Mwandishi:
ULY CLINIC
Mhariri:
ULY CLINIC
Imeboreshwa:
27 Novemba 2026, 07:28:36

Mbinu za kufanya mtoto anywe dawa
Watoto wengi hukataa dawa kwa sababu ya ladha au hofu. Mbinu zinazosaidia ni kuigiza unakunywa, kwa sababu watoto huiga, kutumia bomba la kupimia dawa na kuweka dawa kidogo kidogo ndani ya shavu, si nyuma ya koo, kumpa kitu kitamu au baridi baada ya dawa, kumsifu, na kwa mtoto mkubwa kumweleza kwa nini anahitaji dawa. Dawa nyingine zinaweza kuchanganywa na kijiko kimoja au viwili vya chakula laini, kama mfamasia ameruhusu.
Inapokuja suala la kumpa mtoto dawa, wazazi wengi huumiza vichwa. Hata kama dawa ni tamu, mara mtoto anapotambua kuwa anachopewa ni dawa huanza kulia, na ukifanikiwa kumpa hujitapisha, kwa sababu mwili wake umeona alichopewa si rafiki. Hii ni moja ya njia za mtoto kuhakikisha kuwa anachokula kipo salama. Makala hii inaeleza mbinu za kumsaidia mtoto anywe dawa kwa usalama, namna sahihi ya kupima dozi, mambo ya kuepuka, na nini cha kufanya akitapika dawa.
Je, unatumia mbinu gani kufanya mtoto anywe dawa?
Kama mzazi au mlezi wa mtoto mdogo, unapaswa kujifunza mambo mengi kwa mtoto ambayo yatakusaidia ufanikiwe kumnywesha dawa pasipo kukataa. Mara nyingi watoto hujifunza mambo mengi kutoka kwa wazazi au watu wanaomzunguka na kufanya uchunguzi na kujaribu kama wanaweza kufanya kile wanachokiona.
Mfano endapo mtoto chini ya mwaka mmoja ataona unakula chakula, hata kama ni kikali, au kichungu, naye atapenda aonje na kuendelea kula vile vile kwa sababu mzazi unafanya hivyo. Hivyo hivyo unaweza kutumia saikolojia hii kumfanya mtoto anywe au ale dawa au chakula. Zifuatazo ni baadhi ya njia unazoweza kutumia:
Kuigiza unatumia dawa hiyo
Kutumia chombo tofauti cha kumnyweshea dawa
Kuchanganya dawa na chakula
Kubadilisha njia ya kumpa dawa
Kuigiza unatumia kile unachompa
Njia hii humfanya mtoto aone anachopewa ni kitu kizuri na salama. Unachopaswa kufanya ni kumrubuni kama unakunywa kwanza na kumpa naye atumie.
Kutumia chombo tofauti cha kumnyweshea dawa

Njia hii hutumiwa sana na huwa na matokeo mazuri. Mambo ya kuzingatia kwenye njia hii ni kubadili chombo ulichozoea kukitumia wakati unampa dawa siku za nyuma, mfano badala ya kutumia kifuniko cha dawa au kijiko, tumia chuchu ya maziwa au kiziba mdomo kinachoruhusu kuweka dawa au chombo chochote ambacho hajazoea kukitumia kwa dawa. Hakikisha unaweka dawa kwenye chombo hicho mbali naye ili asione unachokifanya. Unaweza pia kutumia boksi tupu la juisi, na kadhalika ili kumfanya anywe dawa.
Bomba la kupimia dawa
Bomba la plastiki lisilo na sindano ndilo chombo bora kwa watoto wadogo. Weka ncha yake pembeni ya mdomo, ndani ya shavu, na sukuma dawa kidogo kidogo huku ukimpa muda wa kumeza. Usimwagie dawa nyingi nyuma ya koo, kwa sababu huweza kumsakama na kuingia kwenye njia ya hewa.
Kuchanganya dawa na chakula

Kuna baadhi ya dawa ambazo zinaweza kuchanganywa na chakula hivyo kumfanya mtoto atumie dawa pasipo yeye kufahamu.
Kwa mtoto anapenda sharubati au juisi, unaweza kutumia kopo la juisi ukalifungua mbele yake na kumpa anywe. Hakikisha unaweka dawa kwenye kopo la juisi kisha kulifunga mbali na upeo wa macho yake kabla ya kulifungua mbele yake na kumpa. Na kama unataka kumpa juisi halisi ya matunda, tia dawa kwanza kwenye bilauri mbali na upeo wa macho yake kisha unapokuwa kwenye upeo wake wa macho mimina juisi kidogo akiwa anaona na kumpa na akinywa unaweza muongezea nyingine. Ili kufanya njia hii iwe na mafanikio mimina juisi kwenye glasi yako pia ili kumsindikiza wakati naye anakunywa glasi yake yenye dawa bila kufahamu.
Mambo ya kuzingatia ni kuhakikisha kuwa kiwango cha chakula unachowekewa akimalize ili atumie dozi ya dawa anayotakiwa kutumia kwa wakati huo.
Pia unapaswa kufahamu kuwa baadhi ya dawa huwa hazitumiki na chakula au chakula aina fulani tu, hivyo kabla ya kutumia njia hii soma masharti ya dawa husika kama inaruhusiwa kutumika na chakula au la ili kuepuka kupunguza uwezo wa dawa kufanya kazi au kutengeneza mchanganyiko ambao si salama kwa mtoto.

Muhimu: changanya dawa na kiasi kidogo tu, kijiko kimoja au viwili, cha chakula laini au juisi, si glasi nzima wala mlo mzima. Mtoto asipomaliza, hapati dozi kamili. Uliza mfamasia kama dawa hiyo inaruhusiwa kuchanganywa na chakula, na kama inaweza kusagwa au kufunguliwa.
Kuhusu kubadilisha njia ya kutoa dawa
Dawa ya kumeza haipaswi kuwekwa kwenye njia ya haja kubwa. Dawa za kumeza zimetengenezwa kufyonzwa tumboni, na kuziweka puruni huweza kufanya zisifanye kazi au kuchubua. Baadhi ya dawa, kama dawa ya homa na maumivu, zipo katika umbo maalumu la kuwekwa puruni, kwa mtoto asiyeweza kumeza au anayetapika. Hizo hutumika tu zikiandikwa na mtoa huduma, kwa dozi aliyoelekeza.
Kwa mtoto anayependa kunyonya vidole, baada ya kunawa mikono kwa sabuni na maji safi, unaweza kuchovya kidole kwenye dawa na kumpa alambe, taratibu hadi dawa yote iishe. Njia hii hufaa kwa kiasi kidogo cha dawa.
Kumbuka
Unashauriwa kuwasiliana na daktari wako kabla ya kumpa mtoto dawa yoyote ile kwa usalama wake. Mtaalamu wa afya anaweza kukusaidia kumpa mtoto dozi kamili kulingana na uzito na umri wake.
Unapaswa kupima dozi ya dawa kwa kutumia chombo kile kile ambacho umepewa na mtaalamu wa afya ili kuhakikisha kuwa anapata dozi sahihi.
Katika kutumia njia zote hizi, haupaswi kuwa na haraka ya kumpa dawa, mpe taratibu ili isiwe ugomvi na kuona anachopewa ni kibaya.
Mambo mengine ya kuzingatia
Wasiliana na daktari kabla ya kuvunja au kusaga dawa au kuchanganya na chakula kama vile vyakula vya wanyama wa baharini, barafu, nyama, mboga za majani na kadhalika.
Changanya dawa na chakula kidogo ili kuondoa ladha ya dawa na kuifanya iwe na ladha nzuri. Hii husaidia kuficha ladha ya dawa kwa mtoto, kuchanganya na kiasi kidogo cha kitu kitamu pia huweza kusaidia.
Baadhi ya dawa zinaweza kuongezewa kiasi kidogo cha chakula, sharubati au maji. Changanya kwa kiasi kidogo kama kijiko kimoja au viwili vya chakula au sharubati au maji yaliyotiwa sukari.
Kama mtoto hapendi ladha ya dawa, mpatie kitu kitamu kabla ya kumpa ili kupoteza ladha mbaya, pipi huzubaza tezi za ladha za ulimi na hivyo kufanya asihisi ladha ya dawa.
Kama mtoto ni mkubwa, mweleze umuhimu wa kunywa dawa ili aelewe kwanini unampa na kwa ajili ya nini. Mfano dawa hii itasaidia kuondoa maumivu yako ya tumbo.
Ikiwezekana chagua namna gani utampa dawa mfano kwa kumpa mwenyewe ashike kijiko, sindano au kikombe kunywa badala ya kumlazimisha.
Mpongeze mtoto mkubwa kama akiweza kumeza dawa kwa maneno au hata kumpa zawadi kama stika, kumruhusu akacheze na kadhalika
Usimpatie dawa mara baada ya kumwadhibu mtoto. Huweza kufikiria dawa ni sehemu ya adhabu
Usimtishie mtoto au kumpiga kama asipokunywa dawa.
Mpatie maji baada ya kunywa dawa.
Usimwambie mtoto kuwa dawa ni pipi au juisi. Akiamini hivyo, anaweza kuitafuta na kunywa nyingi akiwa peke yake, na kupata sumu.
Kupima dozi kwa usahihi
Tumia bomba la kupimia au kikombe kilichokuja na dawa, si kijiko cha jikoni.
Soma kiasi kwa mililita kama ulivyoandikiwa, na uliza kama huelewi.
Usiongeze wala kupunguza dozi bila ushauri.
Andika muda wa kila dozi ili usirudie au kusahau.
Maliza dawa zote za kuua bakteria hata kama mtoto amepata nafuu.
Mtoto akitapika dawa
Kama mtoto ametapika ndani ya dakika 15 hadi 30 baada ya kunywa dawa, na unaona dawa imetoka, uliza mtoa huduma au mfamasia kama arudie dozi. Usirudie dozi mwenyewe kwa dawa kama za malaria, degedege au moyo bila ushauri. Kama anatapika kila dawa au kila kitu, mpeleke kituo cha afya.
Usimlazimishe kwa nguvu
Usimbane pua, usimwagie dawa akiwa amelala chali analia, wala kumpiga. Njia hizi huongeza hatari ya dawa kuingia kwenye njia ya hewa, na humfanya aogope dawa zaidi. Mkalishe wima au nusu wima, mshike kwa upole, na mpe muda.
Dalili za hatari
Mpeleke mtoto kituo cha afya mara moja kama hawezi kumeza kabisa, anatapika kila kitu, amelegea, ana degedege, anapumua kwa shida, au amevimba uso au midomo baada ya dawa. Soma mtoto akiwa na homa.
Hitimisho
Kumpa mtoto dawa huwa rahisi zaidi kwa subira na mbinu sahihi: kuigiza unakunywa, kutumia bomba la kupimia na kuweka dawa ndani ya shavu, kuchanganya na kiasi kidogo tu cha chakula kama inaruhusiwa, kumsifu, na kumweleza mtoto mkubwa. Pima dozi kwa chombo sahihi, usiweke dawa ya kumeza puruni, usimlazimishe kwa nguvu, na uliza mtoa huduma kama mtoto ametapika dawa au anakataa kabisa.
Maswali yanayoulizwa mara kwa mara
1. Kwa nini mtoto hutapika dawa?
Mara nyingi kwa sababu ya ladha chungu, harufu, kulazimishwa, au dawa kuingia nyuma ya koo kwa wingi. Kumpa kidogo kidogo ndani ya shavu, akiwa amekaa wima, na kumpa kitu kitamu au baridi baada ya dawa hupunguza kutapika.
2. Naweza kuchanganya dawa na maziwa ya chupa?
Haishauriwi kuchanganya na chupa nzima ya maziwa, kwa sababu mtoto asipomaliza hapati dawa yote, na baadhi ya dawa haziendani na maziwa. Kama mfamasia ameruhusu, changanya na kiasi kidogo tu cha maziwa au chakula laini.
3. Naweza kusaga kidonge na kumpa mtoto?
Baadhi ya vidonge vinaweza kusagwa, lakini vingine haviruhusiwi, hasa vyenye ganda maalumu au vinavyoachia dawa taratibu. Uliza mfamasia kwanza. Mara nyingi dawa hiyohiyo ipo kama sharubati kwa watoto.
4. Nitumie kijiko cha chai kupima dawa?
Usitumie kijiko cha jikoni, kwa sababu ukubwa wake hutofautiana na huleta dozi isiyo sahihi. Tumia bomba la kupimia au kikombe kilichokuja na dawa, ukisoma kiasi kwa mililita kama ulivyoandikiwa.
5. Mtoto mkubwa anakataa kabisa dawa. Nifanye nini?
Mweleze kwa lugha rahisi dawa inamsaidiaje, mpe uchaguzi kama kunywa kwa kikombe au bomba, mruhusu ashike mwenyewe, na msifu akimaliza. Kama bado anakataa, mwambie mtoa huduma; anaweza kuchagua dawa yenye ladha nzuri au umbo jingine.
6. Ni salama kumpa mtoto pipi baada ya dawa?
Kitu kitamu kidogo baada ya dawa kinaweza kuondoa ladha mbaya, lakini usiite dawa pipi. Piga mswaki baada ya dawa tamu za usiku ili kulinda meno, na hifadhi dawa juu mahali mtoto hawezi kufikia.
Maelezo haya ni ya kielimu tu, ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kiafya baada ya kusoma makala hii.
Ikiwa unataka ushauri zaidi kutoka ULY CLINIC, wasilisha swali lako kwa kubofya mawasiliano yetu
Imeandikwa,
27 Novemba 2026, 07:24:13
Rejea za mada hii:
Yin HS, et al. Unit of measurement used and parent medication dosing errors. Pediatrics. 2014;134(2):e354–61.
World Health Organization. Pocket book of hospital care for children. 2nd ed. Geneva: WHO; 2013.
Mennella JA, Spector AC, Reed DR, Coldwell SE. The bad taste of medicines: overview of basic research on bitter taste. Clin Ther. 2013;35(8):1225–46.

