top of page

Mwandishi:

ULY CLINIC

Mhariri:

ULY CLINIC

Imeboreshwa:

1 Oktoba 2026, 15:52:07

Kusimama kwa Uume wa Mtoto

Huanzia Lini, Kwa nini hutokea na ni wakati gani kunakuwa Tatizo?

Mzazi anaweza kumuona mtoto mchanga wakati wa kumbadilisha nepi na kugundua kuwa uume wake umesimama. Mzazi mwingine anaweza kumuona mtoto akisimamisha uume wakati wa kuoga, wakati wa kulala au wakati wa kuguswa eneo la siri. Hali hii inaweza kuwafanya wazazi kujiuliza:


Je, kusimama kwa uume huanza wakati wa balehe, au mtoto anaweza kuwa na hali hii tangu akiwa mchanga?

Kitaalamu, kusimama kwa uume huanza mapema sana katika ukuaji wa mtoto wa kiume. Tafiti za uchunguzi wa watoto ambao bado hawajazaliwa zimeonyesha kwamba uume unaweza kujaa damu na kusimama hata katika kipindi cha mwisho cha ujauzito. Katika utafiti wa watoto wa kiume wenye umri wa wiki thelathini na sita hadi thelathini na tisa za ujauzito, kusimama kwa uume kulionekana mara kadhaa wakati wa uchunguzi na kulihusishwa kwa kiasi kikubwa na vipindi vya usingizi wakati macho yanajongea kwa kasi(REM).


Hivyo, kusimama kwa uume si jambo linalosubiri mtoto afikie balehe. Mtoto mchanga anaweza kupata kusimama kwa uume kwa sababu ya utendaji wa kawaida wa mfumo wa fahamu na mishipa ya damu, bila kuwa na mawazo, nia au uelewa wowote kuhusu ngono. Kadiri mtoto anavyokua, kusimama huendelea kutokea, hasa wakati wa usingizi, na wakati wa balehe mabadiliko ya homoni na ukuaji wa mfumo wa uzazi huambatana na kuongezeka kwa mara kwa mara na ukubwa wa kusimama.


Makala hii inaeleza kusimama kwa uume kuanzia kipindi cha kabla ya kuzaliwa, mtoto mchanga, utoto na kuelekea balehe; inaeleza kwa nini hutokea, mzazi anaweza kuona dalili gani na ni wakati gani hali hiyo inahitaji mtoto achunguzwe na mtoa huduma wa afya.


Kusimama kwa uume ni nini?

Kusimama kwa uume ni hali ambayo uume huongezeka ugumu kutokana na kuongezeka kwa damu ndani ya tishu maalumu za uume. Mishipa ya damu inayosambaza uume hubadilika na kuruhusu damu kuingia zaidi, huku utokaji wa damu ukipungua kwa muda. Mchakato huu hudhibitiwa na mwingiliano wa mfumo wa fahamu, mishipa ya damu na tishu za uume.


Kwa hiyo, kusimama kwa uume ni sehemu ya kawaida ya utendaji wa mwili wa mwanaume, na si jambo linalotokea kwa sababu ya mawazo ya kingono pekee. Mtoto anaweza kuwa na kusimama bila kuelewa maana yake, bila kuwa na nia yoyote ya kingono na bila hata kugusa uume wake.


Hii ndiyo sababu kusimama kwa uume kunaweza kuonekana katika hatua mbalimbali za maisha ya mtoto. Tafiti za watoto wenye umri wa miaka mitatu hadi kumi na nane zimeonyesha kuwa kusimama kwa uume wakati wa usingizi hutokea pia katika utoto, na mara kwa mara huongezeka kadiri mtoto anavyokaribia balehe.


Uume wa mtoto huanza kusimama kuanzia umri gani?

Uwezo wa uume kusimama huanza mapema sana, hata kabla mtoto hajazaliwa. Uchunguzi wa kutumia picha za mawimbi ya sauti kwa watoto wa kiume walio tumboni umeonyesha vipindi vya kusimama kwa uume katika wiki za mwisho za ujauzito. Hii inaonyesha kwamba mfumo unaohusika na kusimama kwa uume huwa tayari unafanya kazi kabla ya kuzaliwa.


Baada ya kuzaliwa, mtoto mchanga anaweza pia kupata kusimama kwa uume. Hali hii inaweza kuonekana wakati wa kubadilishwa nepi, kuogeshwa au kuguswa eneo la siri, lakini inaweza pia kutokea bila kichocheo kinachoonekana. Kwa hiyo, kusimama kwa uume kwa mtoto mchanga si ishara kwamba mtoto ameanza kuelewa masuala ya ngono; ni sehemu ya utendaji wa kawaida wa mwili.


Kinachobadilika zaidi mtoto anapofikia balehe si kuanza kwa uwezo wa kwanza wa uume kusimama, bali kuongezeka kwa mara kwa mara, muda na ukubwa wa kusimama, pamoja na mabadiliko mengine yanayotokana na kuanza kwa shughuli kubwa zaidi ya homoni za uzazi. Tafiti za kusimama kwa uume wakati wa usingizi kwa watoto zimeonyesha kuwa hali hii ipo hata kabla ya balehe na huongezeka pamoja na ukuaji wa mtoto na kuanza kwa mabadiliko ya balehe.


Kwa nini uume wa mtoto mchanga husimama?

Kwa mtoto mchanga, kusimama kwa uume ni sehemu ya utendaji wa kawaida wa mfumo wa fahamu na mishipa ya damu. Mfumo huu unaweza kuanzisha mabadiliko ya mtiririko wa damu ndani ya uume bila mtoto kuwa na uelewa wowote kuhusu tukio hilo.


Kusimama kunaweza kuonekana baada ya msisimko mdogo wa eneo la siri, kwa mfano wakati wa kumbadilisha nepi au wakati wa kuoga. Hata hivyo, si lazima kila kusimama kuwe na kichocheo ambacho mzazi anaweza kukitambua. Kusimama kunaweza pia kutokea wakati mtoto amelala au bila sababu inayoonekana. Utafiti wa watoto walio tumboni pia umeonyesha uhusiano mkubwa kati ya kusimama kwa uume na vipindi vya usingizi wa kipindi cha macho kujongea kwa kasi, jambo linalosaidia kueleza kwa nini kusimama kunaweza kutokea bila mtoto kuwa macho au kufikiri kuhusu chochote.


Kwa hiyo, mzazi akimwona mtoto mchanga akiwa na uume uliosimama, hali hiyo kwa kawaida inaweza kuwa sehemu ya kawaida ya utendaji wa mwili. Kusimama kwa muda mfupi hakumaanishi mtoto ana tatizo, wala hakumaanishi ameanza kuwa na tabia au mawazo ya kingono.


Nitajuaje kama uume wa mtoto mchanga umesimama?

Kwa mtoto mchanga, mzazi anaweza kuona uume ukiwa umeinuka zaidi kuliko kawaida na kuwa mgumu zaidi. Wakati mwingine tofauti hiyo inaweza kuonekana wazi wakati wa kumbadilisha nepi au kumwosha mtoto.


Hata hivyo, mzazi hahitaji kuushika, kuubana au kuuchochea uume ili kuthibitisha kama unaweza kusimama. Kusimama ni tukio linalotokea kwa vipindi, na hakuna sababu ya mzazi kulifanya kuwa kipimo cha kila siku cha afya ya mtoto.


Kutokuona uume ukisimama wakati wa kumbadilisha nepi pia hakumaanishi kwamba hauwezi kusimama. Kusimama kunaweza kutokea wakati mtoto amelala au katika muda mfupi ambao mzazi haupo, na tafiti za watoto zimeonyesha kuwa kusimama wakati wa usingizi ni jambo la kawaida katika hatua mbalimbali za utoto.


Kwa hiyo, uwepo wa kusimama kwa uume ni sehemu ya kawaida ya ukuaji wa mtoto wa kiume, lakini tukio moja la kutokuona kusimama haliwezi kutumiwa peke yake kuamua kwamba mtoto ana tatizo. Tathmini ya afya ya mtoto inapaswa kuangalia ukuaji wake kwa ujumla, hali ya viungo vya uzazi, mkojo, ukuaji wa mwili na, anapofikia umri unaofaa, mabadiliko ya balehe.


Kusimama kwa uume hubadilika mtoto anapokua

Mtoto mchanga, mtoto wa miaka michache na kijana anayekaribia balehe wanaweza wote kupata kusimama kwa uume, lakini namna hali hiyo inavyojitokeza hubadilika kadiri mwili unavyokua.


Katika miaka ya mwanzo, kusimama kunaweza kuwa kwa muda mfupi na kutokea bila sababu inayotambulika. Katika utoto, kusimama wakati wa usingizi huendelea kutokea. Tafiti za watoto wenye umri wa miaka mitatu hadi kumi na nane zimeonyesha kuwa kusimama wakati wa usingizi huonekana katika utoto na huongezeka kwa ujumla kadiri umri unavyoongezeka, huku mabadiliko makubwa zaidi yakionekana wakati wa kuelekea balehe.


Wakati wa balehe, mfumo wa homoni za uzazi huanza kufanya kazi kwa kiwango kikubwa zaidi. Hii huambatana na ukuaji wa uume na korodani, kuongezeka kwa homoni za kiume na kuongezeka kwa kusimama kwa uume. Kwa hiyo, balehe haianzi uwezo wa uume kusimama, bali huleta hatua mpya ya ukuaji ambayo kusimama huwa mara kwa mara zaidi na kuambatana na mabadiliko mengine ya kijinsia ya mwili.


Ni wakati gani kusimama kwa uume kunakuwa tatizo?

Kusimama kwa uume kwa muda mfupi kwa mtoto kwa kawaida si tatizo. Kinachohitaji tahadhari zaidi ni pale uume unapobaki umesimama kwa muda mrefu isivyo kawaida, hasa ikiwa mtoto anaonekana kuwa na maumivu au hali hiyo haipungui.


Kusimama kwa uume kunakodumu kwa muda mrefu kunaweza kuwa hali ya kitabibu inayojulikana kama priapizimu. Kwa mtoto mchanga hali hii ni nadra sana, na tafiti zinaonyesha kwamba visa vingi vilivyoripotiwa kwa watoto wachanga huweza kuisha vyenyewe, lakini hali inayoendelea inahitaji kutathminiwa ili kutofautisha kusimama kwa kawaida na hali ya kitabibu.


Kwa mtoto wa umri wowote, uume uliosimama kwa muda mrefu pamoja na maumivu, ugumu mkubwa au kutopungua unapaswa kuchukuliwa kwa uzito na mtoto apelekwe kwa mtoa huduma wa afya. Hii ni tofauti kabisa na kusimama kwa kawaida kwa muda mfupi ambako hujitokeza na kisha uume hurudi katika hali yake ya kawaida.


Je, mtoto ambaye mzazi hajawahi kumuona akisimika ana tatizo?

Kusimama kwa uume si tukio linalotokea kwa ratiba maalumu. Mtoto anaweza kuwa na kusimama mara kadhaa lakini mzazi asione hata moja kwa sababu matukio hayo yanaweza kutokea wakati wa usingizi au wakati wa kubadilisha mkao.


Hii ndiyo sababu kutokumuona mtoto akiwa na uume uliosimama si kipimo kizuri cha kuamua kama mfumo wake wa uume unafanya kazi. Mtoa huduma hatarajii mzazi awe amerekodi mara ambazo uume wa mtoto umesimama.


Kwa mtoto mchanga na mtoto mdogo, tathmini ya afya ya mfumo wa uzazi huangalia mambo mengi zaidi: muundo wa uume, uwepo na nafasi ya korodani, kukojoa, ukuaji wa mtoto na dalili nyingine za viungo vya uzazi.


Kusimama kwa uume na kukojoa

Kibofu cha mkojo kilichojaa kinaweza kuhusishwa na kusimama kwa uume kwa baadhi ya watoto wadogo. Hii inaweza kuwa sababu mzazi akamwona mtoto akiwa na uume uliosimama kabla ya kukojoa au baada ya kuamka kutoka usingizini.


Hata hivyo, si kila kusimama kwa uume kunatokana na kibofu kilichojaa. Kwa watoto wadogo, kusimama kunaweza kutokea kwa sababu mbalimbali au bila sababu inayoweza kutambuliwa.


Jambo muhimu ni kutenganisha mambo mawili: kusimama kwa uume na uwezo wa kukojoa. Mtoto anayekojoa vizuri lakini mzazi hajawahi kumuona akisimama si lazima awe na tatizo la kusimama kwa uume.


Kusimama wakati wa usingizi

Uume unaweza kusimama wakati mtoto amelala. Hili linaweza kutokea hata kwa mtoto ambaye hajafikia umri wa kuelewa mambo ya kingono.


Mabadiliko ya kawaida katika mfumo wa fahamu wakati wa usingizi yanaweza kuhusishwa na vipindi vya kusimama. Kwa hiyo, mtoto anaweza kuwa na kusimama wakati amelala bila mzazi au mtoto mwenyewe kujua.


Katika balehe, kusimama wakati wa usingizi na wakati wa kuamka huwa jambo linalotambulika zaidi. Hii ndiyo sababu baadhi ya vijana huamka asubuhi wakiwa na uume uliosimama.


Kusimama wakati wa usingizi, kwa kutokuwepo kwa maumivu au dalili nyingine zisizo za kawaida, ni sehemu ya fiziolojia ya kawaida ya uume.


Kusimama kwa uume katika vipindi tofauti vya ukuaji


Kipindi cha kichanga: kuzaliwa hadi siku ishirini na nane

Katika kipindi hiki, uume unaweza kusimama kwa muda mfupi na kisha kurudi katika hali yake ya kawaida.

Kichocheo kidogo wakati wa kubadilisha nepi, kuoga au kugusa eneo la siri kinaweza kuchangia hali hii. Kibofu kilichojaa pia kinaweza kuhusika.


Kwa mtoto mchanga, kusimama kwa muda mfupi bila maumivu si jambo linalohitaji kutibiwa. Kinachohitaji tahadhari ni hali tofauti kabisa Uume kubaki umesimama kwa muda mrefu, hasa ikiwa kuna maumivu, mabadiliko ya rangi au mtoto anaonekana kuwa katika hali isiyo ya kawaida.


Baada ya kichanga: miezi ya mwanzo hadi utoto

Uwezo wa uume kusimama unaendelea kuwepo baada ya mtoto kutoka kipindi cha kichanga. Hata hivyo, mzazi anaweza asione kusimama mara kwa mara. Mtoto anaweza kupata kusimama wakati wa usingizi, wakati kibofu kimejaa, wakati wa kuguswa au bila sababu inayoonekana.


Katika kipindi hiki, hakuna idadi maalumu ya kusimama ambayo mtoto anatakiwa kuwa nayo kila siku. Kwa hiyo, si sahihi kusema mtoto wa mwaka mmoja, miwili au mitatu lazima awe anasimika mara fulani kwa siku.


Utoto wa mapema

Mtoto anapokuwa mkubwa kidogo, anaweza pia kuanza kugusa sehemu zake za siri kama sehemu ya kujitambua mwili.


Hii haimaanishi kwamba mtoto anaelewa ngono kama mtu mzima. Watoto hujifunza kuhusu miili yao kupitia kugusa, kuona na kuhisi sehemu mbalimbali za mwili.


Mzazi anaweza kutumia hatua hii kumfundisha mtoto majina sahihi ya sehemu za mwili, usafi, faragha na kwamba sehemu za siri ni sehemu binafsi. Kumtisha au kumdhalilisha mtoto kunaweza kumfanya ashindwe kuzungumza baadaye anapopata tatizo la kiafya katika eneo hilo.


Umri wa shule kabla ya balehe

Katika umri huu, kusimama kwa uume bado kunaweza kutokea bila mtoto kuwa na mawazo ya kingono.

Msuguano wa nguo, kugusa eneo hilo wakati wa kuoga, kubadilisha mkao, usingizi au shughuli za kawaida za mfumo wa fahamu vinaweza kuhusishwa na kusimama.


Mtoto anaweza kuanza kuona aibu anapotambua kwamba uume wake unasimama. Hii ni kawaida, na mzazi anaweza kumsaidia kuelewa kwamba mwitikio huo wa mwili si jambo la aibu.


Kipindi cha balehe

Wakati wa balehe, kusimama kwa uume huwa cha mara kwa mara zaidi. Mabadiliko ya homoni huenda sambamba na ukuaji wa korodani na uume, kuongezeka kwa nywele sehemu za siri, mabadiliko ya sauti na mabadiliko mengine ya mwili.


Katika kipindi hiki, kusimama kunaweza kutokea bila mtoto kugusa uume na bila kuwa na mawazo ya kingono. Kinaweza kutokea shuleni, wakati wa kukaa, wakati wa kuamka au katika mazingira mengine yasiyohusiana na ngono. Hii ni sehemu ya kawaida ya kukomaa kwa mfumo wa uzazi.


Je, kusimama kwa uume ni ishara kwamba mtoto ameanza kubalehe?

Kusimama kwa uume pekee hakuthibitishi kwamba mtoto ameanza balehe. Mtoto anaweza kupata kusimama kabla ya kuonekana kwa mabadiliko mengine ya balehe. Kwa hiyo, mtoa huduma anapotathmini balehe huangalia ukuaji wa mtoto kwa ujumla, si kusimama kwa uume pekee.


Mabadiliko yanayoweza kuonyesha kuanza kwa balehe ni pamoja na kuongezeka kwa ukubwa wa korodani, ukuaji wa uume, kuanza kwa nywele sehemu za siri, kuongezeka kwa kasi ya ukuaji na baadaye mabadiliko ya sauti.


Kwa hiyo, mzazi anayemwona mtoto akiwa na uume uliosimama mara moja au mara kadhaa hapaswi kutumia tukio hilo pekee kusema kwamba mtoto ameanza balehe.


Je, kutokuwepo kwa kusimama kunaweza kuonyesha tatizo?

Hapa kuna tofauti muhimu kati ya kutokumuona mtoto akisimika na kutokuwa na uwezo wa kusimama.

Mzazi hawezi kuthibitisha kutokuwa na uwezo wa kusimama kwa mtoto kwa kutokuona tukio hilo. Kusimama kunaweza kutokea wakati wa usingizi au wakati ambao mzazi hayupo.


Kwa mtoto mkubwa au kijana, ikiwa kuna wasiwasi kuhusu kutokuwepo kabisa kwa kusimama pamoja na dalili nyingine za kuchelewa kwa balehe, matatizo ya viungo vya uzazi au magonjwa mengine, mtoa huduma anaweza kufanya tathmini ya kina.


Hata hivyo, hakuna kiwango cha kusimama ambacho mtoto anapaswa kufikia kila siku ili kuthibitisha kwamba yuko salama kiafya. Sayansi haitumii hesabu ya mara ngapi mtoto anapaswa kusimika kwa siku kama kipimo cha kawaida cha afya.


Kusimama kwa uume na ukubwa wa uume

Wazazi wengine huchanganya kutokuonekana kwa kusimama na kuwa na uume mdogo. Uume wa mtoto mchanga huwa mdogo kuliko wa mtoto mkubwa na wa kijana, na ukubwa hubadilika kadiri mtoto anavyokua. Kwa watoto wadogo, muonekano wa uume unaweza pia kuathiriwa na mafuta yaliyopo kwenye eneo la chini ya tumbo na namna uume ulivyojificha ndani ya ngozi.


Kwa hiyo, ukubwa wa uume ukiwa umetulia haupaswi kutumiwa peke yake kutabiri uwezo wa uume kusimama au uwezo wa kupata watoto baadaye. Tathmini ya ukubwa wa uume kwa mtoto hufanywa kwa vipimo maalumu vya kitabibu inapokuwa kuna sababu ya kufanya hivyo.


Kusimama kwa uume hakumaanishi mtoto ana uwezo wa kupata watoto

Hili ni jambo muhimu kwa wazazi kulielewa. Kusimama kwa uume na uwezo wa kupata mtoto ni mambo mawili yanayohusiana na mfumo wa uzazi lakini si kitu kimoja. Kusimama kunahusu zaidi mabadiliko ya mtiririko wa damu na utendaji wa mishipa ya fahamu na tishu za uume.


Uwezo wa mwanaume kupata mtoto baadaye unategemea mambo mengine, hasa ukuaji na utendaji wa korodani, uzalishaji wa mbegu za kiume, mfumo wa kusafirisha mbegu, homoni na mambo mengine ya afya ya uzazi.


Kwa hiyo, mtoto anaweza kuwa na kusimama kwa uume lakini bado hatuwezi kutumia jambo hilo kusema atakuwa na uwezo wa kupata watoto baadaye. Vivyo hivyo, kutomuona mtoto akisimama hakutoshi kusema atakuwa na tatizo la uzazi.


Je, kitovu kikidondokea kwenye sehemu za siri mtoto wa kiume hawezi kupata watoto?

Hili ni imani inayoweza kusikika katika jamii, lakini halina msingi wa kitabibu unaoonyesha kwamba kitovu cha mtoto kikidondokea au kugusa sehemu zake za siri husababisha utasa wa baadaye.


Kamba ya kitovu baada ya mtoto kuzaliwa hubaki ikiwa imeunganishwa na kitovu cha mtoto kwa muda, kisha hukauka na kudondoka. Mchakato huo unahusiana na uponaji wa sehemu ya kitovu baada ya mtoto kuachana na kondo la nyuma; hauamui namna korodani zitakavyokua au uwezo wa mtoto kuzalisha mbegu za kiume baadaye. Ushahidi kuhusu utunzaji wa kitovu huzingatia hasa kuzuia maambukizi ya kitovu na kuhakikisha kinapona vizuri.


Uwezo wa kupata watoto baadaye unahusiana na ukuaji na utendaji wa mfumo wa uzazi. Kwa mwanaume, sababu za utasa zinaweza kuhusisha matatizo ya uzalishaji wa mbegu, idadi ya mbegu, mwendo wa mbegu, muundo wa mbegu, matatizo ya kusafirisha mbegu na matatizo mengine ya mfumo wa uzazi.


Kwa hiyo, mzazi hapaswi kuogopa kwamba kitovu kikigusa au kudondokea sehemu za siri za mtoto kitamfanya asiweze kupata watoto. Hakuna ushahidi wa kitabibu unaothibitisha uhusiano huo.


Kusimama kwa uume na tohara

Tohara haimaanishi kwamba mtoto lazima awe na kusimama zaidi au kidogo. Uume unaweza kusimama kabla au baada ya tohara kwa sababu mfumo unaosababisha kusimama unahusisha mishipa ya fahamu, mishipa ya damu na tishu za uume, si govi pekee.


Baada ya tohara, mtoto anaweza kupata kusimama kama kawaida. Kwa mtoto mchanga, hali hii inaweza kutokea wakati wa kupona na si lazima iwe ishara kwamba kidonda kina tatizo.


Hata hivyo, ikiwa kusimama baada ya tohara kunaambatana na kutokwa damu nyingi, uvimbe unaoongezeka, kubadilika kwa rangi ya uume, homa, usaha au mtoto kuonekana kuwa katika maumivu makali, anapaswa kuchunguzwa.


Je, kusimama kwa uume kunaweza kuumiza?

Kusimama kwa kawaida hakupaswi kusababisha maumivu. Mtoto mkubwa anaweza kuhisi uume ukiwa na mvutano wakati umesimama, lakini maumivu makali au yanayorudia si sehemu ya kawaida ya kusimama.


Kusimama kwa muda mrefu na kwa maumivu ni hali tofauti. Hali hiyo inaweza kuonyesha kwamba damu imekwama ndani ya tishu za uume na inaweza kuhitaji matibabu ya haraka.


Kusimama kwa uume kwa muda mrefu: ni lini hali inabadilika kuwa tatizo?

Katika watoto, hali ya kusimama kwa uume kwa muda mrefu inayodumu saa nne au zaidi bila kuhusishwa na msisimko wa kawaida huainishwa kama hali ya kitabibu inayohitaji tathmini. Aina inayotokana na damu kushindwa kutoka vizuri ndiyo inayohitaji haraka zaidi kwa sababu inaweza kusababisha ukosefu wa oksijeni katika tishu za uume na uharibifu wa kudumu.


Kwa watoto, ugonjwa wa selimundu ni sababu muhimu ya hali hii. Sababu nyingine zinaweza kujumuisha baadhi ya magonjwa ya damu, dawa fulani, majeraha na wakati mwingine sababu haipatikani.


Kwa mtoto mchanga, hali ya kusimama kwa muda mrefu ni nadra na ina tabia tofauti na ile inayotokea kwa watoto wakubwa. Aina ya mtoto mchanga mara nyingi huwa haina maumivu na inaweza kuisha yenyewe, lakini mtoto anayekuwa na kusimama kwa muda mrefu bado anahitaji tathmini ya kitabibu ili kutofautisha hali salama na hali inayohitaji matibabu.


Mtoto mwenye ugonjwa wa selimundu anahitaji uangalizi maalumu

Kwa mtoto mwenye ugonjwa wa selimundu, kusimama kwa uume kwa muda mrefu au vipindi vinavyorudia ni jambo ambalo mzazi anapaswa kulijua mapema.


Ugonjwa huu unaweza kuathiri mtiririko wa damu na kuongeza uwezekano wa aina fulani ya kusimama kwa muda mrefu. Vipindi vinavyorudia vinaweza pia kutokea kabla ya tukio refu na lenye maumivu.


Kwa hiyo, familia yenye mtoto mwenye ugonjwa wa selimundu inapaswa kuwa na maelekezo ya wazi kutoka kwa timu inayomtibu kuhusu hatua za kuchukua dalili zinapoanza. Miongozo ya mfumo wa mkojo kwa watoto inapendekeza ushirikiano kati ya wataalamu wa mfumo wa mkojo na wataalamu wa magonjwa ya damu katika hali hizi.


Kusimama kwa uume kwa mtoto mchanga kwa muda mrefu

Hapa kuna tofauti muhimu ambayo wazazi wengi hawajui. Kusimama kwa muda mfupi kwa mtoto mchanga ni jambo la kawaida. Lakini kusimama kunakodumu kwa saa nyingi ni jambo tofauti na huitwa kusimama kwa uume kwa muda mrefu wa kipindi cha kichanga.


Hali hii ni nadra sana. Katika visa vingi vilivyochapishwa, hasa pale mtoto hana maumivu na uume unaendelea kuwa na mzunguko mzuri wa damu, hali imeweza kuisha yenyewe kwa uangalizi wa kitabibu. Sababu inayotambulika wakati mwingine ni kuongezeka kwa chembe nyekundu za damu, lakini katika visa vingi sababu haipatikani.


Kwa hiyo, mzazi hapaswi kujaribu kutibu hali hiyo nyumbani. Mtoto mchanga mwenye kusimama kwa muda mrefu anapaswa kuonekana na mtoa huduma ili kutathmini rangi ya uume, maumivu, mtiririko wa damu na hali nyingine zinazoweza kuhusika.


Mambo ambayo mzazi hapaswi kufanya

Mzazi hapaswi kujaribu kubana uume wa mtoto ili kuumaliza kusimama. Pia si salama kutumia dawa za mtu mzima, dawa za kienyeji au njia nyingine zisizoelekezwa na mtoa huduma ili kujaribu kuufanya uume ulale.


Kwa kusimama kwa kawaida kwa muda mfupi, hakuna matibabu yanayohitajika. Mtoto anahitaji tu kuachwa katika hali yake ya kawaida.


Ikiwa kusimama ni kwa muda mrefu, kuna maumivu au kuna dalili nyingine zisizo za kawaida, hatua sahihi ni kutafuta huduma ya kitabibu badala ya kujaribu kulazimisha uume ulale nyumbani.


Ni wakati gani mzazi ampeleke mtoto hospitali?

Mtoto anapaswa kuchunguzwa haraka ikiwa:

  • Uume umesimama kwa muda mrefu na haushuki

  • Kusimama kunaambatana na maumivu

  • Uume unaendelea kuwa mgumu sana kwa muda mrefu

  • Kuna mabadiliko yasiyo ya kawaida ya rangi

  • Kuna uvimbe mkubwa

  • Hali imeanza baada ya jeraha kwenye uume, nyonga au eneo la kati ya mapaja

  • Mtoto ana ugonjwa wa selimundu na amepata kusimama kwa muda mrefu au kwa maumivu

  • Mtoto anaonekana kuwa katika maumivu makali au hali yake ya jumla imebadilika


Kwa kusimama kwa muda mrefu kwa aina inayotokana na damu kukwama, kuchelewa kutibiwa kunaweza kuongeza hatari ya uharibifu wa tishu za uume.


Hitimisho

Kusimama kwa uume ni sehemu ya kawaida ya fiziolojia ya mtoto wa kiume na huanza tangu kipindi cha kichanga, si wakati wa balehe pekee. Kwa mtoto mchanga na mtoto mdogo, kunaweza kutokea wakati wa usingizi, kibofu kikiwa kimejaa, wakati wa kuguswa au bila sababu inayoonekana; kadiri mtoto anavyoingia balehe, kusimama huwa cha mara kwa mara zaidi kutokana na mabadiliko ya ukuaji na homoni.


Mzazi pia hapaswi kuwa na hofu kwa sababu hajawahi kumuona mtoto mdogo akiwa na uume uliosimama, kwa kuwa kusimama kunaweza kutokea wakati ambao mzazi haoni. Vilevile, hakuna ushahidi kwamba kitovu kudondokea au kugusa sehemu za siri husababisha mtoto wa kiume kushindwa kupata watoto baadaye. Kinachohitaji uchunguzi ni kusimama kwa muda mrefu, hasa kunakoambatana na maumivu au dalili nyingine zisizo za kawaida.


Kwa ujumla, lengo si mtoto kuwa na idadi fulani ya kusimama kwa siku; lengo ni ukuaji wa kawaida wa mfumo wa uzazi na kutambua mapema dalili zinazoashiria tatizo.


Maswali yanayoulizwa Mara kwa Mara kuhusu kusimama kwa uume wa mtoto

1. Nitajuaje kama mtoto wangu mchanga uume wake unasimama ikiwa siwezi kuuona kila wakati?

Kwa mtoto mchanga, mzazi anaweza kutambua kusimama kwa kuangalia mabadiliko ya muda katika mwonekano wa uume. Uume unaweza kuonekana umeinuka, kuwa mgumu zaidi kuliko kawaida na wakati mwingine kuonekana umejaa zaidi. Hali hiyo inaweza kuonekana wakati wa kumbadilisha nepi, kuoga au kumvalisha mtoto.


Hata hivyo, hakuna sababu ya mzazi kujaribu kuuchunguza uume kila wakati. Kusimama kunaweza kutokea wakati mtoto amelala au wakati mzazi hajamtazama, na kunaweza kudumu muda mfupi. Kwa hiyo, kutokumuona mtoto akiwa amesimama si ushahidi kwamba hali hiyo haitokei.


Kwa mtoto mwenye afya, jambo la msingi ni kuangalia afya ya mfumo wa uzazi kwa ujumla. Ikiwa mtoto anakojoa vizuri, hana maumivu, hana uvimbe au mabadiliko yasiyo ya kawaida ya uume na anaendelea kukua vizuri, mzazi hahitaji kuhesabu matukio ya kusimama ili kujiridhisha kwamba uume wake unafanya kazi.

2. Je, mtoto wa kiume anaweza kupata kusimama kwa uume kabla hata hajaanza kutambua sehemu zake za siri?

Mfumo wa mwili unaosababisha kusimama huanza kufanya kazi mapema kuliko uwezo wa mtoto kuelewa maana ya ngono. Hii ndiyo sababu mtoto mchanga anaweza kuwa na kusimama hata akiwa hana ufahamu wa kile kinachotokea katika mwili wake.


Kusimama kwa uume ni matokeo ya mwingiliano wa mfumo wa fahamu, mishipa ya damu na tishu za uume. Mifumo hiyo haianzi kufanya kazi wakati wa balehe; ipo na inafanya kazi tangu mapema katika maisha.


Kwa hiyo, mzazi anapomwona mtoto mchanga akiwa na uume uliosimama hapaswi kutafsiri tukio hilo kwa kutumia fikra za ngono za mtu mzima. Kwa mtoto mdogo, tukio hilo linaweza kuwa mwitikio wa kawaida kabisa wa mwili usio na maana ya kingono.

3. Kwa nini mtoto mmoja anaweza kuonekana akisimika mara nyingi na mwingine mzazi wake haoni kabisa?

Watoto hutofautiana katika muda ambao kusimama hutokea na katika mazingira ambayo mzazi anaweza kukiona. Mtoto mmoja anaweza kupata kusimama wakati wa kubadilisha nepi, wakati mwingine anaweza kupata wakati wa usingizi.


Pia, urefu wa kila tukio hutofautiana. Tukio linalodumu kwa muda mfupi linaweza kuisha kabla mzazi hajaligundua. Hivyo, tofauti kati ya watoto wawili haimaanishi moja kwa moja kwamba mmoja ana tatizo na mwingine hana.


Hakuna kiwango cha idadi ya kusimama kwa siku ambacho kinatumiwa kama kipimo cha kawaida cha afya ya mtoto. Kwa hiyo, mzazi hapaswi kuwalinganisha watoto wawili kwa kuangalia mara ngapi uume wao unaonekana kusimama. Tathmini ya kitabibu hutegemea hali nzima ya mtoto.

4. Je, mtoto anaweza kupata kusimama kwa uume wakati wa kukojoa au baada ya kukojoa?

Kibofu kilichojaa kinaweza kuchangia kusimama kwa uume kwa baadhi ya watoto wadogo kwa sababu mifumo ya fahamu inayohusiana na kibofu na sehemu za siri iko karibu katika udhibiti wake.


Hii inaweza kufanya mzazi aone uume wa mtoto ukiwa umesimama kabla ya kukojoa, hasa mtoto anapoamka baada ya kulala. Kwa mtoto mwingine, kusimama kunaweza kuonekana baada ya kukojoa au wakati wa kubadilishwa nepi.


Hata hivyo, uhusiano huu si kanuni kwamba kila mtoto anapaswa kusimama kila anapokuwa na kibofu kilichojaa. Kusimama kwa uume kuna sababu nyingi za kawaida, na wakati mwingine hutokea bila kichocheo kinachoweza kutambuliwa.

5. Je, kusimama kwa uume kunaweza kutumika kujua kama korodani za mtoto zinafanya kazi vizuri?

Kusimama kwa uume huonyesha kwamba baadhi ya mifumo ya fahamu na mishipa ya damu inayohusika na uume inaweza kutoa mwitikio, lakini haiwezi kutumiwa peke yake kutathmini utendaji wote wa korodani.


Korodani zina kazi nyingi, ikiwa ni pamoja na kutengeneza homoni na baadaye kutengeneza mbegu za kiume. Kazi hizi hazipimwi kwa kuangalia tu kama uume unasimama.


Kwa mtoto, mtoa huduma anayetathmini ukuaji wa mfumo wa uzazi ataangalia pia uwepo na nafasi ya korodani, ukubwa na ukuaji wa viungo vya uzazi, ukuaji wa mwili na mabadiliko ya balehe inapofika wakati wake. Hivyo, kusimama ni sehemu moja tu ya mfumo mpana wa uzazi.

6. Je, uume mdogo wa mtoto unapokuwa umetulia unaweza kumaanisha hautasimama vizuri baadaye?

Muonekano wa uume ukiwa umetulia hauwezi kutabiri moja kwa moja uwezo wake wa kusimama baadaye.


Uume hubadilika kwa ukubwa kadiri mtoto anavyokua, na muonekano wake ukiwa umetulia unaweza pia kuathiriwa na joto, ngozi inayouzunguka na mafuta yaliyo katika eneo la chini ya tumbo. Hivyo, wazazi wanaweza kupata picha isiyo sahihi ikiwa watahukumu afya ya uume kwa kuuangalia ukiwa umetulia pekee.


Wakati kuna wasiwasi wa kitabibu kuhusu ukubwa wa uume, mtoa huduma anaweza kufanya kipimo maalumu kinacholinganishwa na viwango vya watoto wa umri husika. Uamuzi huo haupaswi kufanywa kwa kuangalia uume kwa macho pekee au kwa kuulinganisha na wa mtoto mwingine.

7. Kuna imani kwamba kitovu kikidondokea kwenye sehemu za siri za mtoto wa kiume hawezi kupata watoto. Ukweli wa kitabibu ni upi?

Kamba ya kitovu inapodondoka baada ya kuzaliwa ni sehemu ya kawaida ya mchakato wa kupona kwa kitovu. Kitovu kudondokea kwenye uume hakihamishi uwezo wa uzazi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, wala mahali kinapodondokea hakubadilishi ukuaji wa korodani au mfumo wa uzazi.


Utafiti kuhusu kitovu cha mtoto huzingatia hasa muda wa kukauka na kudondoka, usafi, na hatari ya maambukizi ya kitovu. Hakuna ushahidi wa kitabibu unaoonyesha kwamba kamba ya kitovu ikigusa au kudondokea sehemu za siri husababisha mtoto wa kiume kuwa tasa baadaye.


Uwezo wa kupata watoto baadaye hutegemea mambo mengine ya mfumo wa uzazi, kama ukuaji wa korodani, uzalishaji na ubora wa mbegu za kiume, mfumo wa kusafirisha mbegu, homoni na afya ya jumla. Kwa hiyo, imani hiyo haipaswi kutumiwa kumtia mzazi hofu au kumfanya afanye matibabu yasiyo ya lazima.

8. Je, mtoto akiguswa sehemu za siri na uume ukasimama, mzazi anapaswa kuzuia hilo?

Kuguswa au kupapaswa kwa eneo la siri kunaweza kuchochea mwitikio wa kawaida wa mishipa ya fahamu na kusababisha uume kusimama. Kwa mtoto mchanga, hili linaweza kutokea wakati wa kuogeshwa au kubadilisha nepi bila mtoto kuwa na nia yoyote ya kufanya jambo hilo.


Mtoto anapokuwa mkubwa, kugusa sehemu zake za siri kunaweza pia kuwa sehemu ya kujifunza kuhusu mwili wake. Mzazi anaweza kuweka mipaka ya faragha bila kumwambia mtoto kwamba mwili wake ni mchafu au kwamba amefanya jambo la aibu.


Ikiwa kugusa huko kunatokana na kuwashwa, maumivu, vidonda, uchafu, harufu isiyo ya kawaida au matatizo ya kukojoa, hali hiyo inahitaji kutathminiwa kama tatizo la afya. Hapo lengo si kuzuia tabia tu, bali kutafuta sababu ya mtoto kutokuwa na raha.

9. Je, kusimama kwa uume wakati wa balehe kunamaanisha kijana alikuwa akifikiria ngono?

Kusimama kwa uume wakati wa balehe kunaweza kutokea bila kijana kupanga, kugusa uume wake au kuwa na mawazo ya kingono. Mabadiliko ya homoni na mfumo wa fahamu wakati wa balehe yanaweza kusababisha kusimama kutokee bila kutarajiwa.


Hii ndiyo sababu kijana anaweza kupata kusimama akiwa darasani, kwenye usafiri, wakati wa kuzungumza na watu au wakati mwingine katika mazingira ambayo hayana uhusiano wowote na ngono. Hali hiyo inaweza kumfanya kijana aone aibu, lakini ni sehemu ya mabadiliko ya kawaida ya mwili.


Mzazi anaweza kumsaidia kijana kwa kumweleza kwamba mwitikio huo unaweza kutokea bila hiari na kwamba si jambo la kuaibisha. Elimu hiyo humsaidia kijana kuelewa mwili wake bila kuhusisha kila kusimama na tabia au nia ya kingono.

10. Ikiwa mtoto ana kusimama kwa uume kwa muda mrefu, mzazi anatakiwa kuangalia mambo gani kabla ya kufika hospitali?

Jambo la kwanza ni kuangalia muda ambao uume umeendelea kuwa umesimama, kama mtoto ana maumivu, kama uume unaendelea kuwa mgumu sana na kama kuna mabadiliko ya rangi au uvimbe. Taarifa hizi humsaidia mtoa huduma kutofautisha kusimama kwa kawaida na hali ya kitabibu.


Mzazi pia anapaswa kumweleza mtoa huduma kama mtoto ana ugonjwa wa selimundu, ugonjwa mwingine wa damu, amepata jeraha katika eneo la nyonga au uume, au ameanza kutumia dawa mpya. Taarifa hizi zinaweza kusaidia kutafuta chanzo cha kusimama kwa muda mrefu.


Muhimu zaidi, mzazi asijaribu kubana uume, kuuchoma, kutumia dawa za mtu mwingine au kutumia dawa za kienyeji ili kuumaliza kusimama. Kusimama kwa muda mrefu, hasa kunakoambatana na maumivu, kunaweza kuhitaji matibabu ya haraka ili kulinda tishu za uume na kupunguza hatari ya madhara ya baadaye.


Maelezo haya ni ya kielimu tu, ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma makala hii.

Ikiwa unataka ushauri zaidi kutoka ULY CLINIC, wasilisha swali lako kwa kubofya mawasiliano yetu

Imeandikwa,

1 Oktoba 2026, 14:43:54

​

  1. Donaldson JF, Rees RW, Steinbrecher HA. Priapism in children: a comprehensive review and clinical guideline. J Pediatr Urol. 2014;10(1):11-24. doi:10.1016/j.jpurol.2013.07.024. PubMed – PMID 24135215

  2. Jesus LE, Dekermacher S. Priapism in children: review of pathophysiology and treatment. J Pediatr (Rio J). 2009;85(3):194-200. doi:10.2223/JPED.1884. PubMed – PMID 19455267

  3. European Association of Urology. EAU Guidelines on Paediatric Urology: Emergencies in Paediatric Urology – Priapism. Arnhem: EAU; 2026. EAU Guidelines – Paediatric Urology

  4. European Association of Urology. EAU Guidelines on Sexual and Reproductive Health: Priapism. Arnhem: EAU; 2026. EAU Guidelines – Priapism

  5. Broderick GA, Kadioglu A, Bivalacqua TJ, Ghanem H, Nehra A, Shamloul R. Priapism: pathogenesis, epidemiology, and management. J Sex Med. 2010;7(1 Pt 2):476-500. doi:10.1111/j.1743-6109.2009.01625.x. PubMed search – Broderick et al.

bottom of page