top of page

Maelezo ya majibu ya maswali mbalimbali ya kiafya

Picha ya vipele uumeni

Vipele kwenye uume vina visababishi vingi – baadhi ni maumbile ya kawaida yasiyo na madhara (vipele lulu, Fordyce, tezi za Tyson), na vingine ni maambukizi yanayohitaji matibabu (sunzua, malengelenge/herpes, kaswende, folikulaitisi, fangasi, molluscum). Muonekano husaidia kutofautisha: mpangilio, rangi, kama vinauma, kuwasha au kutoa maji. Picha peke yake haitoshi kwa uhakika – mtoa huduma ndiye huthibitisha.

Tarehe ya kushika ujauzito

Tarehe ya kushika ujauzito ni karibu siku ya uovuleshaji – yai linapotoka kwenye ovari na kurutubishwa ndani ya saa 12 hadi 24. Kwa mzunguko wa siku 28, ni karibu siku 14 baada ya siku ya kwanza ya hedhi ya mwisho; kwa mizunguko mingine, karibu siku 14 kabla ya hedhi iliyotarajiwa. Kwa kuwa mbegu huishi hadi siku 5, tendo lililoleta mimba linaweza kuwa hadi siku 5 kabla. Ultrasound ya mapema hukadiria kwa usahihi zaidi.

Kutokwa ute wenye harufu mbaya ukeni

Ute wenye harufu mbaya ukeni mara nyingi husababishwa na vajinosisi ya bakteria, inayoleta ute mwepesi wa kijivu au mweupe na harufu ya samaki inayozidi baada ya tendo la ndoa au hedhi. Visababishi vingine ni trikomona, inayoleta ute wa njano au kijani wenye povu na muwasho; kitu kilichosahaulika ukeni, kinacholeta harufu kali sana; kisonono, klamidia na PID pamoja na maumivu; na mara chache saratani ya shingo ya kizazi.

Kipimo cha UKIMWI negative

Kipimo cha VVU kuwa hasi (negative) maana yake ni kwamba hakuna virusi vya UKIMWI wala kinga dhidi yake vilivyogunduliwa wakati wa kupima. Uhakika wa majibu hutegemea muda uliopita tangu tukio la hatari, yaani dirisha la matazamio, na aina ya kipimo. Kipimo cha maabara cha antijeni na antibodi huona maambukizi mengi ndani ya siku 18 hadi 45, wakati vipimo vya haraka vya antibodi, vinavyotumika sana Tanzania, na vya kujipima vinaweza kuchukua hadi siku 90.

Malengelenge ukeni: Visababishi na Tiba

Malengelenge madogo yenye maji yanayouma sehemu za siri, yanayopasuka na kuwa vidonda, mara nyingi ni herpes ya sehemu za siri (HSV). Shambulio la kwanza huwa kali zaidi – maumivu makali hasa wakati wa kukojoa, homa, tezi za kinena kuvimba – na huweza kurudi mara kwa mara kwa ukali mdogo. Herpes si UKIMWI, lakini vidonda huongeza hatari ya kuambukizwa au kuambukiza VVU, hivyo pima VVU na kaswende. Dawa za kuzuia virusi (aciclovir, valaciclovir) hupunguza muda na maumivu zikianzishwa mapema. Visababishi vingine ni majipu, fangasi, mzio na majeraha.

Mtoto kuchelewa kutembea

Watoto wengi huanza kutembea wenyewe kati ya miezi 8 na 18, kulingana na WHO. Mtoto wa mwaka mmoja ambaye bado hajatembea mara nyingi yuko ndani ya muda wa kawaida. Wengine hukaa muda mrefu wakitambaa au kutembea kwa kushikilia vitu. Mtoto asiyetembea kufikia miezi 18, asiyesimama kwa kushikilia kufikia miezi 12, au aliyepoteza uwezo aliokuwa nao anahitaji uchunguzi wa mtoa huduma.

bottom of page