top of page

Maelezo ya majibu ya maswali mbalimbali ya kiafya

Kuna aina ngapi za seli mundu?

Selimundu ni kundi la magonjwa ya kurithi ya hemoglobini. Mtu hupata ugonjwa akirithi kinasaba S kutoka kwa mzazi mmoja na kinasaba kingine kisicho cha kawaida kutoka kwa mzazi mwingine. Aina kuu: HbSS (kali zaidi na ya kawaida zaidi Tanzania), HbSβ⁰ thalassaemia (kali kama SS), HbSC (ya wastani) na HbSβ⁺ thalassaemia (nyepesi). Aina nyingine ni HbSD, HbSO-Arab na HbSE. Mwenye HbAS (sickle cell trait) ni mbebaji tu, si mgonjwa.

Daktari Si Mganga wa Kienyeji: Hawezi Kutambua Ugonjwa kwa Dalili Moja Tu

Daktari hatambui ugonjwa kwa ramli wala kwa kusikia dalili moja – anategemea mchakato wa kisayansi: kusikiliza historia ya dalili, kuuliza maswali ya ziada, kuchunguza mwili, kufikiria orodha ya magonjwa yanayowezekana, na kuomba vipimo vinavyohitajika. Dalili kama upele, kichwa kuuma au kuchoma kukojoa zina visababishi vingi tofauti vinavyohitaji tiba tofauti. Kuomba dawa kwa kutaja dalili moja tu huleta hatari ya tiba isiyo sahihi, usugu wa dawa na kuchelewesha ugonjwa hatari. Kikokotoo kilicho kwenye ukurasa huu kinaonyesha jinsi dalili moja inavyoweza kuwa na visababishi vingi.

Kwa nini nakosa hedhi lakini kipimo cha ujauzito kinaonyesha negative?

Kwanza, kipimo kinaweza kuwa kimefanywa mapema mno – rudia baada ya siku 7, kwa mkojo wa asubuhi. Kama bado ni hasi, kukosa hedhi huweza kusababishwa na msongo, kupungua au kuongezeka uzito sana, mazoezi makali, PCOS, tezi ya shingo, homoni ya maziwa (prolactin) kuwa juu, kunyonyesha, njia za uzazi wa mpango kama sindano (Depo) au P2, na kukaribia komahedhi. Mara nyingi hedhi hurudi chanzo kikiondoka. Kukosa hedhi miezi 3 mfululizo (au miezi 6 kwa aliyekuwa na mzunguko usio na mpangilio) kunahitaji uchunguzi.

Jinsi ya kupata mtoto wa kike

Jinsia ya mtoto huamuliwa na mbegu ya mwanaume: mbegu yenye kromosomu X huleta msichana, na yenye Y huleta mvulana. Kila mimba ni tukio jipya, na nafasi ya kupata msichana ni karibu nusu kwa nusu, hata kama tayari mna wavulana kadhaa.

Je, mimba imeingia lini?

Kwa mzunguko wa siku 29 na hedhi iliyoanza tarehe 4, uovuleshaji hutarajiwa karibu tarehe 18 (siku 14 kabla ya hedhi inayofuata). Tendo la tarehe 18 na 19 lilikuwa siku za juu kabisa za kushika mimba bila kinga yoyote, hivyo mimba ina uwezekano mkubwa zaidi kutokana na tendo hilo. Hata hivyo tendo la tarehe 14 na 15 haliwezi kuondolewa kabisa: P2 hushindwa wakati mwingine, hasa ikimezwa karibu na uovuleshaji, na mbegu huweza kuishi hadi siku 5. Hakuna kipimo kinachoweza kutofautisha siku 3 hadi 4.

Majira na dawa za kifafa

Baadhi ya dawa za kifafa (carbamazepine, phenytoin, phenobarbital, primidone, oxcarbazepine, topiramate) huongeza kasi ya ini kuvunja homoni, hivyo vidonge vya majira, kiraka, pete na hata kipandikizi hufanya kazi kidogo na mimba inaweza kutokea. Njia zinazofaa zaidi ni kitanzi cha shaba, kitanzi cha homoni na sindano (Depo). Kwa upande mwingine, vidonge vyenye estrojeni hushusha kiwango cha lamotrigine na kuongeza degedege. Valproate inahitaji kinga ya uhakika kwa sababu huleta kasoro kwa mtoto.

bottom of page