastani pamoja na mazoezi ya nguvu siku 2–3, na kutokaa muda mrefu bila kusimama. Kuzuia sukari kushuka: pima sukari kabla ya mazoezi – ikiwa chini ya 5.0 mmol/L (90 mg/dL), kula kitu chenye wanga (k.m. tunda, mkate) kwanza; ikiwa juu sana (zaidi ya 15 mmol/L) pamoja na ketoni kwa mwenye kisukari aina ya 1, usifanye mazoezi makali; beba sukari ya haraka (soda isiyo ya diet, juisi, glukosi); fanya mazoezi saa 1–3 baada ya kula; jua kwamba sukari huweza kushuka hata saa kadhaa hadi 24 baadaye (usiku) – pima kabla ya kulala. Daktari huweza kurekebisha insulini au dawa kwa siku za mazoezi. Dalili za sukari kushuka: kutetemeka, jasho, njaa kali, moyo kwenda mbio, kizunguzungu, kuchanganyikiwa. Huduma ya kwanza: gramu 15–20 za sukari ya haraka, pima baada ya dakika 15, rudia kama bado chini, kisha kula chakula.

Kukonda sana, je shida inaweza kuwa nini?

Kukonda ni kupungua kwa uzito, mafuta na misuli. Kupungua uzito kwa zaidi ya 5% ndani ya miezi 6–12 bila kukusudia kunahitaji uchunguzi. Tanzania, visababishi vya kwanza kuchunguza ni kifua kikuu, VVU, kisukari kisichodhibitiwa, tezi ya shingo kufanya kazi kupita kiasi, lishe duni, minyoo na magonjwa ya utumbo, sonona na wasiwasi, pombe na dawa za kulevya, na saratani. Kwa wazee, matatizo ya meno, kumeza, upweke na dawa ni muhimu. Watu wengine ni wembamba kwa asili – kama uzito ni thabiti, wanakula vizuri na wana nguvu, si ugonjwa.

Je, mtoto wa miezi 5 anapaswa kula chakula gani?

Mtoto wa miezi 5 anapaswa kunyonya maziwa ya mama PEKEE – bila maji, uji, matunda wala chakula kingine – hadi atimize miezi 6, kama WHO na Wizara ya Afya wanavyoshauri. Maziwa ya mama yanatosha virutubisho na maji yote. Kama mama hawezi kunyonyesha, mtoto apewe maziwa maalumu ya watoto (formula) kwa ushauri. Chakula cha nyongeza huanza miezi 6 kamili, kuanzia uji mzito na vyakula vilivyopondwa.

Jinsi ya kupunguza kichefuchefu na kutapika wakati wa ujauzito

Kichefuchefu na kutapika huwapata wajawazito wengi, hasa wiki 6 hadi 16, na mara nyingi hupungua baada ya wiki 16 hadi 20. Kula milo midogo mara kwa mara, kuepuka harufu zinazokuudhi, kunywa maji kidogo kidogo na kutumia tangawizi husaidia wengi. Kidonge cha madini chuma kikiongeza kichefuchefu, kimeze usiku. Kama hayo hayatoshi, mtoa huduma anaweza kukupa dawa salama kwa ujauzito. Kushindwa kula na kunywa kwa saa 24, kupungua uzito au mkojo mweusi – hospitali.

Je, naweza zuia mimba kwa kutumia p2 siku moja kabla?

P2 (levonorgestrel) ni kidonge cha dharura kinachofanya kazi kwa kuchelewesha au kuzuia yai kutoka. Ukimeza kabla ya tendo, huweza kutoa kinga fulani kama yai halijatoka bado, lakini haitoi kinga ya uhakika kwa siku zinazofuata, haikukingi tendo la siku 2–3 baadaye kwa uhakika, na matumizi ya mara kwa mara huvuruga hedhi. Ndiyo maana P2 si njia ya kawaida ya uzazi wa mpango. Ikiwa umekunywa P2 jana na leo umefanya tendo bila kinga, kinga yako si ya uhakika – njia bora ni kitanzi cha shaba ndani ya siku 5, au kuanza njia ya kudumu. Kwa anayehitaji kinga ya mara kwa mara, vidonge vya kila siku, sindano au kipandikizi ni salama na bora zaidi.

Namna ya kufahamu urefu wa mzunguko wa hedhi

Urefu wa mzunguko ni idadi ya siku kuanzia siku ya KWANZA ya hedhi moja hadi siku moja kabla ya hedhi inayofuata kuanza. Kwa mfano: hedhi 13/12, 11/1, 13/2 na 12/3 – mizunguko ni siku 29, 33 na 28; wastani karibu siku 30. Mzunguko wa kawaida kwa mtu mzima ni siku 24 hadi 38, na kutofautiana hadi siku 7 hadi 9 kati ya miezi ni kawaida. Kwa wastani wa siku 30, uovuleshaji ni karibu siku ya 16 na siku za hatari karibu siku ya 11 hadi 16.

bottom of page