top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

ULY CLINIC

Dkt. Peter A, MD

20 Agosti 2026, 05:09:52

shahawa-zenye-damu-ulyclinic-compressor.
Homon Imbalance: Dalili, Visabaishi, Uchunguzi na Tiba

Homon Imbalance: Dalili, Visabaishi, Uchunguzi na Tiba

Mvurugiko wa homoni au Kuharibika (kupotea) kwa uwiano wa homoni mwilini ikijulikana na watu wengi na kitiba kama tatizo la 'Homon imbalance' au homoni imbalansi ni tatizo ambalo linaweza kutokewa kwa mtu yeyote awe mwanaume au mwanamke Watoto na watu wakubwa.


Kuna dalili nyingi zinaweza kutokea kumaanisha tatizo la homoni imbalance, dalili hutegemea aina ya homoni iliyoathiriwa.


Kuharibika kwa uwiano wa homoni mwilini hutoka na kupungua au kuongezeka kwa homoni kwenye damu. Mabadiliko yanaweza kuwa kidogo sana lakini bado yakaonyesha dalili za kuonekana.


Katika Makala hii imezungumzia kuhusu kutowiana kwa homoni mwilini kwa wanawake, wanaume, Watoto na wanawake walio kwenye komahedhi, visababishi na matibabu ya kutowiana kwa homoni.


Visababishi

  • Matibabu ya saratani(dawa za satatani)

  • Haipothairoidizimu

  • Haipathairoidizimu

  • Sindromu ya kushing

  • Ugonjwa wa Kisukari

  • Haipogonadizimu

  • Thairoidaitizi

  • Aina Fulani za dawa

  • Msongo wa mawazo

  • Kutokula vema

  • Magonjwa ya kula

  • Haipaplezia ya tezi ya adreno

  • Saratani mbalimbali kama saratani tezi ya pituitari na thairoidi

  • Uvimbe usio saratani kwenye tezi mbalimbali

  • Matumizi ya dawa za homoni


Visababishi kwa wanawake

  • Ujauzito

  • Kunyonyesha

  • Ugonjwa wa polisistiki ovari

  • Matumizi ya dawa za uzazi wa mpango

  • Kutojitosheleza awali kwa ovari

  • Komahedhi kabla ya wakati

  • Komahedhi


Dalili

Dalili kwa Watoto
  • Kutoota vema kwa nywele

  • Sauti kutokuwa laini kwa wanawake, na kutokuwa nzito kwa wanaume

  • Kuchelewa kukua kwa uume na korodani

  • Kukua sana kwa misuli ya mikono na miguu kusikowiana na kiwiliwili

  • Kutokupata misuli kwa wanaume

  • Kuota kwa matiti makubwa kwa wanaume na wanawake kutokukua kwa matiti

  • Kutokupata hedhi kwa wakati

  • Kutokukua vema au kutokukua kwa wanawake na wanaume


Dalili kwa wanawake
  • Ngozi kufubaa kwenye maeneo ya mikunjo haswa shingoni na maeneo ya kinena na chini ya matiti

  • Maoteo ya vipele mshikizo

  • Kukauka kwa uke(uke kukosa majimaji)

  • Kusinyaa kwa uke

  • Maumivu wakati wa kujamiana

  • Kutokwa jasho wakati wa usiku

  • Kupata hedhi nzito au isiyoeleweka

  • Kuota nywele za wanaume mfano ndevu n.k

  • Kuota chunusi

  • Nywele kukatika kirahisi

  • Kuongezeka uzito au kushindwa kupunguza uzito


Dalili kwa wanaume
  • Kukua kwa matiti kama ya wanawake

  • Kupungua hamu ya kujamiana

  • Ugumba

  • Kupungua kwa ndevu au kutoota kwa ndevu na nywele zsehemu zingine

  • Mifupa kuvunjika kirahisi

  • Matatizo ya kutosimamisha uume

  • Kutokuwa makini

  • Maumivu ya matiti

  • Kupoteza ujazo wa misuli ya mwili/kutokupata misuli mikubwa.


Dalili za ujumla

Kumbuka dalii hizi hutegemea aina ya homoni yenye shida. Si lazima mtu awe na dalili zot endo asemekane kuwa ana tatizo la kutowiana kwa homoni mwilini.

  • Kuwa na uzito mkubwa usioelezeka au kupungua uzito usioelezeka

  • Jasho kupita kawaida

  • Kupata shida ya kulala

  • Kushindwa kuhisi joto au baridi

  • Kuwa na ngozi kavu sana

  • Kubadilika kwa shinikizo la damu

  • Kubadilika kwa mapigo ya moyo

  • Mifupa kuwa mikavu

  • Kubadilika kwa kiasi cha sukari kwenye damu

  • Woga na wasiwasi

  • Kuchoka kusiko kwa kawaida

  • Kuongeza kiu

  • Hali ya huzuni

  • Kichwa kuuma

  • Tumbo kujaa gesi

  • Hamu ya kula kubadilika

  • Kupunguza hisia za mapenzi

  • Kuwa na nywele nyembamba

  • Ugumba

  • Uso kujaa

  • Uso wa duara

  • Kutokuona vizuri

  • Shingo kuvimba

  • Maumivu ya matiti

  • Sauti kuwa nzito kwa wanaume


Visababishi

Sababu zinazopelekea homoni kutokuwiana ni kama :

  • Kuwa na msongo wa mawazo wa muda mrefu

  • Kisukari

  • Kuzalishwa kwa wingi kwa homoni ya glucagon

  • Kuzalishwa kwa wingi kwa Homoni ya Insulin

  • Kuzalishwa kwa homoni chache za tezi ya thyroid

  • Kuzalishwa kwa wingi kwa homoni za tezi ya thyroid

  • Wingi au uchache wa homoni ya parathyroid

  • Mlo dhaifu

  • Kuwa na uzito kupita kiasi

  • Dawa za mbadala za homoni

  • Kuwa na uvimbe kwenye pituitary

  • Kuzalishwa kwa wingi wa homoni ya Cortisol (Cushing’s syndrome)

  • Kuzalishwa kwa uchache kwa homoni ya aldosterone na cortisol (Addison’s disease)

  • Kupata mzio mkali

  • Saratani zinazohusisha mfumo wa homoni

  • Matibabu ya kikemikali na mionzi

  • Kuwa na iodine chache

  • Kuwa katika mazingira yenye sumu kama za kuulia wadudu na magugu


Matibabu ya nyumbani

Matibabu ya nyumbani na namna ya kusaidia kurekebisha uwiano wa homoni mwilini

Mabadiliko ya homoni yanaweza kusababishwa na sababu mbalimbali, hivyo si kila tatizo la homoni linaweza kutibiwa nyumbani pekee. Baadhi ya hali huhitaji vipimo na matibabu maalumu kutoka kwa mtaalamu wa afya. Hata hivyo, hatua za maisha ya kila siku zinaweza kusaidia mwili kudhibiti uzalishaji na matumizi ya homoni na kupunguza baadhi ya dalili.

Kula mlo kamili na wenye virutubisho muhimu

Lishe bora ina mchango mkubwa katika afya ya mfumo wa homoni kwa sababu mwili hutumia virutubisho kutoka kwenye chakula kutengeneza na kusawazisha homoni.

Inashauriwa kula:

  • Mboga za aina mbalimbali

  • Matunda

  • Vyakula vyenye protini kama mayai, samaki, nyama isiyo na mafuta, kunde na maharage

  • Nafaka zisizokobolewa

  • Mafuta yenye afya yanayopatikana kwenye samaki, parachichi, karanga na mbegu

Ni muhimu kupunguza ulaji wa sukari nyingi, vyakula vilivyosindikwa sana na mafuta yasiyo na afya, kwa sababu vinaweza kuchangia kuongezeka uzito na kuvuruga udhibiti wa sukari mwilini.

Kudumisha uzito unaofaa

Uzito mkubwa au mafuta mengi mwilini yanaweza kuathiri uwiano wa baadhi ya homoni, hasa homoni zinazohusiana na insulini na homoni za uzazi.

Kwa wanawake, kupunguza uzito kwa kiwango kinachofaa kunaweza kusaidia kuboresha mzunguko wa hedhi kwa baadhi ya wenye ugonjwa wa polisistiki ovari.

Kwa wanaume na wanawake, kupunguza uzito kupita kiasi kunaweza kusaidia kuboresha matumizi ya sukari mwilini, kupunguza uchovu na kuboresha afya kwa ujumla.

Kupunguza uzito kunapaswa kufanyika taratibu kupitia mabadiliko ya lishe na kuongeza shughuli za mwili badala ya kutumia njia hatarishi.

Kufanya mazoezi mara kwa mara

Mazoezi husaidia mwili kutumia nishati vizuri, kuboresha usikivu wa insulini na kusaidia udhibiti wa uzito.

Mazoezi yanayoweza kusaidia ni pamoja na:

  • Kutembea kwa kasi

  • Kukimbia taratibu

  • Kuogelea

  • Mazoezi ya kuongeza nguvu za misuli

Ni muhimu kuchagua kiwango cha mazoezi kinacholingana na uwezo wa mwili na hali ya afya ya mtu.

Kupunguza msongo wa mawazo

Msongo wa mawazo wa muda mrefu unaweza kuathiri homoni zinazohusika na hali ya tahadhari mwilini na unaweza kuathiri usingizi, uzito, hamu ya kula na mfumo wa uzazi.

Njia zinazoweza kusaidia kupunguza msongo ni:

  • Kupata muda wa kupumzika

  • Kufanya mazoezi

  • Kulala vya kutosha

  • Kufanya shughuli zinazomfurahisha mtu

  • Kuzungumza na watu wa karibu au mtaalamu inapohitajika

Kupata usingizi wa kutosha

Usingizi una mchango mkubwa katika udhibiti wa homoni mbalimbali mwilini.

Kukosa usingizi wa kutosha kunaweza kuathiri homoni zinazodhibiti:

  • Hamu ya kula

  • Hisia

  • Matumizi ya nishati mwilini

  • Msongo wa mawazo

Mtu mzima anashauriwa kupata takribani saa 7 hadi 9 za usingizi kwa usiku kulingana na mahitaji ya mwili wake.

Kuepuka matumizi yasiyo sahihi ya dawa za homoni

Dawa za homoni kama zile zinazotumika kwa uzazi wa mpango, tiba ya kubadilisha homoni au kuongeza homoni za kiume zinapaswa kutumika kwa ushauri wa mtaalamu.

Kutumia dawa hizi bila uchunguzi kunaweza kuongeza au kupunguza homoni zisizohitajika na kusababisha madhara.

Kupunguza matumizi ya pombe na kuepuka sigara

Pombe nyingi na sigara vinaweza kuathiri utendaji wa baadhi ya tezi zinazohusika na uzalishaji wa homoni na vinaweza kuathiri afya ya mfumo wa uzazi.

Kuacha sigara na kupunguza pombe kunaweza kusaidia kuboresha afya ya mwili kwa ujumla.

Kuepuka mazingira yenye kemikali hatarishi

Baadhi ya kemikali zinazopatikana kwenye mazingira kama dawa za kuulia wadudu, baadhi ya kemikali za viwandani na uchafuzi wa mazingira zinaweza kuathiri mfumo wa homoni kwa baadhi ya watu.

Hatua za kujikinga ni pamoja na:

  • Kutumia vifaa vya kinga unapofanya kazi na kemikali

  • Kuosha matunda na mboga kabla ya kula

  • Kuepuka matumizi yasiyo ya lazima ya kemikali nyumbani

Usitumie virutubisho vya kusawazisha homoni bila ushauri

Bidhaa nyingi zinazoahidi "kusawazisha homoni" hazijathibitishwa kuwa zinafaa kwa kila mtu na baadhi zinaweza kuingiliana na dawa au kusababisha madhara.

Kabla ya kutumia virutubisho au dawa za asili kwa ajili ya homoni, ni muhimu kujua kwanza ni homoni gani ina tatizo na chanzo chake.

Wakati wa kutafuta matibabu hospitalini

Mabadiliko ya maisha yanaweza kusaidia, lakini mtu anapaswa kumuona mtaalamu wa afya ikiwa ana:

  • Kukosa hedhi kwa muda mrefu

  • Ugumu wa kupata ujauzito

  • Dalili za homoni zinazoendelea au zinazozidi kuwa mbaya

  • Kupungua au kuongezeka uzito bila sababu

  • Uvimbe shingoni

  • Mabadiliko makubwa ya ukuaji kwa mtoto

  • Dalili za kupungua kwa homoni za uzazi kwa mwanaume au mwanamke

Kutambua chanzo cha tatizo ndiyo njia bora ya kupata matibabu sahihi ya mvurugiko wa homoni.


Maswali 10 yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu mvurugiko wa homoni (Hormoni imbalance) na majibu yake ya kina

1. Ni hatua gani naweza kuchukua ili kuziweka homoni sawa na kuweza kushika mimba?

Mvurugiko wa homoni unaweza kuathiri uwezo wa kupata ujauzito kwa sababu homoni zina jukumu kubwa katika mzunguko wa hedhi, kutokea kwa yai kutoka kwenye ovari, maandalizi ya ukuta wa kizazi na uzalishaji wa mbegu za kiume. Hata hivyo, si kila tatizo la kupata ujauzito husababishwa na homoni, hivyo ni muhimu kutafuta chanzo halisi.


Hatua ya kwanza ni kufanyiwa uchunguzi ili kujua ni homoni gani imevurugika. Vipimo vinaweza kuangalia homoni zinazohusiana na uzalishaji wa mayai, homoni za tezi ya shingo, homoni ya prolaktini, sukari mwilini na wakati mwingine hali ya ovari kulingana na dalili za mtu.

Mambo yanayoweza kusaidia kuboresha uwiano wa homoni ni pamoja na kudumisha uzito unaofaa, kula mlo kamili wenye protini, mboga, matunda na mafuta yenye afya, kufanya mazoezi, kupunguza msongo wa mawazo na kupata usingizi wa kutosha.



Kwa baadhi ya wanawake, hasa wenye ugonjwa wa ovari wenye vifuko vingi vya maji (polisistiki ovari), kupunguza uzito hata kwa kiwango kidogo kunaweza kusaidia kurekebisha mzunguko wa hedhi na kuongeza uwezekano wa kupata ujauzito. Wengine wanaweza kuhitaji dawa maalumu za kusaidia uzalishaji wa mayai au kurekebisha homoni kulingana na sababu iliyogunduliwa.

2. Je, mvurugiko wa homoni unaweza kuisha wenyewe bila matibabu?

Uwezekano wa homoni kurudi katika uwiano wa kawaida hutegemea chanzo cha tatizo. Baadhi ya mabadiliko ya homoni hutokea kwa muda mfupi na yanaweza kurekebika yenyewe, mfano mabadiliko yanayotokea wakati wa ujauzito, baada ya kujifungua au wakati wa msongo mkubwa wa muda mfupi.


Hata hivyo, baadhi ya matatizo ya homoni husababishwa na magonjwa au mabadiliko ya tezi zinazozalisha homoni, hivyo yanaweza kuhitaji matibabu maalumu ili kurekebisha hali hiyo.


Kumekuwa na watu wengi wanaojaribu kutumia virutubisho au dawa za asili bila uchunguzi, lakini ni muhimu kujua kuwa si kila dalili inayofanana na mvurugiko wa homoni husababishwa na homoni. Uchunguzi husaidia kuepuka kutumia matibabu yasiyo sahihi.

3. Mvurugiko wa homoni unaweza kusababisha kuchelewa au kukosekana kwa hedhi?

Homoni zina nafasi kubwa katika kudhibiti mzunguko wa hedhi. Mabadiliko katika homoni zinazodhibiti ovari, tezi ya pituitari au tezi thairoidi yanaweza kufanya hedhi ichelewe, iwe nzito, iwe isiyo na mpangilio au ikosekane kabisa.


Sababu zinazohusiana na homoni zinazoweza kuathiri hedhi ni pamoja na ugonjwa wa polisistiki ovari, mabadiliko ya homoni ya tezi ya shingo, kuongezeka kwa homoni ya prolaktini na kushuka kwa uzalishaji wa homoni za uzazi.

Hata hivyo, kukosa hedhi


kunaweza pia kusababishwa na ujauzito, kupungua au kuongezeka uzito sana, mazoezi makali, msongo wa mawazo au baadhi ya dawa. Kwa hiyo, uchunguzi wa sababu ni muhimu.

4. Nina dalili za mvurugiko wa homoni lakini vipimo vyangu viko kawaida, inawezekana?

Ndiyo, inawezekana mtu kuwa na dalili zinazofanana na mvurugiko wa homoni lakini vipimo vya awali vikaonekana kawaida.


Sababu ni kwamba dalili nyingi za homoni zinafanana na matatizo mengine. Mfano, uchovu, kuongezeka uzito, mabadiliko ya hisia au kukosa usingizi vinaweza kusababishwa na msongo wa mawazo, matatizo ya lishe, usingizi hafifu au magonjwa mengine.


Pia, baadhi ya homoni hubadilika kulingana na muda wa siku, hatua ya mzunguko wa hedhi au hali ya mwili wakati kipimo kinapofanyika. Wakati mwingine vipimo vinahitaji kurudiwa au kuongezwa kulingana na historia ya mgonjwa.


Daktari huangalia mchanganyiko wa dalili, uchunguzi wa mwili na vipimo badala ya kutegemea kipimo kimoja pekee.

5. Mvurugiko wa homoni unaweza kusababisha kuongezeka uzito hata kama sili sana?

Homoni zinaweza kuathiri namna mwili unavyotumia na kuhifadhi nishati. Baadhi ya mabadiliko ya homoni yanaweza kufanya mtu kuongeza uzito au kushindwa kupunguza uzito licha ya jitihada.


Mfano, matatizo ya tezi ya shingo yanaweza kupunguza kasi ya matumizi ya nishati mwilini. Pia, mabadiliko ya homoni yanayohusiana na insulini yanaweza kuathiri matumizi ya sukari na kuhifadhi mafuta mwilini.


Hata hivyo, uzito huathiriwa na mambo mengi kama kiasi cha chakula, shughuli za mwili, usingizi, msongo wa mawazo na vinasaba. Si kila ongezeko la uzito husababishwa na homoni.

6. Je, mvurugiko wa homoni unaweza kuathiri uwezo wa mwanaume kupata mtoto?

Homoni zina umuhimu mkubwa katika uzalishaji wa mbegu za kiume, hamu ya tendo la ndoa na utendaji wa mfumo wa uzazi wa mwanaume.


Mabadiliko ya homoni yanaweza kusababisha:

  • Kupungua kwa uzalishaji wa mbegu za kiume

  • Kupungua hamu ya tendo la ndoa

  • Matatizo ya kusimamisha uume

  • Kupungua kwa misuli ya mwili

  • Kupungua kwa ndevu au nywele za mwili

Sababu zinaweza kuwa matatizo kwenye korodani, tezi ya pituitari, uzito mkubwa, baadhi ya dawa au magonjwa mengine.


Mwanaume mwenye changamoto ya kupata mtoto huhitaji uchunguzi wa mfumo wa uzazi pamoja na vipimo vya mbegu za kiume na homoni kulingana na hali yake.

7. Ni vyakula gani vinaweza kusaidia kurekebisha homoni?

Hakuna chakula kimoja kinachoweza "kusawazisha homoni" moja kwa moja, lakini mlo bora husaidia mwili kutengeneza na kutumia homoni kwa njia inayofaa.

Lishe yenye manufaa huwa na:

  • Protini za kutosha kwa ajili ya ujenzi wa mwili

  • Mboga na matunda yenye vitamini na madini

  • Mafuta yenye afya kama yale yanayopatikana kwenye samaki, karanga na mbegu

  • Vyakula vyenye nyuzinyuzi vinavyosaidia udhibiti wa sukari mwilini


Kupunguza vyakula vilivyosindikwa sana, sukari nyingi na mafuta yasiyo na afya kunaweza kusaidia hasa kwa watu wenye matatizo yanayohusiana na uzito na insulini.


Hata hivyo, kama kuna ugonjwa maalumu wa homoni, lishe pekee inaweza isiwe tiba kamili.

8. Msongo wa mawazo unaweza kuvuruga homoni?

Msongo wa mawazo wa muda mrefu unaweza kuathiri mfumo wa homoni kwa sababu mwili huongeza uzalishaji wa homoni zinazohusiana na hali ya tahadhari kama kotisoli.

Mabadiliko haya yanaweza kuathiri:

  • Usingizi

  • Hamu ya kula

  • Uzito

  • Mzunguko wa hedhi

  • Hamu ya tendo la ndoa


Kwa baadhi ya wanawake, msongo mkubwa unaweza kufanya hedhi ibadilike au kuchelewa kwa sababu unaathiri mawasiliano kati ya ubongo na mfumo wa uzazi.


Kupunguza msongo kupitia usingizi wa kutosha, mazoezi, mbinu za kupumzika na kupata msaada wa kihisia kunaweza kusaidia afya ya homoni.

9. Mvurugiko wa homoni baada ya kujifungua huchukua muda gani kuisha?

Baada ya kujifungua, mwili hupitia mabadiliko makubwa ya homoni ili kurudi katika hali ya kawaida na pia kusaidia uzalishaji wa maziwa kwa anayenyonyesha.

Mabadiliko haya yanaweza kusababisha:

  • Kubadilika kwa hisia

  • Uchovu

  • Mabadiliko ya hedhi

  • Mabadiliko ya hamu ya tendo la ndoa

  • Mabadiliko ya uzito


Kwa wanawake wengi, homoni hurudi taratibu kadri miezi inavyopita. Hata hivyo, baadhi ya matatizo yanaweza kuhitaji uchunguzi, mfano matatizo ya tezi thairoidi yanayoweza kutokea baada ya kujifungua.


Ikiwa dalili ni kali, zinaendelea kwa muda mrefu au zinaathiri maisha ya kila siku, ni muhimu kupata ushauri wa mtaalamu.

10. Ni lini ninapaswa kwenda hospitali kwa sababu ya dalili za mvurugiko wa homoni?

Si kila mabadiliko ya mwili yanahitaji dharura, lakini baadhi ya dalili zinahitaji uchunguzi wa mapema.

Ni vizuri kumuona mtaalamu ikiwa mtu ana:

  • Kukosa hedhi kwa muda mrefu bila sababu inayoeleweka

  • Kutokwa damu nyingi au isiyo ya kawaida

  • Ugumu wa kupata ujauzito

  • Kupungua uzito au kuongezeka uzito bila sababu

  • Ukuaji wa nywele nyingi zisizo za kawaida kwa mwanamke

  • Kupungua sana kwa hamu ya tendo la ndoa

  • Matatizo makubwa ya kusimamisha uume

  • Uvimbe shingoni

  • Mabadiliko makubwa ya hisia au uchovu usioelezeka


Uchunguzi wa mapema husaidia kutambua chanzo na kuanza matibabu yanayofaa kabla tatizo halijawa kubwa.


ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii

Imeandikwa:

17 Aprili 2020, 21:58:37

Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini

[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]

Rejea za mada hii:

  1. Melmed S, Auchus RJ, Goldfine AB, Koenig RJ, Rosen CJ. Williams Textbook of Endocrinology. 15th ed. Philadelphia: Elsevier; 2024.

  2. Gardner DG, Shoback D. Greenspan’s Basic & Clinical Endocrinology. 11th ed. New York: McGraw Hill; 2023.

  3. Jameson JL, De Groot LJ, de Kretser DM, Giudice LC, Grossman AB, Melmed S, et al. Endocrinology: Adult and Pediatric. 8th ed. Philadelphia: Elsevier; 2024.

  4. Endocrine Society. Clinical Practice Guidelines. Washington, DC: The Endocrine Society; 2024.

  5. Chaker L, Bianco AC, Jonklaas J, Peeters RP. Hypothyroidism. Lancet. 2017;390(10101):1550-1562. doi:10.1016/S0140-6736(17)30703-1.

  6. De Leo S, Lee SY, Braverman LE. Hyperthyroidism. Lancet. 2016;388(10047):906-918. doi:10.1016/S0140-6736(16)00278-6.

  7. Teede HJ, Tay CT, Laven JJE, Dokras A, Moran LJ, Piltonen T, et al. Recommendations from the 2023 International Evidence-based Guideline for the Assessment and Management of Polycystic Ovary Syndrome. J Clin Endocrinol Metab. 2023;108(10):2447-2469. doi:10.1210/clinem/dgad463.

  8. Fleseriu M, Hashim IA, Karavitaki N, Melmed S, Murad MH, Petersenn S, et al. Hormonal replacement in hypopituitarism in adults: an Endocrine Society clinical practice guideline update. J Clin Endocrinol Metab. 2016;101(11):3888-3921. doi:10.1210/jc.2016-2118.

  9. Bornstein SR, Allolio B, Arlt W, Barthel A, Don-Wauchope A, Hammer GD, et al. Diagnosis and treatment of primary adrenal insufficiency: an Endocrine Society clinical practice guideline. J Clin Endocrinol Metab. 2016;101(2):364-389. doi:10.1210/jc.2015-1710.

  10. Nieman LK, Biller BMK, Findling JW, Newell-Price J, Savage MO, Stewart PM, et al. The diagnosis of Cushing’s syndrome: an Endocrine Society clinical practice guideline. J Clin Endocrinol Metab. 2008;93(5):1526-1540. doi:10.1210/jc.2008-0125.

  11. Grossman A, Johannsson G, Quinkler M, Zelissen P. Perspectives on the management of adrenal insufficiency: clinical insights. Endocr Connect. 2013;2(2):R1-R12. doi:10.1530/EC-13-0022.

  12. Fauser BCJM, Tarlatzis BC, Rebar RW, Legro RS, Balen AH, Lobo R, et al. Consensus on women’s health aspects of polycystic ovary syndrome. Fertil Steril. 2012;97(1):28-38.e25. doi:10.1016/j.fertnstert.2011.09.024.

  13. Grossman M, Hoermann R, Wittert G. Male hypogonadism. Lancet Diabetes Endocrinol. 2015;3(10):782-792. doi:10.1016/S2213-8587(15)00161-5.

  14. Ross DS, Burch HB, Cooper DS, Greenlee MC, Laurberg P, Maia AL, et al. 2016 American Thyroid Association guidelines for diagnosis and management of hyperthyroidism and other causes of thyrotoxicosis. Thyroid. 2016;26(10):1343-1421. doi:10.1089/thy.2016.0229.

  15. American Diabetes Association Professional Practice Committee. Standards of Care in Diabetes—2024. Diabetes Care. 2024;47(Suppl 1):S1-S321. doi:10.2337/dc24-SINT.

  16. Hall JE. Guyton and Hall Textbook of Medical Physiology. 15th ed. Philadelphia: Elsevier; 2021.

  17. Santoro N, Epperson CN, Mathews SB. Menopause and work: the role of hormonal changes and symptoms. J Clin Endocrinol Metab. 2015;100(9):3397-3403. doi:10.1210/jc.2015-2236.

bottom of page