top of page

Maelezo ya majibu ya maswali mbalimbali ya kiafya

Kutokwa na ute ukeni ni dalili ya kuingia hedhi?

Inaweza kuwa, lakini si dalili ya uhakika. Baada ya uovuleshaji, homoni ya projesteroni hufanya ute kuwa mzito, mweupe au kama krimu – na kwa wanawake wengi huongezeka siku chache kabla ya hedhi. Dalili nyingine za hedhi kukaribia ni matiti kujaa na kuuma, tumbo kujaa, maumivu kidogo ya chini ya tumbo, chunusi na mabadiliko ya hisia. Hata hivyo, ute mweupe mzito pia hutokea mimba changa – hivyo hedhi ikichelewa, pima mimba.

Je, Kuona au kusikia kile ambacho wengine hawaoni wala kusikia ni ugonjwa wa akili au ni mtazamo wa ukweli ambao sayansi ya sasa bado haijauelewa?

Kusikia sauti au kuona vitu ambavyo wengine hawavioni (halusino) si mara zote ugonjwa wa akili. Tafiti zinaonyesha asilimia 5–15 ya watu wazima husikia sauti wakati fulani maishani bila ugonjwa wowote – mfano wakati wa msiba, kukosa usingizi, kuamka au kusinzia, au katika muktadha wa kidini na kitamaduni. Ubongo hujenga uzoefu wetu kwa kutabiri na kutafsiri taarifa, na sayansi bado haielewi kila kitu. Hata hivyo, halusino huweza kuwa dalili ya hali zinazotibika: homa kali na kuchanganyikiwa (delirium), malaria kali, dawa za kulevya au kuacha pombe, kifafa, kipandauso, magonjwa ya ubongo, sonona kali, bipola na skizofrenia. Kipimo muhimu si "ni kweli au si kweli" bali: je, uzoefu huu unaleta mateso, hofu, au kushindwa kuishi maisha ya kila siku, au unaamrisha kujidhuru?

Mazoezi ya kuboresha uwezo wa kusimamisha uume

Mazoezi ya misuli ya sakafu ya nyonga (Kegeli) yanaweza kumsaidia mwanaume kuboresha uwezo wa kusimamisha uume na kuudumisha, na kudhibiti kumwaga mapema. Katika utafiti mmoja wa majaribio, karibu 4 kati ya 10 waliofanya mazoezi kwa miezi 3–6 walirudi kwenye uwezo wa kawaida; tafiti kubwa zaidi zinahitajika kuthibitisha kwa wengi. Mazoezi ya mwili kwa ujumla (kutembea haraka, kukimbia, kuogelea) huboresha mishipa ya damu na pia husaidia. Mazoezi haya hayaongezi urefu wala unene wa uume. Uume kutosimama huweza kuwa dalili ya kisukari, presha au ugonjwa wa moyo – pima.

Uume haujitoshelezi wenyewe, namna unavyotumika huongeza kuridhika kwa mwanamke

Kuridhika kwa mwanamke kingono hakutegemei ukubwa wa uume pekee. Tafiti zinaonyesha wanawake wengi hufikia kilele kwa msisimko wa kinembe (kisimi), na wengi wanahitaji msisimko huo pamoja na tendo. Maandalizi ya kutosha, kumjua mwenzi, kuzungumza, kusikiliza mwitikio wake na kubadilika – kasi, kina, mkao, aina ya mguso – huleta tofauti kubwa kuliko ukubwa. Kuingia kwa kina sana kunaweza kuleta maumivu kwa baadhi ya wanawake.

Je, ukubwa wa uume una mchango kwa mwanamke kuridhika kwa kingono?

Tafiti zinaonyesha ukubwa wa uume huchangia kidogo tu kwa baadhi ya wanawake – unene zaidi ya urefu – lakini si kipimo kikuu cha kuridhika kingono. Mambo makubwa zaidi ni mawasiliano, maandalizi na msisimko wa kutosha, kuchochea kisimi (wanawake wengi hufika kileleni kwa kuchochewa kisimi), ukaribu wa kihisia, na afya ya wote wawili. Wastani wa uume uliosimama ni karibu sentimita 13, na wanaume wengi wanaodhani wana uume mdogo wako katika kiwango cha kawaida. Dawa, vidonge, krimu na vifaa vya kuongeza ukubwa havina ushahidi na huweza kudhuru.

Kutembea Pekupeku

Kutembea peku (bila viatu) kwenye nyasi au mchanga safi huweza kuimarisha misuli ya nyayo na kuleta utulivu. Tafiti ndogo za "earthing" au "kuungana na ardhi" zilionyesha matokeo mazuri – maumivu na uchovu kupungua, usingizi na hisia kuboreka, na mabadiliko kwenye damu. Kwa kuwa zilihusisha watu wachache (10 hadi 60), tafiti kubwa zinahitajika kuthibitisha kama faida hizi zinapatikana kwa watu wengi. Wakati huo huo, Tanzania kutembea peku kuna hatari halisi: minyoo ya ndoano kupenya ngozi, funza, pepopunda kupitia vidonda, na vidonda visivyohisiwa kwa wenye kisukari.

bottom of page