top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

ULY CLINIC

ULY CLINIC

20 Agosti 2026, 05:09:52

shahawa-zenye-damu-ulyclinic-compressor.
Akalazia: Dalili, Visababishi, Vipimo na Matibabu

Akalazia: Dalili, Visababishi, Vipimo na Matibabu

Akalazia (Achalasia): Tatizo la umio linalosababisha kushindwa kumeza chakula na vinywaji

Muhtasari wa makala: Akalazia ni ugonjwa nadra wa mfumo wa chakula unaotokea pale ambapo misuli na mishipa ya fahamu ya umio inaposhindwa kufanya kazi vizuri. Hali hii husababisha chakula na vinywaji kushindwa kupita kutoka kwenye umio kwenda tumboni, na mgonjwa kuhisi kama chakula kimekwama kifuani. Ingawa akalazia haiwezi kuponywa kabisa kwa kurejesha kazi ya mishipa iliyoharibika, matibabu mbalimbali yanaweza kusaidia kupunguza dalili, kuboresha uwezo wa kumeza na kuzuia madhara ya muda mrefu.

Akalazia ni nini?

Akalazia ni ugonjwa unaoathiri umio, ambao ni mrija unaosafirisha chakula kutoka mdomoni kwenda tumboni.

Kwa kawaida, tunapomeza chakula:

  1. Misuli ya umio husukuma chakula kwenda chini kupitia mjongeo maalumu unaoitwa peristalisisi

  2. Kifaa cha misuli kinachoitwa koki ya chini ya umio hulegea na kufunguka ili chakula kiingie tumboni.

  3. Baada ya chakula kupita, koki hii hufunga ili kuzuia tindikali ya tumboni kurudi kwenye umio.


Kwa mtu mwenye akalazia, mfumo huu huvurugika. Misuli ya umio hushindwa kusukuma chakula vizuri na koki ya chini ya umio hushindwa kulegea ipasavyo.


Matokeo yake ni kwamba chakula na vinywaji hukwama kwenye umio na kusababisha dalili mbalimbali.


Akalazia hutokea kwa watu wangapi?

Akalazia ni ugonjwa nadra sana. Inakadiriwa kutokea kwa takribani:


Mtu 1 kati ya watu 100,000 kila mwaka.

Tatizo hili linaweza kumpata mtu wa umri wowote, lakini mara nyingi huonekana zaidi kwa watu wenye umri kati ya:


Miaka 25 hadi 60.

Huathiri wanaume na wanawake kwa kiwango kinachokaribiana.


Dalili za akalazia

Dalili za akalazia huanza taratibu na zinaweza kuchukua miaka kabla ya kutambuliwa. Watu wengi huanza kuona shida ndogo ya kumeza lakini huizoea mpaka tatizo linapokuwa kubwa.


1. Kushindwa kumeza chakula (Disfagia)

Hii ndiyo dalili kuu ya akalazia.

Mgonjwa anaweza kuhisi:

  • Chakula kimekwama kifuani baada ya kumeza.

  • Maji au vinywaji havishuki vizuri.

  • Lazima anywe maji mengi ili kusaidia chakula kushuka.

  • Lazima abadili mkao wa mwili ili chakula kipite.


Baadhi ya wagonjwa hujaribu:

  • Kurusha mabega nyuma.

  • Kunyoosha shingo.

  • Kutembea baada ya kula.

  • Kunywa maji mengi.


Njia hizi zinaweza kusaidia kwa muda, lakini haziondoi tatizo. Tofauti na magonjwa mengi ya kuziba njia ya chakula, akalazia mara nyingi husababisha shida ya kumeza vyakula vigumu na vinywaji kwa pamoja.


2. Kurudisha chakula mdomoni(kucheua)

Chakula kilichokwama kwenye umio kinaweza kurudi mdomoni bila kutapika.


Mgonjwa anaweza:

  • Kuamka usiku na kukuta chakula kimerudi mdomoni.

  • Kukohoa baada ya kulala.

  • Kuhisi ladha ya chakula kilicholiwa muda uliopita.


Hali hii inaweza kusababisha chakula kuingia kwenye njia ya hewa na kuongeza hatari ya:

  • Maambukizi ya mapafu (Nimonia ya kupaliwa).

  • Kikohozi cha muda mrefu.


3. Maumivu ya kifua

Baadhi ya wagonjwa hupata:

  • Maumivu katikati ya kifua.

  • Hisia ya kubanwa kifuani.

  • Maumivu yanayofanana na matatizo ya moyo.


Maumivu haya hutokana na:

  • Misuli ya umio kujikaza kupita kiasi.

  • Chakula kujikusanya ndani ya umio.


Kwa sababu yanaweza kufanana na maumivu ya moyo, ni muhimu kufanyiwa uchunguzi sahihi.


4. Kiungulia

Baadhi ya wagonjwa hupata hisia ya:

  • Moto kifuani.

  • Kuwaka kooni.

  • Ladha chungu mdomoni.

Ingawa dalili hizi zinaweza kufanana na ugonjwa wa kucheua tindikali (GERD), katika akalazia mara nyingi husababishwa na chakula kukaa muda mrefu kwenye umio.


5. Kupungua uzito

Kutokana na:

  • Kushindwa kula vizuri.

  • Kuogopa kula kwa sababu chakula kinakwamia.

  • Mwili kutopata virutubisho vya kutosha.

Kupungua uzito bila sababu maalumu ni dalili inayohitaji uchunguzi.


6. Kuhisi uvimbe au kitu kimekwama kooni

Baadhi ya wagonjwa huhisi:

  • Kuna kitu kimekaa kooni.

  • Koo limejaa.

  • Kuna presha kwenye kifua au koo.


7. Kwikwi na kikohozi

Chakula au maji yanaporudi juu yanaweza kuchochea:

  • Kikohozi.

  • Kwikwi.

  • Kukereketa koo.


Visababishi vya Akalazia

Chanzo halisi cha akalazia bado hakijulikani.

Hata hivyo, wataalamu wanaamini tatizo hutokana na kuharibika kwa seli za mishipa ya fahamu inayodhibiti misuli ya umio.

Mishipa hii inapoharibika husababisha matatizo mawili makubwa:


1. Kukosekana kwa mjongeo wa kawaida wa umio

Kwa kawaida, umio husukuma chakula kuelekea tumboni kwa mawimbi ya misuli.

Kwa mtu mwenye akalazia:

  • Misuli ya umio haikandamizi chakula vizuri.

  • Chakula hubaki ndani ya umio.

  • Umio huanza kutanuka kadri muda unavyokwenda.


2. Koki ya chini ya umio kushindwa kulegea

Koki ya chini ya umio huwa haifunguki vizuri wakati wa kumeza.

Hii husababisha:

  • Chakula kushindwa kuingia tumboni.

  • Chakula kukusanyika sehemu ya chini ya umio.

  • Kuongezeka kwa ukubwa wa umio.


Kwa nini mishipa hii huharibika?

Sababu bado haijathibitishwa, lakini nadharia mbalimbali zimependekeza:


1. Mwitikio wa kinga ya mwili

Mwili unaweza kushambulia kimakosa seli zake za mishipa ya fahamu.


2. Maambukizi ya virusi

Baadhi ya tafiti zimependekeza kuwa virusi vinaweza kuchochea uharibifu wa mishipa kwa watu wenye vinasaba vinavyowafanya kuwa katika hatari.


3. Sababu za kijenetiki

Ingawa si ugonjwa wa kurithi kwa kawaida, baadhi ya watu wanaweza kuwa na uwezekano mkubwa kutokana na mabadiliko fulani ya vinasaba.


Vipimo na Uchunguzi wa akalazia

Kwa sababu dalili za akalazia zinaweza kufanana na magonjwa mengine ya mfumo wa chakula kama saratani ya umio, kucheua tindikali (GERD), au kuziba kwa umio, vipimo maalumu vinahitajika ili kuthibitisha tatizo.

Daktari huanza kwa kuuliza kuhusu dalili, muda ambao tatizo limekuwepo, aina ya chakula kinachosababisha shida, kupungua uzito, na historia nyingine za kiafya. Vipimo muhimu vinavyotumika kutambua akalazia ni:


1. Kipimo cha kupima mjongeo wa umio (manometri ya umio)

Hiki ndicho kipimo muhimu zaidi na kinachotumika kuthibitisha akalazia.

Katika kipimo hiki:

  • Mrija mwembamba wenye vihisi maalumu hupitishwa kupitia puani hadi kwenye umio.

  • Mrija huo hupima shinikizo na jinsi misuli ya umio inavyofanya kazi wakati wa kumeza.

  • Daktari huangalia kama misuli ya umio inasukuma chakula vizuri na kama koki ya chini ya umio inalegea.


Kwa mtu mwenye akalazia, kipimo kinaweza kuonyesha:

  • Kupungua au kutokuwepo kwa mjongeo wa kawaida wa umio (peristalsis).

  • Koki ya chini ya umio kushindwa kulegea vizuri wakati wa kumeza.

  • Kuongezeka kwa shinikizo kwenye sehemu ya chini ya umio.

Kwa sasa, aina mbalimbali za akalazia hutambuliwa kwa kutumia High-resolution manometry (HRM) ambayo hutoa picha sahihi zaidi ya namna umio unavyofanya kazi.


2. Kipimo cha kumeza bariamu

Hiki ni kipimo kinachotumia aina maalumu ya kimiminika kinachoitwa barium ambacho huonekana vizuri kwenye picha ya X-ray.

Katika kipimo hiki:

  • Mgonjwa hunywa kimiminika chenye barium.

  • Picha za X-ray huchukuliwa wakati barium ikishuka kwenye umio.

Kwa mtu mwenye akalazia, picha inaweza kuonyesha:

  • Umio kuwa umetanuka.

  • Chakula au kimiminika kukaa kwenye umio kwa muda mrefu.

  • Sehemu ya chini ya umio kuwa nyembamba kama ncha ya kalamu, hali inayojulikana kama "bird-beak appearance".

Kipimo hiki husaidia kuona ukubwa wa tatizo na mabadiliko yaliyotokea kwenye umio.


3. Endoskopi (Kipimo cha kamera kwenye umio)

Endoscopy ni kipimo kinachotumia kamera ndogo iliyopo kwenye mrija laini unaopitishwa kupitia mdomoni hadi kwenye umio na tumbo.

Kipimo hiki husaidia:

  • Kuangalia ndani ya umio moja kwa moja.

  • Kuona kama kuna kuziba.

  • Kuchukua sampuli za seli (biopsy) kama inahitajika.


Endoskopi ni muhimu kwa sababu baadhi ya magonjwa yanaweza kufanana na akalazia, hasa:

  • Saratani ya sehemu ya chini ya umio.

  • Saratani ya juu ya tumbo.

  • Vidonda au makovu yanayozuia chakula kupita.

Kwa kawaida mgonjwa hupewa dawa za kumsaidia kutulia au usingizi mwepesi kabla ya kipimo.


4. X-ray ya kifua

X-ray ya kifua si kipimo kikuu cha kuthibitisha akalazia, lakini wakati mwingine inaweza kutoa dalili zinazoashiria tatizo.

Inaweza kuonyesha:

  • Umio uliopanuka.

  • Kuwepo kwa chakula au hewa ndani ya umio.

  • Kupungua kwa hewa tumboni.

Hata hivyo, X-ray pekee haiwezi kuthibitisha akalazia.


Aina za Akalazia

Kwa kutumia kipimo cha high-resolution manometry, akalazia hugawanywa katika aina kuu tatu:


Akalazia aina ya kwanza

Hii ni aina ambayo:

  • Umio umepoteza kabisa uwezo wa kusukuma chakula.

  • Misuli ya umio huwa dhaifu sana.


Akalazia aina ya pili

Hii ndiyo aina inayopatikana mara nyingi zaidi.

Hutokea ambapo:

  • Umio hauwezi kusukuma chakula kawaida.

  • Kuna shinikizo ndani ya umio wakati wa kumeza.

Wagonjwa wenye aina hii mara nyingi hujibu vizuri zaidi matibabu.


Akalazia aina ya tatu

Hii huitwa pia spastic achalasia.

Katika aina hii:

  • Misuli ya umio hukaza kwa nguvu zisizo za kawaida.

  • Wagonjwa wanaweza kupata maumivu makali ya kifua.

  • Mara nyingi huhitaji matibabu maalumu zaidi.


Tofauti kati ya Akalazia na Ugonjwa wa kucheua tindikali (GERD)

Watu wengi huchanganya akalazia na kiungulia au GERD kwa sababu baadhi ya dalili zinafanana.

Akalazia

GERD

Chakula hukwama kifuani

Asidi hupanda kutoka tumboni(kucheua)

Tatizo kubwa ni kushindwa kumeza

Tatizo kubwa ni kiungulia

Umio hushindwa kusukuma chakula

Koki ya chini ya umio huwa dhaifu

Mara nyingi chakula hurudi mdomoni bila kutapika

Mara nyingi kuna ladha ya tindikali

Huhitaji vipimo maalumu kama manometri

Mara nyingi hugunduliwa kwa dalili


Matibabu ya Akalazia

Lengo kuu la matibabu si kuponya uharibifu wa mishipa ya fahamu, bali ni:

  • Kupunguza kizuizi kwenye sehemu ya chini ya umio.

  • Kuruhusu chakula kuingia tumboni.

  • Kuboresha uwezo wa mgonjwa kula.

  • Kuzuia matatizo ya muda mrefu.


Chaguo la matibabu hutegemea:

  • Umri wa mgonjwa.

  • Aina ya akalazia.

  • Ukubwa wa kutanuka kwa umio.

  • Afya kwa ujumla.


1. Dawa

Dawa zinaweza kutumika kwa baadhi ya wagonjwa, hasa wale ambao hawawezi kufanyiwa matibabu ya kuingilia moja kwa moja.

Dawa zinazotumika zaidi ni:


Nitrates

Mfano:

  • Isosorbide dinitrate.


Calcium channel blockers

Mfano:

  • Nifedipine.

Dawa hizi husaidia:

  • Kulegeza misuli ya koki ya chini ya umio.

  • Kupunguza shinikizo kwenye eneo linalozuia chakula.

Kwa kawaida hutumika kabla ya kula.


Changamoto za dawa

Ingawa zinaweza kusaidia, zina mapungufu:

  • Athari zake hupungua kadri muda unavyokwenda.

  • Hazifanyi kazi kwa wagonjwa wengi kwa muda mrefu.

  • Huenda zikasababisha madhara kama:

    • Maumivu ya kichwa.

    • Kizunguzungu.

    • Kushuka kwa shinikizo la damu.

Kwa sababu hiyo, dawa mara nyingi si tiba ya kwanza kwa wagonjwa wengi.


2. Kutanua umio kwa puto

Hii ni moja ya tiba zinazotumika sana.

Katika utaratibu huu:

  • Puto maalumu huwekwa kwenye sehemu ya chini ya umio.

  • Puto hupulizwa ili kulegeza na kuvunja baadhi ya nyuzi za misuli ya koki.

  • Chakula hupata nafasi ya kupita tumboni.


Faida:

  • Hupunguza sana shida ya kumeza.

  • Haihitaji upasuaji mkubwa.


Changamoto:

  • Baadhi ya wagonjwa huhitaji kurudia matibabu.

  • Kuna hatari ndogo ya kupasuka kwa umio.

  • Baadhi ya wagonjwa wanaweza kupata asidi kurudi juu baada ya matibabu.


3. Upasuaji wa Heller mayotomi

Hii ni tiba ambayo imekuwa ikitumika kwa muda mrefu.

Katika upasuaji huu:

  • Daktari hukata sehemu ya misuli iliyokaza kwenye koki ya chini ya umio.

  • Hii husaidia chakula kupita tumboni kwa urahisi.

Mara nyingi hufanyika kwa njia ya:


Upasuaji wa kutumia Laparoscopic Heller myotomy

ambayo hutumia mikato midogo tumboni.

Faida:

  • Hutoa nafuu kubwa kwa wagonjwa wengi.

  • Athari zinaweza kudumu kwa miaka mingi.

Baada ya upasuaji, mara nyingi hufanyika utaratibu wa kuzuia asidi kurudi juu unaoitwa fundoplication, kwa sababu kulegeza koki kunaweza kuongeza uwezekano wa GERD.


4. POEM (Upasuaji misuli ya umio kupitia kinywa kwa kutumia kifaa chenye kamera)

Hii ni tiba mpya zaidi ya akalazia, katika upasuaji huu wa POEM:

  • Kifaa chenye kamera huingizwa kwenda kweney umio kupitia mdomoni.

  • Daktari hutengeneza njia ndani ya ukuta wa umio ili chakula kiweze kupita.

  • Misuli iliyokaza hukatwa kutoka ndani bila kufungua tumbo kwa upasuaji mkubwa.


Faida:

  • Hakuna mikato ya nje.

  • Kupona huwa haraka.

  • Hufanya kazi vizuri hasa kwa aina ya tatu ya akalazia yenye misuli inayokaza sana.


Changamoto:

  • Inaweza kuongeza hatari ya asidi kurudi juu baada ya matibabu.

  • Inahitaji daktari mwenye uzoefu maalumu.


Madhara ya akalazia yasipotibiwa

Ingawa akalazia si ugonjwa unaoua kwa haraka, kutotibiwa kunaweza kusababisha matatizo mbalimbali kutokana na chakula na vinywaji kukaa muda mrefu kwenye umio. Kadri muda unavyokwenda, umio unaweza kuendelea kutanuka na kupoteza uwezo wake wa kufanya kazi vizuri. Madhara yanayoweza kutokea ni pamoja na:


1. Kutokana na chakula kukwama kwenye umio

Chakula kinapokaa muda mrefu kwenye umio kinaweza kusababisha:

  • Hisia ya kujaa kifuani.

  • Maumivu ya kifua.

  • Harufu mbaya ya mdomo.

  • Kurudisha chakula mdomoni.

Baadhi ya wagonjwa wanaweza kurudisha chakula walichokula hata baada ya masaa kadhaa au wakati wa kulala.


2. Maambukizi ya mapafu (Nimonia ya kupaliwa)

Hili ni tatizo muhimu hasa kwa wagonjwa wanaorudisha chakula usiku. Chakula au maji yanaporudi juu yanaweza kuingia kwenye njia ya hewa badala ya kurudi tumboni.

Hii inaweza kusababisha:

  • Kikohozi cha muda mrefu.

  • Homa.

  • Maumivu ya kifua.

  • Kupumua kwa shida.

  • Maambukizi ya mapafu.

Hatari hii huwa kubwa zaidi kwa wagonjwa wenye umio uliotanuka sana.


3. Kupungua uzito na utapiamlo

Kwa sababu mgonjwa hupata shida kula, anaweza:

  • Kupunguza kiasi cha chakula.

  • Kuepuka vyakula fulani.

  • Kuogopa kula mbele ya watu.


Matokeo yake yanaweza kuwa:

  • Kupungua uzito.

  • Udhaifu wa mwili.

  • Upungufu wa virutubisho muhimu.


4. Umio kutanuka sana (Megaesofagasi)

Akalazia ikikaa muda mrefu bila matibabu inaweza kusababisha:

  • Umio kupanuka sana.

  • Misuli ya umio kudhoofika zaidi.

  • Chakula kukaa kwa muda mrefu zaidi.

Katika hatua hii, matibabu yanaweza kuwa magumu zaidi kwa sababu umio huwa umepoteza uwezo mkubwa wa kusukuma chakula.


5. Saratani ya umio

Wagonjwa wenye akalazia wana hatari kubwa zaidi ya kupata mabadiliko ya saratani kwenye seli za umio kuliko watu wasio na tatizo hili. Sababu inayodhaniwa ni:

  • Chakula kukaa muda mrefu kwenye umio.

  • Kuwashwa kwa muda mrefu kwa ukuta wa umio.

  • Mabadiliko ya seli kutokana na uchochezi wa muda mrefu.


Aina ya saratani inayohusishwa zaidi ni Saratani ya seli Squamous za umio. Kwa sababu hii, baadhi ya wataalamu hupendekeza ufuatiliaji wa wagonjwa wenye akalazia ya muda mrefu, hasa wale wenye umio uliopanuka sana.


Ushauri wa maisha kwa mtu mwenye akalazia

Matibabu ya hospitali ndiyo muhimu zaidi, lakini mabadiliko haya yanaweza kusaidia kupunguza dalili:


1. Kula chakula kidogo kidogo

Badala ya kula chakula kingi mara moja:

  • Kula kiasi kidogo lakini mara nyingi.

  • Tafuna chakula vizuri kabla ya kumeza.


2. Kunywa maji wakati wa kula

Maji yanaweza kusaidia chakula kushuka kwa baadhi ya wagonjwa. Hata hivyo, kama maji yenyewe yanakwama, ni muhimu kumuona daktari.


3. Epuka kula kabla ya kulala

Inashauriwa: Kumaliza kula angalau saa 2–3 kabla ya kulala, hii husaidia kupunguza kurudi kwa chakula wakati wa usingizi.


4. Lala ukiwa umeinua kichwa

Kwa wagonjwa wanaorudisha chakula usiku: Kuinua sehemu ya kichwa cha kitanda kunaweza kusaidia kupunguza kurudi kwa chakula.


5. Epuka vyakula vinavyoongeza dalili zako

Hakuna chakula maalumu kinachosababisha akalazia, lakini baadhi ya watu huona dalili zikiongezeka baada ya:

  • Vyakula vigumu sana.

  • Vyakula vikavu bila maji.

  • Kula haraka.


Wakati gani mtu mwenye shida ya kumeza anatakiwa kumuona daktari?

Ni muhimu kutafuta ushauri wa kitabibu ikiwa mtu ana:

  • Kushindwa kumeza chakula kinachozidi kuongezeka.

  • Chakula kukwama mara kwa mara kifuani.

  • Kupungua uzito bila sababu.

  • Kurudisha chakula mara kwa mara.

  • Kikohozi cha muda mrefu hasa usiku.

  • Maumivu ya kifua yanayojirudia wakati wa kula.

Shida ya kumeza si dalili ya kawaida na inahitaji uchunguzi ili kujua chanzo.


Maswali yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu akalazia

1. Je, akalazia ni ugonjwa wa saratani?

Hapana. Akalazia yenyewe si saratani. Ni ugonjwa wa mfumo wa chakula unaosababishwa na kushindwa kufanya kazi kwa mishipa ya fahamu na misuli ya umio.


Hata hivyo, watu wenye akalazia ya muda mrefu wanaweza kuwa na hatari iliyoongezeka ya kupata saratani ya umio kutokana na chakula kukaa muda mrefu kwenye umio na kusababisha mabadiliko ya muda mrefu kwenye seli. Ndiyo maana wagonjwa wengine huhitaji ufuatiliaji wa karibu na daktari.

2. Je, akalazia inaweza kupona kabisa?

Kwa sasa hakuna tiba inayoweza kurudisha mishipa ya fahamu iliyoharibika kwenye umio kuwa kawaida.

Hata hivyo, matibabu yanaweza kupunguza sana dalili na kumwezesha mgonjwa kula vizuri.

Matibabu kama:

  • Kutanua umio kwa puto.

  • Upasuaji wa Heller myotomy.

  • POEM.

yanaweza kutoa nafuu ya muda mrefu kwa wagonjwa wengi.

3. Je, akalazia inaweza kusababisha kifo?

Kwa kawaida akalazia yenyewe si ugonjwa unaosababisha kifo moja kwa moja.

Lakini ikiwa haitatibiwa inaweza kusababisha matatizo makubwa kama:

  • Maambukizi makali ya mapafu kutokana na chakula kuingia kwenye njia ya hewa.

  • Utapiamlo mkubwa.

  • Saratani ya umio kwa baadhi ya wagonjwa.

Kupata uchunguzi na matibabu mapema hupunguza hatari hizi.

4. Kwa nini chakula kinakwama kifuani lakini si kooni?

Tatizo la akalazia hutokea kwenye umio, hasa sehemu ya chini karibu na tumbo. Mtu anaweza kuhisi chakula kimekwama katikati ya kifua kwa sababu eneo hilo ndilo chakula kinaposhindwa kupita.


Tofauti na matatizo ya koo, mara nyingi mtu mwenye akalazia anaweza kuanza kumeza vizuri lakini chakula hukwama baada ya kushuka chini.

5. Je, akalazia inaweza kuchanganywa na ugonjwa wa kawaida wa kiungulia?

Ndiyo. Baadhi ya watu huchanganya akalazia na kucheua tindikali kwa sababu zote zinaweza kusababisha:

  • Hisia ya kuwaka kifuani.

  • Kurudi kwa chakula mdomoni.

  • Maumivu ya kifua.


Lakini akalazia mara nyingi huambatana zaidi na:

  • Kushindwa kumeza chakula.

  • Chakula kukwama.

  • Kurudisha chakula ambacho hakijameng'enywa.

6. Je, akalazia inaweza kurithiwa kutoka kwa wazazi?

Kwa watu wengi, akalazia si ugonjwa wa kurithi. Hata hivyo, kuna baadhi ya hali nadra ambapo mabadiliko ya vinasaba yanaweza kuongeza uwezekano wa kupata ugonjwa huu.

7. Je, mtu mwenye akalazia anaweza kula vyakula vyote?

Watu wengi wanaweza kula vyakula mbalimbali baada ya kupata matibabu.

Kabla ya matibabu, baadhi ya vyakula vinaweza kuwa vigumu kumeza hasa:

  • Nyama ngumu.

  • Vyakula vikavu.

  • Mkate mkavu.

Ni muhimu kutafuna vizuri na kula taratibu.

8. Je, dawa za kiungulia zinaweza kutibu akalazia?

Hapana. Dawa za kupunguza asidi tumboni kama vizuia pumpu protoni (PPI) zinaweza kusaidia kama mgonjwa ana kiungulia kinachosababishwa na asidi, lakini hazitatibu tatizo kuu la akalazia.

Tatizo kuu ni kushindwa kulegea kwa koki ya chini ya umio na kupotea kwa mjongeo wa umio.

9. Je, akalazia inaweza kutokea ghafla?

Mara nyingi hapana. Akalazia kwa kawaida huanza taratibu na dalili huongezeka polepole kwa miezi au miaka. Mwanzo mgonjwa anaweza kuona:

  • Chakula kigumu kama nyama au mkate kinaanza kushuka kwa shida.

  • Anahitaji kunywa maji ili kusaidia chakula kushuka.

  • Anaanza kubadilisha namna ya kula bila kujua kuwa kuna tatizo.


Kadri muda unavyokwenda, shida inaweza kuanza kuhusisha hata vinywaji kama maji.

Kwa sababu dalili huendelea polepole, baadhi ya wagonjwa huchelewa kutafuta matibabu wakidhani ni tatizo la kawaida la chakula.

10. Je, akalazia inaweza kuwapata watoto?

Ndiyo, lakini ni nadra sana. Watoto wanaweza kupata akalazia ingawa mara nyingi ugonjwa huu huonekana zaidi kwa watu wazima. Kwa mtoto, dalili zinaweza kuwa:

  • Kushindwa kula vizuri.

  • Kutapika au kurudisha chakula mara kwa mara.

  • Kupungua uzito au kushindwa kuongeza uzito.

  • Kikohozi cha mara kwa mara.

  • Maambukizi ya mapafu yanayojirudia.

Kwa watoto, tatizo linaweza kuchanganywa na matatizo mengine ya ulaji au mfumo wa chakula, hivyo uchunguzi wa daktari bingwa ni muhimu.

11. Je, akalazia inaweza kumpata mwanamke mjamzito?

Ndiyo, ingawa ni nadra. Mimba inaweza kufanya dalili za akalazia kuonekana zaidi kwa baadhi ya wanawake kutokana na:

  • Mabadiliko ya homoni.

  • Shinikizo la mimba kwenye viungo vya ndani.

  • Mabadiliko ya mfumo wa mmeng'enyo wa chakula.


Changamoto kubwa kwa mjamzito mwenye akalazia ni kuhakikisha:

  • Anapata chakula cha kutosha.

  • Hapunguki uzito.

  • Mtoto anapata virutubisho vinavyohitajika.

Matibabu wakati wa ujauzito hupangwa kwa uangalifu kulingana na ukali wa dalili na umri wa mimba.

12. Je, mtu mwenye akalazia anaweza kuishi maisha ya kawaida?

Ndiyo. Watu wengi wenye akalazia wanaweza kuendelea na maisha ya kawaida baada ya kupata matibabu sahihi. Matibabu yanaweza:

  • Kuboresha uwezo wa kula.

  • Kupunguza kurudi kwa chakula.

  • Kuongeza ubora wa maisha.

Hata hivyo, kwa sababu tatizo la mishipa ya fahamu haliwezi kurekebishwa kabisa, wagonjwa wanahitaji kufuatiliwa kwa muda mrefu.

13. Ni matibabu gani bora zaidi kwa akalazia?

Hakuna tiba moja inayofaa kila mgonjwa.

Uchaguzi wa matibabu hutegemea:

  • Aina ya akalazia.

  • Umri wa mgonjwa.

  • Afya yake kwa ujumla.

  • Uzoefu wa kituo cha matibabu.


Kwa ujumla:

  • Kutanua umio kwa puto

  • Hufaa kwa wagonjwa wengi na inaweza kutoa nafuu nzuri.

  • Upasuaji wa Heller mayotomi

  • Ni tiba yenye mafanikio ya muda mrefu, hasa kwa wagonjwa wanaofaa kufanyiwa upasuaji.


Ni njia ya kisasa yenye mafanikio makubwa, hasa kwa wagonjwa wenye aina ya tatu ya akalazia.

Daktari bingwa wa mfumo wa chakula au daktari bingwa wa upasuaji wa mfumo wa chakula husaidia kuchagua njia bora.

14. Je, baada ya matibabu akalazia inaweza kurudi tena?

Ndiyo, inaweza. Matibabu mengi hulenga kupunguza kizuizi kwenye sehemu ya chini ya umio, lakini hayarudishi mishipa ya fahamu iliyoharibika.

Kwa hiyo baada ya miaka kadhaa baadhi ya wagonjwa wanaweza kuona:

  • Kurudi kwa shida ya kumeza.

  • Chakula kuanza kukwama tena.

  • Kuongezeka kwa dalili.

Mgonjwa anapaswa kurudi hospitali akiona dalili zinarudi.

15. Je, akalazia husababisha tumbo kujaa gesi au kuvimbiwa?

Kwa kawaida akalazia huathiri zaidi umio, si utumbo.

Lakini baadhi ya wagonjwa wanaweza kuhisi:

  • Tumbo kujaa.

  • Usumbufu tumboni.

  • Kushindwa kula kiasi kikubwa cha chakula.

Hii mara nyingi hutokana na kubadilika kwa namna ya kula au chakula kuchelewa kushuka tumboni.

16. Je, mtu mwenye akalazia anaweza kunywa pombe au kahawa?

Hakuna ushahidi kwamba pombe au kahawa husababisha akalazia. Hata hivyo, baadhi ya watu wanaweza kuona dalili zikiongezeka baada ya kutumia:

  • Pombe.

  • Kahawa nyingi.

  • Vinywaji vyenye gesi.


Sababu ni kwamba vitu hivi vinaweza kuongeza usumbufu kwenye mfumo wa chakula au kuchochea kiungulia kwa baadhi ya watu. Mgonjwa anapaswa kutambua vyakula au vinywaji vinavyoongeza dalili zake binafsi.

17. Je, akalazia inaweza kusababisha harufu mbaya ya mdomo?

Ndiyo, inaweza, cakula kinapokaa muda mrefu kwenye umio:

  • Kinaweza kuoza au kuchachuka.

  • Kinaweza kusababisha bakteria kuongezeka.

  • Kinaweza kutoa harufu mbaya.

Harufu hii mara nyingi hupungua baada ya tatizo kutibiwa.

18. Je, mtu mwenye akalazia anaweza kufanya mazoezi?

Ndiyo. Mazoezi kwa ujumla ni salama na yana faida kwa afya, hata hivyo:

  • Epuka kula chakula kingi kabla ya mazoezi.

  • Kama chakula hurudi wakati wa mazoezi, zungumza na daktari.

  • Wagonjwa wenye dalili kali wanapaswa kwanza kutibiwa.

19. Je, akalazia inaweza kuchanganywa na saratani ya umio?

Ndiyo. Baadhi ya dalili zinaweza kufanana, hasa:

  • Kushindwa kumeza.

  • Kupungua uzito.

  • Chakula kukwama.


Ndiyo maana endoskopi ni muhimu kwa baadhi ya wagonjwa ili kuhakikisha hakuna uvimbe au saratani inayozuia chakula kupita.

20. Ni lini mgonjwa mwenye akalazia anatakiwa kwenda hospitali haraka?

Mgonjwa anatakiwa kutafuta msaada wa haraka ikiwa ana:

  • Kushindwa kabisa kumeza hata maji.

  • Kupungua uzito sana.

  • Kutapika damu.

  • Maumivu makali ya kifua.

  • Kupumua kwa shida baada ya kurudisha chakula.

  • Homa na kikohozi kinachoendelea.


Dalili hizi zinaweza kuonyesha tatizo kubwa linalohitaji matibabu ya haraka.


ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii

Imeandikwa:

21 Julai 2026, 08:47:49

Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini

​

[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]

Rejea za mada hii:

  1. Park W, Vaezi MF. Etiology and pathogenesis of achalasia: current understanding. Am J Gastroenterol. 2005;100(6):1404-1414.

  2. Spechler SJ, Castell DO. Classification of oesophageal motility abnormalities. Gut. 2001;49(1):145-151.

  3. Pandolfino JE, Kahrilas PJ. AGA technical review on the clinical use of esophageal manometry. Gastroenterology. 2005;128(1):209-224.

  4. Pandolfino JE, Gawron AJ. Achalasia: a systematic review. JAMA. 2015;313(18):1841-1852.

  5. Vaezi MF, Pandolfino JE, Vela MF. ACG clinical guidelines: diagnosis and management of achalasia. Am J Gastroenterol. 2013;108(8):1238-1249.

  6. Oude Nijhuis RAB, Zaninotto G, Roman S, Boeckxstaens GE, Fockens P, Langendam MW, et al. European guidelines on achalasia: United European Gastroenterology and European Society of Neurogastroenterology and Motility recommendations. United European Gastroenterol J. 2020;8(1):13-33.

  7. Bechara R, Inoue H, et al. Peroral endoscopic myotomy (POEM): current status and future perspectives. Gastrointest Endosc Clin N Am. 2016;26(2):237-247.

  8. Sawas T, Vela MF, Yadlapati R, et al. The course of achalasia one to four decades after initial treatment. Aliment Pharmacol Ther. 2017;45:553-560.

bottom of page