top of page

Maelezo ya majibu ya maswali mbalimbali ya kiafya

Kuimalisha kibofu cha mkojo

Kuimarisha kibofu hufanywa kwa mazoezi ya misuli ya sakafu ya nyonga (Kegel) na mazoezi ya kibofu (kukojoa kwa ratiba na kuchelewesha kukojoa taratibu). Ni tiba ya kwanza ya mkojo kuponyoka kwa wanawake – hasa baada ya kujifungua na wakati wa komahedhi – na pia kwa wanaume baada ya upasuaji wa tezi dume. Kunywa maji ya kutosha (si kidogo kupita kiasi), kupunguza kahawa, chai kali, soda na pombe, kupunguza uzito na kutibu kukosa choo husaidia. Matokeo huonekana baada ya wiki 6–12. UTI, kisukari, na kibofu kutomwagika kabisa vichunguzwe kwanza.

Kutokwa na Ute Mwingi Ukeni: Sababu, Dalili na Wakati wa Kuonana na Daktari

Kutokwa na ute ukeni ni njia ya kawaida ya uke kujisafisha na kujilinda dhidi ya maambukizi. Ute huongezeka kawaida karibu na [ovulesheni](/kamusi-tiba/ovulesheni-ovulation), ukiwa mwingi, laini na unaovutika kama ute wa yai bichi, na pia kabla ya hedhi, wakati wa ujauzito, kwa wanaotumia vidonge vya majira, na wakati wa msisimko wa kimapenzi. Ute mwingi usio na harufu kali, kuwasha wala maumivu kwa kawaida si tatizo.

Vyakula gani vinasababisha tumbo kuunguruma sana?

Tumbo kuunguruma (borborygmi) ni sauti ya gesi, maji na chakula vikisogea utumboni – ni kawaida, hasa ukiwa na njaa au baada ya kula. Vyakula vinavyoongeza gesi na kuunguruma kwa wengi: maharage, njegere na dengu (sukari ngumu – oligosaccharides), kabichi, brokoli, kaliflawa na sukuma wiki, maziwa kwa wasiovumilia laktosi, soda na vinywaji vyenye gesi, vyakula vyenye mafuta mengi, nyuzilishe nyingi ghafla, vitunguu, na vitamu bandia kama sorbitol (kwenye big G isiyo na sukari na baadhi ya juisi). Kila mtu ni tofauti – andika vyakula vinavyokuletea dalili. Usiache vyakula vyenye afya kabisa: loweka maharage usiku na kumwaga maji, pika vizuri, ongeza nyuzilishe taratibu, kula polepole. Kuunguruma pamoja na kuharisha mara kwa mara, kupungua uzito, damu kwenye choo au maumivu makali si kwa sababu ya chakula tu – chunguza.

Uume kutoa usaha na kuvimba

Usaha na uvimbe wa uume mara nyingi husababishwa na magonjwa ya zinaa kama kisonono, klamidia na trikomonasi, maambukizi ya mrija wa mkojo, au kuvimba kwa kichwa cha uume na govi (balanaitisi) kunakotokana na fangasi, bakteria, usafi duni au kisukari. Govi kukwama nyuma ya kichwa cha uume (paraphimosis) ni dharura. Usaha ni ishara ya maambukizi yanayohitaji kipimo na dawa sahihi, si kujitibu kwa dawa za dukani.

Kutoka damu nyingi baada ya kutoa mimba shida ni nini?

Baada ya mimba kutoka, kwa njia yoyote, damu kama ya hedhi kwa siku kadhaa, inayopungua taratibu kwa wiki mbili hadi nne, ni kawaida. Damu nyingi, yaani kulowanisha pedi nzito mbili au zaidi kila saa kwa masaa mawili mfululizo, mabonge makubwa, kizunguzungu au kuzimia, si kawaida na inahitaji kituo cha afya mara moja. Visababishi vikuu ni mabaki ya mimba ndani ya kizazi, kizazi kushindwa kujikaza, maambukizi, jeraha la kizazi au shingo yake, na mara chache mimba iliyotunga nje ya kizazi isiyogundulika. Matibabu ni dawa za kukaza kizazi, kusafisha kizazi kwa njia salama, antibiotiki kwa maambukizi, na kuongezewa damu inapohitajika. Huduma ya baada ya mimba kuharibika (PAC) ni halali, ya haraka, na inapatikana bila kuhukumiwa.

Kuumwa na misuli bila ya sababu hasa ya mapaja husababishwa na nini?

Maumivu ya misuli ya mapaja bila sababu iliyo wazi mara nyingi hutokana na uchovu wa misuli (kutembea, kusimama, kupanda ngazi, kukaa mkao mmoja muda mrefu), misuli kukaza usiku (cramps), kukosa maji au madini (potasiamu, magnesiamu, kalsiamu), na mafua au maambukizi ya virusi (mwili mzima kuuma). Visababishi vingine muhimu: dawa – hasa za cholesterol (statins), baadhi ya dawa za VVU na diuretics; upungufu wa vitamini D (maumivu ya mifupa na misuli, udhaifu); tezi ya shingo kufanya kazi chini; kisukari (maumivu ya mishipa ya fahamu, ganzi); mishipa ya fahamu ya mgongo kubanwa (maumivu yanayoshuka kutoka kiunoni, sciatica); maumivu ya nyonga yanayosambaa pajani; damu kuganda kwenye mshipa (DVT – mguu mmoja kuvimba, joto, kuuma); na kwa wazee wa miaka 50+, polymyalgia rheumatica (maumivu na ugumu wa mabega na mapaja asubuhi). Mara chache, misuli kuvunjika (rhabdomyolysis) baada ya mazoezi makali sana – mkojo mweusi kama chai – ni dharura. Uchunguzi hutegemea dalili: vipimo vya damu (CK, madini, TSH, sukari, vitamini D), na ultrasound ya mishipa kama kuna uvimbe.

bottom of page