top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

ULY CLINIC

Dkt. Sospeter Mangwella, MD

Dalili za gono kwa mwanaume
shahawa-zenye-damu-ulyclinic-compressor.

21 Desemba 2025, 08:51:40

Dalili za gono kwa mwanaume

Gono ni ugonjwa wa zinaa unaojitokeza sana hasa kwa vijana, ugonjwa huu huambukizwa kwa njia ya ngono na mwenza mwenye maambukizi,  inaweza kuwa ngono ya uume na uke, uume na njia ya haja kubwa au ngono ya mdomo. Mwanume anaweza kuwa na gono na akaonesha dalili au asioneshe dalili yoyote. Endapo ataonesha dalili huwa za wastani na huweza kuchanganywa  na dalili za magonjwa mengine mfano UTI.


Je, ni zipi dalili za gono kwa mwanaume?

Kama ilivyoainishwa hapo awali, mwanaume anaweza kuwa na gono na akaonesha au asioneshe dalili zozote. Endapo ataonesha dalili basi dalili hizo zitaonekana kulingana na sehemu iliyoathirika kama ifuatayo;


Gono inayoathiri via vya uzazi

Huathiri kibofu cha mkojo, mrija wa mkojo wa urethra na korodani (hutokea kwa nadra), huwa na dalili hizi;

  • Kuhisi hali ya kuungua kwa kibofu wakati wa kukojoa

  • Maumivu wakati wa kukojoa

  • Kutokwa na uchafu uumeni ambao unaweza kuwa na rangi nyeupe, njano au kijani

  • Maumivu au kuvimba kwa korodani


Gono inayoathiri njia ya haja kubwa

Hutokea sana kwa wanaume wanaoshiriki ngono kinyume na maumbile na wenza wenye maambukizi, huwa na dalili hizi;

  • Kutokwa na uchafu

  • Maumivu

  • Miwasho

  • Kutoka damu au kupata choo chenye matone ya damu

  • Maumivu wakati wa kujisaidia


Gono inayoathiri kinywa na koo

Huwapata wanaume wanaofanya ngono ya mdomo na wenza wenye maambukizi.

Mara nyingi maambukizi katika sehemu hii hayaambatani na dalili  zozote, hata kama dalili zitaonekana huwa ni vigumu kutofautisha dalili hizo na dalili zingine za magonjwa ya kinywa na koo , na hivyo utambuzi wake huwa mgumu na kuchelewesha matibabu.

Dalili hizi zinaweza kuonekana

  • Maumivu ya koo

  • Kuhisi mikwaruzo kwenye koo

  • Kuhisi koo kukuaka

  • Koo kuwa jekundu

  • Homa

  • Kuvimba kwa mitoki katika shingo


Hitimisho

Gono ni ugonjwa wa zinaa unaoambukizwa kwa njia ya ngono na unaweza kuathiri via vya uzazi, njia ya haja kubwa, au kinywa na koo kwa mwanaume. Dalili zake zinaweza kujitokeza au kutokujitokeza, na mara nyingi hujitokeza kulingana na sehemu iliyoathirika.


Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara

1. Kwa nini baadhi ya wanaume wanaoumwa gono hawana dalili yoyote?

Gono inaweza kubaki bila dalili kwa sababu mwili wa mwanaume unaweza kudhibiti au kuchelewesha kuonesha dalili. Hii inafanya utambuzi kuwa mgumu, na huongeza hatari ya kueneza maambukizi kwa wenza bila kujua.

2. Je, maambukizi ya gono yanaweza kuathiri afya ya mwanaume hata bila dalili?

Ndiyo. Hata pale hakuna dalili, bakteria au virusi vinaweza kusababisha uchochezi wa siri, kupungua kwa uwezo wa kiume, au hatari ya kuambukiza wenza. Utambuzi wa mapema unasaidia kuzuia madhara haya.

3. Ni kwa namna gani gono huenea ndani ya mwili wa mwanaume?

Gono inaweza kuenea kutoka kwenye mrija wa mkojo wa urethra hadi kwenye kibofu cha mkojo, korodani, au hata kwenye njia ya haja kubwa. Maambukizi yanapopanuka bila matibabu yanaweza kusababisha maumivu sugu au kuvimba kwa viungo hivyo.

4. Kwa nini utambuzi wa gono ya kinywa na koo ni changamoto?

Dalili zake ni ndogo au hazionekani wazi na mara nyingi zinafanana na magonjwa mengine ya kinywa kama uvimbe wa matezi koo au homa ya kawaida, hivyo madaktari huweza kuchelewesha utambuzi bila uchunguzi wa maabara.

5. Zipi ni dalili za gono zinazotofautiana kulingana na sehemu ya mwili iliyohusika?

Dalili zinategemea eneo la maambukizi: njia ya mkojo husababisha hisia za kuungua au uchafu, njia ya haja kubwa husababisha maumivu na damu kwenye choo, na kinywa/koo husababisha maumivu ya koo au uvimbe wa tezi koo. Uelewa wa tofauti hizi husaidia kutambua gono mapema.

6. Je, gono inaweza kusababisha matatizo ya kudumu kwa via vya uzazi vya mwanaume?

Ndiyo. Endapo gono haitatibiwa mapema, inaweza kusababisha uvimbekinga sugu au uvimbe wa mrija wa mkojo wa urethra na korodani, jambo linaloweza kupunguza uwezo wa kujamiana au kuzaa.

7. Kwa nini miwasho na damu kwenye njia ya haja kubwa ni ishara muhimu ya uchunguzi?

Hii ni ishara ya maambukizi makali au uvimbe kwenye njia ya haja kubwa(puru), unaoweza kuonyesha gono inayotokana na ngono ya kinyume na maumbile. Kutambua ishara hizi mapema husaidia kuzuia ugonjwa usiene na kuzuia matatizo ya mkojo na utumbo.

8. Ni hatua gani za kinga ambazo mwanaume anaweza kuchukua kuzuia gono?

Kutumia kondomu kila wakati wa ngono, kuepuka ngono na wenza wenye dalili za maambukizi, na kufanya vipimo vya afya mara kwa mara. Kujua hali ya kiafya ya mwenza ni muhimu pia.

9. Gono inaathirije uhusiano wa kijamii na kihisia kwa wanaume?

Maambukizi yasiyotambuliwa mara moja yanaweza kuleta hofu, aibu, au mashaka ya kuanzisha uhusiano wa kimapenzi. Pia, kueneza ugonjwa kwa wenza bila kujua kunaweza kusababisha migongano ya kihisia.

10. Kwa nini uchunguzi wa mapema ni muhimu hata pale mwanaume hana dalili?

Kwa sababu gono linaweza kusambaa bila dalili na kusababisha matatizo ya kiafya kwa mwanaume na wenza wake. Uchunguzi wa mapema unasaidia kugundua maambukizi ya siri na kuanza matibabu kabla ya kuenea kwa viungo au wenza wengine.

11. Je, kuuma kwa kiuno kwa mwanaume ni dalili ya gono?

Hapana moja kwa moja. Kuuma kwa kiuno pekee si dalili ya uhakika ya gono, lakini linaweza kutokea endapo gono limesambaa au limeleta maambukizi ya ndani.

12. Gono inawezaje kusababisha maumivu ya kiuno?

Gono ikiacha kutibiwa, linaweza kusababisha:

  • Maambukizi ya tezi dume

  • Maambukizi ya korodani au mirija ya mbegu (epididimaitis)Hali hizi zinaweza kuleta maumivu ya kiuno, nyonga au chini ya tumbo.

13. Ni magonjwa gani mengine yanaweza kusababisha kiuno kuuma kwa mwanaume?

Sababu za kawaida ni:

  • Maumivu ya misuli au mgongo

  • Maambukizi ya njia ya mkojo (UTI)

  • Mawe kwenye figo

  • Maambukizi ya tezi dume yasiyo ya gono

  • Kukaa muda mrefu au kubeba vitu vizito


ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii

Imeandikwa:

3 Desemba 2024, 13:41:21

Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini

[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]

Rejea za mada

1. About Gonorrhea. Centers for Disease Control and Prevention. https://www.cdc.gov/gonorrhea/about/index.html. Imechukuliwa 03.12.2024

2. Gonorrhoea (Neisseria gonorrhoeae infection). Health Organization (WHO). https://www.who.int/news-room/fact-sheets/detail/gonorrhoea-(neisseria-gonorrhoeae-infection). Imechukuliwa 03.12.2024

3.Gonorrhea: Treatment update for an increasingly resistant organism – PMC. https://pmc.ncbi.nlm.nih.gov/articles/PMC4366410/. Imechukuliwa 03.12.202

bottom of page