Mwandishi:
Mhariri:
Dkt. Benjamin M, MD
ULY CLINIC
13 Julai 2025, 11:25:30

Dalili za UKIMWI
UKIMWI (Upungufu wa Kinga Mwilini) ni hatua ya mwisho ya maambukizi ya muda mrefu ya Virusi vya Ukimwi (VVU). VVU hushambulia seli za kinga za mwili (seli aina ya CD4) na kuufanya mwili kuwa dhaifu kupambana na maradhi mengine. Sio kila mtu mwenye VVU ana UKIMWI; mtu anaweza kuishi na VVU kwa miaka mingi bila dalili iwapo atapata matibabu kwa wakati.
Tofauti ya VVU na UKIMWI
VVU | UKIMWI |
Ni virusi vinavyosababisha UKIMWI | Ni hatua ya mwisho ya maambukizi ya VVU |
Mtu anaweza kuwa na VVU bila dalili kwa miaka mingi | UKIMWI huonekana baada ya kinga ya mwili kushuka/kuporomoka |
Dawa za kufubaza VVU huzuia virusi kuharibu kinga | Bila dawa, kinga huporomoka na huonekana dalili sugu |
Dalili za UKIMWI
Baadhi ya watu hupata dalili za awali zinazofanana na mafua makali. Dalili hizi huisha zenyewe na huchukuliwa kimakosa kama mafua ya kawaida. Dalili hizo za awali hujumuisha;
Homa ya ghafla
Koo kuwasha au kuuma
Maumivu ya kichwa
Maumivu ya misuli na viungo
Harara na vipele vya muda
Kukohoa kwa kiasi
Vidonda vya mdomo
Kuvimba tezi za shingoni
Kuharisha kwa muda mfupi
Kumbuka: Si kila mtu hupata dalili hizi. Wengi huendelea kuishi bila dalili kwa muda mrefu.
Hatua za maambukizi ya VVU
Hatua | Maelezo |
1. Awamu ya awali (Acute HIV) | Wiki chache baada ya maambukizi. VVU husambaa mwilini haraka. Dalili ni za mafua makali. |
2. Hatua ya utulivu (Clinical latency) | VVU huendelea kuzaliana taratibu. Hakuna dalili kwa miaka mingi (5–10) bila dawa. |
3. Hatua ya UKIMWI | Kinga ya mwili hushuka sana. Mtu huanza kupata magonjwa nyemelezi. |
Dalili za hatua ya mwisho (UKIMWI)
Watu ambao hawajaanza kutumia dawa za kufubaza VVU mapema huweza kuingia katika hatua ya UKIMWI. Dalili kuu ni:
Kupungua uzito kupita kiasi (wasting syndrome)
Kikohozi kisichopona
Kuharisha mfululizo zaidi ya mwezi
Kelele au maumivu ya kifua (pneumonia)
Kunyonyoka nywele na kukauka ngozi
Ulimi kuwa na tabaka jeupe (oral thrush)
Vipele au harara zisizotibika kwa kawaida
Tezi kuvimba sehemu mbalimbali (shingo, kwapani, kinena)
Homa sugu au ya kurudiarudia
Kutokwa jasho sana usiku
Uchovu mkali na udhaifu wa mwili
Jedwali la dalili kwa muhtasari
Aina ya Dalili | Dalili Mahususi |
Mapema (siku 7–28) | Homa, koo, maumivu ya misuli, harara, vipele, kuharisha, uvimbe wa mitoki |
Dalili za VVU zinazoendelea | Tezi kuvimba, kikohozi, kutoona vizuri, kupungua uzito taratibu |
UKIMWI kamili | Thrush ya mdomo, kupungua uzito mkubwa, nimonia, harara, jasho la usiku, fangasi wa ngozi, TB ya mapafu au ya tezi |
Jinsi ya kuzuia UKIMWI
Fanya vipimo vya mara kwa mara vya VVU
Tumia kondomu sahihi kila tendo la ndoa
Epuka kutumia sindano moja kwa watu tofauti
Mwanamke mjamzito afanyiwe uchunguzi mapema
Anza kutumia dawa za kufubaza VVU (ARVs) mara baada ya kugundulika na maambukizi
Dawa za VVU na umuhimu wake
Dawa za kufubaza virusi (ARVs) haziponyi VVU lakini huzuia kuendelea kwa ugonjwa hadi kufikia UKIMWI
Tanzania hutoa dawa hizi bila malipo kwenye vituo vyote vya afya
Dawa hizi huimarisha kinga na kuwezesha mtu kuishi maisha ya kawaida, kufanya kazi na kuzaa salama
Wakati gani wa kumwona daktari?
Muone daktari haraka kama:
Una dalili yoyote iliyoelezwa hapo juu
Umefanya tendo la ngono lisilo salama
Una historia ya VVU kwa mwenza au familia
Unahitaji ushauri kuhusu upimaji wa VVU
Hitimisho
UKIMWI ni hali inayoweza kuzuilika iwapo VVU vitagunduliwa mapema na kuanza dawa. Usione haya kufanya kipimo cha VVU, kwani hatua moja ya ujasiri inaweza kukuokoa wewe na familia yako. Kumbuka: VVU haina sura – pima, jua hali yako, ishi kwa ujasiri.
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii
Imeboreshwa,
13 Julai 2025, 11:25:30
Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini
[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]
Rejea za mada
World Health Organization (WHO). Consolidated Guidelines on HIV Prevention, Testing, Treatment, Service Delivery and Monitoring. Geneva: WHO; 2021.
UNAIDS. Global HIV & AIDS statistics — Fact sheet. Geneva: UNAIDS; 2023.
Centers for Disease Control and Prevention (CDC). HIV Basics. https://www.cdc.gov/hiv.
National AIDS Control Programme (NACP), Tanzania. Mwongozo wa Kitaifa wa Huduma za VVU/UKIMWI Tanzania. Wizara ya Afya; 2022.
Fauci AS, Lane HC. HIV disease: AIDS and related disorders. In: Jameson JL, Fauci AS, Kasper DL, et al. Harrison’s Principles of Internal Medicine. 20th ed. McGraw-Hill; 2018.