top of page

Maelezo ya majibu ya maswali mbalimbali ya kiafya

Uwezekano wa kuambukizwa VVU kwa kushiriki bila Kinga

Ndiyo, inawezekana kushiriki ngono bila kondomu na mtu mwenye VVU na usiambukizwe – hatari kwa tendo moja la ukeni kwa mwanaume ni karibu 1 kati ya 2,500, na kwa mwanamke karibu 1 kati ya 1,250, ikiwa mwenza hatumii ARV. Lakini hatari hujilimbikiza kwa matendo mengi, na huongezeka kwa magonjwa ya zinaa, kutotahiriwa, damu ya hedhi, na virusi vingi (maambukizi mapya). Ikiwa mwenza yuko kwenye ARV na virusi havipimiki kwa miezi 6 au zaidi, hakuna maambukizi kwa ngono (U=U / K=K). Hatua sasa: PEP ndani ya saa 72 ikiwa tukio ni la karibuni, na vipimo vya VVU.

Kutoboka kwa meno husambaa kati ya jino moja na jingine?

Kuoza kwa meno husababishwa na utando wa bakteria (plaque) unaogeuza sukari kuwa tindikali inayotoboa jino. Jino lililooza haliambukizi jino jirani moja kwa moja, lakini mazingira yale yale – sukari, utando, chakula kukwama kati ya meno – huoza meno mengine pia, hasa yale yanayogusana. Bakteria wanaosababisha kuoza wanaweza kuhamishwa kutoka kwa mzazi kwenda kwa mtoto kupitia mate (kupuliza chakula, kushirikiana kijiko).

Norethisterone na Hedhi

Norethisterone ni dawa ya homoni ya jamii ya projestojeni inayotumika kusogeza hedhi kwa muda (mfano safari, harusi, michezo) na kutibu matatizo kama hedhi nzito, isiyo na mpangilio au endometriosisi, kwa maelekezo ya mtoa huduma. Huzuia ukuta wa kizazi kushuka; hedhi huja siku 2 hadi 3 baada ya kuacha dawa. Si kinga ya mimba – tumia kondomu au njia nyingine. Kwa sababu sehemu ya dawa hubadilika mwilini kuwa estrojeni, haifai kwa wenye historia ya damu kuganda au vihatarishi vyake.

Ni yapi madhara ya Misoprostol?

Misoprostol hutumika hospitali kuzuia na kutibu damu nyingi baada ya kujifungua, katika huduma ya mimba kuharibika, kuandaa shingo ya kizazi, na kukinga vidonda vya tumbo kwa wanaotumia dawa za maumivu. Maudhi ya kawaida ni maumivu ya tumbo, damu, kichefuchefu, kuharisha, kutetemeka na homa ya muda mfupi. Damu nyingi, homa zaidi ya siku 1, harufu mbaya au maumivu makali ni dalili za hatari.

Je, maji kwenye Cul-de-sac ni dalili ya PID? Ukweli wa kisayansi

Cul-de-sac (pouch of Douglas) ni nafasi nyuma ya mfuko wa uzazi. Maji kidogo hapo ni ya kawaida kwa wanawake wengi – hasa baada ya ovuleshaji (yai linapotoka), wakati wa hedhi, au sisti ndogo kupasuka. Kwa hiyo "maji kidogo kwenye cul-de-sac" kwenye ultrasound peke yake si utambuzi wa PID. PID hutambuliwa kwa dalili (maumivu ya nyonga) pamoja na uchunguzi wa daktari unaoonyesha maumivu ya mlango wa kizazi, mfuko au ovari kuguswa, na hupimwa kwa magonjwa ya zinaa. Maji mengi, yenye vipande au damu, pamoja na maumivu makali au kipimo cha mimba chanya ni ya hatari – huweza kuwa mimba nje ya kizazi iliyopasuka.

Kuoga baada ya Kujifungua kwa Upasuaji: Mwongozo Kamili

Baada ya upasuaji wa kujifungua, mama anaweza kuoga kwa bomba au kumwaga maji (shower) kuanzia saa 24 baada ya upasuaji, au kama mtoa huduma alivyoelekeza kuhusu bandeji. Maji ya uvuguvugu yanafaa; maji hayana madhara kwenye mshono yakiruhusiwa kutiririka juu yake bila kusugua. Kausha mshono kwa kugusagusa na taulo safi. Epuka kukaa ndani ya beseni, kuogelea au kuoga maji ya moto sana hadi mshono upone kabisa (mara nyingi wiki 2–6). Kizunguzungu siku za mwanzo ni kawaida – kaa kwenye kiti au mtu awe karibu. Maji ya bomba safi yanatosha; hakuna haja ya dawa za kuongeza kwenye maji.

bottom of page